Monday, January 19, 2015

SOMA MKUSANYIKO WA HABARI KUU ZILIZOPEWA UZITO KATIKA KURASA ZA MAGAZETI YA LEO,TZ

Huu ni mkusanyiko wa Stori zilizopewa Headlines kwenye Magazeti ya leo January 19, 2015

nir_series.jpg__470x264_q85_crop
MWANANCHI
Wananchi wa Jimbo la Vunjo Mkoani Kilimanjaro wamechanga Sh200,000 za nauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili aweze kufika jimboni humo kutoa somo la Katiba.
Fedha hizo zilitolewa juzi na kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati akihutubia mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti katika miji ya Himo na Moshi Mjini kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kuwaamini wagombea wa Ukawa na kuwapa ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa NCCR-Mageuzi, Getrude Pwila alisema kama hazitatosha kwa nauli ya Jaji Warioba, wako tayari kuchangishana kuongeza.
Tunataka tuelimishwe hii Katiba Inayopendekezwa kwa sababu hatuko tayari kuipigia kura kwa sababu hatuielewi, hatujaiona wala kuisoma na kuielewa,” alisema Pwila kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo.
Katibu huyo, alimwomba Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, amwombe Jaji Warioba kwenda katika jimbo hilo kuendesha kongamano kama alivyofanya katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam na wao wako tayari kumgharimia.
Jaji Warioba alipoulizwa kuhusu maombi hayo, alisema hajayapokea na hajui lolote.
MWANANCHI
Wanafunzi 150 kati ya 1,000 waliojiunga na masomo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) mwaka jana wamebainika kuwa na ujauzito waliopewa na wenzao chuoni hapo.
Utafiti wa usawa na jinsia uliofanywa na chuo hicho kati ya Juni na Novemba mwaka jana umebaini kuwa wanafunzi wanaopata ujauzito ni wale wa mwaka wa kwanza.
Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa chuo hicho, Dk Dativa Shilla katika warsha ya uchaguzi na uhusiano wa kijinsia iliyofanyika chuoni hapo na kusema hali hiyo inatokana na kuwapo kwa vitendo vya ukatili, manyanyaso na ubabe unaofanywa na wanachuo wa kiume dhidi ya wale wa kike na hivyo kuwalazimisha kufanya mapenzi bila hiyari yao.
“Kupitia utafiti huu tumeona hakuna usawa wa kijinsia wa kupata elimu baina ya mwanamke na mwanamume kwa sababu mwenye ujauzito hawezi kufanya vizuri katika masomo yake ukilinganisha na mhusika wa kiume,” alisema.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho Gosbeth Kihanga ambaye alikiri kuwapo kwa vishawishi chuoni hapo na kudai kuwa inachangiwa na ugumu wa maisha hasa kwa wanafunzi wa kike.
MWANANCHI
Ile dhana ya kuwa mafuta ya kupoza transfoma yanaibwa na wauza chipsi, imebainika siyo ya kweli baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa yanatumiwa viwandani kuendesha mitambo, kuchanganywa katika vipodozi na mengine yakisafirishwa nchi za nje.
Taarifa zinasema kuwa wanaoiba mafuta hayo ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pia huchukua nyaya za shaba katika transfoma hizo kwa ajili ya kutengeneza mapambo mbalimbali kama herini, mkufu na bangili.
Kutokana na wizi huo, mwaka jana pekee transfoma 34 zenye ukubwa mbalimbali ziliibiwa mafuta na shaba, hivyo kuisababishia Tanesco hasara ya Sh306 milioni.
Meneja Mwandamizi, Masoko na Mauzo wa Tanesco, Injinia Nicholaus Kamuleka alisema utafiti uliofanywa na wahandisi wa shirika hilo unaonyesha kuwa mafuta ya transfoma yanaibwa kwa ajili shughuli mbalimbali.
“Kazi ya mafuta ya transfoma ni kupoza nguvu ya umeme mkubwa,” alisema Injinia Kamuleka na kuongeza kuwa mafuta hayo pia huchanganywa na ya gari,”– Kamuleka.
NIPASHE
Wakati maazimio nane yaliyotolewa na Bunge kwenye mkutano wa 16 na 17 mwishoni mwa mwaka jana kuhusiana na kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya Sh. Bilioni 300 za akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yakiwa hayajatekelezwa yote, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema watu waliofikishwa mahakamani katika sakata hilo ni dagaa tu na kwamba kambare (vigogo) wanaendelea kutanua.
