SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
YAMENIKUTA SALMA MIE 9 Inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria Tanga, Moshi, Arusha , Babati hadi Singida kila siku asubuhi, Freys wapo Tanga barabara ya 12 na kwa Singida wapo Kituo kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani, 0622 292990
ILIPOISHIA
Geti lilipokuwa wazi aliingia
kwenye gari akaiingiza gari ndani. Tukashuka sote. Alikwenda kufunga geti.
Alipomaliza tukaingia ndani ya nyumba yake.
“Shoga asante, acha niende nikatayarishe
mambo” nikamuaga shoga yangu kabla ya kutoka kwenda kwangu.
Nilifungua mlango wa nyumba
nikaingia ndani. Wakati nikiwa jikoni nikitafuta mahali pa kuficha vile
vipakiti, nikasikia mlango ukigongwa. Nikaviacha vile vipakiti kwenye mkoba
wangu, nikaenda kufungua mlango.
Nikashituka kuona alikuwa
mgeni. Alikuwa mdogo wake Ibrahim aliyekuwa akikaa Dar. Alikuwa anaitwa Mashaka
lakini mwenyewe alijiita meshack.
Alikuwa ni mdogo wake Ibrahi
shangazi kwa mjomba.
“Oh shemeji, karibu sana” nikamkaribisha huku
nikipokea begi alilokuwa amelipachika kwenye bega lake.
“Asante, habari ya hapa?”
“Nzuri, za safari”
Baada ya kulipokea begi
niliingia nalo ndani.
“Nashukuru ni nzuri, sijui
nyinyi hapa”
Meshack aliingia akafunga
mlango.
Nikamkaribisha sebuleni
lakini begi lake nilikwenda kuliweka kwenye chumba cha
wageni.
Nilipotoka Meshack
aliniuliza.
“Kaka yuko wapi?”
“Yuko kazini kwake, hapa
anarudi jioni sana,
si ana taarifa kuwa unakuja?”
“Anayo taarifa na leo asubuhi
wakati najiandaa kuja huku nilimpigia simu kumjulisha kuwa ninakuja”
SASA ENDELEA
“Ngoja nimpigie nimjulishe
kuwa umeshafika”
Nikachukua simu yangu na kumpigia.
“Heloo!” Sauti ya Ibrahim
ikasikika kwanye simu.
“Shemeji ameshafika”
nikamwambia.
“Shemeji yupi?” akaniuliza.
“Shemeji Mashaka kutoka Dar”
“Oh alinipigia simu asubuhi
kunijulisha kuwa anakuja lakini nilisahau kukuambia. Amefika sasa hivi”
“Ndiyo namkaribisha hapa”
“Mwambie ninakuja, tunafunga
ofisi”
“Sawa”
Nikakata simu kisha
nikamwambia shemeji.
“Anakuja”
Kutokana na ule muda aliofika
shemeji nilikisia kuwa hakuwa amekula chakula cha mchana, nikaona angalau
nikamtayarishie chai ya maziwa imchangamshe hadi usiku.
“Shemeji naenda jikoni”
nikamuaga na kuondoka kwenda jikoni kumtayarishia chai.
Chai ilikuwamo kwenye chupa.
Nilichukua slesi tatu za mikate, nilimpakia siagi na kumuandalia kwenye sahani
pamoja na kikombe cha chai nikampelekea.
“Karibu shemeji” nikamwambia
wakati nikimuwekea sahani.
“Asante shemeji”
Nikakaa kando yake
kumzungumzisha huku akiendelea kunywa chai.
Alipomaliza kunywa chai
alinishukuru. Nikaenda kuiondoa ile sahani na kuirudisha jikoni. Nikarudi tena
pale sebuleni. Tuliendelea kuzungumza hadi mume wangu alipotokea. Niliwaacha
wakisalimiana nikaingia chumbani.
Nilijilaza kitandani na
kuanza kuwaza jinsi ya kuifanya ile dawa yangu wakati kulikuwa na mgeni ambaye
angekula kile chakula. Isitoshe nisingeweza kufunga bomba na kusingizia maji
yamekatika wakati kulikuwa na mgeni huyo.
Nilijimbia kama itagundulika
kuwa maji yanatoka ispikuwa niliyafunga na kusingizia kuwa maji yamekatika,
ningeeleweka vibaya mbele ya mgeni. Ningeonekana kama nimemfungia yeye na
kwamba sikuvutiwa na ujio wake.
Nikaona nimpigie simu shoga
yangu Rita.
“Tumepata mgeni” nikamwambia
Rita alipopokea simu yangu.
“Ni nani?” Rita akaniuliza.
“Ni shemeji yangu, ndugu
yake mume wangu. Sasa sijui itakuwaje?”
“Kwani yeye atakuzuia nini?”
“Si ile dawa nilitakiwa
niitie kwenye chakula”
“Kama
nakumbuka vizuri yule mzee alikwambia hata wewe mwenyewe unaweza kula hicho
chakula, kwani si kuna huyo mdogo wake mwingine mnayeishi naye. Si pia atakula
hicho chakula?”
“Sasa kama hilo si tatizo, kuna tatizo jingine.
Nikiyafunga yale maji, si nitaonekana nimemfungia mgeni? Si unakumbuka
tulikubaliana nisingizie kuwa maji yamekatika ili huyu bwana aoge kwenye ndoo?”
“Kwani huyo mgeni atakaa kwa
siku ngapi?”
“Sijajua bado”
“Unaweza kusubiri hadi
atakapoondoka”
“Naona nachelewa”
“Sasa utafanya nini?”
“Sina la kufanya, itabidi
nisubiri hadi atakapoondoka lakini ndio hivyo moyo waumia”
“Subira huvuta heri msichana,
acha pupa” Rita akaniambia kwa mzaha. Tukacheka.
“Najua kuwa subira huvuta
heri lakini ngoja ngoja nayo huumiza matumbo”
Wakati nasema hivyo mume
wangu akafungua mlango ghafla na kuingia ndani. Nikazuga hapo hapo.
“Basi shoga tutaongea
baadaye, ngoja nimuhudumie mume wangu ndio amerudi sasa hivi kutoka kazini”
Sikungoja jibu lake nikakata
simu.
“Unazungumza na nani?”
Ibrahim aliposikia namsema akaniuliza.
“Nazungumza na jirani yangu
Rita” nikamwambia huku nikinyanyuka kitandani.
“Umempa chakula mgeni?”
“Nilimpatia chai tu na slesi
tatu, hakukuwa na chakula”
“Jioni utapika nini?”
“Mh! Sijajua bado. Ulitaka
njipike nini?”
“Labda ukaange chipsi, viazi
si vipo?”
“Viazi vipo”
“Kaanga chipsi na mayai”
Baada ya kuzungumza hivyo na
Ibrahim nilitoka mle chumbanni nikaingia jikoni na kuanza kumenya viazi. Mpaka
inafika saa mbili usiku, chipsi kwa mayai ya kukaanga zikawa tayari. Ndani ya
friji kulikuwa na jagi la juisi ya matunda. Nikaenda nalo mezani.
Baada ya kuyayarisha mlo huo
nikaenda sebuleni kumuita mume wangu na shemeji zangu.
Tulikula pamoja. Baada ya kula wenzangu waliondoka na kuruidi
sebuleni, wakaniacha nikiondoa vyombo.
Muda wa kulala ulipowadia
nilimuuliza Ibrahim kama mdogo wake aliyekuja
kutoka Dar alikuwa amepata likizo kazini kwake.
“Sijamuuliza kama alipata
likizo” Ibrahim akanijibu.
Nikataka nimuulize ataondoka
lini lakini niliona swali hilo
halikuwa la msingi kumuuliza mume wangu hasa kwa kuzingatia kuwa yule alikuwa
ndugu yake.
Asubuhi ya siku iliyofuata
nilifurahi Ibrahim alipoondoka na mgeni wake. Walikwenda kunywa chai huko huko.
Walipoondoka tu nikaenda kwa
Rita.
Baada ya kusalimiana naye
aliniuliza “Vipi?”
“Mpango wangu umekwama”
nikamwambia huku nikiketi kwenye kochi.
“Kwa sababu ya huyo mgeni?”
“Na sijui ataondoka lini!”
Rita alipoona nimechukia
akanicheka na mimi nikajidai kucheka.
“Huyo mgeni siku zote haji,
anangoja nina mipango yangu ndio anakuja. Si balaa hili!”
“Pengine hatakaa sana, ni wasiwasi wako tu”
“Kama hatakaa sana ndivyo ninavyotaka”
Mgeni huyo alikaa kwetu kwa
siku nne. Usiku wa siku hiyo ya nne akaniambia kuwa kesho yake ataondoka kurudi
Dar kwani alikuja kutujulia hali tu. Nilifurahi sana aliponiambia hivyo.
Asubuhi ya siku iliyofuata
Mashaka akaondoka kurudi Dar. Nikaona sasa nitumie ile nafasi kufanya ile dawa
yangu. Ilipofika jioni nilijaza maji kwenye ndoo zote na kwenye mabeseni kisha
nikaenda kufunga mita ya maji.
Mume wangu alipokuja
nikatangulia kumwambia kuwa maji yalikuwa yamekatika.
“Yamekatika saa ngapi?” akaniuliza.
“Hivi jioni”
“Sasa tutaoga nini?”
“Niliwahi kuchota. Nimejaza
ndoo zote”
“Oh! Umefanya vizuri sana”
Ilipofika usiku yeye alikuwa
wa kwanza kwenda kuoga. Aliponiambia nimtayarishie maji, nikaenda kukichukua
kipakiti kimoja kati ya vile viwili nilivyopewa na mganga, nikachota ile dawa
na kuitia mara tatu kwenye ndoo kama
alivyoniagiza yule mganga.
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment