HADITHI
YALIYOTUKUTA TANGA (3)
ILIPOISHIA
Tulikwenda kwenye mlango,
Erick akabisha mlango huo na punde tu ukafunguliwa na msichana aliyeonekana kama msomali. Alikuwa mweupe na mwembamba kiasi.
Alipotuona alishituka na kutuambia.
“Assalam alaykum”
Erick ambaye alikuwa amezoea
salaam hizo za kipwani ndiye aliyemuitikia.
Nilidhani afande Erick
angemuulizia mwenye nyumba lakinihakufanya hivyo, alitoa kitambulisho chake
akamuonesha yule msichana.
“Sisi ni polisi wa upelelezi
kutoka jeshi la polisi. Tumepata taarifa kuwa humu ndani mnauza madawa ya
kulevya. Je ni kweli?”
Msichana aliposikia hivyo
alishituka.
“Si kweli” akajibu kwa
kubabaika.
“Sawa. Sasa kilichotuleta
hapa ni kufanya upekuzi katika nyumba hii”
“Ngoja nimuite mama”
Aliposema hivyo mwanamke
mmoja mzee akatokea nyuma yake.
“Mnataka nini?” akatuuliza.
Kidogo alikuwa na lafidhi ya kiarabu.
SASA ENDELEA
Erick akamueleza kazi yetu na
kusudio lililotuleta kwenye nyumba ile.
“Karibuni” mwanamke huyo
akatuambia.
Tukaingia ndani.
“Sisi hatufanyi biashara hiyo
na wala hatuijui. Sisi tunauza mapambo ya wanawake tu” Mwanamke huyo akatuambia
tulipokuwa ndani.
“Tumepata taarifa ya
kuaminika kuwa mnauza madawa ya kulevya, kwa hiyo tunataka tufanye upekuzi humu
ndani” Erick akamwambia.
“Sawa. Fanyeni upekuzi wenu.
Sisi hatuwezi kuwazuia. Lakini kuingilia faragha ya mtu si jambo zuri”
Tukaanza kufanya upekuzi wetu
bila kuwepo na shahidi wala mwenyekiti wa mtaa. Tulianza kupekua kwenye lile
duka. Kisha tukaendelea kwenye vyumba vingine. Tulipoingia chumbani kwa yule
binti nilimuona Erick akitoa kitu kwa siri mfukoni mwake kisha akainama chini
ya kitanda.
Aliponyanyuka alionyesha kile
kitu alichokitoa mfukoni mwake, akauliza.
“Hiki ni nini?”
Erick alikuwa ameshika kete
tatu za madawa ya kulevya. Alikuwa amemtumbulia macho yule mwanamke.
“Nimekuuliza hiki nini?”
“Sisi tutajuaje? Kitu
umekishika wewe halafu unatuuliza sisi, hatuwezi kujua” Yule mwanamke alimjibu.
Erick alijifanya ananusa zile
kete kisha akaniambia.
“Ni kete za madawa ya
kulevya. Ndiyo haya tuliyokuwa tunayatafuta”
“Zinaonekana kuwa ni kete
kweli” nikamkubalia.
“Hebu nusa”
Alinisogezea kete hizo kwenye
pua yangu. Nikazinusa.
“Ni kokeni yenyewe!” nikasema
na kuongeza. “Kweli sasa nimeamini hawa watu wanafanya biashara ya madawa ya
kulevya”
Ilikuwa kama nimemchochea
Erick. Akamtazama yule mwanamke kwa macho makali.
“Mama ulikuwa unakataa?
Tumekuta kete hizi za madawa ya kulevya chini ya kitanda cha binti yako!”
Mwanamke huyo na binti yake
walibaki kushangaa.
“Kete za madawa ya kulevya
ndio nini?” Mwanamke huyo akauliza.
Binti yake akabetua mabega.
“Sijui”
“Bila shaka kutakuwa na kete
nyingi humu ndani. Ngoja tuendelee kupekua” Erick akasema.
Tuliingia katika chumba
kingine ambacho kilikuwa ni cha yule mwanamke. Katika kupekua tulikuta kisanduku
cha shaba
kilichowekwa ndani ya kabati. Tulipokifungua tulikuta kimejaa mapambo ya
dhahabu.
“Mmepata wapi dhahabu hii?”
Erick akawauliza.
“Sisi tunafanya biashara ya
dhahabu” Yule binti akamjibu.
“Hii pia itakuwa mali
iliyopatikana kwa njia ya haramu!”
“Hapana, tunanunua kihalali”
Msichana ndiye aliyekuwa akisema. Yule mwanamke alionekana kama
amepandwa na presha.
“Mtakwenda kujieleza vizuri
polisi”
“Mnataka kutupeleka polisi?”
Yule mwanamke aliyekuwa kimya sasa aligutuka na kuuliza.
“Kama
hamtaki kwenda polisi tunaweza kuzungumza na kuyamaliza hapa hapa. Hii kesi ni
kubwa sana”
“Huyu mama pia hataweza
kifungo” Na mimi nikasisitiza.
“Sasa mnataka tuzungumze
nini?” Mwanamke huyo akatuuliza.
“Hujui? Utatupa kiasi gani
ili tukuachie?”
“Mimi siwezi kutoa rushwa kwa
sababu hatujafanya kosa lolote”
Maneno yale yalimuudhi Erick.
Nikaona uso wake umebadilika.
“Hamjafanya kosa lolote, si
ndio…?” akasema huku akitoa simu. Hapo hapo akawapigia polisi wenzetu waliokuwa
kituoni. Aliwaeleza kilichotokea na kwamba alikuwa anahitaji gari.
Je nini kitaendelea? Usikose
kuendelea na hadithi hii hapo kesho.
No comments:
Post a Comment