Tangakumekuchablog
Handeni, WAZIRI
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mohongo, amelitaka Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kupunguza bei ya umeme na kupunguza gharama ya kunganisha
wateja wapya, ili kila mwananchi kumudu
gharama ya nishati hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya
siku ya kwanza ya kutembelea miradi ya
Rea Mkoani Tanga, Muhongo alisema shirika hilo hupandisha bei ya umeme lakini
huwa haishushi bei hivyo na kulitaka kupunguza
ili mwananchi wa kipato cha chini aweze kumudu.
Alisema Serikali ya awamu ya tano
ndani ya miaka mitano inataka mwananchi wa mjini na vijijini awe anatumia
nishati hiyo ya umeme majumbani na kumudu gharama zake.
“Ili kwenda na sera ya Tanzania kuwa
nchi ya viwanda ndani ya miaka mitano tunataka umeme umeshasambaa nchini kote
mjini na vijijini, mwekezaji wa ndani na nje umeme usiwe kuwa ni kikwazo”
alisema Muhongo na kuongeza
“Lakini yote hayo hayatafanikiwa
kama shirika halitapunguza bei ya umeme majumbani na gharama ya ufungaji kwa
kweli hiki ndio kilio cha watanzania wote hivyo niwatake kupunguza kwani kila
siku huwa munapandisha na kusahau kupunguza” alisema
Akizungumzia miradi ya Rea vijijini,
Muhongo alisema hakutokuwa na fidia mradi utakapopita na yoyote ambaye
atang’ang’ania kulipwa mradi huo utabadilisha uelekeo.
Alisema Serikali ikiendelea kulipa
fidia pesa zote za mradi zitaenda kwa kulipa wananchi fidia na mradi kukwama
hivyo kuwataka wananchi kutambua kuwa mradi huo ni kwa maslahi yao wenyewe.
Alisema pesa zilizotengwa kwa ajili
ya usambazaji umeme vijijini ni za usambazaji na sio za kuwalipa wananchi fidia
hivyo kijiji au mwananchi ambaye atataka kulipwa fidia atambue kuwa pesa hizo hazipo
na hakuna.
“Serikali haijatenga kuwalipa fidia
wananchi ili kupisha mradi wa usambazaji umeme vijijini, na yoyote ambaye
anadhani kuwa kuna pesa hizo asijidanganye na kupoteza muda” alisema Waziri
huyo wa Nishati na Madini
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano
ili kuhakikisha umeme huo unasambazwa nchini kote na wananchi kufaidika pamoja
na kutoa fursa za maendeleo kwa wananchi na wawekezaji.
Mwisho
No comments:
Post a Comment