Friday, October 7, 2016

YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 15

HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE 15
ILIPOISHIA
nyumbani nikaona gari inanifungia breki miguuni, nikashituka. Nilipotupa macho nikaona ni ile Rav 4 ya yule kijana niliyekutana naye siku ile kwa yule mganga.
    Akatoa kichwa kwenye dirisha la gari na kunisalimia.
    “Asalaam alaykum”        
    "Alaykum salaam" nikamjibu huku nikitabasamu.
    "Habari za huko?" nikamuuliza
    "Nzuri. Ingia nikusindikize" akaniambia.
    Nikazunguuka upande wa pili wa gari nikajipakia.
    "Umekuja lini?" nikamuuliza.
    "Nimekuja juzi"
    "Mzee hajambo?"
    "Hajambo"
    "Nilikuwa nataka kwenda kumuona nimjulishe hali ya mgomjwa lakini sijapata nafasi" Nilisingizia nafasi lakini ukweli ni kuwa sikuwa na pesa ya nauli.
   "Kwani yule bwana mpaka sasa hajapona?"
   "Bado hajapona. Tuna hali mbaya kweli hivi sasa!"
   "Ninakuona, sivyo ulivyokuwa"
SASA ENDELEA
   "Mume hawezi kufanyakazi, hatuna pesa. Yaani sijui nikwaambie nini!"
   "Pole sana"
   Tulikuwa tumeshafika kwenye kile kituo cha daladala alichonishusha siku ile. Akasimamisha gari na kutoa pochi mfukoni.  Akaifungua na kuchomoa kitita cha noti, akanipa.
   "Chukua hii laki moja itawasaidia kwa siku mbili tatu" akaniambia.
   Kwa wakati ule niliona ni hela kubwa sana. 
 "Ahsante, nakushukuru sana" nikamwaambia.
"Sasa ungependa kwenda lini kwa mzee?" akaniuliza.
"Siku yoyote tu"
"Basi kesho nikienda huko nikupitie twende pamoja"
"Kwani wewe unalala wapi?" nikamuuliza.
SASA ENDELEA
"Mimi ninalala huku mjini"
"Mna nyumba yenu huku mjini?"
"Hapana. Nyumba yangu ipo Dar. Nikija huku ninalala hoteli"
"Hoteli gani?"
"Mtendele Hotel. Ipo pale Chuda. Ni Hoteli ninayoitumia kila ninapokuja Tanga kwa sababu huduma zake ni bora sana"
Nikafikiri kidogo kisha nikamuuliza 
"Utanipitia saa ngapi twende huko Kisosora?"
"Saa nne asubuhi"
"Basi nitakusubiri hapa kwenye kituo cha daladala"
"Sawa" akaniambia.Tukaagana.
 
Kutokana na shida tuliyokuwa nayo pale nyumbani, pesa
nilizopewa na yule kijana nilizificha ziwe akiba yangu. Sikutaka mume wangu ajue kuwa nilikuwa na kiasi hicho cha pesa.
Baada ya kumaliza kupika nilimtengea chakula mume wangu nikamuacha aendelee kula, mimi nilikwenda kukaa uani na sahani yangu. Sikutaka kula naye. Kusema kweli japokuwa ni mimi niliyemsababishia upofu, sikuwa nikimuona raha tena. Hata tulipokuwa tunalala usiku tulilala tukiwa mzungu wa nne. Nilikuwa nikielekea upande wangu.
 
Sasa niliamini kuwa mapenzi ya kweli yapo kwenye pesa. Kama pesa hakuna na matumaini ya kuzipata hayapo tena, hakuna mapenzi. Wakati mwingine hali inapokuwa ngumu sana nyumbani mimi ndiye niliyelazimika kutoka kwenda kwa ndugu zangu kuwaomba pesa za matumizi.
 
Mume wangu mwenyewe alikuwa ameshagundua kuwa nilikuwa nimebadilika. Sikuwa yule Salma wa mwanzo. Hata ile lugha ya kistaarabu kwake nilikuwa sinayo tena. Wakati mwingine nilikuwa nikimjibu mbovu na yeye kwa kujua hakuwa na uwezo na alikuwa akinitegemea mimi, alikuwa akinyamaza.
 
Wakati ninakula pale uani nilisikia akiniita. Kwa kweli sauti yake ilikuwa ikinikera sana kwa sababu ya kuniita kila wakati.
 
Nikajifanya kama sikumsikia, nikanyamaza kimya. Akaniita mara ya pili na ya tatu.Kelele zake zikanifanya nihamaki.
 
“Wataka nini babu wewe!?” nikamuuliza kwa sauti ya juu na kuongeza.
 
“Huchoki kuniita?”
 
“Njoo mke wangu” akaniambia kwa sauti ya upole.
 
“Mimi ninakula, unataka nini?”
 
“Kumbe umekwenda kula huko?”
 
