SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
YAMENIKUTA SALMA MIE 10 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Freys Coach ifanyayo safari zake Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku, kwa mawasiliano 0622 292990
ILIPOISHIA
Baada ya kusalimiana naye
aliniuliza “Vipi?”
“Mpango wangu umekwama”
nikamwambia huku nikiketi kwenye kochi.
“Kwa sababu ya huyo mgeni?”
“Na sijui ataondoka lini!”
Rita alipoona nimechukia
akanicheka na mimi nikajidai kucheka.
“Huyo mgeni siku zote haji,
anangoja nina mipango yangu ndio anakuja. Si balaa hili!”
“Pengine hatakaa sana, ni wasiwasi wako tu”
“Kama hatakaa sana ndivyo ninavyotaka”
Mgeni huyo alikaa kwetu kwa
siku nne. Usiku wa siku hiyo ya nne akaniambia kuwa kesho yake ataondoka kurudi
Dar kwani alikuja kutujulia hali tu. Nilifurahi sana aliponiambia hivyo.
Asubuhi ya siku iliyofuata
Mashaka akaondoka kurudi Dar. Nikaona sasa nitumie ile nafasi kufanya ile dawa
yangu. Ilipofika jioni nilijaza maji kwenye ndoo zote na kwenye mabeseni kisha
nikaenda kufunga mita ya maji.
Mume wangu alipokuja
nikatangulia kumwambia kuwa maji yalikuwa yamekatika.
“Yamekatika saa ngapi?”
akaniuliza.
“Hivi jioni”
“Sasa tutaoga nini?”
“Niliwahi kuchota. Nimejaza
ndoo zote”
“Oh! Umefanya vizuri sana”
Ilipofika usiku yeye alikuwa
wa kwanza kwenda kuoga. Aliponiambia nimtayarishie maji, nikaenda kukichukua
kipakiti kimoja kati ya vile viwili nilivyopewa na mganga, nikachota ile dawa
na kuitia mara tatu kwenye ndoo kama
alivyoniagiza yule mganga.
SASA ENDELEA
Nilipoona bado ilikuwa
ikielea juu ya maji, nilitia mkono wangu nikatibuatibu yale maji, ile dawa
ikapotea.
Wakati mume wangu anaoga
nilikuwa nikitayarisha chakula mezani, ile dawa nyingine nikaitia kwenye wali
upande ule ambao nitamtilia yeye kwenye sahani.
Baada ya kuoga mume wangu
alikuja mezani. Mara tu alipoketi kwenye kiti nilimsikia akisema.
“Mbona kichwa kinaniuma
halafu macho yanniwasha?”
Akawa anayafikicha fikicha
macho yake.
“Hicho kichwa kimekuanza saa
ngapi?” nikamuuliza.
“Kimenianza wakati huu huu”
“Basi kula chakula halafu ule
dawa”
Hapo hapo nikamuona akitikisa
kichwa na kutazama kila upande kwa haraka haraka kabla ya kuniambia.
“Haa! Mke wangu macho yangu
yamefunga kiza, sioni kitu!”
“Huoni kitu kwa sababu gani?”
nikamuuliza.
“Sijui” akaniambia huku
akijitahidi kuyafumba macho yake na kuyafumbua.
“Au ni kwa sababu ya hicho
kichwa ulichosema kinakuuma?”
“Kichwa hakiwezi kusababisha
macho yasione kabisa. Mimi sioni kabisa”
Wakati akisema Ibrahim
alikuwa akiyaangaza macho yake kila upande kutafuta mwanga.
“Mke wangu nimepofuka macho!”
akaniambia kwa sauti iliyotia huruma.
Nikaguna. Maelezo hayo
yalikuwa yamenishangaza.
“Hebu nitazame nione macho
yako” nikamwambia.
Mume wangu akageuza uso wake
upande wangu. Macho yake yalikuwa ni mazima lakini yalionesha wazi kuwa
hayakuwa yakiona kitu.
“Huoni kabisa?” nikamuuliza.
“Sioni”
“Mbona macho yako ni mazima
na yako kama kawaida?”
“Sasa sijui kilichonitokea.
Hii hali nimeiona baada ya kumaliza kuoga”
Isijekuwa ni ile dawa
niliyomtilia kwenye maji aliyooga ndiyo iliyompofua macho mume wangu? Nikajiuliza
kimoyomoyo.
Wakati nikijiuliza hivyo
Ibrahim alikuwa akijitahidi kuyafikicha macho yake huku akijaribu kutazama bila
mafanikio.
“Sijui ni kitu gani
kimenitokea jamani?” akajisemea peke
yake.
“Hebu nisubiri hapo hapo”
nikamwambia na kuinuka.
Niliingia chumbani nikiwa
nimekishika kile kipakiti cha dawa
niliyomtilia kwenye chakula. Nikakitazama vizuri. Hapo hapo niligundua
kuwa nilikuwa nimechanganya zile dawa. Ile dawa niliyoambiwa nimtilie kwenye
chakula ndiyo niliyomtilia kwenye maji ya kuoga na ile niliyoambiwa nimtilie
kwenye maji ya kuoga nilimtilia kwenye chakula.
Sasa nikajiuliza ile dawa
ndiyo iliyompofua macho Ibrahim kwa sababau niliitumia kinyume na
nilivyoagizwa?
Nikamsikia Ibrahim akiniita.
Nikatoka mle chumbani na
kumfuata pale kwenye meza.
Ibrahim alinigundua kuwa
nimefika kwa kunipapasa.
“Bado huoni kabisa”
nikamuuliza.
“Sioni, naona kiza kitupu.
Yuko wapi Zacharia?”
“Nafikiri yuko nje”
“Hebu muite”
Nikatoka nje na kumuita Zacharia
mdogo wake. Zacharia alinifuata mezani akijua nimemuitia chakula.
“Huyu hapa” nikamwambia
ibrahim.
“Zacharia!” Ibrahim akamuita.
Zacharia mwenyewe alishituka
kuitwa na kaka yake kwa sauti kubwa akiwa yuko karibu naye kabisa.
“Ndiyo kaka”
“Nilikuwa nimekwenda kuoga,
sasa natoka bafuni nije hapa nikaona kichwa kinaniuma. Mpaka nafika hapa macho yangu yakazima kabisa. Hivi
tunavyozungumza sioni kabisa”
“Alah! Huoni kabisa” Zacharia
akamuuliza kwa mshangao.
“Sioni. Tangu muda huo
nilikuwa namueleza shemeji yako kuwa sioni”
“Ina maana ni macho yenyewe
tu hayaoni au kuna sababu?”
“Sijui”
Zacharia akaguna.
“Isije kuwa nina presha, kwa
maana kichwa kilianza kuniuma?’
“Labda ni presha” nikaitilia
nguvu hoja ya presha.
“Basi twende tukapime. Kama ni presha upate tiba yake”
“Subiri nikavae twende”
Ibrahim alisema huku akijitahidi kuinuka kwenye kiti.
Nilimshika mkono nikamuongoza
kuelekea chumbani. Tulipokuwa chumbani nilimvua saruni aliyokuwa amejifunga
nikampa suruali na shati. Alipovaa nilimwambia achukue pesa za hospitali.
Akafungua kabati na kupapasa
kabla ya kuukamata mkoba wake ambao huweka pesa.
“Hebu nitolee shilingi laki
moja” akaniambia huku akinipa ule mkoba.
Niliuchukua nikaufungua.
Ndani ya mkoba huo mlikuwa na vitita vya noti ambavyo hesabu yake alikuwa
akiijua mwenyewe. Pesa hizo ndizo alizokuwa akizizungusha kwenye baishara yake.
Nilihesabu shilingi laki moja
nikampa. Hakugundua kuwa ninampa pesa hizo mpaka nilipozigusisha kwenye mkono
wake. Akazipokea na kuzitia mfukoni.
Niliurudisha ule mkoba kwenye
kabati kisha nikatoka naye.
“Zacharia uko wapi?” akauliza
mara tu tulipotoka chumbani.
“Niko hapa” Zacharia
aliyekuwa amekaa kwenye meza alimjibu.
“Njoo unishike mkono twende,
nafikiri hii itakuwa ni presha” Ibrahim akamwambia kisha akakumbuka kitu.
“Hebu tutolee ufunguo wa
gari, nimeusahau” akaniambia.
Nikarudi chumabni na kuchukua
funguo ya gari nikampa Zacharia.
“Gari utaendesha wewe”
nikamwambia.
“Itabidi”
Zacharia akamshika kaka yake
mkono wakatoka.
Nilipobaki peke yangu mle
ndani nilikwenda ikata ile sehemu ya chakula niliyoitia ile dawa kwa ajili ya
Ibrahim, nikaenda kuimwaga kwenye pipa.
Nilihofia kwamba huenda
Ibrahim akirudi kutoka hospitali atataka kula. Nilikuwa sitaki ale ile dawa
ambayo ilikuwa ni ya kuoga.
Yasije yakatokea mengine,
nikajiambia.
Nikataka nimpigie simu Rita
nimwambie, lakini niliogopa kutoa ile siri kwamba mume wangu amepofuka macho
kwa sababu ya ushirikina wangu.
Lakini nilipanga kwamba kila
itakavyokuwa kesho yake niende kwa yule mganga nimueleze hali iliyotokea,
pengine angeweza kuwa na ufumbuzi.
Kwa upande mwingine nilijipa
moyo kwamba huenda dawa ile aliyooga siyo iliyomfanya mume wangu asione bali ni
presha kama mwenyewe alivyokuwa anahisi.
Niliomba Mungu iwe ni presha
kweli. Kama itakuwa si presha itakuwa ni ile
dawa, nilijiambia.
Ilipita karibu saa nzima,
nikampigia simu Zacharia. Zacharia alipopokea simu nikamuuliza.
“Enhe mmefika hospitali?”
ITAENDELEA Kesho usikose hapahapa tangakumekuchablob
|
No comments:
Post a Comment