Aidha, wabunge wengine wawili kutoka miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),  wamesema Mkutano wa 18 wa Bunge ujao watawasha moto kama Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo  hatakuwa amewajibishwa ama kujiuzulu mwenyewe.
Alisema watuhumiwa watano  walioanza kufikishwa mahakamani wiki iliyopita ni sawa na dagaa huku kambare wakiendelea kulindwa kwa maslahi ya baadhi ya viongozi wa Serikali na vigogo wakuu wa sataka hilo ni pamoja na Profesa Muhongo; Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka.
Alisema inashangaza kuona hadi sasa vigogo hao hawajachukuliwa hatua ikiwamo ya kufukuzwa kazi, kurudisha fedha hizo pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
NIPASHE
Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi,  wameteka mabasi saba ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Jiji la Arusha na Nairobi, Kenya na kupora mali na fedha ambavyo thamani yake haijafahamika.
Tukio hilo ambalo limethibitishwa na Jeshi la polisi, Mkoani Arusha ilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Mbuga Nyeupe, wilayani Longido Mkoa wa Arusha baada ya watu hao kuweka mawe barabarani na kuwamuru abiria wote kutemka mmoja baada ya mwingine, kulala chini na kuwapekua kila kitu walichokuwa nacho.
Akisimulia mkasa huo, dereva wa basi la Perfect Trans, Joseph John, alisema kuwa watu hao waliokuwa na silaha za jadi yakiwamo mashoka, mapanga  na sime, waliteka mabasi hayo majira ya saa 8 usiku.
Hao jamaa walikuwa kama 50  hivi kwani waliteka magari yetu ambayo yalikuwa yamefuatana, wametuvua hadi viatu, saa yaani walipekua hadi wanawake waliamriwa kuvua nguo na kuporwa urembo wenye nakshi ya madini ya vito,” alisema John.
Alisema yeye alikuwa dereva wa kwanza kufika na basi katika eneo hilo na kuwa alipoona mawe yamepangwa kati kati ya barabara, aliamua kusimama  na alipokuwa akijaribu kuyakwepa, alipigwa jiwe usoni hali iliyomfanya ashindwe kukimbia.
Hata wengine walikuwa hawajafunika nyuso zao, tukio lilidumu kwa dakika zaidi ya shirini, kila walipomaliza kupekua watu wa basi moja waliwaamuru warudi ndani ya gari,”– Joseph John.
MTANZANIA
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeifungia daladala zinazofanya safari zake Kimara hadi Kariakoo kwa siku 30 kutokana na kuwatoza abiria nauli ya Sh. 800 tofauti na iliyopangwa na mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Michael Kisaka alisema wameamua kuwafungia na endapo watakiuka masharti hayo watachukuliwa hatua zaidi za kisheria.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa abiria walitozwa nauli ya Sh. 800 badala ya Sh. 500 kwa safari ya ruti hiyo.
Huo ni ukiukwaji wa Kanuni namba 34 na 35 ya Kanuni za Leseni ya Usafirishaji kwa Magari ya Abiria ya mwaka 2007,”– Kisaka.
Aidha, wamiliki walitakiwa kuwasilisha barua zenye maelezo na vielelezo kuhusu hatua zilizochukua dhidi ya dereva na kondakta.
MTANZANIA
Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabuza Serikali PACZitto Kabwe ameibuka tena na utata wa shilingi bilioni 821 ambazo Serikali ya Tanzania imelieleza Shirika la fedha la Kimataifa IMF, kwamba imezitumia katika mradi wa ujenzi wa bomba la gesi toka Mtwara hadi Dar es salaam.
Mradi huo umegharimu dola za Marekani bilioni 1.55 kati yake asilimia 95 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya Exim ya China na 5% ni fedha za Serikali ya Tanzania.
Zitto ameibuka na utata huo zikiwa zimepita siku chache alipoonyesha wasiwasi juu ya matumizi makubwa ya fedha kwenye mradi huo mwanzoni mwa mwezi huu.
Alisema Shirika la maendeleo ya petrol nchini TPDC ilipowasilisha kwa kamati yake Novemba 3 mwaka jana  inaonyesha kuwa fedha ambazo Tanzania ilikua imetoa ni dola za Marekani 31.3.
Fedha ambazo Serikali imeahidi kutoa ni dola 61.4 za Marekani na ambazo tayari ilishatoa ni dola 31.3 lakini barua ya Tanzania kwenda IMF inasema Serikali kwa mwaka wa fedha  ilitumia dola za Marekani milioni 464 sawa na bilioni 821…huu ni utata inabidi tupate maelezo ya kutosha” Zitto.
Hakuna story itakayokupita mtu wangu ,niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia,tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment