HADITHI inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria Freys Coach inayofanya safari kati ya Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku na hufanya hivyo kutoka Singida kila siku saa 12 asubuhi 0622 292990
YAMENIKUTA SALMA MIE 4
ILIPOISHIA
Mama huyo alicheka niliposema
‘mgonjwa wangu’
“Haya nawaacha kidogo”
Akaondoka.
“Nikupatie kinywaji gani kaka?”
salama akaniuliza.
“Hapana, sihitaji kinywaji
chochote”
“Kwanini, tunayo juisi ya
parachichi”
“Nitakuja kunywa siku
nyingine, usijali”
Tukaendelea kuzungumza kwa
karibu nusu saa. Wakati nataka kuondoka nilimuachia Salma shilingi elfu
hamsini.
“Hizi zitakusaidia kununua
vitu vidogo vidogo” nikamwambia.
“Asante kaka, nashukuru”
Salma alikwenda kumuita mama
yake ili niagane naye. Mama huyo alipokuja akanishukuru kwa mara nyingine kwa
msaada nilioutoa kwa mwanawe siku alipopata ajali.
SASA ENDELEA
Jina langu ni Salama Aboud,
nilikuwa mtoto wa tatu wa mzee Aboud ambaye alifariki dunia wakati mimi nikiwa
darasa la saba.
Katika kipindi chote hicho nilikuwa
nikiishi na mama yangu ambaye alikuwa akinipenda na kunidekeza sana.
Kutokana na utoro wangu wa
shule nilishindwa kuendelea na masomo ya sekondari. Niliacha masomo nikiwa
kidato cha tatu. Vile mama yangu alikuwa anashindwa kunikemea na kwa vile
hakukuwa na mtu mwingine wa kunisema kitu, basi nilifanya vile nilivyotaka
mimi.
Kaka zangu walionitangulia
mmoja alikuwa amefariki, wawili walikuwa wakikaa Dodoma kwa baba mdogo.
Siku ile niliyopata ajali
walikuja Tanga kunijulia hali kisha waliondoka kurudi Dodoma.
Sikujua ni kitu gani
kilichofanya nimzowee sana
Ibrahim. Pengine ni kutoka na wema alionifanyia siku ile nilipopata ajali.
Kwanza nilimchukulia kama msamaria mwema lakini mazoea yetu yalipozidi nilianza
kumpenda na nikawa na hisia ya kuishi na mtu kama
Ibrahim.
Nilivutiwa sna na staili yake
ya maisha na tabia yake. Lakini Ibrahim hakuwa akionesha kutambua mawazo yangu.
Jambo hilo lilikuwa likinikera sana. Kusema kweli nilikuwa ninatamani tuwe
wapenzi.
Usishangae kwamba nilikuwa
nikiwaringia sana
wanaume. Walitokea wanaume wawili waliotaka kunioa nikawakataa bila sababu
yoyote.
Mama yangu kwa kufuatisha
mawazo yangu, naye aliwatolea nje.
Mara kwa mara mama alikuwa
akiniuliza.
“Utaolewa lini mwanangu, wenzako
wote wameolewa?”
“Hao walioolewa waache
waolewe, mimi niache tu”
“Sasa utakaa hivi hivi mpaka
lini?”
“Kwani kuna mume aliyekwambia
ananitaka nikamkataa?”
“Si walikuja vijana wawili
ukawakataa mwanangu”
“Bado unawakumbuka tu”
“Nawakumbuka kwa sababu sioni
dalili ya kutokea mume mwingine, naona kama
umejitia nuksi”
“Muda wangu wa kuolewa
ukifika nitaolewa tu mama”
Haukupita muda mrefu ndipo
alipojitokeza Ibrahim.
Ibrahim nilimuonesha dalili
zote za mapenzi kwani haikuwa rahisi kwangu mimi mwanamke kumueleza wazi kuwa
nimempenda.
Siku moja nikaukata mzizi wa
fitina. Nilimtumia meseji nikamwambia.
“Natamani ningekuwa mke wako
Ibrahim”
Akarudisha jibu na kuniuliza.
“Kwanini?”
Nikamtumia meseji nyingine ya
kumwambia.
“Nimependa tabia zako”
Akanijibu tena kwa kuniambia.
“Kama
ungependa tuoane subiri nijiandae”
Kwa sababu nilikuwa nampenda,
jibu lake hilo likanifurahisha.
Siku ya pili yake tulikutana
katika hoteli moja tukazunguza sana
kuhusu mapenzi.
Akaniambia yeye ni muangalifu
sana katika
kutafuta mchumba lakini katika siku chache tulizokuwa pamoja amegundua kuwa
ninafaa kuwa mchumba wake. Ibrahim hakujua alikuwa amenifurahishaje kutokana na
kauli yake hiyo.
Dhamiri yetu ikatimia. Baada
ya kuzungumzia uchumba kwa wiki kadhaa, hatimaye Ibrahim akaleta barua ya
uchumba kwa mama yangu.
Mama yangu aliipokea kwa
mikono miwili kwa sababu nilishamueleza jinsi nilivyokuwa ninampenda Ibrahim.
Mama alimfahamisha baba mdogo
aliyekuwa Dodoma
kuwa kumeletwa barua ya uchumba ya Salma.
Baba mdogo akanipigia simu
kuniuliza kama nimempenda huyo mchumba.
“Nimempenda ndio maana
nilimuelekeza aje kwetu” nikamjibu.
“Nimesikia kuwa ndiye yule
aliyekusaidia ulipopata ajali?”
“Ndiye yeye”
“Imekuwa heri. Huyo ni
mchumba mwema. Mimi pia nimemkubali”
Baada ya baba mdogo
kuzungumza na mimi alimpigia mama akamwambia kuwa na yeye amekubaliana na huo
uchumba.
Mbali ya kumjulisha baba mdogo,
mama pia aliwajulisha wajomba, yaani ndugu zake. Wote wakaukubali uchumba huo na
jibu likapelekwa kwa Ibrahim kuwa uchumba wake umekuwa makubuli, yaani
umekubaliwa.
Sasa ikawa ni mipango ya
harusi. Mipango ya harusi yetu ilichukua karibu miezi mitatu. Nataka niseme
ukweli kuwa tangu nijuane na Ibrahim mpaka tunakuwa wachumba sikuwahi kutembea
naye hata siku moja.
Mimi sikutaka jambo hilo kwa sababu baadhi ya
wanaume ukishatemmbea nao hubadili mawazo na kutafuta wachumba wengine.
Ibrahim pia hakuonesha kuwa
na uchu wa wasichana. Alipoona dhamiri yangu ilikuwa ni kuoana, hakuwahi hata
siku moja kunishawishi tufanye kitu.
Kwa hilo
peke yake nilimsifu na kuona alikuwa mwanaume madhubuti aliyeweza kuuzuia moyo
wake. Ni wanaume wachache sana wenye tabia kama ya Ibrahim.
Ndoa yetu ilifungwa siku ya
ijumaaa saa saba na nusu. Ilifungwa katika msikiti wa Chumbageni baada ya
mshuko wa swala ya ijumaa.
Mimi nilikuwa niko nyumbani
nikimsubiri mume atoke msikitini. Tangu asubuhi nilikuwa saluni nikipambwa na
kuchorwa piko. Nilirudishshwa nyumbani saa sita.
Nilipelekwa saluni nikitokea
kwa kungwi ambako nilikaa kwa wiki maja nikifundwa jinsi ya kuishi na mume.
Nakumbuka somo moja muhimu
nililolipata kwa kungwi ni kuwa nisimnyime mume wangu anapotaka penzi hata kama niko jikoni napika.
“Acha kazi zako ukamridhishe
mumeo” kungwi wangu aliniambia.
Ibrahim aliporudi nyumbani
kutoka msikitini alifuatana na watu watatu mmojawapo akiwa sheikh
aliyetuozesha.
Ibahim alinipa mkono mke
wake. Na hii ni kawaida. Mume akishakuoa akiingia chumbani hukupa mkono.
Sheikh akatuombea dua na
kututaka tuishi maisha marefu, tupate watoto wema, tuishi kwa upendo na
kuaminiana. Lakini akaongeza sentesi moja mabayo sikuipenda. Alisema.
“Mvumiliane, msameheane,
muaminiane lakini kama itatokea mnaachana
muachane kwa wema”
Kichwa changu kilikuwa
kimefunikwa kwa mtandio unaoonya. Sheikh aliposema hivyo, niliinua uso wangu
niliokuwa nimeuinamisha chini. Nikamtupia jicho Ibrahim huku yale maneno, “Kama itatokea mnaachana muachane kwa wema…” yakipita
akilini mwangu.
Wakati namtupia jicho Ibrahim
nilikuwa kama namuuliza. “Hivi tutakuja kuachana
mimi na wewe?”
Moyoni mwangu sikutarajia
kwamba hilo
lingeweza kutokea kwa vile sheikh alishatuambia tuvumiliane, tusameheane na
tuaminiane.
Niliamini kwa falsafa ya
kuvumiliana, kusameheana na kuaminiana, suala la kuachana lingekuwa mbali sana na ndoa yetu.
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekucha blog usikose uhondo huu nini kitatokea baada ya wawili hao kufunga ndoa na ile kauli ya Sheikh kusema mukiokosana muachane kwa wema
No comments:
Post a Comment