Tangakumekuchablog
Korogwe, WAZIRI
wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, amemuagiza Afisa Madini Mkoa wa Tanga,
Zephania Maduhu kuirejesha migodi ambayo
wawekezaji wameshindwa kuiendeleza.
Pia amewaagiza vijana kuunda vikundi
kuweza kupata mikopo kwenye taasisi za fedha na kuweza kuendeleza uchimbaji wa madini
kutoka wadogowado hadi kuwa wakubwa na
kuweza kutoa ajira kwa wengine.
Akizungumza kwenye mkutano wa
hadhara juzi kijiji cha Dindira Tarafa ya Bungu, Muhongo alisema kama kuna
migodi ambayo wawekezaji wameshindwa kuiendeleza hakuna
sababu ya kuachwa na ni lazima kurejeshwa kwa wananchi.
Alisema vijana wengi wanakosa ajira
ilhali rasilimali zipo pamoja na fursa mbalimbali za kujiletea kipato hivyo
kumuagiza afisa madini kupitia upya leseni na mikataba ya wawekezaji wa migodi
hiyo.
“Nimesikia kuwa kuna migodi mitano
hapa ambayo wawekezaji wameshindwa kuhuisha leseni zao, hii ina maana kuwa
wameshindwa na kutuambia kuwa irudi kwa wananchi” alisema Muhongo na kuongeza
“Kama fursa za maendeleo zipo lakini
zimekaliwa na watu wachache sisi kama Serikali hatukubaliani nazo na nakuomba
wewe afisa madini mwenye dhamana kupitia upya leseni zao” alisema
Alisema Serikali inataka kuona kila
mmoja anafanya kazi za kujiletea maendeleo na haitaki kuona mtu anashinda
kwenye vijiwe ambavyo havina tija zaidi kuukumbatia umasikini wa kujitakia.
Kwenye mkutano huo wa wananchi,
Waziri Muhongo alitoa nafasi za watu kumi kuuliza ama kuhoji kuhusiana na sekta
ya Nishati na Madini ambapo wengi walisema migodi iliyopo imefungwa na wao
kukosa ajira.
Walisema awali ambapo migodi hiyo
ikifanya kazi vijana wengi walikuwa wakipata ajira ambayo kumuona kijana mitaani akizurura lilikuwa
jambo la nadra kijijini hapo.
“Mheshimiwa tumefurahi kukuona na kuja
kwetu hasa ukiwa wewe ndio mtibabu mkuu
wa changamoto zetu za nishati na madini,
hapa tumerudi katika umasikini ambao tunajitakia ilhali tumezungukwa na madini”
alisema Rajab Mbwana
Alisema migodi toka kufungwa vijana
wengi wamejikalia vijiweni na hawana kazi hivyo kumtaka ujio wake kutafuta
mwekezaji mwengine ama migodi hiyo kukabidhi wananchi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment