Saturday, August 20, 2016

HADITHI ,MWANAMKE SEHEMU YA 60

SIMULIZI A FAKI A FAKI
 
MWANAMKE 60
 
ILIPOISHIA
 
Esmail rafiki yake Abdi nilikuwa nikimfahamu vizuri. Bila shaka na yeye alikuwemo katika ule mpango wa kutaka kuniua.
 
Nikajimbia sitawaachia wachukue dhahabu ile pamoja na dola za Kimarekani ambazo Abdi alikwishanipa
 
“Hawa watu kweli ni majambazi!” nikajiambia kimoyomoyo na kuongeza.
 
“Huu walionifanyia ni ujambazi kamili. Lakini nitapambana nao!”
 
Nilirudi kwenye gari langu nikaliwasha na  kuondoka.
 
Kwanza nilikwenda kwenye zahanati moja nikaoshwa lile jeraha kisha nikafungwa dawa. Nilipotoka katika zahanati hiyo nilikwenda katika duka la nguo nikanunua pama na kulivaa kuficha lile jaraha.
 
Nikaendesha gari kuelekea nyumbani kwangu huku nikiwaza jinsi majambazi hao wa Abdi walivyonizunguka. Nilishukuru kwamba nilikuwa na afya njema, vinginevyo kile chuma walichonipiga kichogoni kingenimaliza kabisa.
 
“Fedha haina udugu wala urafiki” niliwaza kimoyo moyo.
 
Abdi alitaka kuniua kwa sababu ya fedha. Alijua nikishakufa atampata jini ambaye atampa fedha ili atajirike, ainunue Mogadishu yote iwe mali yake.
 
Wenzake nao walinipiga chuma bila kujali ningedhurika kiasi gani kwa sababu ya fedha. Abdi alivunja udugu na wenzake walivunja urafiki kwa sababu ya kitu fedha.
 
Nikaendelea kujiambia, sasa mimi ni nani niiachie, nitawatafuta na kuwasulubu. Watajua mimi nani.
 
Nilirudi nyumbani nikamueleza Shamsa masahibu yaliyonipata. Nilimuonesha lile jaraha ambalo nilikuwa na hakika kwamba  nilipigwa chuma.
 
SASA ENDELEA
 
Shamsa aliposikia ile habari alisikitika sana.
 
“Pole sana. Walitaka kukuua” akaniambia.
 
“Lakini sikufa na nimeshawajua, sitawaachia”
 
“Utawatafuta?” Shamsa akaniuliza.
 
“Sitawaachia wachukue ile dhahabu pamoja na dola zangu. Abdi alikwishanipa mimi”
 
“Watakuumiza!”
 
“Hawathubutu. Kama ni kwa ngumi hakuna yeyote anayeweza kusimama na mimi. Nina hakika nitawagaragaza vibaya sana”
 
“Una uhakika na unachokisema?”
 
“Mirungi imeshawamaliza, hawanitishi!”.
 
“Sasa sikiliza nikuambie”
 
“Unataka uniambie nini?”
 
“Mimi napajua anapokaa Esmail. Sasa nataka ukimfuata twende sote”
 
“Hakuna tatizo, tutakwenda lakini ujue kama litazuka suala la ngumi tutazichapa”
 
“Kama tumekubaliana hivyo, sawa”
 
Shamsa akaingia chumbani. Alipotoka alikuwa amebadili nguo. Alivaa baibui na ndani yake alivaa jinzi.
 
“Twende” akaniambia.
 
Tukatoka. Wakati tunataka kujipakia kwenye gari Shamsa aliniambia.
 
“Nitaendesha mimi”
 
Nikampisha kwenye sukani. Shamsa aliliwasha gari tukaondoka. Tulikwenda katika eneo moja lililokuwa kando kidogo ya jiji hilo. Tuliingia katika  mtaa mmoja uliokuwa mtulivu.
 
“Mtaa huu ndio anaoishi Esmail” Shamsa akaniambia na kuongeza.
 
“Nyumba yake ni ile pale yaliposimama magari”
 
Niliyaona magari hayo. Yalikuwa yameegeshwa nje ya nyumba ya saba mbele yetu.
 
Shamsa alikuwa amepunguza mwendo. Kitu ambacho kilinipa moyo ni kuwa moja ya gari hilo ndilo lile nililoliona limeegeshwa kule shamba.
 
SEkunde chache tu baadaye tukawa tumeifikia nyumba hiyo. Shamsa akaliegesha gari nyuma ya gari la Esmail. Wakati analizima moto gari hilo tuliona mtu akitoka katika nyumba hiyo. Alikuwa amebeba begi lililokuwa limejaa na alionekana dhahiri kuwa alikuwa na wasiwasi na alikuwa akikimbizia kitu.
 
Alishuka haraka haraka kwenye baraza ya nyumba akajipakia kwenye lile gari lililokuwa mbele ya gari la Esmail na kuondoka kwa kasi.
 
Tulishuka haraka kwenye gari tukaenda kwenye mlango wa nyumba ya Esmail. Mimi nilitaka kubisha mlango lakini Shamsa aliusukuma. Mlango ukafunguka. Shamsa akaingia na mimi nikamfuata.
 
Kisaikolojia tu nilikgundua kuwa Shamsa alikuwa amebadillika. Macho yake yalionesha dhahiri kuwa alikuwa amepanga shari.
 
Kusema kweli sikujua nini kingetokea humo ndani.
 
“Je nini kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii HAPO KESHO.

No comments:

Post a Comment