Tuesday, October 11, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE

HADITHI Inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria ya FREYS COACH, Tanga hadi Singida kila siku kupitia Moshi, Arusha na Babati , kwa mawasiliano 0622 292990
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 17
 
ILIPOISHIA
 
“Atakuwaje tayari kunioa wakati hajaniona?” nikamuuliza.
 
Mganga akacheka. 
 
“Ameshakuona na amekupenda lakini tatizo ni hilo kwamba una mume”
 
Hapo nikashangaa kidogo.
 
“Ameniona wapi?” nikamuuliza yule mganga.
 
Badala ya kunijibu alicheka kisha akanyanyuka ili atoke mle chumbani.
 
“Babu mbona huniambii, unatoka?”
 
Mzee alikuwa ameshafika kwenye mlango akageuka na kuniambia. 
 
 “Zungumza na mwenzako, yeye atakuambia”
 
Aliponiambia hivyo akatoka mle chumbani. Yule kijana akakaa pale alipotoka baba yake.
 
“Naona baba amekupenda, anataka uwe mkwe wake” kijana huyo akaniambia.
 
“Anataka niwe mkwe wake kwa nani?” nikamuuliza.
 
“Mimi nilikuja hapa Tanga kutafuta mke. Kwa kweli siku ile ya kwanza nilipokuona nilikupenda na nikamueleza baba. Akaniambia kuwa una mume wako. Lakini kama nyumbani kwako kuna matatizo twende zetu Dar”
 
Nikainamisha kichwa changu chini, nusu ilikuwa kwa aibu na nusu kufikilia yale maneno aliyoniambia. Nikawa namtazama kwa kumuiba. Nilimtazama kichwani mpaka miguuni. Kwa kweli alikuwa amevaa nguo za thamani na alionekana mtanashati na mwenye pesa lakini…...
 
“Mbona uko kimya?” akaniuliza alipoona nimenyamaza.
 
“Nafikilia hayo maneno uliyoniambia”
 
“Umeyaonaje?”
 
“Si wezi kukujibu kwa sasa, acha nikafikirie kwanza”
 
“Kitakachoendelea kuniweka hapa Tanga kwa sasa itakuwa ni jibu lako”
 
“Kwani wewe unafanyakazi gani?” nikamuuliza.
 
“Mimi ni mfanyabiashara”
 
“Una duka?”
 
“Sina duka isipokuwa huchukua oda kwa wenye maduka halafu ninakwenda nchi za nje kama vile Dubai au China kununua bidhaa na kuwaletea”
 
Aliponiambia hivyo niligutuka, nikajiambia kimoyomoyo.  “Kumbe huyu kijana ana pesa za maana”
 
 
Hapo hapo moyo wangu ukaanza kupata tamaa.
 
“Ni bidhaa gani unazoleta?” nikamuuliza.
 
“Chochote ninachoagizwa, magari, pikipiki, tv, mafriji na hata nguo za wanawake na wanaume”
 
Nikamtazama tena alivyokuwa amevaa kisha nikamuuliza.
 
“Unaishi wapi?”
 
“Mimi nipo Masaki. Nina nyumba yangu pale”
 
“Huna mke?”
 
“Sijaoa bado, ndiyo nimekuja huku kwetu kutafuta mke. Unajua ninaposafiri kwenda nje ya nchi sina mtu wa kumuachia nyumba. Kuna siku nyumba yangu ilivunjwa nilipokuwa sipo”
 
Maelezo yake yalikwisha nilainisha. Alikuwa na sifa zote mbili nilizokuwa ninazihitaji.
 
Kwanza alikuwa na pesa. Na pili alikuwa mtanashati. Sura yake pia ilikwisha nivutia na alionekana mpole. Ningeweza kumjibu pale pale kuwa nipo tayari kwenda naye Dar lakini sikutaka anione nilikuwa rahisi. Angeweza kunidharau. Nikamuwekea kikwazo.
 
“Lakini si unajua niko kwenye ndoa?”
 
“Muhimu ni kukubaliana mimi na wewe. Tukisha kubaliana tutajua nini la kufanya” Chinga akaniambia.
 
Nikanyanyuka kwenye kiti. 
 
“Acha nikafikilie hilo suala halafu nitakujibu kama ndiyo au hapana”
 
Chinga naye akanyanyuka. 
 
“Nitegemee lini jibu lako? Si unajua nataka kurudi Dar?” akaniuliza.
 
“Wewe umesema hutaondoka, unasubiri jibu langu”
 
“Ndiyo lakini nikikaa sana hapa Tanga kazi zangu zinaharibika”
 
“Usijali nitakujibu haraka, sitapenda kazi zako ziharibike kwa ajili yangu”
 
“Kwa hiyo ndiyo unakwenda zako?”
 
“Ndiyo ninakwenda zangu. Mzee ameshaniambia hakuna dawa”
 
“Si tutarudi wote?”
 
“Wewe pia unarudi mjini?”
 
“Ninakurudisha wewe tu”
 
“Haya twende”
 
“Subiri nimuage mzee”
 
Chinga akatoka. Mimi nikarudi kuketi. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa na baba yake.
 
“Babu ninakwenda zangu” nikamwaambia yule mganga.
 
“Sasa tutaonana lini tena?” akaniuliza.
 
Nikatabasamu na kumuangalia Chinga.
 
“Tutaonana siku yeyote isiyokuwa na jina”
 
“Mwenzako si atakupeleka na gari?”
 
“Ameniambia atanipeleka”
 
“Basi vizuri. Tutaonana hiyo siku utakayo kuja” mzee akaniambia.
 
Nikatoka na Chinga.. Mimi nilikuwa mbele. Chinga alikuwa nyuma yangu.Tulipokuwa nje akaniambia kuwa alikuwa amesahau kitu. 
 
“Nisubiri ndani ya gari” akaniambia huku akirudi ndani.
 
Hakuchukua muda akatoka. Alinikuta nimeshajipakia. Akaliwasha gari tukaondoka.
 
“Uliishia darasa la ngapi?” Chinga akaniuliza wakati gari likiwa katika mwendo  wa spidi hamsini nilipoangalia kwenye kioo cha kuonyesha mwendo wa gari..
 
“Niliishia kidato cha nne”
 
“Shule gani?”
 
“Shule ya Sekondari ya Usagara”
 
“Mimi pia nilisomea Usagara. Nilipomaliza kidato cha sita ndipo nilipokwenda Dar kujiunga na chuo”
 
“Chuo gani?”
 
“Chuo Kikuu cha Mlimani”
 
“Nilichukua Digrii yangu pale mwaka juzi”
 
“Ukaenda wapi?”
 
“Nilibaki pale pale Dar lakini sikutaka kazi za kuajiriwa. Niliamua kuwa mfanyabiashara”
 
“Kwanini sasa umechelewa kuoa?” nikamuuliza
 
“Ah! Kwanza nilikuwa natengeneza maisha yangu. Kwa sasa ndiyo ninapaswa nioe kwa sababu nyumba ninayo, nina gari mbili za kutembelea na natumaini moja itakuwa ni yako na pia nimejiwekea akiba ya kutosha benki”
 
Kusema kweli kijana huyo alifanikiwa kunichota kiakili na kisaikolojia. Alikuwa na sifa zote za kuwa mume wangu. Nikawa najiuliza kwanini niliolewa na Ibrahim na nisiolewe na yeye?
 
Ingawa nafasi ya kuolewa na yeye ilikuwa imeshanijia na ilikuja wakati mzuri lakini ilikuwa na changamoto. Mimi tayari nilikuwa mke wa mtu na ili niweze kuolewa na mume mwingine ni lazima niachike kwa mume wa kwanza. Nisingeweza kuolewa nikiwa ndani ya ndoa.
 
Wazo la kudai talaka kwa Ibrahim likanijia. Lakini niliona suala hilo lilikuwa gumu kwa wakati huu. Ibrahim asingeitoa hata kwa kumshikia bastola.
 
Nikajiuliza  nitaendelea kuteseka na yeye hadi lini wakati kuna mtu anayenihitaji. Kwa umri wangu na uzuri niliokuwa nao haikupasa niendelee kuishi na Ibrahim, mwanaume aliyekwisha poteza sifa za kuishi na mimi.
 
Sikuwa nikiwaza kabisa kwamba ni mimi niliyemfikisha Ibrahim katika yale maisha ya mateso kwa tamaa zangu za kidunia.
   
Chinga alinifikisha kwenye kile kituo cha daladala alikonichukua. Kituo hicho sasa kilikuwa ndio mahali petu pa kuanzia safari zetu na kuzimalizia.
 
Kwa mara ya kwanza tulipeana namba za simu ili tuweze kuwasiliana. Nikamuahidi kwamba majibu yangu atayapata kwenye simu.
 
Kabla sijateremka kwenye gari alitoa pochi yake akanipa tena shilingi laki moja.
 
“Zitakusaidia katika matatizo yako”akaniambia na kuongeza.
 
“Ukiwa na tatizo lolote la pesa usisite kuniambia”
 
“Ahsante. Nashukuru sana.Sasa acha niende”
 
“Sawa, basi utanipigia muda wowote utakaopenda”
 
“Sawa”
 
Nikafungua mlango wa gari na kushuka. Nikiwa nje ya gari nilimpungia mkono wa kumuaga na yeye akanipungia.
 
Nikaondoka zangu. Na yeye akaondka na gari. Nilipitia kwenye bucha ya nyama nikanunua kilo moja ya nyama kisha nikaenda kwenye duka ninalonunulia vitu. Nikanunua kilo mbili za mchele na mahitaji mengine kisha nikarudi nyumbani.
 
Sebuleni nilimkuta shemeji Zacharia akiangalia Tv. Ibrahim hakuwepo. Nikajua alikuwa chumbani amelala. Sikuingia chumbani kwa kuwa nilijua angeniuliza ninakotoka kwa vile nilichelewa sana.
 
Nikaingia katika chumba kingine ambacho huweka nguo zangu za kufanyia kazi za nyumbani. Nikabadili nguo nilizokuwa nimevaa kisha nikaingia jikoni na kutayarisha ile nyama. Nyama ilipokuwa jikoni nilichambua mchele. Nilikuwa nimekusudia kupika pilau.
 
Baada ya masaa mawili pilau ikawa tayari. Nikatenga chakula juu ya meza. Nikamwaambia shemeji akamchukue kaka yake waende wakale. Mimi nilijipakulia kwenye sahani yangu nikaenda kuketi uani peke yangu.
 
Wakati ninakula kile chakula nilikuwa nikimuwaza Chinga na jinsi nitakavyoweza kuwa naye. Nilijiambia itakuwa ni uzembe kuacha aoe mke mwingine wakati alikuwa ameshanipenda na amekuwa akinipa pesa nyingi.
 
“Nitaendelea kuishi na hili zezeta hadi lini? Mwisho nitakosa hata nguo ya kuvaa” nikajisemea peke yangu.
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment