Europa League: Feyenoord 1-0 Man Utd
Manchester United
walionyesha mchezo usio wa kuridhisha mechi yao ya kwanza katika ligi
ndogo ya Ulaya, Europa League ugenini na kuchapwa 1-0 na Feyenoord.
Jose Mourinho alifanya mabadiliko manane kwenye kikosi chake kilicholazwa na Manchester City.Kombora la Anthony Martial, ambalo lilienda nje, ilikuwa fursa pekee waliyopata wageni hao kipindi cha kwanza.
Zlatan Ibrahimovic aliingia kama nguvu mpya na mpira wake wa kichwa alipopata fursa ulienda nje na hakuweza kuwasaidia.
Badala yake, Nicolai Jorgensen, aliyeonekana kuotea, ndiye aliyekuwa na bahati. Alimtumia krosi Tonny Vilhena ambaye alifungia Feyenoord bao la ushindi dakika ya 79.
Ibrahimovic alikaribia kusawazisha lakini frikiki yake iliokolewa akijaribu mara ya pili na kipa wa zamani wa Liverpool Brad Jones, aliyekuwa kwenye lango la Feyenoord.
Kichapo hicho kina maana kwamba United sasa wameshindwa mechi nne mtawalia za ugenini Ulaya kwa mara ya kwanza.
Pogba ahangaika
Paul Pogba, aliyerejea United kwa bei ya £89m iliyovunja rekodi ya dunia akitokea Juventus Agosti, alionekana kukosa nidhamu yake na kushindwa kudhibiti wapinzani mechi waliyoshindwa na Manchester City Jumamosi.
Kucheza na Ander Herrera na Morgan Schniederlin safu ya kati dhidi ya Feyenoord kulionekana kumpa uhuru wa kucheza vyema zaidi lakini alishindwa kufanya hivyo.
Alionekana kutokuwa na haraka, sawa na ilivyokuwa kwa kikosi chote cha United kipindi cha kwanza.
Manchester United walikuwa bila mshambuliaji wao, nahodha, Wayne Ronney.
Manchester United watarejea uwanjani Jumapili Ligi ya Premia ugenini dhidi ya Watford saa nane mchana.
No comments:
Post a Comment