Manchester City kumsajili Wilfred Bony .
Mabingwa watetezi wa ligi ya England Manchester City wanatarajiwa kuanza mazungumzo na klabu ya Swansea city wakiwa na lengo la kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast Wilfred Bony.
City wamepanga kumsajili mshambuliaji huyo na wanatarajiwa kupeleka ofa ya kwanza ambayo inaaminika kufikia paundi milioni 25 .
City wanakuwa timu ya kwanza kupeleka ofa kwa ajili ya mshambuliaji huyo huku wakifahamu kuwa anasakwa na timu kadhaa zikiwemo Real Madrid na Liverpool.
Mwenyekiti wa Swansea Huw Jenkins amekanusha habari za kuwepo kwa mpango wa kuuzwa kwa mchezaji huyo japo tayari mazungumzo baina ya viongozi wa Man City na wawakilishi wa Bony yameanza baada ya mkutano uliofanyika hapo jana (jumatano) na kama kila kitu kikienda kama ilivyopangwa City itamsajili mchezaji huyo .
Hata hivyo endapo usajili huo utakamilika Manchester City haitaweza kumtumia Bony kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu kutokana na adhabu ya kukiuka misingi ya sheria za usimamizi wa fedha maarufu kama Financial Fair Play ambako hawaruhusiwi kuongeza mchezaji mwingine kwenye kikosi chao cha ligi ya mabingwa .
Bony anatazamwa na City kama mtu atakayekuwa mbadala wa yoyote kati ya washambuliaji wao watatu Stevan Jovetic, Sergio Aguerro na Edin Dzeko ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha ambayo yameikosesha City washambuliaji kiasi cha kulazimika kutumia wachezaji kama David Silva na James Milner kwenye nafasi ya ushambuliaji .
No comments:
Post a Comment