KUMEKUCHABLOG
DAR ES SALAAM ,MTANDAO wa kutetea haki za binadamu Tanzania (THRDC) imeyataka
mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali pamoja na viongozi wa dini kuunda
mtandao utakaowezesha kutokomeza vitendo vya kikatili na ukiukaji wa haki za
binadamu nchini.
Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wanachama na Asasi zisizo
za Serikali, Mkurugenzi wa Mtandao wa Tanzania Human Rights Deffenders
Coalition (THRSC),Onesmo Olengurumwa, alisema viongozi wa dini na Asasi ziko na
nafasi kubwa katika kutokomeza ukiukwaji wa haki za binadamu Tanzania.
Alisema watetezi wa haki za binadamu wako katika vitisho
kutokana na ujasiri wao wa kufichua na kuzungumza hadharani matendo ya baadhi
ya watu wanaoleta vitisho na wanaovunja haki za bianadamu.
“Mafunzo haya tumeyaleta kwenu ninyi kama watetezi wa haki
za binadamu kwa kuwafunda usalama na kutathmini athari kwa watetezi wa haki za
binadamu----hii ni kutokana na vitisho muvipatavyo munaporiti” alisema na
kuongeza
“Kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu tunatambua mengi huibuka
lakini tunaamini hayatatokea na tunaomba yasitokee na ndio maana tumewaiteni
hapa kuwapa mbinu za usalama na kuwa watetezi wetu wakubwa katika maeneo yenu”alisema
Akizungumzia waandishi wa habari kipindi cha kampeni na
uchaguzi mkuu mwaka huu, Mkurugenzi huyo aliwataka kuwa makini wakati
wanaporipoti taarifa za wagombea na kuepuka kutumiliwa kwa maslahi ya mtu
mmoja.
Alisema vipindi hivyo huibuka mengi kwa waandishi wa habari
na kupokea vitisho kutokana na kusema kwao ukweli na hivyo kuwataka kutumia
weledi wao wa taaluma ya upashaji habari ili kuweza kuisadia jamii kupata
habari za ukweli na uhakika.
Kwa upande wake,Afisa ulinzi na usalama wa Mtandao wa
(THRDC)Benedict Ishabakaki,ameitaka jamii kutopuuza vitisho wanapovipokea kwa
njia ya simu au katika mitandao ya kijamii na badala yake waripoti katika
mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Alisema kupuuza kitisho chochote kinaweza kuleta athari
katika maisha ya mtu na hivyo ni vyema kila jambo kulichukulia kama dhara na kuwa mwepesi wa
kuliripoti na kulichunguza na kuweza kuchukuliwa hatua ili kutokomeza ukiukwaji
wa haki za binadamu.
“Suala la ulinzi na usalama ni la mtu mwenyewe ila unaweza
pia ukamsaidia mwenzako kama unaona kuna kitisho kwa mwenzako unalitolea
taarifa au kulisemea kwa vyombo husika” alisema Ishabalaki
Alisema ni jukumu la kila mmoja kuwa mtetezi wa haki za
binadamu na kutambua mbinu za kujilinda na kuwa wasiri wa kutoa taarifa za
vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na hivyo kuitaka jamii kuwa watetezi
wa haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment