SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE
ILIPOISHIA
Esmail alifungua mlango wa
chumba kimojawapo.
“Unataka kwenda wapi?” Shamsa
akamuuliza.
“Lile begi liko humu”
“Huwezi kuingia peke yako.
Ngoja tuingie sote”
Shamsa akaingia pamoja na
Esmail ndani ya kile chumba na mimi nikawafuata.
Kilikuwa chumba kilichotumika
kama astoo. Esmail alilitoa begi alilokuwa amelificha nyuma ya kabati bovu.
Wakati anampa begi hilo
Shamsa alipambana na risasi ya kichwa. Esmail akaanguka chini. Shamsa
akalichukua lile begi.
Alilifungua na kulitazama
ndani kasha akaniambia.
“Twende zetu”
Tukatoka na kujipakia kwenye
gari.
Tulirudi nyumbani. Shamsa
akanimabia tusilale nyumbani tutakamatwa. Tulikusanya nguo zetu pamoja na vitu vyetu muhimu tukavitia kwenye begi
kisha tukatoka tena.
Tulijipakia kwenye gari.
Shamsa akaniambia tunakwenda katika mji ulioko mpakani mwa Kenya ili tuondoke
nchini humo.
SASA ENDELEA
Tulipofika katika mji huo
tulikodi chumba katika hoteli moja. Lengo letu lilikuwa ni kusubiri wakati wa
usiku tuvuke mpaka kwa njia za panya ili tuingie Kenya. Tulipanga lile gari
tulilokuwa nalo tulitelekeze pale pale hoteli. Tusiwengeweza kuingia nalo Kenya
kwani tungeweza kukamatwa kirahisi.
Tukiwa katika chumba cha
hoteli tulishangawa tulipoona tangazo kwenye televisheni lililohusu kuuawa kwa
Abdi na Esmail. Msemaji wa polisi alieleza kuwa polisi wanashuku kwamba watu
hao waliuawa na mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Amour ambaye alikuwa
mfanyakazi wa Abdi.
Huku picha yangu ikioneshwa
katika tangao hilo msemaji huyo wa polisi aliendelea kueleza kuwa polisi
wananitafuta kuhusiana na mauaji hayo na kwamba nilikimbia mara tu baada ya kufanya unyama huo.
Aidha taarifa hiyo ilieleza
kuwa baada ya kufanya uuaji huo nilipora mamilioni ya pesa na watu hao
kukimbia.
Msemaji wa polisi akaelea
kuwa yeyote atakayetoa taarifa ya kukamatwa kwangu atazawadiwa mamilioni ya
pesa za Somalia.
Kutokana na mshituko na
mshangao nilioupata nikatazamana na Shamsa.
“Kumbe polisi wananitafuta!”
nikamwambia Shamsa.
“Usijali, sisi tutaondoka
usiku huu kwenda Kenya”
“Unadhani hawatanikamata?”
“Watakupata wapi. Nani anajua
kama uko hapa?”
“Basi tuharakishe tuondoke”
“Hapa itabidi tuondoke saa
nne usiku. Tutakaa tu humu chumbani”
Ilipofika saa tatu nikaona
gari la polisi likisimama mbele ya hoteli. Nilikuwa niikichungulia kwenye
dirisha nikaliona. Niliona polisi sita waliokuwa na bunduki wakishuka kutoka
kwenye gari hilo.
Shamsa njoo uone!”
nikamwambia Shamsa.
“Kitu gani?”
“Polisi wamekuja. Nadhani
wamepata taarifa kuwa niko hapa”
“Wamejuaje” Shamsa akaniuliza
huku akisogea kwenye dirisha na kuchungulia.
“Watu wameiona picha yangu
iliyotolewa kwenye lile tangazo. Inawezekana wamepigiwa simu na wafanyakazi wa
hii hoteli baada ya kuiona ile picha”
“Usijali”
“Kwanini unaniambia nisijali
wakati nitakamatwa wakati wowote?”
“Amour hutakamatwa. Kaa
kwenye kitanda nikwambie”
Nikakaa kwenye kitanda na
Shamsa naye akakaa na kunitazama.
“Unajua kwamba uko na Zena?”
Shamsa akaniambia kwa kuniuliza.
“Huyo Zena yuko wapi?”
nikamuuliza.
“Ni mimi”
“Wewe ni Zena! Shamsa
unafanya mzaha!”
“Si mzaha. Mimi ni Zena
kweli. Wewe ulioana na Zena si Shamsa. Sikiliza nikueleze…”
Shamsa akanipa hadithi ya
ajabu iliyonishangaza. Aliniambia kwamba alipoona Abdi alikuwa anataka
kuniozesha Shamsa akajigeuza yeye Shamsa na Shamsa halisi alimfanya kuwa
taahira na alimsafirisha katika mji mwingine.
Aliniambia kwamba siku zote
nilikuwa nikiishi naye nikimdhani kuwa ni Shamsa kumbe siye.
Hadithi ile ilinishitua sana.
Nikamwambia Shamsa.
“Nitaaminije kuwa wewe ni
Zena na si Shamsa?”
“Subiri” Shamsa akaniambia na
kuufinika uso wake kwa kanga.
“Sasa nifunue hii kanga”
Sauti yake ikaniambia.
Nikaifunua ile kanga.
Nilipomtazama. Nikaona alikuwa ameshabadilika na kuwa Zena. Wakati mimi
nimepatwa na mshangao, yeye alikuwa anatabasamu.
“Kumbe ni kweli!”
nikajisemea.
“Je utaendelea kuniogopa tena
wakati umeshanizoea?” Zena akaniuliza huku akiendelea kutabasamu.
Unadhani ningemjibu nini
wakati polisi wameshafika pale hoteli?”
“Sitakuogopa tena”
“Nimefurahi kusikia kauli
yako hiyo”
Mara tukasikia mlango
unagongwa kwa kishindo. Nikajua walikuwa ni wale polisi. Walikuwa
wameshaelekezwa chumba tulichokuwemo.
“Sasa Zena tutafanyaje?”
nikamuuliza Zena.
KESHO KESHO KESHO
No comments:
Post a Comment