HADITHI SEHEMU YA 5
Hadithi hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria Freys Coach ifanya safari zake kuanzia Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku, Ofisi za Freys Tanga zipo barabara ya 12 Ngamiani Stend ya zamani ya Mikoani, simu 0622 292990
HADITHI
YAMENIKUTA SALMMA MIE 5
ILIPOISHIA
Baada ya sheikh kutuombea dua
hiyo, sherehe za ndoa yetu zikaendelea hadi usiku wa manane. Lakini mimi na
Ibrahim tuliondoka mapema kwenda nyumbani kwake Usagara.
Usiku wa siku ile ndio kwa
mara ya kwanza, mimi nilimjua Ibrahim na yeye alinijua mimi kwa maana kwamba
ndio tulikutana kwenye sita kwa sita.
Baada ya kitendo hicho cha
siku ya kwanza, ndio nilimpenda zaidi Ibrahim na naamini hata yeye alinipenda
zaidi.
Ibrahim na mimi tukawa
tumefungua ukurasa mpya wa maisha.
Maisha ya siku za mwanzo
mwanzo yalikuwa ya upendo sana.
Ibrahim akitoka katika shughuli zake hurudi nyumbani. Kadhalika na mimi sikuwa
mtu wa kutoka toka wala wa kwenda kwa majirani.
Na hilo ni funzo nililolipata
kwa kungwi wangu kuwa nikiwa kwa mume wangu niachane na safari zisizokuwa na
msingi na pia niepukane na mashoga na majirani wasio wazuri.
SASA ENDELEA
Jirani yangu mmoja wa nyumba
tuliyopakana nayo upande wa kushoto alihama nyumba, akaja mpangaji mwingine,
mtu mmoja na mke wake.
Huyo mwanaume alikuwa mtu
mzima kidogo, alifikia umri wa miaka hamsini wakati mke wake alikuwa bado
msichana ila alikuwa amenizidi mimi kidogo kwa umri.
Baada ya kuishi na majirani
hao kwa mwezi mmoja nikajikuta nimependa staili yao ya maisha. Kila mmoja wao alikuwa na
gari. Mume mtu alikuwa na gari lake
na mke naye alikuwa na
gari lake.
Aliyekuwa akifanya kazi ni
mume, mke alikuwa yuko nyumbani tu wakati wote. Lile gari alikuwa akilitumia
kwenda sokoni au kwenda safari zake nyingine.
Mwanaume huyo anapoondoka nyumbani
asubuhi hurudi jioni na anaporudi huwa hatoki tena. Vicheko vyao wakati wa
usiku vilikuwa vikisikika hadi ndani kwetu.
Taratibu nilijikuta
nikizooeana na mke wa huyo jamaa.
Kulikuwa na siku kulikuwa na
tatizo la kukatika maji. Msichana huyo
akaja nyumbani kwangu asubuhi na kubisha mlango.
Niliposikia mlango unabishwa
nilikwenda kuufungua nikamkuta amesimama mbele ya mlango.
“Mmeamkaje jamani?”
akanisalimia.
“Hatujambo, sijui wewe”
nikamjibu.
“Samahani jirani yangu,
nataka kukuuliza huku kwenu maji yanotoka?”
“Hayatoki” nikamjibu na
kuongeza.
“Yalikatika tangu jana usiku”
“Basi mwenzako sina habari
kuwa maji yamekatika, nafungua bomba nakuta tupu. Mume wangu anataka ajimwagie
aende kazini. Hukuweka akiba kidogo ukanigaia”
“Nina tenki la juu, huwa
naweka akiba ya maji. Maji yanapokatika sipati taabu”
“Mh mwenzangu umenizindua.
Nitamwambia mume wangu naye anunue”
“Sasa lete ndoo uje umchotee”
“Asante jirani, ngoja nikachukue
ndoo”
Msichana huyo aliondoka.
Nilifunga mlango nikaenda kufungua mlango wa uani na kumsubiri.
Alipotokea nikamuita.
“Njoo kwenye mlango huu”
Msichana huyo akaingia katika
mlango huo wa uani. Nilikwenda naye kwenye bomba nikamwambia aweke ndoo yake.
Nikamfungulia maji.
Ndoo yake ilipojaa
akaniambia.
