HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE 13 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria ya FREYS COACH ifanyayo safari Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku saa 12 asubuhi, 0622 292990
ILIPOISHIA
Akauza lile gari. Pesa hizo
nazo zikaisha kwa chakula na kuwalipa madaktari. Siku za mwanzo mwanzo marafiki
zake waliokuwa wanakuja nyumbani kumjulia hali walikuwa wakimpa pesa kumsaidia.
Lakini mwisho marafiki hao walichoka. Nikawa sioni mtu.
Tulifikia mahali umeme
ulikatwa nyumbani kwa sababu tulikuwa na deni kubwa. Tukawa tunatumia taa za
mafuta
Kwa vile niliona lile tatizo
lilianzia kwa yule mganga wa kienyeji nikarudi tena kule kule kumueleza hali
halisi.
“Mpaka dakika hii ni kwamba
mume wangu bado haoni” nikamwambia.
“Bado haoni hadi sasa?”
Mganga akajidai kuniuliza kwa mshangao.
“Bado”
“Nilipoona hutokei nilijua
mume wako amepona”
“Tulikuwa tunashughulikia
matibabu ya hospitali. Kwa kweli tumetumia pesa nyingi sana bila mafanikio. Mume wangu kwa sasa
haweza kufanya kazi, pesa hatuna. Juzi juzi ameuza gari lake na
pesa tulizopata pia zimekwisha. Imefikia hadi nyumbani tumekatiwa umeme!”
SASA ENDELEA
Nilipomwambia hivyo mganga
huyo aligwaya. Uso wake ukaonesha wazi kufedheheka.
“Sasa nyinyi mmeharibu”
akaniambia.
“Tumeharibu nini?”
“Wakati ule nilipokupa zile
dawa zangu, kama uliona hazikumsaidia ungerudi
kunieleza. Badala yake mmekwenda kuchanganya na matibabu ya kizungu. Hizi dawa
zangu zina miko”
“Sasa ningefanyaje wakati
mume wangu alipoona dawa hazikumsaidia ametaka apelekwe hospitali na huko
ameambiwa hawezi kuona tena”
Mganga akanyamaza kimya.
Baada ya kupita sekunde chache aliniambia.
“Kama
ungerudi tena nina hakika hivi sasa mume wako angekuwa anaona”
“Sasa ndio nimerudi hivi”
“Umechelewa!”
“Nimechelewa kivipi?”
nikamuuliza.
Mganga akanyamaza kimya.
Alionesha alikuwa na jibu lakini hakutaka kulitoa, labda aliona halikuwa jibu la kufurahisha.
Na mimi sikutaka kumuuliza
tena, nikabaki kimya nikiwaza.
Baada ya ukimya wa sekunde
kadhaa mganga akanimabia.
“Basi njoo kesho nahitaji
kupata muda wa kulichunguza hilo
tatizo la mume wako”
“Utalichunguzaje tatizo la
mume wangu bila mwenyewe kuwepo hapa?” nikamuuliza.
“Ninajua mwenyewe, wewe nenda
zako kesho njoo”
“Nimekuelewa lakini naomba
unifanyie bidii kwani hali ya maisha yetu imekuwa ngumu kwa sasa. Mume wangu
hawezi kwenda kufanya kazi kutokana na
hali aliyonayo”
“Umeshanieleza na
nimeshakuelewa”
“Sawa”
Nikanyanyuka na kumuaga yule
mganga kisha nikatoka. Nilitoka nikiwa na matumaini madogo sana
ya mume wangu kupona lakini kama wasemavyo
waswahili uongo wa mganga, nafuu ya mgonjwa.
Hata kama yule mganga atakuwa
ananidanganya, bado nitaendelea kufuatilia maelezo yake kwa sababu sikuwa na
jinsi. Niliyataka mwenyewe na nimeshayapata.
Siku iliyofuatia nikarudi
tena kwa mganga huyo. Sikukuta watu pale nje lakini nilikuta gari jipya aina ya
Rav 4 limeegeshwa.
Kwa vile sikukuta watu
nilikwenda kubisha mlango moja kwa moja.
“Pita ndani” nikaisikia sauti
ya mganga ikiniambia kutoka ndani. Nikaingia.
Nilimkuta mganga huyo
akizungumza na kijana mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kiti.
Kwa kudhani alikuwa mteja
nilisita kwenye mlango.
“Karibu ukae” mganga
akanisisitiza.
Nikawaamkia kabla ya kukaa
kwenye jamvi.
