SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 66
ILIPOISHIA
Mama akabadili lugha na
kuanza kuongea na Zena kwa ukali.
Walijibizana kwa muda kidogo
kisha Zena akaniambia.
“Si tumekubaliana tuje huku
tuoane?”
Kabla sijajibu yule mama
akamuuliza Zena kwa Kiswahili.
“Muoane kwa idhini ya nani?”
Zena akanyamaza kimya.
“Mwenye idhini ni baba yako,
umeshamwambia?” mwanamke huyo akamuuliza Zena.
“Si ndiyo tumekuja hivi?”
“Sasa mwambie baba yako,
akikukubali uoane na huyo kijana ndio mtaweza kuoana”
“Wewe pia si unaweza kutoa
idhini”
“Nitoe idhini mimi ni
mwanume?”
Yule mama alipouliza swali
hilo na kukosa jibu aligeuka na kuondoka. Nikamuona Zena akishusha pumzi ndefu.
“Kwanini mama yangu anapokuuliza
maswali unasita kujibu?’ akaniuliza.
“Sijui nijibu nini”
“Kwani mimi na wewe si
tumekwishaoana kule Somalia?”
“Mimi nilioana na Shamsa.
Baadaye ndio ukatokea wewe”
“Ulioana na mimi si Shamsa,
si nilikwambia?”
SASA ENDELEA
Nikanyamaza kimya.
“Huyu mama nilitarajia
atakuwa upande wangu, naye ameshaanza kuleta taabu” Zena akajisemea peke yake
kisha akainuka na kuniambia.
“Twende”
“Twende wapi?’ nikamuuliza
huku nikiinuka.
“Nifuate”
Tukatoka katika lile jabali
ambalo ukiingia ndani yake ni kama uliyeingia kwenye nyumba, tukaelekea katika
jabali jingine dogo lililokuwa kando ya lile.
Tulipoingia katika jabali hilo Zena aliniambia kuwa
pale ilikuwa ni sahemu yake ya kupumzika.
“Tukae hapa” akaniambia.
Palikuwa na sebule ndogo iliyokuwa na mito
iliyowekwa chini.
Tukakaa.
“Amour usiwe muoga. Kama utaulizwa umenipenda, sema ndio usisitesite.
Ukisitasita watajua nimekulazimisha”
Wakati Zena akiniambia hivyo
akaingia jini mmoja aliyekuwa kifua wazi. Alikuwa amejifunga shuka nyeupe
kiunoni. Ndevu zake nyeupe zilikuwa zikikaribia kufika kweye tumbo lake kubwa.
Kifua chake kilikuwa kimejaa manyoya meupe na marefu.
Alimsalimia Zena kisha
akamwambia ana ujumbe kutoka kwa baba yake Mzee Jabalkeys.
“Anasemaje?” Zena akamuuliza.
“Amenituma nikwambie kwamba
huyo kijana uliyekuja naye umrudishe huko huko ulikomtoa”
Moyo wangu ulishituka na
kuanza kwenda mbio.
“Nitamrudishaje wakati
tumekuja kuoana na ametaka kuwajua wazazi wangu!” Zena akasema.
“Unajua baba yako
amekasirishwa na kitendo chako cha kutaka kuoana na binaadamu. Amesema yeye hawezi
kutoa idhini uoane na binaadamu na hataki kabisa kusikia kitu kama
hicho”
“Lakini wenyewe si
tumeshakubaliana”
“Lakini Zena wewe ni jinni,
utaolewaje na binaadamu halafu mtaishi vipi?”
“Majini wanaoa binaadamu na
wengine wanaolewa na binaadamu labda useme baba hajui tu”
“Hata kama ni hivyo lakini
huko ni kukiuka kawaida yetu. Hilo
jambo halifai”
“Kama
yeye baba amesema hivyo basi mimi nitajiozesha mwenyewe, si lazima nipate
idhini yake”
“Sasa huo ni ukosefu wa adabu
kwa baba yako”
“Potelea mbali!”
“Sasa nikamwambie hivyo?”
“Nenda”
Yule jinni aliyeonekana
kukasirika akatoka na kumuacha Zena akigomba peke yake.
“Najuta kuja huku! Wazee gani hawa wasiolewa mambo.
Wamekuwa washamba kiasi hiki!”
Ghafla nikamuona mzee
mwingine aliyekuwa amefuatana na yule mzee aliyeondoka pamoja na mzee mwingine.
“Wewe mtoto mwenye laana
ulimjibu nini huyu Subyani?” Yule mzee akamuuliza Zena kwa sauti ya ukali.
“Lakini baba ungenisikiliza
mimi mwenyewe badala ya kusikiliza watumishi wako. Hao wanaongeza maneno”
“Mimi sihitaji kukusikiliza
kwa sababu najua wewe umekuwa jeuri na asi. Ninachokwambia ni kwamba mrudishe
huyu kijana ulikomtoa na kwamba sitaki kusikia tena kwamba unataka kuoana na
binaadamu!”
Zena akafura kama chatu.
“Mimi lazima nitaoana naye,
iwe itakavyokuwa. Kama hamtaki nitajiozesha
mwenyewe!”
Zena akainuka pale alipokuwa
ameketi akatoka kwa hasira huku yule mzee niliyemdhania kuwa ndiye Jabalkeys
akimtazama.
“Huyu mtoto amekuwa shetani
kabisa, si jini tena” akasema kisha akanisogelea mimi.
“Mwanangu amekutoa wapi yule
shetani?” akaniuliza.
“Amenitoa kwetu”
“Wapi”
“Tanga”
“Mlikubaliana mje muoane
huku?”
“Yeye ndiye aliyekuwa
analazimisha. Amenitia kwenye matatizo mengi. Naomba msaada wako”
“Hata kama nitawambia hawa
watumishi wangu wakurudishe, bado ataendelea kukufuata na atakusumbua lakini
suala lake nitalipeleka kwa Sultani wetu. Wewe
subiri hapa hapa”
Majini hao wakaondoka.
Nikabaki peke yangu. Sikujua Zena alikuwa amekwenda wapi na angerudi saa ngapi.
Na pia sikujua ningeendelea kukaa pale hadi muda gani. Kusema kweli ile hali ya
Zena kuanza kutibuana na wazazi wake ilianza kunitia hofu.
Baada ya kama
nusu saa hivi yule jini aliyekuja kwanza akarudi peke yake akiwa ameshika
bahasha.
“Begi lako ni lipi na lipi?”
akaniuliza.
Nikamuonesha yale mabegi
mawili niliyokwenda nayo. Yule jini akayabeba yote mawili kisha akaniambia.
“Twende”
Nikatoka naye katika lile
jabali tukashika njia ambayo mimi na Zena tulikwenda nayo. Tukashuka chini
baharini. Ikumbukwe kwamba muda ule ulikuwa ni usiku lakini ulikuwa usiku wa
mbalamwezi.
ITAENDELEA kessho hapahapa tangakumekuchablog usikose uhondo ;;;;;;
No comments:
Post a Comment