Mkusanyiko wa zile Stori muhimu zilizoandikwa kwenye Magazeti ya leo Tanzania January 14, 2015
JAMBOLEO
Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini,amesema watu wanaosema wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM waliotangaza nia ya kuwania kiti cha Urais, hawana sifa, wanataka watoto au marafiki zao wagombee nafasi hiyo wakiona ndiyo wenye sifa.
Aidha amesema iwapo kuna mtu mwenye ushahidi kuwa wagombea hao wanatoa fedha ili wapate nafasi hiyo,wathibitishe kwa vielelezo ama ushahidi.
Nyalandu alisema hayo ikiwa ni siku moja baada ya Mkongwe wa CCM Kingunge Ngombale Mwiru kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wagombea waliotangaza na wanaotajwa kutaka kugombea Urais,hawana sifa na wanatumia fedha ili wapate nafasi.
Alisema kuna watu wanataka kusikia watoto wao,wajomba zao na marafiki zao wakitangaza nia hiyo ndiyo wawasifie jambo ambalo si zuri kwa maslahi ya Taifa na Watanzania.
Alisema iwapo nchi ikiendeshwa kwa misingi ya watu kutoka familia za watu fulani ili waonekane wanafaa itakua ni jambo la kusikitisha.
JAMBOLEO
Kamati ya bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa LAAC imebaini harufu ya ufisadi na uzembe katika Halmashauri ya jiji la Dar es salaam.
Hali hiyo ilisababisha wajumbe kuwaomba watendaji ikiwemo Meya wa Jiji, Didas Masaburi kupisha kamati ya muda kujadili taarifa zao.
Hiyo ilitokana na baadhi ya wajumbe kuhoji kwa nini jiji walikataa kumpatia Simon Group akaunti kwa ajili ya kufanya malipo ya hisa zilizokua zikiuzwa na jiji la Dar es salaam.
Wajumbe hao walisema kuwa jiji walitaka kuuza hisa na wlaiingia mkataba na kampuni ya Simon Group ambaye ndiye mnunuzi wa hisa zote.
TANZANIA DAIMA
Jeshi la Polisi wakishirikiana na Chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi TAS, wanatarajia kuendesha operesheni ya kuwasaka na kuwakamata waganga wa kienyeji maarufu kama wapiga ramli.
Polisi wamefikia hatua hiyo baada ya matukio ya kutekwa kwa albino kuongezeka huku moja ya tukio linaloendelea kuumiza vichwa vya watu ni kupotea kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emmanuel lililotokea jijini M wanza Disemba 27 mwaka jana.
Kutokana na tukio hilo jeshi la polisi kwa kushirikiana na Chama hicho wameunda kikosi cha watu sita kitakachoshirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa, vitongoi na vijiji kuwasaka wapiga ramli wanaowahadaa watu wanaotafuta utajiri na uongozi.
Waziri wa mambo ya ndani Mathias Chikawe amesema Serikali imepiga marufuku wapiga ramli wote nchi nzima baada ya kubaini ndio wanaowashawishi watu kupeleka viungo vya albino.
TANZANIA DAIMA
Familia zenye watoto wanaotumia maziwa aina ya Lactogen namba moja na namba mbili wametahadharishwa juu ya kuwepo kwa maziwa hayo ambayo hayafai kwa matumizi ya watoto.
Ofisa habari wa Mamlaka ya Chakula Tanzania TFDA Gaudensia Simwanza alisema kumekuwepo na maziwa bandia ya kopo ambayo hutumika kwa matumizi ya watoto.
Alisema ingawa baadhi ya maziwa hayo yamesajiliwa, lakini yapo ambayo hayajasajiliwa na yanaendelea kuwepo sokoni na yanapitishwa kwa njia ya panya kama ilivyo kwa dawa za kulevya.
“Kopo la maziwa linatakiwa kuandikwa kwa lugha inayoeleweka, yaani kiswahili kwa wale wasiojua lugha ya kingereza na kwa lugha ya kingereza wale wanaojua,”alisema Simwanza.
MWANANCHI
Mmoja wa makada wa CCM anayewania nafasi ya Urais January Makamba ameandika kitabu kinachoelezea nia yake hiyo ya kugombea.
Kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza mikakayi ya mwanasiasa huyo kijana iwapo atapitishwa na Chama chake ili kuwania na hatimaye kushika nafasi hiyo ya juu kitaifa.
Katika kitabu hicho chenye kurasa 196 Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, amesema Rais ajaye lazima awe na tafakuri pana na nia ya kuendeleza nchi na siyo kuwa na kaulimbiu nyepesi za afya bure,elimu bure zisizo na ufafanuzi ili kuwahadaa wananchi.
Kitabu hicho kimeandikwa na mchambuzi wa makala za siasa Padri Privatus Karugendo kimebeba sera na mikakati yake kiundani ya kuongoza nchi iwapo atapatiwa dhamana na CCM kugombea urais.
MWANANCHI
Idadi ya wajawazito wanaojifungua kwa upasuaji nchini imeongezeka kwa asilima 31 katika kipindi cha miaka 11.
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Muhimbili Agnes Mtawa takwimu zinaonyesha kuwa waliojifungua kwa njia hiyo mwaka 2000 walikua ni asilimia 19 lakini ilipofikia mwaka 2011 walifikia asilimia 50.
Alisema tafiti znatakiwa kufanyika ili kubaini chanzo chake.
Mtawa alisema licha ya kujifungua kwa upasuaji kuwa njia salama lakini utaratibu huo unaonekana ni hatari kwa wajawazito.
Mkunga katika hospitali hiyo Gloria Mkusa alisema kwa mwaka huzalisha wanawake wengi kwa upasuaji kuliko kawaida.
NIPASHE
Naibu Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba ameibuka na mpya baada ya kujifananisha na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na aliyekua Waziri wa Mkuu Edward Sokoine kwa madai kuwa na msimamo usiyoyumba katika masuala yenye maslahi kwa Taifa.
Alisema suala la yeye kuitwa Sokoine halijaanza leo kwani hata alipokua anasoma alikua anaitwa Nyerere mara Sokoine hasa kutokana na misimamo yake isiyoyumba.
Alisema viongozi waliopewa uongozi wanawajibu mkubwa wa kutetea haki za wanyonge kwani wapo watu ambao hawana fursa ya kusema na jambo hilo likiachwa ipo siku mawe yatasema na haitajulikana nini kitatokea.
“Mimi ipo kwenye Chama na nimepewa jukumu la kusimamia miiko na misingi ya chama ,hivyo nisingependa niwe miongoni mwa wanaovunja miiko, tutavuka mto, tukishavuka, tutaangalia“alisema Nchemba.
NIPASHE
Idadi ya vijana wahalifu maarufu Panya road sasa imeongezeka na kufikia 1,438 huku baadhi ya wazazi na wakazi wa maeneo ya Magomeni na mwenge wakilijia juu jeshi la Polisi kwa madai kuwa operesheni hiyo inawahusisha wasiohusika.
Idadi hiyo imeongezeja katika Mikoa ya Kipolisi ya Temeke, Ilala na Kinondoni ambapo waliokamatwa ni pamoja na wapiga debe katika vituo vya daladala,, wacheza kamari, wavuta bangi, watumiaji wa dawa za kulevya na watumiaji wa pombe aina ya gongo.
Joyce Mbaruku mkazi wa Magomeni alisema operesheni hiyo inayofanywa na jeshi la Polisi ni ya uonevu kwani wanakamata watu hovyo bila kufanya uchunguzi na kuwahusisha na kundi la Panya road.
Alisema ameshangazwa na taarifa za kukamatwa kwa vijana wake wawili wakihusishwa na kundi hilo kwani anafahamu fika tabia za watoto wake na wamekamatwa katika mtaa ambao ni wageni na hawafamu sababu ya kukamatwa kwao.
Nakuhakikishia kwamba nitakufikishia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia,tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment