SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE
ILIPOISHIA
“Wanakushangaa kwani
hawawajui binaadamu? Wewe si binaadamu wa kwanza kufika huku”
“Na hao binaadamu wengine
wanafikaje huku?”
“Wanaletwa na majini wao
kufundishwa uganga au kutembea tu. Tena wanakaa muda mrefu hadi wanajua lugha
yetu”
“Na mimi naweza kuwaona hao
binaadamu wenzangu?”
“Huku kila mmoja ana lake.
Siwezi kujua wako wapi na hao waliowaleta sihusiani nao”
Tukafika katika jabali moja
lililokuwa na mnara mrefu. Zainush akaniambia kuwa pale ndio kwao.
Wakati tunataka kuingia
kwenye mlango wa jabali hilo
wakaja majini watatu kutupokea. Walikuwa wanawake watupu tena wasichana wadogo.
Lugha ya Zena ikabadilika, akawa anaongea kikwao.
Walitupokea yale mabegi
wakatangulia nayo ndani na sisi tukafuata nyuma. Zena akaniambia kuwa wale
walikuwa wadogo zake.
“Sisi tuko thelathini,
wanawake tuko kumi na saba, waliobaki ni wanaume”
“Mko wengi sana. Nyote ni baba mmoja na mama mmoja?”
“Baba mmoja na mama mmoja”
“Wewe ni wa ngapi kuzaliwa?”
“Ni wa saba lakini kwa
wanawake mimi ni wa pili”
“Hao ndugu zako wengine wako
humu?”
“Wale wakubwa wana masikani
zao zingine. Walioko hapa ni wale wadogo tu”
Tukafika mahali ambapo
tulikuta pazia zito la rangi nyeupe.
SASA ENDELEA
Zena alilipenua pazia hilo
tukapita na kutokea kwenye chumba kipana kilichokuwa kama sebule. Kilikuwa
kimetandikwa mazulia yenye mistari rangi tatu tofauti, rangi nyeupe, rangi
nyekundu na rangi ya bahari.
Kulikuwa na mito ya pamba ya kukalia ambayo ilikuwa
imewekwa chini kuzunguka sebule nzima.
Wale wadogo zake Zena
walielekea kwingine. Zena akaniambia.
“Tukae hapa”
Akatangulia yeye kukaa kwenye
mto mmojawapo na mimi nikakaa kwenye mto mwingine.
“Hapa ndio nyumbani kwetu”
akaniambia.
Nilikuwa nikikizungushia macho
kile chumba kuangalia nakshi zilizokuwa zimetiwa mle ndani. Kwa mbali nikasikia
harufu kama ya marashi na udi wa Unguja.
“Kwa hiyo wazazi wako wako
hapa?” nikamuuliza Zena.
“Wako hapa. Mama yangu
atakuja sasa hivi, yuko ndani”
Haikutimu hata dakika moja
mwanamke mmoja wa kiarabu akachomoza na kusogea karibu yetu. Alikuwa mtu mzima sana. Mwili wake wote
ulikuwa umezibwa na shuka nyeupe. Sikuweza kuona hata miguu yake.
Kilichokuwa kikionekana ni
uso wake. Ingawa alikuwa mwanamke lakini alikuwa na ishara za kutoka sharafa.
Alikuwa na macho ya kijivu yaliokuwa na mboni zilizounda mstari mwembamba.
Akatuambia. “Assalaam
alaykum”
Tukamuitikia. “Waalayka
ssalaam”
Baada ya hapo mwanamke huyo
alibadili lugha akawa anaongea kijini na Zena. Sikuelewa walikuwa wakizungumza
nini.
Yule mama hakukaa. Alibaki
amesimama vile vile. Wakati anazungumza na Zena mara kwa mara alikuwa
akinitazama mimi.
Mwishowe Zena akaniambia kwa
Kiswahili.
“Umemuona mama yangu”
“Ndiye huyu?” nikamuuliza
huku nikiogopa kumtazama kutokana na macho yake.
“Ndiye yeye lakini hajui
Kiswahili vizuri. Hutaweza kuzungumza naye”
Yule mama akacheka.
“Ninajua. Kwanini yeye ajue
mimi nisijue” akaniambia kwa Kiswahili chenye lafidhi ya kiarabu kisha
akaniuliza.
“Unaitwaje mwanangu?”
“Naitwa Amour”
“Mmekubaliana nini na Zena?”
Kidogo nilisita kujibu. Zena
akanitazama na kuniambia.
“Mwambie”
“Aliniambia tuje huku” nikamjibu.
“Kufanya nini?”
Nikamtazama tena Zena.
“Amour unaulizwa, mbona
unanitazama mimi”
“Nisaidie kujibu, wewe ndiye uliyenileta
huku”
Mama akabadili lugha na
kuanza kuongea na Zena kwa ukali.
Walijibizana kwa muda kidogo
kisha Zena akaniambia.
“Si tumekubaliana tuje huku
tuoane?”
Kabla sijajibu yule mama
akamuuliza Zena kwa Kiswahili.
“Muoane kwa idhini ya nani?”
Zena akanyamaza kimya.
“Mwenye idhini ni baba yako,
umeshamwambia?” mwanamke huyo akamuuliza Zena.
“Si ndiyo tumekuja hivi?”
“Sasa mwambie baba yako,
akikukubali uoane na huyo kijana ndio mtaweza kuoana”
“Wewe pia si unaweza kutoa
idhini”
“Nitoe idhini mimi ni
mwanume?”
Yule mama alipouliza swali
hilo na kukosa jibu aligeuka na kuondoka. Nikamuona Zena akishusha pumzi ndefu.
“Kwanini mama yangu anapokuuliza
maswali unasita kujibu?’ akaniuliza.
“Sijui nijibu nini”
“Kwani mimi na wewe si
tumekwishaoana kule Somalia?”
“Mimi nilioana na Shamsa.
Baadaye ndio ukatokea wewe”
“Ulioana na mimi si Shamsa,
si nilikwambia?”
ITAENDELEA kesho ni kitatokea ungana nami hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment