SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
YAMENIKUTA SALMA MIE 11inaletwa kwenu kwa hisnai kubw aya Kampuni ya Mabasi yaendayo Mikoani, Freys ni mabingwa wa kusafirisha abiria, Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku, simu 0622 292990
ILIPOISHIA
Nilipobaki peke yangu mle
ndani nilikwenda ikata ile sehemu ya chakula niliyoitia ile dawa kwa ajili ya
Ibrahim, nikaenda kuimwaga kwenye pipa.
Nilihofika kwamba huenda
Ibrahim akirudi kutoka hospitali atataka kula. Nilikuwa sitaki ale ile dawa
ambayo ilikuwa ni ya kuoga.
Yasije yakatokea mengine,
nikajiambia.
Nikataka nimpigie simu Rita
nimwambie, lakini niliogopa kutoa ile siri kwamba mume wangu amepofuka macho
kwa sababu ya ushirikina wangu.
Lakini nilipanga kwamba kila
itakavyokuwa kesho yake niende kwa yule mganga nimueleze hali iliyotokea,
pengine angeweza kuwa na ufumbuzi.
Kwa upande mwingine nilijipa
moyo kwamba huenda dawa ile aliyooga siyo iliyomfanya mume wangu asione bali ni
presha kama mwenyewe alivyokuwa anahisi.
Niliomba Mungu iwe ni presha
kweli. Kama itakuwa si presha itakuwa ni ile
dawa, nilijiambia.
Ilipita karibu saa nzima,
nikampigia simu Zacharia. Zacharia alipopokea simu nikamuuliza.
“Enhe mmefika hospitali?”
SASA ENDELEA
“Tumefika na kaka amepimwa
presha”
“Ikoje?’ nikamuulizza haraka.
“Iko juu kidogo lakini
daktari ametuambia macho yake hayakutokana na presha”
“Ni nini?”
“Ametuambia ni suala
linalohitaji uchunguzi. Ametushauri kesho twende kwa mtaalamu wa macho”
“Sasa mko wapi?”
“Ndio tunarudi”
“Sawa”
Nikakata simu.
Jibu la zacharia lilizidi
kunitia wasiwasi na nikahisi kwamba hakukuwa na kingine kilichompofua macho
mume wangu isipokuwa ni ile dawa niliyomtilia kwenye maji yake ya kuoga.
Wakati wanafika nyumbani
nilijisikia kupata uoga kutokana na ile hisi ya hatia kwamba mimi ndiye
niliyempofua macho mume wangu.
Ibrahim na Zacharia
walipoingia ndani Zacharia alikuwa amemshika mkono kaka yake. Akaenda naye hadi
lilipokuwa kochi
akamkalisha.
“Kaa hapa” akamwambia.
Ibrahim akakaa.
“Mke wangu, daktari
tuliyemuendea hakugundua tatizo” Ibrahim akanimbia kabla ya kumuuliza chochote.
Alinyamaza kwa sekunde chache
kama mtu aliyekuwa akiwaza jambo kisha
akaongeza.
“Ameniambia nisubiri kesho
niende nikaonane na mtaalamu wa macho anifanyie uchunguzi”
Nilikuwa nimesimama
nikimtazama Ibrahim wakati akizungumza. Kusema kweli nilimuhurumia sana. Nikakaa kwenye kochi lililokuwa karibu
naye.
“Salma umenisikia
nilivyokwambia?” Ibrahim akaniuliza alipoona nipo kimya.
“Nimekusikia. Tutasubiri hadi
hapo kesho kama alivyokwambia huyo daktari
mkaonane na huyo mtaalamu wa macho”
“Sijui hili tatizo limetokana
na nini?” Ibrahim akauliza kama aliyekuwa
akijiuliza mwenyewe kisha akatikisa kichwa kusikitika.
“Kwani kichwa bado kinauma”
nikajidai kumuuliza.
“Kwa sasa kichwa kimeacha. Tatizo
liko kwenye macho”
“Tusubiri hiyo kesho, sasa
mwende mkale chakula”
“Mimi sitakula tena.
Nimeshapatwa na wasiwasi”
“Nenda ukale japokuwa kidogo”
“Sisikii tena njaa”
“Unataka ulale hivyo hivyo”?
“Nitalaa tu”
Aliposema hivyo Ibrahim
akauelekeza uso wake upande aliosimama Zacharia.
“Zacharia nenda ukale
chakula” akamwambia mdogo wake.
“Sasa kaka kwanini wewe
hutaki kula?” Zacharia akamuuliza.
“Siwezi. Ile njaa pia sina
tena”
“Twende ukale japokuwa kidogo
kaka”
“Wewe nenda tu, mimi niache”
Zacharia akamtazama kaka yake
kisha akaondoka kwenda mezani.
“Hapa ninawaza mengi, kama macho yangu hayataona tena, kazi zangu nyingi
zitaharibika” Ibrahim akaniambia.
Nilikubaliana naye kimoyo
moyo.
“Mimi nina imani kuwa ukishughulikiwa
na hao wataalamu wa macho utaweza kuona” nikamwambia kumpa moyo lakini moyoni
mwangu nilikuwa nimeshapanga kurudi kwa yule mganga kutakapokucha.
Niliamini kuwa kama tatizo hilo limetokana na dawa
zake, anaweza kujua jinsi ya kumtibu.
Usiku ule si Ibrahim wala
mimi aliyepata usingizi. Nililala nikiwa macho kwa muda mrefu kitandani.
Baadaye niliinuka nikaketi kitandani na kuanza kuwaza huku nikimtazama Ibrahim
alivyokuwa akijigeuza geuza pale kitandani. Ilikuwa ni dalili kuwa hata naye
hakuwa amelala usingizi.
Nikiwa nimeshika tama
nilikuwa nikimfikiria mume wangu huku nikijiuliza endapo hatatibika na atabaki kuwa kipofu,
nini kitatokea katika maisha yetu?
Kweli tutaweza kupata
maendeleo na kuishi maisha ya furaha endapo mume mwenywe atakuwa hawezi kufanya
kazi kwa sababu haoni?”
Kwa upande mwingine nilijuta
kukubali ushawishi wa Rita wa kwenda kwa mganga kumroga mume wangu. Nilikuwa
nikijiambia kama nisingekwenda kwa mganga,
macho ya mume wangu yasingepofuka.
Asubuhi kulipokucha
nilikwenda kuyafungua yale maji kwenye mita, nikamsindikiza mume wangu bafuni
kwenda kuoga. Alipomaliza kuoga nilimuandalia chai. Akanywa pamoja na mdogo
wake.
Muda wa kwenda hospitali
ulipowadia nilimwambia kuwa baadaye nitatoka kwenda sokoni. Nilimwambia hivyo
kwa makusudi ili kama watawahi kurudi na
kunikosa wajue kuwa nimekwenda sokoni. lakini lengo langu lilikuwa ni kwenda
kwa yule mganga.
Ibrahim na Zacharia walipoondoka,
na mimi nikatoka. Sikutaka kwenda kwa Rita. Nilikwenda kwenye kituo cha
bodaboda nikapakiwa kwenye pikipiki na kuelekea Kisosora.
Nilipofika niliitafuta nyumba
ya yule mganga hadi nikaigundua. Nilimwambia mwenye bodaboda anisubiri.
Nilipokwenda kwenye kile kibanda cha mganga
sikukuta mtu yeyote nikapiga hodi.
“Pita ndani” sauti ya mganga
ikasikika kutoka ndani.
Nikaingia. Nilimkuta mganga
ameketi akikatakata vipande vya mizizi.
“Shikamoo” nikamwamkia.
“Marahaba. Habari ya tangu juzi?”
“Ni nzuri kama
si nzuri”
“Kwanini?”
“Nimefanya makosa. Ile dawa
ambayo uliniambia nimtilie mume wangu kwenye chakula niliikosea nikamtilia
kwenye maji ya kuoga”
“Eh! Ile dawa haitaki povu la
aina yoyote. Kama alioga na sabuni inaweza
kumletea matatizo”
“Ndiyo hivyo, alipomaliza
kuoga akanimabia haoni…”
“Haoni mpaka hivi sasa?”
“Haoni. Dawa yenyewe
nilimtilia jana, siku ile uliponipa alikuja mgeni nyumbani nikashindwa
kumuwekea”
Mganga akanyamaza kimya. Uso
wake ulionesha kuwa ile habari ilikuwa imemshitua.
“Sasa sikiliza, njoo kesho. Kuna
dawa nitakwenda kukuchumia umfikichie kwenye macho yake”
“Nije kesho saa ngapi?”
“Njoo asubuhi. Nitakwenda
kuichuma leo jioni”
“Sawa, basi nitakuja kesho
asubuhi”
Nilipomaliza kuzungumza na
mganga huyo nikamuaga na kuondoka. Nilipofika kwenye mlango niligeuza uso wangu
nikamtazama. Nilimfuma alikuwa akinitazama kwa nyuma kwa jicho ambalo halikuwa
la kawaida. Sikuweza kujua alikuwa ananifikiria nini.
Mwendesha bodaboda alikuwa
akinisubiri. Nikajipakia tukaondoka. Nilipitia sokoni nikanunua nilivyonunua na
kurudi nyumbani. Ibrahim na mdogo wake walikuwa
hawajarudi. Nikaanza kupika.
Kidogo yale maelezo ya yule
mganga kwamba atanipa majani ambayo nitamfikichia mume wangu machoni mwake,
yalinipa matumaini.
Nikawaza sasa jinsi ya
kumfikichia hayo majani machoni mwake. Nikajiambia itabidi nimueleze kwamba
nimepewa majani hayo na mtaalamu wa kienyeji na ameniambia kuwa yanaweza
kukusaidia.
Ibrahim na Zacharia walirudi
majira ya saa sita mchana. Ibrahim
akanieleza kuwa amefanyiwa uchunguzi na macho yake yamegundulika kuwa hayakuwa
na tatizo.
“Nimepewa dawa hizi nitumie
kwa siku tatu” akaniambia.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment