SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
YAMENIKUTA SALMA MIE 6
ILIPOISHIA
“Wangu mimi hatugombani, ni
mgumu tu. Kila siku yeye hana pesa lakini biashara anafanya. Sijui pesa zake
zinakwenda wapi!”
“Basi ana mwanamke nje, ndiye
anayemla. Mwenzangu wala chuya, mchele waliwa na mwenzio!”
Rita aliponiambia hivyo
alinicheka na mimi nikajidai kucheka lakini moyo wangu ulipata fadhaa sana nilipohisi kuwa inaweza
kuwa ni kweli mume wangu akawa na msichana
wa nje anayekula pesa zake.
Siku ile niliwaza sana yale maneno
aliyoniambia shoga yangu.
Mume wangu aliporudi jioni
nilijaribu kumwambia.
“Mume wangu huninunulii hata pikipiki
na mimi”
“Unataka pikipiki ya nini mke
wangu?”
“Pikipiki ya nini? Watu
wananunuliwa magari, wewe unasema pikipiki ya nini?”
“Kama
ni gari si hili tunalo”
“Hilo ni la kwako. Mimi nataka pikipiki”
“Tuombe Mungu, kazi zangu
zikienda vizuri nitakununulia”
“Utaninunulia lini?”
SASA ENDELEA
“Si nimekwambia ufanye
subira. Mambo yakiwa mazuri utapata pikipiki, hata gari”
“Yako ni hayo tu kila siku.
Wanaume wengine hawapendi hata kuwapendezesha wake zao!”
“Salma usiige mambo ya watu.
Kwa vile umemuona jirani yako ana gari na wewe unataka ununuliwe gari. Wewe
unajua mume wake anafanya kazi gani?”
“Wala sio hivyo. Mimi nina
akili zangu na naangalia maisha yangu. Siigi mtu mimi. Kama
ninataka pikipiki ninaitaka kwa shida yangu. Tatizo ni kuwa kila ninachokwambia
mume wangu lazima ukipinge”
Ibrahim akajidai kucheka.
“Si kweli. Mbona vitu vingi
nakununulia. Nguo nakununulia pamoja na kukutimizia mahitaji mengine. Sema wewe sasa unataka
makubwa”
“Haya basi nayaishe. Naona
labda kuna mwenzangu wa pembeni maana siku hizi umebadilika sana”
Siku ile nilijaribu tu
kumpima mume wangu ili nione atanijibu nini. Lakini jibu lake lilikuwa
ni la kukatisha tamaa. Sikamini kabisa kuwa kwa kipato cha mume wangu
angeshindwa kuninunulia pikipiki.
Pia sikuamini kuwa mwaname
huyo angeshindwa kunitimizia mahitaji yangu mengine ninayotaka kama anavyofanyiwa shoga yangu na mume wake.
Pegine ulikuwa ni ugumu au
roho mbaya inayotokana na mila zilizopitwa na wakati zinazowadharaulisha
wanawake kwa wanaume.
Baada ya siku ile sikumuuliza
kitu tena Ibrahim lakini ndani ya moyo wangu nilishaamua kama tabia ya Ibrahim
itaendelea kuwa ile nisingeweza kupata
maendeleo kama wanawake wenzangu.
Nilikaa kama siku tatu hivi
nikiwaza, siku ya nne yake nikaenda kwa yule rafiki yangu. Nilimkuta amekaa
sebukeni akitizama filamu kwenye televisheni yake.
“Vipi shoga?” akaniuliza.
“Ah mambo ya mume wangu
yananichokesha!” nikamwambia huku nikiketi kwenye kochi.
Shoga yangu Rita akanicheka.
“Yamekuchokesha vipi shoga?”
“Ugumu shoga! Mume wangu ni
mgumu sana. Juzi
nilijaribu tu kumuomba aninunulie pikipiki, eti anajidai kuniuliza pikipiki ya
nini…gari si hili tunalo”
“Labda hana pesa”
“Sio kutokuwa na pesa, sema
ni mgumu. Pesa anazo lakini ana dharau, hataki maendeleo yangu. Nimeshamuona
yule si mume ni gume gume”
Shoga yangu akacheka tena
lakini mimi sikucheka nilijifanya nimekasirika.
“Kweli nakwambia shoga…yule
si mume ni gume gume”
“Siku ile nilikwambia mwendee
kwa songoma ukaleta gozi gozi. Si unamuona huyu mume wangu nimemnyoosha, haoni
wala hasikii, nikikohoa tu ananiuliza wataka nini mke wangu?”
“Na hilo
la songoma ndilo lililonileta, nataka unipeleke na mimi nikamtengeneze, awe kama mume wako. Nikimuona amekaa sawa, namwambia
anijengeee nyumba”
Mimi na shoga yangu tukacheka
pamoja.
“Na huyo songoma mwenyewe
akikufanyia dawa zake utakuja kuniambia. Lazima mumeo atakujengea nyumba” Rita
akaniambia na kuzidi kunipa moyo.
“Sasa utanipeleka lini
shoga?”
“Siku yoyote utakayotaka,
mimi niko tayari”
“Nataka unipeleke kwa huyo
huyo aliyekufanyia wewe”
“Na ndiko huko huko
nitakakokupeleka”
“Na itachukua siku ngapi hadi
matokeo yaonekane?”
“Si siku nyingi. utamuona
akibadilika kidogo kidogo”
Nilinyamaza kidogo kufikiri
kisha nikamuuliza.
“Tunaweza kwenda kesho?”
“Tunaweza lakini iwe asubuhi,
mpaka saa sita twe tumerudi”
“Na mimi pia muda wangu mzuri
ni wa asubuhi, yule bwana akienda kazini. Najua akiondoka harudi mpaka jioni”
“Harudi mchana kuja kula?”
“Zamani ndio alikuwa anarudi
kula lakini siku hizi akiondoka ndio mpaka jioni. Sijui anakula kwa huyo mke
mwenzangu!”
“Yote utayajua huko huko
kwa huyo mganga”
“Kama
ana mwanamke atanieleza?”
“Atakueleza yote”
“Nataka nijue, uwezekano huo
wa kwa na mwanamke upo”
“Sasa basi wewe jiandae,
nikikupigia simu kesho asubuhi unakuja, tunakwenda zetu”
“Ni mbali sana”
“Mganga mwenyewe yuko
Kisosora”
“Si tutakwenda na gari yako”
“Tutakwenda na gari yangu, usijali.
Hapo Kisosora hata lita moja ya petroli haimaliziki”
“Tutatia lita moja”
“Mbona mume wangu ananitilia
ya kutosha. Ananiwekea mafuta ya wiki nzima”
“Acha mambo yaende vizuri, na
mimi keshokutwa nitakuwa na gari langu. Mwanaume pesa anazo lakini ni mgumu sana. Hataki hata nijue
katika akaunti yake ya benki ana shilingi ngapi”
“Tena nakwambia ukimuweka
sawa, hata jina la akaunti yake ya benki anaweka la kwako?”
“Acha shoga! Kwani wewe mume
wako ameweka jina lako kwenye akaunti yake?”
“Mimi amenifungulia akaunti
yangu kabisa, ananiwekea pesa kila mwezi”
“Na mimi itakuwa hivyo hivyo.
Nitamwambia anifungulie akanti benki”
Siku ile nilirudi nyumbani
kwangu nikiwa na furaha na ndoto za kupata tajiri. Kama mume wangu atanijengea
nyumba, ataninunulia gari, atanifungulia akaunti benki, nitajiona kama
nimeshakuwa tajiri.
Mume wangu aliporudi nyumbani
jioni nilimchangamkia sana
kuliko kawaida yangu kwa vile nilishajua mahali ambapo nitakwenda kumnyoosha.
Kwa vile ingekuwa ni mara
yangu ya kwanza kwenda kwa waganga, siku ile sikupata usingizi kwa mawazo.
Mawazo yangu yalikwenda mbali
nikawa nawaza wakati mume wangu akiwa bwege langu akinitii kwa kila kitu.
Nilijiambia wakati huo maisha
yangu yatakuwa mazuri sana.
Fedha za mume wangu nitakuwa nakaa nazo mimi.
Asubuhi kulipokucha nilianza
kufanya usafi wa nyumbani kwangu. Sikushughulika kubandika chai mapema kwa
sababu mume wangu alikuwa akiondoka asubuhi bila kunywa chai. Ananywea huko huko,
yeye na mdogo wake.
Muda wao wa kutoka ulipowadia
Ibrahim alinifuata uani akaniaga.
“Nimekuachia pesa za sokoni
kitandani” akaniambia.
“Hizo ni pesa au visenti.
Pesa utakuja kuniachia nitakapokutengeneza” nikamjibu kimoyomoyo.
Alipoondoka na mdogo wake
nikaenda bafuni kuoga. Nilipomaliza nilivaa. Nikaenda kuketi sebuleni kwangu kusubiri
Rita anipigie simu.
Nilipoona kimya na muda
unakwenda nikampigia mimi.
“Shoga habari ya asubuhi?”
nikamuuliza alipokea simu.
“Nzuri shoga, mume wangu ndio
ameondoka sasa hivi. Nilikuwa nataka kukupigia kukwambia jitayarishe”
“Nimeshajitayarisha shoga”
“Basi njoo, mimi najiandaa”
Nikarudi chumbani kwangu
kuchukua baibui langu nikalivaa na kupachika mkoba wangu begani, nikatoka.
ITAENDELEA kesho usikose je, Salama afikapo kwa Mganga nini kitatokea?
No comments:
Post a Comment