SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 59
ILIPOISHIA
Abdi alitia mkono kwenye
mfuko wa suruali yake akatoa funguo mbili zilizofungwa pamoja akanipa.
“Ufunguo mmoja ni wa nyumba
yangu iliyoko shamba. Ukiingia ndani katika chumba cha mkono wa kulia kuna
mlango wa kuteremka chini ambako pia kuna chumba. Ukiingia katika chumba hicho
utakuta sefu ya chuma. Utaifungua kwa huo ufunguo wa pili ambao ni mrefu…”
“Kuna nini humo ndani?”
nikamuuliza baada ya kuona amenyamaza.
“Nimeweka sanduku lililojaa
dhahabu pamoja na dola za kimarekani. Kuna dola milioni moja. Utachukua wewe hilo sanduku. Pia
utachukua magari yangu, nyumba zangu na hoteli zangu. Utakuwa mrithi wangu….”
Abdi hakumaliza maneno yake,
sauti yake ilififia akakata roho mikononi mwangu. Bila shaka ile sumu ya lile
joka ilikuwa imeshamuathiri moyo wake.
Nikakiweka kichwa chake chini
huku nikijiambia.
“Ameyataka mwenyewe”
Nilimpekua mifukoni nikachukua
pochi yake pamoja na funguo ya gari na funguo ya nyumbani kwake. Nikasimama na
kutoka kwenye lile shimo. Niliona jamaa wawili miongoni mwa wale watu waliokuwa
pamoja na Abdi wakikimbia. Kumbe walikuw a wakituchungulia ndani ya lile shimo.
Nilitembea kwa hatua za
ukakamavu kuelekea pale lilipokuwa gari la Abdi. Nikafungua mlango wa dereva na
kuliwasha. Nikarudi mjini.
Nilikuwa nimepata majonzi
kweli kweli kutokana na kifo kile cha Abdi. Nilihuzunika kama vile si yeye
aliyekuwa anataka kuniua.
Nilijiambia kama maisha ya
Abdi yamekwisha na maisha yangu pale Somalia pia yamekwisha. Kama
nitaendelea kuishi pale Somalia,
mwenyeji wangu atakuwa nani? Nikajiuliza bila kupata jibu.
Nilifika nyumbani kwangu
nikamueleza Shamsa mkasa mzima uliotokea. Shamsa akashangaa sana.
SASA ENDELEA
“Amenirithisha kila kitu.
Nataka kwenda nyumbani kwake nikapekua. Kama
kutakuwa na kitu muhimu nikichukue”
Shamsa alikuwa akiendelea
kuhuzunika.
“Masikini Abdi. Amejidhulumu
mwenyewe nafsi yake…”
“Muda wake umeshafika” nikamwambia
Shamsa.
“Lakini naona huyo jini bado
anakuandama”
“Bila shaka, lakini ajabu ni
kwamba hajanitokea wala kunisumbua kama
zamani”
“Kama
si yeye ungekufa wewe leo”
“Ni kweli ningekufa. Sasa
mimi naenda kwa Abdi”
“Twende sote” shamsa
akanimbia.
“Twende”
Shamsa akavaa baibui lake tukatoka.
Tulijipakia kwenye gari ya Abdi tukaondoka.
Tulifika nyumba kwa Abdi
nikafungua mlango. Nyumba ilikuwa kimya. Abdi hakuwa na mke wala mtoto na
alikuwa ameshafukuza wafanyakazi wake wote.
Tuliipekua nyumba nzima.
Katika kabati la Abdi lililokuwa chumbani mwake tulikuta shilingi za kisomali
milioni kumi. Shamsa akaniambia tuzichukue. Tukazichukua. Tukafunga milango na
kurudi nyumbani kwetu.
Nilimshusha Shamsa pamoja na
zile shilingi milioni kumi. Nilimwambia kuwa nilitaka kwenda shambani kwa Abdi
kuchukua hilo
sanduku la dhahabu ambalo pia lilikuwa na dola za Kimarekani.
Nikaanza safari ya kuelekea
shambani kwa marehemu Abdi. Nilipofika. Nilikuta gari la Ismail, rafiki yake
Abdi likiwa limeegeshwa mbele ya nyumba ya Abdi.
Niliposhuka kwenye gari
nilikwenda kuujaribu mlango wa nyumba hiyo,. nikakuta ulikuwa umefungwa.
Nikaizunguka ile nyumba kumtafuta aliyekuja na gari lile.
Sikuona mtu. Nikapatwa na wasiwasi. Ghafla nikasikia
hatua za mtu anayenyata nyuma yangu. Nikageuka haraka nitazame nyuma lakini
sikuwahi, nilihisi kitu kizito kama nyundo
kikipiga kichwani kwangu. Hapo hapo nilidondoka na kuzirai.
Nilipozinduka nilijikuta
nilikuwa nimelala mahali pale pale nilipoanguka. Kabla ya fahamu kunijia
sawasawa nilijiuliza nilikuwa wapi na kwanini nilikuwa nimelala chini.
Kichwa kilikuwa kizito kama kilichokuwa kimebebeshwa mzigo na mwili ulikuwa
umechoka utadhani nililala kwenye sakafu kwa masaa kadhaa.
Nilipojaribu kukumbuka nini
kimenitokea, kichwa kiliniuma na nilihisi kizunguzungu.
Lakini taratibu kumbukumbu
zilianza kunijia. Kumbukumbu ya kwanza kunijia ilikuwa ni ile ya kutaka kuuliwa
na Abdi.
Nikakumbuka nilivyokuwa
kwenye shimo huku Abdi akimuihimiza mtu aliyekuwa amempa nyundo apigilie
msumari kwenye utosi wangu.
Kumbukumbu hiyo ilinijia kama sinema ya kutisha akilini mwangu. Ingawa ni tukio
ambalo lilishapita lilinitia hofu kama vile
ndio kwanza linatokea.
Kumbukumbu ya pili kunijia
ilikuwa ni ya kufika katika shamba la Abdi, kusimamisha gari na kukuta gari la
Esmail. Nikakumbuka jinsi nilivyozunguka nyuma ya nyumba ya Abdi kumtafuta
mwenye gari lile lakini ghafla nikasikia hatua za mtu nyuma yangu.
Niliposikia hatua hizo
nikataka kugeuka ili nitazame nyuma lakini sikuwahi kuona kitu, nilishitukia
nikipigwa na kitu kizito kama nyundo kichogoni
kwangu, macho yangu yakafunga kiza na sikuelewa tena kilichotokea.
Nikapeleka mkono wangu
kichogoni na kupapasa pale mahali nilipopigwa, nikaona palikuwa na jeraha na
dami ilitoka na kuganda.
Sasa nikainuka huku
nikijiuliza ni nani aliyekuwa amenipiga. Nilitazama kila upande, sikuona mtu.
Kila wakati nilikuwa najipapasa pale
kwenye kijaraha na kutazama ile damu mkononi mwangu.
Swali la nani aliyenipiga
lilikuwa halina jibu kwani sikuona mtu yoyote. Eneo lote lilikuwa kimya.
Nilirudi kwenye mlango wa ile nyumba, nikauona uko wazi. Wakati nilipokuja na
gari langu mlango huo ulikuwa umefungwa.
Sasa nikaanza kupatwa na
wasiwasi.
Ni nani aliyeufungua huo
mlango wakati funguo nilikuwa nayo mimi?
Wakati najiuliza hivyo
nilijipekua mifukoni. Zile funguo sikuziona. Nikaingia haraka mle ndani.
Niliingia katika kile chumba alichonielekeza Abdi. Milango yote niliikuta wazi.
Nikashuka katika kile chumba cha chini kwa chini ambacho Abdi aliniambia
kulikuwa na sefu ya chuma na ndani ya sefu hiyo kulikuwa na sanduku lenye
dhahabu pamoja na dola za Kimarekani alizokuwa amezificha.
Sefu niliikuta lakini ilikuwa
wazi. Nilipochungulia ndani ya sefu hiyo sikukuta chochote. Sefu ilikuwa tupu kama mkono uliorambwa!
Nikatoka nje ya ile nyumba.
Sasa fahamu zikanijia vizuri. Nilikumbuka wakati ule natoka katika lile shimo
nililoingizwa na kina Abdi, niliona watu wawili wakikimbia. Bila shaka
walisikia wakati Abdi alipokuwa ananiagiza nije nichukue lile sanduku
lililokuwa na dola pamoja na dhahabu.
Kwa kutaka wanufaike wao,
walikimbilia wao kuja hapa lakini wakashindwa ama kuingia katika ile nyumba au
walishindwa kulifungua ile sefu kwa sababu hawakuwa na funguo. Ndipo wakaamua
kunisubiri na mmoja wao ndiye aliyenipiga chuma hadi nikazirai.
Ndio sababu nilikuta lile
gari la Esmail lakini baada ya kuzirai na kurejewa na fahamu, gari hilo sikuliona. Walikuwa
wameshalichukua lile sanduku na kuondoka.
Esmail rafiki yake Abdi
nilikuwa nikimfahamu vizuri. Bila shaka na yeye alikuwemo katika ule mpango wa
kutaka kuniua.
Nikajimbia sitawaachia
wachukue dhahabu ile pamoja na dola za Kimarekani ambazo Abdi alikwishanipa
“Hawa watu kweli ni
majambazi!” nikajiambia kimoyomoyo na kuongeza.
“Huu walionifanyia ni
ujambazi kamili. Lakini nitapambana nao!”
Nilirudi kwenye gari langu
nikaliwasha na kuondoka.
Kwanza nilikwenda kwenye zahanati moja nikaoshwa lile jeraha
kisha nikafungwa dawa. Nilipotoka katika zahanati hiyo nilikwenda katika duka
la nguo nikanunua pama na kulivaa kuficha lile jaraha.
Nikaendesha gari kuelekea
nyumbani kwangu huku nikiwaza jinsi majambazi hao wa Abdi walivyonizunguka.
Nilishukuru kwamba nilikuwa na afya njema, vinginevyo kile chuma walichonipiga
kichogoni kingenimaliza kabisa.
“Fedha haina udugu wala
urafiki” niliwaza kimoyo moyo.
Abdi alitaka kuniua kwa
sababu ya fedha. Alijua nikishakufa atampata jini ambaye atampa fedha ili
atajirike, ainunue Mogadishu yote iwe mali
yake.
Wenzake nao walinipiga chuma
bila kujali ningedhurika kiasi gani kwa sababu ya fedha. Abdi alivunja udugu na
wenzake walivunja urafiki kwa sababu ya kitu fedha.
Nikaendelea kujiambia, sasa
mimi ni nani niiachie, nitawatafuta na kuwasulubu. Watajua mimi nani.
No comments:
Post a Comment