Saturday, January 3, 2015

WAKAZI WA KISIWANI PEMBA WALALAMIKIA NAULI ZA MELI KUWA JUU

Kumekucha blogi

Pemba,WAKAZI wa  kiwani cha Pemba wamelalamika nauli  kubwa za usafiri wa meli kutoka Pemba kwenda Unguja na hivyo kuitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuzirejesha meli zake za Maendeleo na Mapinduzi ili kuwapa unafuu wakazi wa Visiwa hivyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na kumekucha blog wakazi hao walisema kutokuwepo kwa meli za Serikali kama ilivyokuwa zamani kumewapa nguvu makampuni ya usafirishaji kuweka nauli za juu na hivyo kuwanyima fursa baadhi ya watu kuwatembelea jamaa zao visiwani humo.

Walisema awali zilikuwepo meli ya Mapinduzi na Maendeleo na nauli zake kuwa nafuu na hivyo watu wengi kukimbilia meli hizo jambo ambalo lilikuwa likiwapa unafuu baadhi ya wazazi kuwapeleka likizo watoto wao nyakati za shule kufungwa.

“Sasa hivi tunashindwa kuwapeleka watoto wetu likizo kuwatembelea jamaa zao baada ya meli zilizopo nauli zake kuwa juu---hii tunadhani kama ni kukomoana ili watoto wetu shule zikifungwa wasiende popote” alisema Said Sanani

“Nauli kwenda Unguja ni zaidi ya shilingi elfu ishirini kwa sasa na hii ni kutokana meli za mapinduzi na maendeleo ambazo zilikuwa zikimilikiwa na Serikali kupotea machoni” alisema

Aliishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuzirejesha meli zake ikiwa na pamoja na kusimamia nauli kwa vyombo vya baharini na kuacha kung’ang’ani nauli za mabasi na kusahau kuwa kuna wahanga wa vyombo vya baharini kuteseka.

Kwa upande wake mkazi wa mji wa Wete, Faisal Maftah, amewataka wamiliki wa magari yaendayo mjini na vijijini kuwakemea wakondakta wao kuacha kuwachukua wanafunzi kwa madai kuwa wanalipa pesa pungufu.

Alisema tabia hiyo imekuwa ikishamiri nyakati za shule kufungwa na kufunguliwa na  hivyo madereva na makondakta wao wamekuwa wakikaidi kuwachua wanafunzi mbali ya sheria kuwaruhusu.

“Vipindi vya shule kufungwa na kufunguliwa watoto wetu wamekuwa wakinyanyasika sana----wakiona kituo kimejaa watoto hawasimami au hubagua kwa kutangaza kuwa watoto hawabebi” alisema Maftah

Alivitaka vyombo vinavyohusika kukemea tabia hiyo na kuacha manyanyaso kwa wanafunzi na kuweza kuwatembelea ndugu na jamaa zao vipindi vya shule kufungwa.

                                                 Mwisho

No comments:

Post a Comment