SIMULIZI MPYA
YAMENIKUTA SALMA MIE 1
MTUNZI. FAKI A FAKI 0713 340572
Naitwa Ibrahim Amour. Ni
mwenyeji wa Morogoro. Nilisoma morogoro hadi kidato cha sita. Nikafanikiwa
kuingia chuo kikuu cha Mlimani jijini Dar
es Salaam.
Nilipohitimu elimu ya chuo
kikuu na kupata shahada yangu, nilifanikiwa kupata ajira mamlaka ya mapato TRA,
nilifanya kazi kwa miezi michache tu nikahamishiwa Tanga.
Baada ya kuishi katika nyumba
ya wageni kwa siku chache nilifanikiwa kupata nyumba ya kupangisha maeneo ya
Usagara.
Wakati huo nilikuwa sijaoa
bado na nilikuwa na mdogo wangu aliyemaliza kidato cha nne aliyekuwa amekaa
nyumbani huko kwetu Morogoro. Nikamuita ili nikae naye pale nyumbani kwa sababu
nilikuwa peke yangu.
Zacharia akaja Tanga baada ya
kumtumia nauli. Nilikuwa pia na mpango wa kumtafutia kazi sehemu yeyote ambayo
ningefanikiwa.
Kwa vile bado nilikuwa mgeni
katika jiji hilo
nikaona nimsubirishe kwanza ili niweze kuzoeana na wenyeji ambapo ingekuwa
rahisi kumuombea kazi sehemu yoyote.
Nikiondoka asubuhi kwenda
kazini ninamuacha Zacharia nyumbani. Kwa kawaida nikiondoka asubuhi hurudi
jioni.
Mara kwa mara Zacharia alikuwa
akiniuliza kuhusu ule mpango wa kumtafutia kazi. Na mimi nilimjibu asubiri
kwanza.
Baada ya miaka miwili
nikafanikiwa kununua gari. Sasa nikawa naenda kazini na kurudi na gari langu.
Miezi michache baadaye nikanunua kiwanja jirani tu na pale nilipokuwa naishi.
Wakati naanza kujenga msingi
tu, nikapata matatizo kazini. Mimi na maafisa wenzangu watatu tulikamatwa na
polisi tukidaiwa kujihusisha na wizi wa mapato ya serikali.
Tulisimamishwa kazi ili
kupisha uchunguzi. Wakati uchunguzi unaendelea tulikuwa nje kwa dhamana. Baada
ya uchunguzi huo kukamilika tulifikishwa mahakani.
Ilikuwa kesi iliyotuendesha sana. Iliunguruma kwa
karibu miezi minane. Katika kipindi
hicho nilikonda kwa hofu na wasiwasi wa kufungwa. Kwa bahati njema shahidi
muhimu wa kesi ile ambaye angetoa ushahidi ambao ungeniweka mahali pabaya,
alifariki dunia kwa maradhi ya sukari.
Hukumu ilipokuja kutolewa
mwenzangu mmoja akaenda jela miaka saba. Mwingine alionekana hakuwa na hatia.
Mimi nikaachiwa kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha.
Mwenzangu aliyeonekana hakuwa
na hatia alirudishwa kazini. Mimi nikafukuzwa kazi kabisa.
Pia nilishukuru. Niliona bora
kufukuzwa kazi kuliko kufungwa na ukitoka
huko huna kazi.
Hata hivyo mpango wangu wa
kuendeleza ujenzi wa nyumba yangu ambao nilikuwa nimeshauanza ukaishia hapo
hapo.
Nilikuwa na akiba yangu benki
nikaamua kuanzisha mradi wa kuchukua tenda za usambazaji vitu mbalimbali katika
mashirika, taasisi na idara za serikali.
Nikafungua ofisi yangu jirani
na maktaba. Baada ya kujitangaza katika maofisi mbalimbali nilifanikiwa kupata tenda
ndogo ndogo lakini nikitegemea kuwa baadaye ningeweza kupata tenda kubwa kubwa.
Nilikuwa nikisaidiana na
Zacharia na nilikuwa nimeajiri msichana mmoja aliyekuwa akibaki ofisini kwa
ajili ya kazi ndogo ndogo kama vile kufungua ofisi asubuhi na kuifunga jioni,
kupokea simu na kuhifadhi kumbukumbu zetu za kiofisi.
Siku moja nikashuhudia ajali
karibu na ofisi yangu.
Msichana mmoja ambaye alikuwa
akiendesha baskeli aligongwa na gari ndogo ambayo haikusimama.
Wakati tukio hilo linatokea mimi
nilikuwa nikiondoka na gari langu ofisini kwangu. Nikalisimamisha gari karibu
na mahali alipoanguka yule msichana na kuzirai.
Kitu kilichonishitua ni
kwamba alikuwa akitokwa na damu nyingi iliyokuwa ikisambaa barabarani.
Baskeli yake ilikuwa
imeanguka kando yake ikiwa imekunjwa kama
iliyokanyagwa na treni.
Gari lililomgonga lilikimbia
mara tu baada ya ajali kutokea.
Kutokana na kuona ile damu
iliyokuwa ikitoka kwa wingi, nilizima gari nikashuka na kumfuata yule msichana.
Sikuwaza hili wala lile, nilimzoa pale chini bila kujali damu iliyokuwa
ikimtiririka ambayo ilikuwa ikiingia kwenye nguo zangu.
Nilimpakia kwenye siti ya
nyuma ya gari langu, nikajipakia na kumuwahisha hospitali ya Bombo ambapo alipokelewa
na kushughulikiwa.
Sikujua kama angepona
kutokana na ile damu iliyokuwa ikimtoka kwa wingi, nikapwatwa na wasiwasi.
ITAENDELEA kesho
No comments:
Post a Comment