“Huyu hapa ni mwanangu tu, si
mteja kama ulivyodhani” mganga akaniambia
nilipoketi.
Nikamtazamam vizuri kijana
huyo. Alikuwa amevaa vizuri na alionekana kama
alikuwa mgeni.
“Anaishi Dar, amekuja jana
usiku, ndiye mwenye gari yake hapo nje”
“Nimefurahi kumuona…kaka
habari za Dar?” nikamsalimia.
“Nzuri, sijui nyinyi hapa
Tanga? Mnatunyima nini?” kijana huyo akaniuliza huku akitabasamu.
“Jua kali tu na shida za
kilimwengu zimetuandama, ndiyo maana tunahangaika”
Kijana huyo akacheka kidogo.
“Ndio maisha. Maisha ni
kuhangaika”
“Mambo yake huyu mama ni
makubwa” Mganga akadakia kisha akaniambia.
“Nimelichunguza tatizo la
mume wako, nimeona ni kubwa. Siyo kama tulivyodhani hapo mwanzo. Mume wako
amerogwa, kwa hiyo tatizo limekwenda kwenye macho”
Hapo nikashituka.
“Unataka uniambie sio zile
dawa nilizozibadili zilizompofua macho?”
“Zile dawa zilikuwa ni
kisibabu tu lakini kuna tatizo kubwa nyuma yake. Kama
zingekuwa ni zile dawa, mume wako angekuwa ameshapona”
Nikashusha pumzi ndefu kisha
nikamuuliza.
“Sasa tutafanyaje na sisi ni
weupe, pesa zote zimeisha”
“Nitawasaidia hivyo hivyo
kidogo kidogo. Nitakupa dawa zangu aanze kwenda kutumia”
“Sawa”
Wakati mganga huyo
ananiandalia hizo dawa, yule kijana akainuka kwenye kiti.
“Baba, sasa mimi natoka
kidogo” akamwambia baba yake.
“Unakwenda mijini?”
“Ndiyo nataka nifike mjini
mara moja”
“Subiri umsaidie huyu mama,
anaenda huko huko”
“Nimsaidie lifti?”
“Ndiyo. Subiri kidogo”
“Basi namsubiri kwenye gari”
“Sawa”
Yule kijana akatoka.
Mganga huyo alinipatia dawa
za mizizi. Akaniambia nianze kumchemshia na kumywesha mume wangu kikombe kimoja
asubuhi na kikombe kimoja jioni.
“Atatumia kwa siku saba.
Baada ya siku saba utafute laki mbili ili nimfanyie kafara la kuondoa ule
uchawi”
Mganga aliponiambia hivyo niliguna.
“Nitazipata wapi hizo laki
mbili?” nikamuuliza.
“Fanya mipango katika hizi
siku sita. Ni lazima hizo pesa zipatikane kama
unataka mume wako apone kabisa”
Baada ya kuwaza kidogo
nilichukua ile mizizi niliyopewa ambayo mganga huyo alikuwa ameitia kwenye
mfuko wa nailoni, nikainuka.
“Haya nitakwenda kufanya
mipango, kama nikishindwa nitakuja kukwambia”
nikamwambia.
Nilipotoka nje nilimkuta yule
kijana akinisubiri kwenye gari. Aliponiona alinifungulia mlango wa upande wa
pili wa dereva akaniambia.
“Ingia twende”
Nikaingia kwenye gari na
kufunga mlango.
Kijana huyo akaliwasha gari tukaondoka.
Kupata hiyo lifti nilishukuru sana
kwani ningeweza hata kurudi nyumbani kwangu kwa miguu.
“Mimi naitwa Chinga, sijui
mwenzangu unaitwa nani?” Kijana huyo akaanza kuniuliza.
“Miye naitwa Salama”
nikamjibu.
“Huyo mwenye matatizo ni mume
wako?” akaniuliza.
“Ndiyo ni mume wangu”
“Ana matatizo gani?”
“Amepofuka macho. Na sababu
ya kupofuka ni dawa nilizopewa na mzee. Dawa ambayo niliambiwa nimtilie kwenye
chakula nilimtilia kwenye maji ya kuoga.
Baada ya kuoga yale maji, macho yalipofuka hapo hapo”
Kijana huyo nilipomwambia
hivyo alitikisa kichwa kusikitika.
“Ulipomueleza mzee
alikwambiaje?”
ITAENDELEA kesho usikose kujua nini kitajiri hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment