SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE
ILIPOISHIA
Nilitupa macho yangu kwenye
ule msitu uliokuwa mbele yetu kisha nikamuuliza Zena.
“Tunaelekea upande gani?”
“Huko unakoona msitu”
“Huko ndiko kuna mji wenu?”
nikamuuliza.
“Mji uko huko. Twende”
Kusema kweli wakati wote
nilikuwa nimejikaza kiume lakini nilianza kupata hofu tangu Zena aliponiambia
kuwa pale tulikuwa katika ufukwe wa ujinini.
Pengine ningemuuliza ujinini
ipo upande gani katika ramani ya dunia. Katika kusoma kwangu Jeografia kuanzia
shule ya Msingi hadi Sekondari sikuwahi kuiona ramani ya ujinini katika upande
wowote wa dunia.
Lakini niliona swali hilo halikuwa na umuhimu
wa kuliuliza wakati ule. Kama kulikuwa na umuhimu
ulikuwa ni kumuuliza tulifika pale kwa usafiri wa aina gani? Kama
usafiri wenyewe ulikuwa haueleweki hata hiyo ramani ya ujinini inaweza
isieleweke.
“Tuanze kusonga, bado tuna
kipande cha mwendo wa miguu” Zena aliendelea kuniambia huku akitangulia kwenda
mbele kuelekea katika ule msitu uliokuwa unatisha.
Wakati nikimfuata nyuma
nilimuuliza.
“Lakini Zena sitapatwa na
madhara yoyote huku?”
“Madhara kama yapi?”
“Mimi najua kuwa majini
wengine wanadhuru watu?”
“Ni kweli wapo majini
wanaodhuru watu”
Kukiri kwake kwamba kuna
majini wanaodhuru watu kukaniongezea ile hofu yangu.
SASA ENDELEA
“Sasa itakuwaje, si nitakatwa
vipande vipande?”
Nilipomwambia hivyo Zena
akacheka.
“Huwezi kukatwa vipande vipande,
si uko na mimi. Mimi ndiye mwenyeji wako ambaye nitakulinda wewe”
“Utaweza kunilinda Zena?”’
“Bila shaka yoyote. Hakuna jini
yoyote atakayeniuliza chochote kuhusu wewe. Kwanza ukoo wetu unaheshimiwa sana na mimi najulikana
kwamba ni jeuri”
Tuliingia katika ule msitu.
Tulikuta njia nyembemba tukaifuata. Macho yangu yalikuwa yakiangalia kwenye ile
miti.
“Hivi hao majini nitawaona
kwa macho yangu?” nikamuuliza Zena baada ya kimya kifupi.
“Utawaona. Ngoja tutokeze
kwenye mji”
“Wakoje?”
“Wako kama watu tu. Kama
utaona tofauti ni ndogo sana.
Sisi tunakuwa na maumbo ya kiasili na ya kujigeuza kama
binaadamu. Sasa ukimuona jini katika umbo lake la asili ndio atakutishia kidogo
lakini baadaye utawazoea”
“Kwani tutarudi lini huko
Tanga?”
“Labda kesho. Nataka
nikuoneshe kwa wazazi wangu ili wajue mtoto wao anaishi na nani”
Baada ya muda kidogo tuliona
tumetokea katika majabali marefu. Yalikuwa mengi na mengine yalikwenda juu
yakaonekana kama minara.
“Ni kitu gani?” nikamuuliza
Zena.
“Ndio tumetokea kwenye mji
wenyewe”
“Mji ndio huu?”
“Ndio huo unaouona”
“Mnakaa kwenye majabali?”
“Hizo ndio nyumba zetu za
ghorofa”
“Una maana kwamba mle ndani
ya ile minara kuna watu?”
“Si watu ni majini ndio
wanaoishi humo”
Nikawa naikodolea macho ile
minara. Ilikuwa na matundu kama madirisha ya
kuingiza hewa.
Hata hivyo ilionesha kama ilikuwa ni kazi ya kale ya kisanaa. Niligundua kuwa
yale majabali na ile minara ilikuwa imechongwa na kuwezeha kuwa nyumba za
majini.
Karibu minara yote ilikuwa na
rangi nyeupe kama iloiyopakwa chokaa.
Baada ya mwendo mfupi
tulitokea katika eneo la wazi ambalo lilionekana kama
uwanja mpana. Tulikuta viumbe wengi kama watu
wakiwa katika harakati mbali kwenye uwanja huo.
Nilimuuliza Zena pale
palikuwa ni wapi na wale tuliokuwa tukiwaona walikuwa kina nani.
“Hapa ni kwenye gulio. Wale
ni majini, wengine wanauza bidhaa zao na wengine wananunua” Zena akaniambia.
“Sasa ni bidhaa gani
zinazouzwa pale?”
“Bidhaa mbali mbali. Bidhaa
za vyakula na bidhaa nyinginezo”
“Hizo bidhaa wanazipata
wapi?”
“Zinapatikana humu humu.
Bidhaa nyingine zinatoka Bara Arabu, India
na hata China”
“Hizo bidhaa zinafikaje
huku?”
“Kuna majini wanaokwenda
kununua na kuzileta huku”
“Mnatumia pesa gani?”
“Kwa huku kwetu pesa si
muhimu. Mara nyingi biashara inayofanyika ni ya mali
kwa mali.
Unatoa kibaba cha mchele, mwenzako anakupa kibaba cha ngano. Lakini wako majini
wanaouza na kununua vitu kwa pesa. Pesa zinazotumika ni rupia, real ya uarabuni
na pesa za Kichina”
“Pesa za Kitanzania
hazitumiki”
“Hazitumiki”
“Kwanini?”
“Majini hawaendi kununua vitu
kule”
Tulikiuwa tumeshalipita lile
eneo lakini mimi bado nilikuwa nikishangaa shangaa.
Tulikuwa tukipishana na watu
mbalimbali ambao Zena aliniambia kuwa walikuwa ni majini.
Kulikuwa na wengine waliokuwa
wakinitazama kwa macho makali lakini Zena aliniambia nisiwajali.
“Labda wananishangaa kuona
nimekuja katika mji wenu?” nikamwambia.
“Wanakushangaa kwani
hawawajui binaadamu? Wewe si binaadamu wa kwanza kufika huku”
“Na hao binaadamu wengine
wanafikaje huku?”
“Wanaletwa na majini wao
kufundishwa uganga au kutembea tu. Tena wanakaa muda mrefu hadi wanajua lugha
yetu”
“Na mimi naweza kuwaona hao
binaadamu wenzangu?”
“Huku kila mmoja ana lake.
Siwezi kujua wako wapi na hao waliowaleta sihusiani nao”
Tukafika katika jabali moja
lililokuwa na mnara mrefu. Zainush akaniambia kuwa pale ndio kwao.
Wakati tunataka kuingia
kwenye mlango wa jabali hilo
wakaja majini watatu kutupokea. Walikuwa wanawake watupu tena wasichana wadogo.
Lugha ya Zena ikabadilika, akawa anaongea kikwao.
Walitupokea yale mabegi
wakatangulia nayo ndani na sisi tukafuata nyuma. Zena akaniambia kuwa wale
walikuwa wadogo zake.
“Sisi tuko thelathini,
wanawake tuko kumi na saba, waliobaki ni wanaume”
“Mko wengi sana. Nyote ni baba mmoja na mama mmoja?”
“Baba mmoja na mama mmoja”
“Wewe ni wa ngapi kuzaliwa?”
“Ni wa saba lakini kwa
wanawake mimi ni wa pili”
“Hao ndugu zako wengine wako
humu?”
“Wale wakubwa wana masikani
zao zingine. Walioko hapa ni wale wadogo tu”
Tukafika mahali ambapo
tulikuta pazia zito la rangi nyeupe.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment