HADITHI inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria ya Freys inafanyayo safari zake Tanga, Moshi, Arusha , Babati hadi Singida kila siku, Freys hufanya safari zake kama hivyo Singida kila siku. Tanga ofisi zake zipo Tanga barabara ya 12, simu 0622 292990
YAMENIKUTA SALMA MIE 7
ILIPOISHIA
Alipoondoka na mdogo wake
nikaenda bafuni kuoga. Nilipomaliza nilivaa. Nikaenda kuketi sebuleni kwangu kusubiri
Rita anipigie simu.
Nilipoona kimya na muda
unakwenda nikampigia mimi.
“Shoga habari ya asubuhi?”
nikamuuliza alipopokea sim.
“Nzuri shoga, mume wangu ndio
ameondoka sasa hivi. Nilikuwa nataka kukupigia kukwambia jitayarishe”
“Nimeshajitayarisha shoga”
“Basi njoo, mimi najiandaa”
Nikarudi chumbani kwangu
kuchukua baibui langu nikalivaa na kupachika mkoba wangu begani, nikatoka.
SASA ENDELEA
Nilifunga mlango wangu wa
mbele kwa funguo nikaenda nyumbani kwa jirani yangu.
Aliniacha sebuleni kwa karibu
nusu saa kisha naye akatoka na kuniambia.
“Twenzetu”
Tulikwenda nyuma ya nyumba
yake akafungua geti na kulitoa gari.
“Wewe jipakie kabisa, mimi
nafunga geti” akaniambia na kurudi kwenye geti.
Aliingia ndani akalifunga
geti hilo kisha
akazunguka kwa mlango wa mbele.
Alifunga mlango na kuja
kwenye gari. Wakati huo nilikuwa nimeshajipakia nikiwa kando ya siti ya dereva.
Akafungua mlango na kujipakia.
“Sasa twenzetu” akaniambia
huku akiliwasha gari.
Alilirudisha gari kinyume
nyume hadi barabarani. Akaligeuza na tukaanza safari yetu.
“Kinachonikera kwa yule
mganga ni foleni ya watu, yaani ukifika unakuta msururu wa watu wanaomsubiri”
Shoga yangu aliniambia wakati gari likiwa katika mwendo.
“Yeye mwenyewe anakuwa wapi”
nikamuuliza.
“Anakuwepo ila wale watu
wanafika kabla mwenyewe hajaamka. Wanamsubiri hapo nje mpaka aamke, aoge, anywe
chai, unakuta foleni inakuwa ndefu”
“Sasa tutafanyaje shoga,
tutawahi kurudi mapema kweli?”
“Tujaribu kubahatisha,
tunaweza tusikute foleni ndefu. Kuna siku niliwahi kuja sikukuta mtu yeyote
lakini kuna siku nilikuta foleni iliyonikatisha tamaa”
“Ukafanyaje?”
“Ilinibidi nisubiri hivyi
hivyo. Mpaka nashughulikiwa ilikuwa imeshafika saa sita’mchana. Lakini
nashukuru mambo yangu yalikwenda vizuri”
“Kama tutakuta foleni ndefu utaniacha
niendelee kusubiri, hata kama nitaondoka jioni
si kitu”
Dakika chache baadaye tukawa
tumefika katika eneo hilo
la Kisosora. Nyumba ya mganga huyo ilikuwa kibanda kidogo kilichojengwa kwa
miti na udongo. Mbele ya kibanda hicho kulikuwa na nyumba kubwa ya matofali
iliyokuwa haijakalmilika.
Tuliacha gari mbele ya ile
nyumba tukaingia uani. Tulikuta watu ambao hawakuzidi kumi waliokuwa wameketi
kwenye baraza ya kibanda hicho.
“Leo hakuna watu wengi, ni
wale wachache tu” Rita akaniambia.
“Mbona hawajapanga foleni’
nikamuuliza.
“kila mtu anajijua ni wa
ngapi kuingia. Sisi ndio tutakuwa watu wa mwisho. Labda waje wengine nyuma
yetu”
Na sisi tukaenda kwnye ile
baraza. Tuliwasalimia watu tuliowakuta kisha tukakaa.
Wakati tunakaa, mtu mmoja
akatoka ndani ya kile kibanda. Alikuwa ni mteja aliyekwishahudumiwa. Mtu
mwingine akaingia.
Baada ya nusu saa mtu huyo
naye akatoka akaingia mwingine. Yule aliyeingia hakukaa sana, akatoka na kuingia mwingine.
Kitu kilichonipa moyo ni kuwa
foleni ilikuwa ikienda kwa haraka.
Ilikuwa inakaribia kuwa saa
nne na nusu, mimi na Rita tulipoingia.
Mganga mwenyewe alikuwa mzee
aliyekuwa amejifunga kaniki. Chumba chake hakikuwa na mwanaga wa kutosha
kutokana na kuwa na dirisha dogo. Tulipoingia tu nilianza kusikia joto.
“Karibuni” Mganga huyo
akatuambia.
Alikuwa amekaa kwenye jamvi
lililoenea chumba kizima.
Tukakaa kwenye jamvi mbele
yake.
“Shikamoo” Rita akamwamkia na
mimi nikamwammkia.
“Marahaba hamjambo”
“Hatujambo. Naona kama
umenisahau” Rita akamwambia.
Mganga akamtazama vizuri.
“Kama
nakukumbuka”
“Mimi ni Rita. Niliwahi kuja
ukanishughulikia matatizo ya mume wangu”
“Ahaa! Nimekukumbuka.
Uliniambia unaishi Usagara”
“Haswaa! Ni kweli
umenikumbuka”
“Muda mrefu umepita sijakuona
ndio maana nimekusahahu kidogo. Habari za siku?’
“Nzuri. Nimekuletea huyu
mteja, ni rafiki yangu”
“Ana matatizo gani”
“Atakueleza”
Nikataka kumpima yule mganga
kujua uwezo wake.
“Shida yangu nataka
unitazamie ramli?” nikamwambia.
“Hapa ramli ndio nyumbani
kwake, nipe mkono wako” Mganga akaniambia huku akininyooshea mkono wake.
Nikanyoosha mkono wangu na
kumpa. Akaushika na kutazama kiganja changu.
“Huu mstari wa maisha
unaonesha kuwa una tatizo na mume wako. Maisha yako hayaendi vizuri’ Mgaga
akaniambia kisha akanitazama na kuniuliza.
“Kweli au uongo?”
“Ni kweli” nikamjibu.
“Enhe. Matatizo ya mume wako
hayatofautiani sana
na matatizo aliyokuwa nayo mume wa mwenzako. Kweli au uongo?”
“Ni kweli”
“Enhe. Mwanamme pesa anapata
lakini hazionekani. Ugomvi hawishi nyumbani. Kweli au uongo”
“Ni kweli”
“Yaani ni sawa na kusema kuwa
mapenzi hayapo nyumbani. Si kama ilivyokuwa wakati mnaanza sasa maisha. Kweli,
uongo”
“Ni kweli”
Sasa mama una wasiwasi,
unahisi kama mko wengi. Kweli, uongo’
“Ni kweli”
“Alama za kiganja chako
zinanionesha kuwa mumeo ana nyumba ndogo iliyoharibu akili yake”
Hapo hapo nikamtazama Rita kwa mshangao.
“Unasikia maneno hayo. Mimi
nilikwambia utaambiwa kila kitu” Rita akaniambia.
“Yaani mume wangu ana
mwanamke wa nje?” nikamuuliza mganga huyo kwa taharuki.
“Wewe unadhani ni kitu gani
kimeharibu tabia yake?’
“Huyo msichana ndio
amemuharibu?”
“Yaani ndio anampenda kuliko
wewe”
Nikatingisha kichwa changu
kumkubalia.
“Asante kwa kunifahamisha, sasa na
mimi nataka kumkomoa. Nataka amuache huyo mwanamke anipende mimi peke yangu, anijali na kunisikiliza, Kila
ninachomwambia atii”
“Hata kama utataka akununulie
gari atakununulia”
“Nifanyie hiyo kazi,
utahitaji shilingi ngapi?’
“Kwa vile umeletwa na mteja
wangu wa siku nyingi, nitakufanyia shilingi laki moja”
Nikaguna na kumtazama Rita.
Sikuwa nimechukua shilingi
laki moja. Nilikuwa na shilingi elfu hamsini tu kwenye pochi yangu.
“Unajua shoga nilifanya
ujinga nilipoondoka nyumbani, nilichukua shilingi elfu hamsini tu”
“Sasa mimi nitakutolee elfu
hamsini, tukifika nyumbani unirudishie”
“Sawa shoga, nitakurudishia”
Rita akafungua pochi yake na
kutoa shilingi elfu hamsini na mimi nikatoa kiasi kama
hicho kutoka kwenye pochi yangu. Tukampa yule mganga.
“Anaitwa nani mumeo?” Mganga
akaniuliza baada ya kupokea zile pesa.
“Anaitwa Ibrahim Amour”
ITAENDELEA kesho usikupite uhondo huu nini kitatokea pale kwa mganga kabla hawajaondoka na baada ya kuondoka huko mbele
No comments:
Post a Comment