Thursday, September 15, 2016

MABAKI YA NDEGE YALIYOPATIKANA NI MH370

Mabaki yaliyopatikana Pemba,  ni ya MH370

Mabaki ya ndege yaliyopatikana PembaMabaki ya ndege yaliyopatikana katika pwani ya visiwa vya Pemba  yalitoka kwa ndege ya shirika la Malysia Airlines iliyotoweka mwaka 2014, maafisa wa Malaysia wamethibitisha.
Waziri wa uchukuzi wa Malaysia Liow Tiong Lai amesema kupitia taarifa, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kwamba baada ya uchunguzi imebainika kwamba kipande hicho kikubwa cha bati kilichopatikana mwezi Juni ni cha ndege hiyo safari nambari MH370.
Amesema uamuzi huo ulifikiwa na wataalamu kutoka Idara ya Usalama wa Safari za Ndege ya Australia (ATSB) na wale wa kuchunguza usalama wa MH370.
Mapema Julai, waziri wa uchukuzi wa Australia Darren Chester alikuwa amedokeza kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa mabaki hayo yalikuwa ya ndege hiyo.
Alisema muundo wa mabaki hayo, ukubwa wake na muonekano wake viliashiria kwamba yalikuwa ya ndege hiyo ya Malaysia.
Mabaki hayo pia yalikuwa na muhuri wa kuonesha tarehe ya kuundwa kwake ambayo ilikuwa Januari 23, 2002. Ndege hiyo ya Malaysia iliwasilishwa kwa shirika hilo 31 Mei, 2002, kwa mujibu wa tovuti ya shirika la Channel News Asia.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777 ilitoweka Machi 2014, ikiwa na abiria 239 baada ya kupaa kutoka Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia kuelekea Beijing.
Bw Liow amesema mabaki hayo yatachunguzwa zaidi kubaini iwapo kutapatikana ufumbuzi kuhusu kilichotokea hadi ndege hiyo ikatoweka.
Awali, wachunguzi walikuwa wamethibitisha kwamba mabaki yaliyopatikana visiwa vya Reunion mwezi Julai 2015 yalitoka kwa ndege hiyo.
Mabaki mengine yanayodhaniwa kutoka kwa ndege hiyo yamepatikana Msumbiji, Afrika Kusini na visiwa vya Rodrigues, Mauritius.

No comments:

Post a Comment