“Unanipa ndoo hii moja au
nije unipe ya pili, kwa maana hii ataoga mume wangu, bado mimi sasa…”
“Na ya kupikia je…?”
nikamuuliza.
“Hapo sasa!”
Tukacheka.
“Nakwambia hawa watu wa idara
ya maji nao watatupa shida!” akaniambia.
“Njoo uchote shoga yangu
usijali, leo kwangu kesho kwako”
“Ngoja nipeleke hii kwanza…”
Msichana huyo alibeba ile
ndoo akatoka. Niliingia ndani nikaendelea na shughuli zangu. Punde tu
nikamsikia akiniita.
“Jirani nimerudi!”
“Chota tu, nina kazi kidogo”
nikamwambia.
“Asante jirani”
Niliendelea na kazi zangu.
Baadaye nikamsikia tena.
“Nachota hii ya tatu”
“Chota tu” nikamwambia.
Alipomaliza kuchota
aliniambia.
“Haya jirani asante,
nakwenza zangu”
“Haya jirani”
Kutoka siku ile ndipo nilipoanza
urafiki na jirani yangu huyo. Alikuwa akija nyumbani kwangu kuzungumza na
wakati mwingine mimi nilikuwa nakwenda nyumbani kwake. Nikalifahamu jina lake.
Alikuwa anaitwa Rita..
Rita akawa rafiki yangu
mkubwa, tukafikia hadi kuazimana nguo na vitu vingine na pia tulipeana siri
zetu za ndani.
Kutokana na urafiki wetu huo
niliweza kugundua kuwa maisha aliyokuwa akiishi Rita na mume wake hayakuwa kama maisha niliyokuwa ninaishi mimi na mume wangu.
Wenzetu walikuwa wanaishi
maisha ya hali ya juu na ya kifahari. Rita alikuwa akiniambia kila kitu
alichohitaji, mume wake alikuwa akimtimizia. Alihitaji gari akamnunulia. Na
wakati ule tunaanza kufahamiana alikuwa akimjengea nyumba maeneo ya Kange.
“Mume wangu si mgumu,
ananisililiza na kunijali” Rita aliniambia na kuongeza.
“Kila ninachohitaji
ananipatia”
“Basi una raha shoga yangu.
Umepata mume mzuri. Wangu mimi ukitaka kitu mpaka kwa mbinde”
“Lakini hata huyu wangu
aliponioa alikuwa hivyohivyo, nilifanya kumtengeneza”
Nikashituka.
“Ulimtengenezaje shoga?”
“Nilimuendea kwa mganga
nikamlisha madawa mpaka yakamkolea”
“Wacha shoga!. Kumbe kuna
madawa yanayoweza kubadili tabia ya mwanaume?”
“Yapo. Si unamuona mume wangu
alivyo. Sasa nakwambia hakuwa hivi! Kuninunulia nguo ilikuwa ni mpaka
tugombane”
“Wangu mimi hatugombani, ni
mgumu tu. Kila siku yeye hana pesa lakini biashara anafanya. Sijui pesa zake
zinakwenda wapi!”
“Basi ana mwanamke nje, ndiye
anayemla. Mwenzangu wala chuya, mchele waliwa na mwenzio!”
Rita aliponiambia hivyo
alinicheka na mimi nikajidai kucheka lakini moyo wangu ulipata fadhaa sana nilipohisi kuwa inaweza
kuwa ni kweli mume wangu akawa na msichana
wa nje anayekula pesa zake.
Siku ile niliwaza sana yale maneno
aliyoniambia shoga yangu.
Mume wangu aliporudi jioni
nilijaribu kumwambia.
“Mume wangu huninunulii hata
pikipiki na mimi”
“Unataka pikipiki ya nini mke
wangu?”
“Pikipiki ya nini? Watu
wananunuliwa magari, wewe unasema pikipiki ya nini?”
“Kama
ni gari si hili tunalo”
“Hilo ni la kwako. Mimi nataka pikipiki”
“Tuombe Mungu, kazi zangu
zikienda vizuri nitakununulia”
“Utaninunulia lini?”
ITAENDELEA kesho na usikose uhondo huu ini kitatokea
Show details
|
No comments:
Post a Comment