HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE 17
ILIPOISHIA
Alichukua kipande cha kioo
kilichovunjika ambacho kilikuwa juu ya meza akakiweka mbele ya macho yangu.
“Hebu jitazame mwenyewe
ulivyopendeza” akaniambia huku
akitabasamu.
Baada ya kujitazama
nikalivua.
“Walivulia nini, liache tu”
“Niliache la nini, si niko
ndani? Hapo nitakapotoka ndio nitavaa” nikamwambia.
Nikalivua lile juba na kumpa
Konda ambaye alilirudisha ndani ya sanduku.
“Sasa ngoja nikutoe
nikutambulishe kwa wapangaji wangu. Nina wapangaji wawili humu ndani lakini
mwenye mke ni mmoja tu”
Tukatoka ukumbini na Konda. Akawaita ukumbbini wapangaji
wake. Aliyekuja alikuwa mpangaji mmojatu
na alitokea uani.
“Nimekuita kukutambulisha mke
wangu” akamwambia na kuongeza.
“Mke wangu mwenyewe ndiye
huyu”
Yule jamaa alinitazama kisha akasema.
“Nimefurahi kumfahamu”
SASA ENDELEA
Nilipoingia ndani nilimkuta
mume wangu amekaa sebuleni peke yake. Zacharia hakuwepo.
“Habari ya hapa?’
nikamsalimia.
“Nzuri, mbona umechelewa sana?”
“Nilikwenda huko kwa mama
yangu. Kuna mtabibu pale mtaani kwetu amenipa dawa nije nikufanyie”
“Dawa gani?”
“Dawa ya majani. Ameniambia
nikufikichie kwenye macho kwa siku tatu”
“Haya tujaribu”
“Ameniambia nikufanyie
asubuhi na jioni. Asubuhi imeshapita tusubiri jioni tuanze”
“Unanifikichia vipi?”
Nikamueleza vile
nilivyoagizwa na yule mganga.
“Haya utanifikichia tujaribu”
“Amenihakikishia kuwa
itakusaidia”
“Lakini haiwashi machoni?”
“Hakuniambia lakini nafikiri
haiwashi kama inawasha angeniambia”
Baada ya hapo niliingia
jikoni na kuanza kupika. Ile dawa niliitunza mahali pazuri ambapo ingeweza
kukaa bila kukauka.
Ilipofika jioni nilichomoa
majani matatu ya dawa hiyo nikaenda sebuleni ambako mume wangu alikuwa amekaa
nikamwambia alale chini kichalichali ili nimfikichie machoni.
Mume wangu aliondoka kwenye kochi alipokuwa ameketi
akasogea mbele kidogo na kukaa chini kisha akajilaza kichalichali.
Nilichutama na majani yangu nikayashika na kuyafikicha
kabla ya kumkamulia machoni mwake.
Maji maji yaliyotoka kwenye majani hayo yalipomuingia machoni alifumba
macho.
“Usifumbe macho, yafumbue”
nikamwambia. “Yafumbue dawa ikuingie vizuri”
Akayafumbua kiuoga.
“Fumbua bwana!”
“Nimeshayafubua”
“Bado, fumbua zaidi”
Macho yake yalikwishakuwa
maoga. Alishindwa kuyamfumbua sawa sawa.
Nikamkamulia majani
hayo hivyo hivyo. Maji maji machache yalimuingia machoni, mengine yalichirizika
kingoni mwa macho na kumwagika chini.
Nilirudia kumkamulia mara
tatu.
“Umeshamaliza?” akaniuliza.
“Nadhani imetosha”
Alikuwa anataka kuinuka
nikamzuia.
“Ngoja kwanza dawa ikuingie
vizuri, una haraka ya nini?”
Akatulia.
Baada ya dakika tatu hivi nikamwambia
ainuke. Akainuka na kukaa kwenye kochi.
“Yanawasha?” nikamuuliza.
“Yanawasha kwa mbali”
Nilichukua kitambaa nikamfuta
futa yale maji maji yaliyokuwa yamemchirizikia pembeni mwa macho kisha
nikaondoka.
Asubuhi nilimfanyia tena, nikarudia tena jioni.
“Vipi, hujaanza kuona ona”
nikamuuliza.
“Bado. Naona kiza tu”
“Mganga mwenyewe ameniambia
nikufanyie kwa siku tatu”
“Labda mpaka kesho kutwa”
Niliendelea kumfanyia Ibrahim
dawa hiyo kwa siku tatu lakini macho ya Ibrahim hayakuona chochote. Siku ya nne
yake nikarudi tena kwa yule mganga.
Nilipomueleza nilimuona
akikunja uso.
“Bado hajaweza kuona?”
akaniuliza.
“Hajaona bado”
Mganga akafikiri kisha
akaniambia.
“Njoo kesho nitakupa dawa
nyingine”
Nikaondoka. Kwa vile hata
zile dawa alizopewa hospitalini
hazikuweza kumsaidia, kesho yake nilirudi tena kwa yule mganga. Kwa kweli
aliniweka sana.
Alipomaliza kuhudumia wateja wake akaniita na kuniambia niende tena kesho kwani
hakupata nafasi ya kwenda kunichumia dawa nyingine.
Nikaondoka. Siku iliyofuata
Ibrahim alipelekwa hospitali na mdogo wake na mimi nikatoka kwenda kwa mganga.
Nilipofika alinipa dawa ya
ungaunga mweusi, akanimbia nichote kidogo niroweke kwenye maji ya vugu vugu kwa
dakika moja kisha nimpe mume wangu anawe uso.
“Niroweke kwenye maji ya
kiasi gani?” nikamuuliza kwa matumaini.
“Kama
nusu lita hivi”
“Anawe uso yote?”
“Ndiyo anawe yote. Unamtilia
asubuhi na jioni kidogo kidogo”
“Kwa siku ngapi?”
“Kwa siku tatu”
Baada ya mazungumzo hayo
nikaondoka. Nilikuta mume wangu alikuwa amesharudi kutoka hospitali. Alikuwa
amepewa dawa nyingine za kutumia kwa siku tatu.
“Na mimi nimekwenda kwa
mtaalamu mwingine” nikamwambia.
“Amekwambiaje?”
“Baada ya kumueleza matatizo
yako amenipa hii dawa”
“Ni dawa ya aina gani?”
“Ni ya unga unga. Ameniambia
nitie kwenye maji ya vugu vugu kisha uoshe uso asubuhi na jioni”
“Kwa sababu tuna shida
tutafanya” Mume wangu aliponiambia hivyo niliona huzuni sana.
Tulifanya ile dawa kwa siku
tatu bila mafanikio. Zile dawa za hospitali nazo hazikuleta matumaini yoyote.
Kwa vile niliona lile tatizo
lilitokea kwa yule mganga nikarudi tena bila kuchoka. Mganga akanibadilishia
dawa nyingine. Nazo pia hazikufaa.
Kwa upande wa hospitalini
tulimaliza hospitali kadhaa za macho. Mume wangu aliambiwa hawezi kuona tena!
Sasa maisha yetu yalianza
kuwa magumu. Mume wangu alikuwa hawezi tena kufanya kazi. Tulikuwa tunakula
mtaji. Kusema kweli pesa nyingi zilimalizika kwa uchunguzi na matibabu yake.
Mwisho wake akanimabia
anafikiria kuuza ile gari yake ili apate pesa za kuendelea kujitibu. Kulikuwa
na watu ambao walikuwa wakimpa moyo kwamba asikate tamaa.
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose
No comments:
Post a Comment