Wednesday, September 28, 2016

ASKOFU MWAMULAMBA ATOA USHAURI KWA DC


Tangakumekuchablog
Tanga, MWENYEKITI wa Maadili, Amani na Haki za Binadamu wa Madhehebu ya Dini Tanzania (TAG), William Mwamulamba, ametoa rai kwa  mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwailapa kuimaliza migogoro ya ardhi ili  wananchi kuondokana na kupiga foleni Idara ya mipango miji na mahakamani.
Akizungumza wakati wa kujitambulisha ofisi za mkuu wa Willaya  Mwamulamba, alisema migogoro  mingi ya ardhi ni yakupandikizwa na watu aliodai kuwa ni vishoka.
Alisema Tanga ni moja ya Mikoa ambayo imekithiri kwa migogoro ya ardhi hivyo kumuomba  kwa nafasi yake kuhakikisha inakomeshwa na wahusika kufikisha kwenye  vyombo vya sheria.
“Umoja wetu wa viongozi wa dini mbalimbali kwa pamoja tulikuwa hapa  kuchunguza   kero za wananchi na   tumegundua  migogoro ya ardhi inaongoza, na hii ni kuwa kuna watu hutumia fedha zao kuwakandamiza wanyonge” alisema Mwamulamba na kuongeza
“Uendapo ofisi za mipango miji na mahakamani utakuta foleni refu na ukiuliza unambiwa ni migogoro ya ardhi na viwanja, tuseme ukweli chanzo cha migogoro ni vishoka ambao wamo ndani ya ofisi zetu “ alisema
Kwa upande wake , Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Tanga, Askofu Dr, Jotham Mwakimwage, amemuomba  Mkuu huyo wa Willaya kuhakikisha amani ya nchi iliyopo inalindwa na kudumishwa na kutowapa nafasi watu wanaotaka kuivuruga.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakichochewa ili kuwagombanisha wananchi na kusema hali hiyo inafaa kupigwa vikali  na kutopewa nafasi kwani amani iliyopo ikitoweka kila mmoja itamgusa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwailapa, amewashukuru viongozi hao na kuwambia kuwa waendelee kuwa mabalozi wa kuhubiri amani  katika majengo yao ya ibada.
Alisema Serikali itashirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha usalama na amani ya nchi inadumishwa na na watu ambao watakuwa chanzo cha chokochoko watadhibitiwa.
Alisema awali Tanga kulikuwa na kikundi cha wahuni ambao walikuwa wanataka kuichafua na kudai kuwa mipango yao imeshindikana baada ya kuwatokomeza na sasa wamejipanga kwa ulinzi maradufu.
“Tanga kwa asilimia mia iko salama ila tuko na changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo nayo tunaifanyia kazi, nimekuwa nikifanya mikutano ya hadhara kwa wananchi maeneo ambayo iko na migogoro” alisema Mwailapa
Aliwataka wananchi kuacha kujinunulia viwanja na mashamba kinyemela badala yake wafuate taratibu ili kuepuka kutapeliwa na vishoka ambao hujipatia pesa na kugombanisha watu.
                                            Mwisho


 Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwailapa, akimsikiliza mwenyekiti wa Maadili, Amani na Haki za Binadamu wa Madhehebu ya Dini kutoka Kanisa la (TAG), Askofu, William Mwailamba, kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama wa Wilaya ya Tanga.

Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumeikuchablog

No comments:

Post a Comment