“Kula ni kula tu, popote unaweza kula. Sema unataka nini?”
 
Akanyamaza. Nikanyanyuka pale nilipokuwa nimeketi nikaingia ndani. Nilimkuta ameshamaliza kula.
 
“Unataka nini?” nikamuuliza kwa sauti ambayo haikuwa tulivu
 
“Nipeleke sebuleni. Nitakaa hapa mpaka saa ngapi?”
 
“Kwani wewe utajizoesha lini kutembea mwenyewe? Mbona kuna wenzako wasioona wanapapasa kuta wenyewe mpaka wanafika wanakotaka. Utanitegemea mimi mpaka lini? Je kama sipo?”
 
“Zacharia hayupo, ningemuita yeye lakini ametoka mara moja”
 
Nikamshika mkono, akainuka. Nikaenda naye sebuleni.
 
“Sasa kaa hapa kama unataka kukaa, siyo tena uanze kuniitaita!” nikamwambia.
 
“Nivumilie mke wangu usikasirike” akaniambia.
 
“Ningekuwa mimi si ungekwisha nitimua!”
 
Nilipomuambia hivyo akanyamaza kimya.
 
Nikaondoka. Sikurudi tena kule uani, nikaenda kukaa kwenye meza ya chakula kwa vile yeye alikuwa ameondoka. Nikala chakula mpaka nikamaliza. Nikaingia jikoni kuosha vyombo.
 
Wakati ninaosha vyombo mume wangu akaniita tena. Nikaguna. Kama kawaida yangu sikumjibu. Nilimaliza kuosha vyombo kisha nikamfuata.
 
“Si nilikuambia sitaki kuitwaitwa, mimi nina kazi zangu!” nikamwaambia kwa ukali.
 
“Nimekuwa sina raha, kila saa Salma! Salma!Salma! nikufanye nini?”
 
“Sikuiti mimi. Kuna mtu anabisha mlango”
 
Aliponiambia hivyo nikanyea.
 
“Ni nani?” nikamuuliza.
 
“Nitajuaje!”
 
Nikaenda kwenye mlango na kuufungua. Kumbe alikuwa mmoja wa rafiki zake aliokuwa akifanya kazi nao TRA. Nikatahayari kwani nilijua kuwa alikuwa ameyasikia yale maneno niliyomuambia mume wangu.
 
“Karibu shemeji” nikamkaribisha huku nimeinamisha uso wangu kwa aibu.
 
“Ahsante”
 
Jamaa huyo akaingia ndani. Jinsi uso wake ulivyofadhaika, nilihisi aliyasikia yale maneno niliyomuambia Ibrahim.
 
“Habari za nyumbani” nikajidai kumsalimia huku nikitabasamu
 
“Nyumbani ni kwema. Sijui nyinyi hapa?”
 
“Sisi ndiyo kama unavyotuona, kwacha hakuchi lakini siku zinapita”
 
Ibrahim akaisikia sauti ya rafiki yake.
 
“Msangi umenitupa ndugu yangu” akaanza kumshutumu.
 
“Sijakutupa kaka, mihangaiko imekuwa mingi. Unajionaje hali yako kwa sasa?”
 
“Sijambo lakini hali yangu ni ile ile kama unavyoniona. Karibu ukae”
 
Msangi akakaa karibu na Ibrahim. Wakaanza kuzungumza. Na mimi nilikuwa pale pale.
 
Baada ya mazungumzo marefu Msangi akatia  mkono kwenye mfuko wa suruali yake, akatoa noti mbili za elfu kumi kumi.
 
“Nimekuletea hizi senti kidogo zikusaidie kaka”
 
Ibrahim akanyoosha mkono. Msangi akamuwekea kwenye kiganja.
 
“Ahsante ndugu yangu” Ibrahim akamshukuru na kumwambia.
 
“Usiache kunikumbuka. Ukikaa siku mbili tatu uwe unakuja kutujulia hali. Siku nyingine tunashinda bila kuijua riziki”
 
“Sawa kaka. Kuja kuwajulia hali ni lazima nije. Wewe ni kaka yangu, siku ambazo hunioni ni kwamba na mimi pia hali siyo nzuri”
 
“Ninajua. Nakushukuru sana ”
 
Baada ya hapo Msangi akatuaga na kuondoka.
 
Kwa vile nilishaziona zile pesa zilizotolewa na Msangi nikaenda kuketi na Ibrahim ili nimsomeshe ziingie mikononi mwangu.
 
“Mume wangu unajua kuwa nilimkopa jirani pesa tuliyotumia juzi. Sasa kama umepata nipe nimrudishie” nikamwaambia
 
“Mbona hukuniambia tangu hiyo juzi?” akaniuliza.
 
“Ningekuambia ungekuwa nazo hizo pesa za kumlipa?” nikamng’akia.
 
ITAENDELEA
 





No comments:

Post a Comment