HADITHI Inaletwa kwenu kwa hisani kubwa na Kampuni ya Usafirisji abiria kutokea Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku na pia kutokea Singida kuja Tanga kila siku 0622 292990
NDOA YA SALMA 3
ILIPOISHIA
Nilimuandikia namba yangu ya simu na kumuachia. Kwa vile yeye
hakuwa na simu, sikuwa na haja ya kuomba namba yake.
Baada ya hapo nilitoa
shilingi elfu hamsini nikampa.
“Hizi zitakusaidia kwa
matumizi madogo madogo ukiwa hapa hospitalini” nikamwambia.
Msichana alipokea pesa hizo
na kunishukuru.
“Asante kaka”
Yule muufuzi aliondoka na
kutuacha.
“Hivi kaka ile baskeli
niliyokuwa naendesha uliiona?”
“Baskeli yako itakuwa
imechukuliwa na polisi. Ukitoka hapa unaweza kuifuata kituo cha polisi cha
Mabawa”
“Asante kaka”
Baada ya hapo niliagana na
yule msichana. Nilimuahidi kumtembelea tena siku itakayofuata.
Wakati natoka nje ya
hospitali niliona polisi wa usalama barabarani wakisimamisha gari lao. Nikajua
walikuwa wamemtembelea yule msichana.
Nikajipakia kwenye gari langu
na kuondoka.
SASA ENDELEA
Zilipita siku tatu, sikufika
kule hospitali kutokana na kubanwa na majukumu yangu. Siku ya nne yake nikafika
kumjulia hali yule msichana.
Lakini nilikuta kitanda
kikiwa na mgonjwa mwingine. Kulikuwa na
muuguzi aliyekuwa akimpa dawa mgonjwa huyo.
Nikawasalimia wote wawili
kisha nikamuuliza yule muuguzi kuhusu yule majeruhi wa ajali ya gari.
“Unamuulizia Salma?” Muuguzi
huyo akaniuliza lakini kabla sijamjibu akaniambia.
“Salma alishapewa ruhusa
tangu jana”
“Kumbe…!”
Nikaduwaa kidogo kisha
nikamuaga muuguzi huyo na kuondoka.
“Kama
amepata nafuu ndivyo nilivyokuwa ninamuombea” nikajiambia huku nikijipakia
kwenye gari langu.
Nililiwasha moto na kuondoka.
Ikapita wiki nzima. Nilikuwa
ninaendesha gari langu nikitokea gereza la Maweni ambako nilikwenda kuchukua
hundi ya malipo yangu, simu yangu iliyokuwa kwenye mfuko wa shati langu
ilipoita.
Nilitumia mkono wangu wa
kushoto kuitoa na kutazama namba iliyokuwa inanipigia. Sikuweza kuitambua.
Ilikuwa namba ngeni.
Nikajiuliza haraka haraka ni
nani? Sikupata jibu. Nikabonyeza kiwambo cha kupokelea na kuiweka simu karibu
na sikio.
“Hello!”
“Hello! Bila shaka nazungumza
na Ibrahim Amour?” Sauti laini ya kike ikaniuliza kwenye simu.
Nikajikuta nazungusha akili
yangu kujiuliza alikuwa nani.
“Ndiye mimi, nani mwenzangu?”
nikamjibu.
“Naitwa Salma Aboud!”
Kusema kweli moyo wangu
ulishituka.
Hapo hapo nikamkumbuka
msichana aliyekuwa amegongwa na gari wiki moja iliyopita.
“Wewe ndiye yule msichana
uliyepata ajali?” nikamuuliza.
“Ndiye mimi. Nilishapewa
ruhusa hospitali, samahani kwa kuchelewa kukujulisha. Najua huenda
ilikusababishia usumbufu kidogo…”
“Ni kweli, nilifika hospitali
nikaambiwa kuwa uliondoka jana yake. Vipi hali yako?”
“Kwa sasa sijambo kidogo”
“Unaendelea vizuri?”
“Nashukuru Mungu, ninaendelea
vizuri”
“Nakumbuka uliniambia unaishi Chumbageni, ndipo ulipo
hivi sasa?”
“Ndiyo niko nyumbani
Chumbageni”
“Ile baskeli yako uliipata?”
“Sijakwenda kituo cha polisi
kuifuatilia”
“Natumaini itakuwa bado iko. Siku
ukipata nafasi unaweza kwenda kuichukua”
“Sawa kaka. Asante. Kwa mara nyingine
nakushukuru sana
kwa msaada wako. Ukipata nafasi unaweza kunitembelea nyumbani, mama yangu
atafurahi sana
atakapokuona. Nilimueleza jinsi ulivyonisaidia”
“Vizuri. Nitatafuta siku ya
kuja kukuona”
“Sawa. Asante sana
kaka”
“Asante”
Msichana akakata simu.
Nikairudisha simu mfukoni..
“Salma bado ananikumbuka”
nikajiambia kimoyomoyo wakati nikikata kona kuelekea benki.
Siku zikaendelea kupita.
Kulikuwa na siku nilikuwa nikiendesha
gari langu mitaa ya Chumbageni. Kulikuwa na jamaa niliyekuwa nimemfuata. Sasa
wakati narudi ofisini kwangu nikamkumbuka Salma ambaye aliniambia alikuwa
anaishi Chumbage. Nikaliegesha gari langu pembeni mwa barabara kisha nikatoa
simu yangu na kumpigia.
“Hello Salama!” nikasema mara
tu simu ilipopokelewa.
“Kaka Ibrahim. Nimefurahi
kuwa leo umenipigia”
“Niko maeneo ya Chumbageni,
nataka nikujulie hali?”
“Oh! Uko upande upi?”
‘Niko hapa karibu na shule ya
chekechea”
Salma akanielekeza
nyumba yao ilipo. Haikuwa mbali sana na pale. Nikafika.
Nilishuka kwenye gari.
Nilimkuta amesimama mlangoni akinisubiri.
“Oh karibu” alliniambia huku
akitabasamu.
Nilikwenda kwenye mlango,
Salma akanikaribisha ndani.
Nilipita ndani. Upande wa
kushoto wa nyumba hiyo kulikuwa na sebule pana iliyokuwa imepambwa vizuri.
“Karibu ukae” Salma
akaniambia. Tabasamu lilikuwa likiendelea kuchanua usoni kwake.
Nikakaa kwenye kochi mojawapo.
“Ngoja nimuite mama, anataka
kukuona”
Salma aliingia ndani.
Nikabaki nikiyazungusha macho yangu kwenye sebule hiyo.
Punde tu Salama alirudi akiwa
amefuatana na mwanamke mmoja. Kwa mimi mwenyewe nisingeweza kuamini kama yule alikuwa ni mama yake kwani alionekana bado
msichana. Na walionekana kama mtu na mdogo
wake.
“Mama yule kaka aliyenisaidia
siku ile kunipeleka hospitali na kunitolea damu ndiye huyu hapa” Salama
alimwambia mama yake.
“Baba unajisikiaje hali
yako?” Mama huyo akaniuliza kwa furaha.
“Sijambo mama. Shikamoo”
“Marahaba. Habari za siku”
“Ni nzuri, sijui nyinyi hapa”
“Sisi hatujambo. Tunashukuru
Mungu”
“Kaka Ibrahim, huyu ndiye
mama yangu” salma akaniambia huku akiketi.
“Nimefurahi kumuona”
“Leo umeamua kututembelea…”
mwanamke huyo aliendelea kuniambia. Alikuwa bado amesimama na hakuonesha dalili
yoyote kuwa angeketi.
Baada ya kuulizana naye hali akatuambia.
“Haya endeleeni kuzungumza,
mimi niko huko uani nina kazi kidogo”
“Asante,
hata hivyo sitakaa sana.
Nimekuja mara moja tu kumjulia hali
mgonjwa wangu kisha nitaondoka”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment