SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 63
MWANAMKE
ILIPOISHIA
Aliniambia kwamba siku zote
nilikuwa nikiishi naye nikimdhani kuwa ni Shamsa kumbe siye.
Hadithi ile ilinishitua sana.
Nikamwambia Shamsa.
“Nitaaminije kuwa wewe ni
Zena na si Shamsa?”
“Subiri” Shamsa akanimabia na
kuufinika uso wake kwa kanga.
“Sasa nifunue hii kanga”
Sauti yake ikaniambia.
Nikaifunua ile kanga.
Nilipomtazama. Nikaona alikuwa ameshabadilika na kuwa Zena. Wakati mimi
nimepatwa na mshangao, yeye alikuwa anatabasamu.
“Kumbe ni kweli!”
nikajisemea.
“Je utaendelea kuniogopa tena
wakati umeshanizoea?” Zena akaniuliza huku akiendelea kutabasamu.
Unadhani ningemjibu nini
wakati polisi wameshafika pale hoteli?”
“Sitakuogopa tena”
“Nimefurahi kusikia kauli
yako hiyo”
Mara tukasikia mlango
unagongwa kwa kishindo. Nikajua walikuwa ni wale polisi. Walikuwa
wameshaelekezwa chumba tulichokuwemo.
“Sasa Zena tutafanyaje?”
nikamuuliza Zena.
SASA ENDELEA
“Kwanza nataka tukubaliane
kitu kimoja”
“Kitu gani?”
“Utakikubali?”
“Nitakikubali, niambie ni
kitu gani?”
“Nikupeleke kwetu ujinini
tukaithibitishe ndoa yetu kabla ya kurudi Tanga”
“Sasa tutakwendaje huko
Ujinini wakati tutakapotoka tu
ninakamatwa na polisi?”
“Mimi ndiye ninayejua, wewe
kubali tu ninachokwambia”
“Mimi nimeshakubali”
Mlango uliendelea kugongwa.
“Hawa wako ndani wanatusikia
lakini wanaleta jeuri” Tukaisikia sauti ya polisi mmoja akiwambia wenzake nje
ya mlango.
“Basi acha tuvunje mlango”
Tukasikia sauti nyingine ikisema.
“Zena mlango unavunjwa!”
nikamwambia Zena kwa hofu.
Zena akanyanyuka na
kuniambia.
“Na wewe nyanyuka ushike hayo
mabegi yako”
Nikayachukua yale mabegi
mawili, moja nililipachika begani kwangu na moja nililishika mkononi.
Zena naye akalipachika begani
begi lake.
Sasa mlango ulikuwa
unavunjwa!
“Njoo usimame sambamba na
mimi”
Nikajisogeza kwake na kuwa
naye bega kwa bega.
Zena akachora msitari kwenye
sakafu kutoka kulia kwenda kushoto. Ulianza kwenye usawa wake ukafika hadi
kwenye usawa wangu.
Baada ya hapo alinishika
mkono akaniambia.
“Fumba macho yako”
Nikafumba macho.
Sasa mlango ulikuwa
umeshavunjwa na kufunguka.
Nikaona polisi wakiingia kwa vishindo.
“Piga hatua haraka uvuke huo
mstari niliouchora hapo chini” Zena akaniambia.
Nikainua mguu wangu wa kulia
kwa haraka na kupiga hatua kuuvuka mstari huo kabla ya wale polisi kutufikia.
“Sasa fumbua macho yako”
nikasikia sauti tulivu ya Zena ikiniambia.
Nikafumbua macho yangu. Kama ni mshangao, mshangao nilioupata hapo haukuwa na
mfano!
Hatukuwa tena kwenye kile
chumba cha hoteli. Tulikuwa ufukweni mwa bahari! Sikuweza kujua mara moja
tulikuwa kwenye ufukwe wa bahari gani.
Ulikuwa ufukwe wenye mchanga
mweupe na mbele yetu kulikuwa na msitu ulioshiba. Nyuma yetu ndio kulikuwa na
bahari.
Jua lilikuwa limekuchwa
likitoa mionzi ya rangi ya kimanjano iliyokuwa ikimemeta baharini nyuma yetu.
Sikuweza kutambua mara moja
tulikuwa katika ufukwe wa nchi gani uliokuwa ukipendeza kiasi kile. Ufukwe huo
ulikuwa kimya na hakukuwa na chombo chochote kilichokuwa kikionekana baharini.
“Tuko wapi hapa?” nikamuuliza
Zena.
“Ufukweni mwa bahari”
“Bahari ya wapi?”
“Bahari ya kwetu ujinini”
“Mbona tumefika mara moja”
“Kawaida. Lakini
nilikukimbiza wewe usikamatwe na wale polisi”
“Itakuwa bado wako mle
chumbani?”
“Wapo wanashangaa shangaa
lakini wameambilia matupu”
Mabegi tuliyokuwa tumechukua
tulikuwa nayo vile vile. Begi langu moja lilikuwa begani na jingine lilikuwa
mkononi. Na begi alilokuwa amelishika Zena alikuwa bado analo.
Nilitupa macho yangu kwenye
ule msitu uliokuwa mbele yetu kisha nikamuuliza Zena.
“Tunaelekea upande gani?”
“Huko unakoona msitu”
“Huko ndiko kuna mji wenu?”
nikamuuliza.
“Mji uko huko. Twende”
Kusema kweli wakati wote
nilikuwa nimejikaza kiume lakini nilianza kupata hofu tangu Zena aliponiambia
kuwa pale tulikuwa katika ufukwe wa ujinini.
Pengine ningemuuliza ujinini
ipo upande gani katika ramani ya dunia. Katika kusoma kwangu Jeografia kuanzia
shule ya Msingi hadi Sekondari sikuwahi kuiona ramani ya ujinini katika upande
wowote wa dunia.
Lakini niliona swali hilo halikuwa na umuhimu
wa kuliuliza wakati ule. Kama kulikuwa na umuhimu
ulikuwa ni kumuuliza tulifika pale kwa usafiri wa aina gani? Kama
usafiri wenyewe ulikuwa haueleweki hata hiyo ramani ya ujinini inaweza
isieleweke.
“Tuanze kusonga, bado tuna
kipande cha mwendo wa miguu” Zena aliendelea kuniambia huku akitangulia kwenda
mbele kuelekea katika ule msitu uliokuwa unatisha.
Wakati nikimfuata nyuma
nilimuuliza.
“Lakini Zena sitapatwa na
madhara yoyote huku?”
“Madhara kama yapi?”
“Mimi najua kuwa majini
wengine wanadhuru watu?”
“Ni kweli wapo majini
wanaodhuru watu”
Kukiri kwake kwamba kuna
majini wanaodhuru watu kukaniongezea ile hofu yangu.
ITAENDELEA kesho usikose hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment