Friday, January 16, 2015

KISIWA HARISHI

KISIWA CHA HARISHI
 
Napenda kuwaarifu wasomaji wangu kuwa muhusika mkuu katika hdithi yetu ya Kisiwa cha Harishi alifanikiwa kuoana na Yasmin huko Morani Comoro. Hadithi kamili itapatikana kwenye kitabu kitakachotoka hivi karibuni. Sasa anza kusoma hadithi nyingine mpya inayoitwa YALIYONIKUTA TANGA.
 
 
HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA
 
FAKI A FAKI
 
Simu: 0655 340572, 0713 340572
 
Uhamisho wangu wa kikazi kwenda Tanga ulikuja kama adhabu kutokana na ukiukaji wangu wa maadili ya jeshi la polisi nikiwa muajiriwa wa jeshi hilo.
 
Nilijiunga na jeshi la polisi miaka mitano iliyopita mara tu baada ya kuhitimu kidato cha sita huko Kagera ninakotoka.
 
Nilipomaliza mafunzo yangu ya upolisi  huko Moshi nilipangiwa kuanza kazi jijini Dar. Mimi na wenzangu kumi na wanane  tuliuopangiwa kwenda Dar tulifurahi sana na kujiona tulikuwa na bahati kuchaguliwa kwenda Dar kwani wenzetu wengi walikuwa wakililia kupangiwa kazi katika jiji hilo.
 
Kituo changu cha kazi cha kwanza jijini Dar, kilikuwa kituo cha polisi cha Ilala. Pale nilipelekwa peke yangu. Wenzangu walitawanywa katika vituo vingine vilivyotapakaa sehemu mbalimbali za jiji.
 
Katika kipindi cha miaka minne ya mwanzo nilifanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa. Kwa vile kazi yenyewe niliipenda niliifanya kwa kujituma na kwa weledi. Mara kadhaa nilisifiwa na wakuu wangu na kutolewa mfano kwa wengine.
 
 Siku moja mimi na polisi mwenzangu tulitakiwa kusindikiza gari lililochukua mishahara ya wafanyakazi wa kiwanda cha bia kutoka benki moja iliyokuwa barabara ya Samora na kuipeleka kiwandani hapo.
 
Ilikuwa ni kawaida kila ifikapo mwisho wa mwezi, mashirika ya serikali huomba askari kwa ajili ya kusindikiza mishahara ya wafanyakazi kutoka benki.
 
Ilikuwa ni nafasi nzuri ambayo polisi wadowadogo tulikuwa tunaigombania kwa sababu ilikuwa na posho kidogo. Siku hiyo nikapata bahati hiyo mimi na mwenzangu.
 
Tulipakiwa na gari ya kiwanda hicho lililotufuata kituoni. Mimi na mwenzangu kila mmoja alikuwa na bunduki yake aina ya SMG iliyokuwa na risasi tisini.
 
Tulipofika benki tulisubiri nje ya gari. Sanduku la pesa lilipotolewa tulishika bunduki zetu vizuri na kuangaza macho kila upande kuhakikisha usalama wa pesa hizo.
 
Sanduku hilo lilipopakiwa kwenye gari na sisi tulijipakia. Gari likaondoka. Tulifika kiwandani salama. Gari likasimama kusubiri kufunguliwa geti ili tuingie ndani ya eneo la kiwanda.
 
Wakati askari anakwenda kutufungulia geti, gari moja likasimama ghafla ubavuni mwa gari tulilokuwemo. Ndani ya gari hilo mlikuwa na watu watano akiwemo dereva.
 
 Mara tu baada ya gari hilo kusimama watu wawili miongoni mwa watano waliokuwemo ndani, walipenyeza mitutu ya bunduki kwenye madirisha na kuanza kutushambulia kwa risasi za mfululizo.
 
Mimi na polisi mwenzangu tuliinama chini. Risasi zilivunja vioo vya gari vya ubavuni, zikawa zinapita juu ya vichwa vyetu. Maafisa watatu wa kiwanda hicho waliokuwemo ndani ya hilo gari walipoona tunashambuliwa walifungua mlango wa gari wa upande wa pili na kukimbia.
 
Baada ya maafisa hao kukimbia na kuliacha sanduku la pesa ndani ya gari, tulisikia kimya halafu tukasikia hatua za watu wakija mbio. Nikahisi walikuwa ni majambazi waliokuwa wakitushambulia, sasa wanalifuata lile sanduku la pesa baada ya wenyewe kukimbia.
 
Hapo hapo nikatoa mdomo wa bunduki kwenye dirisha na kuanza kufyatua risasi mwenyewe nikiwa nimeinama. Mwenzangu naye alifyatua risasi lakini alikuwa ameinua kichwa chake, akapigwa risasi ya kichwa na kufa pale pale.
 
Nilipomuona mwenzangu ameuawa niliacha kufyatua risasi nikatulia kimya. Nilikuwa nimeinama chini ya dirisha ili watu hao wasinione.
 
Majambazi hao walipoona hatujibu mapigo walijua kuwa wameshatuua. Tamaa ya pesa ikawafanya waharakishe kufungua mlango wa gari wakiamini kuwa wameshazipata pesa hizo.
 
Vile wanafungua tu mlango huo walikutana na mtutu wa bunduki. Niliwafyatulia risasi majambazi wawili bila wao kutegemea wakaanguka kando ya mlango wa gari.
 
Majambazi wengine wawili waliokuwa nyuma yao walipoona wenzao wameshambuliwa na risasi zilikuwa zinaendelea kurindima waligeuka nyuma ili wakimbie lakini hawakulifikia hata gari lao nikawalaza chini wote.
 
Jambazi mmoja aliyekuwa amebaki kwenye gari kwenye siti ya dereva aliliondoa gari hilo kwa kasi kusalimisha maisha yake. Sikutakakumkosa yule jambazi, nikapituka kwenye siti ya dereva amabayo ilikuwa tupu. Gari hilo lilikuwa kwenye moto, nikatia gea na kulifukuza lile gari.
 
Wakati naliondoa gari hilo niliwakanyaga majambazi wawili waliokuwa wamelala chini na kuwatoa matumbo!
 
Gari hilo halikufika mbali nikaliingia ubavuni. Nililibana na kulibamiza  pembeni mwa barabara kisha nikalichota na kulipindua kichwa chini miguu juu, likawa kama mende aliyekufa huku tairi zake zikiendelea kuzunguka zenyewe.
 
Kulikuwa na gari la polisi lililokuwa kwenye doria. Polisi hao walipoona tukio hilo walisimamisha gari. Na mimi nikashukuru kwa kuona nimepata msaada. Nilishuka kwenye gari nikaona gari jingine la kiwanda cha bia likisimama nyuma ya gari la polisi. Bila shaka gari hilo lilikuwa likitufuata nyuma.
 
Polisi wanne walishuka kutoka gari la polisi na maafisa wanne walishuka kutoka gari la kiwanda cha bia, watatu walikuwa ni wale tuliokwenda nao bemki. Nilijua kwamba walikuwa wakifuatilia pesa zao. Nikafungua mlango wa gari nikalitoa lile sanduku la pesa na kuwakabidhi.
 
ITAENDELEA KESHO

No comments:

Post a Comment