Radamel Falcao kusajiliwa moja kwa moja na Man United.
Klabu ya Manchester United inatarajiwa kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia Radamel Falcao mara baada ya usajili wake wa mkopo kumalizika .
Falcao ambaye hadi sasa amekuwa na mabingwa hao wa zamani wa ligi ya England kwa karibu miezi minne tangu aliposajiliwa kwa mkopo akitokea klabu ya Monaco amenaza kucheza mechi mfululizo hali inayoashiria kuwa fiti kiasi cha kumshawishi kocha wa United Louis Van Gaal kuridhia kusajiliwa kwake .
Awali United walikuwa na dhamira ya kumsajili Falcao tangu awali wakati walipomchukua kwa mkopo lakini walikuwa na hofu na afya yake hasa baada ya mchezaji huyo kupata jeraha baya la goti lililomfanya akose michuano ya kombe la dunia nchini Brazil.
Hofu hiyo ilizidi pale ambapo Falcao alipata majeraha kadhaa akiwa na United hali iliyomfanya akose karibu mwezi mzima wa michezo ya ligi ya England huku kocha Louis Van Gaal akiendelea kusisitiza kuwa mchezaji huyo anahitaji kudhihirisha utimamu wake wa mwili kabla ya kupata nafasi ya uhakika kwenye kikosi cha kwanza .
Vipimo ambavyo Falcao amefanyiwa na wataalamu wa afya wa United vimeonyesha kuwa mchezaji huyo amerudi kwenye hali yake ya kawaida na anaweza kumudu kasi ya ligi ya England na kwa sababu hiyo kocha LVG ameridhia usajili wake .
Hivi karibuni habari toka nchini Ufaransa zinasema kuwa wakala wa Falcao Jorge Mendez amekutana na viongozi wa Monaco na viongozi wa United na tayari mipango ya kukamilisha usajili wa moja kwa moja imekamilika na United italipa Euro Milioni 40 kwa ajili ya mchezaji huyo .
Hadi sasa Falcao amefunga mabao mawili akiwa na United huku akianza kucheza mechi karibu zote tangu mwezi wa 12
No comments:
Post a Comment