HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (25)
Nikamwambia Yasmin
“Tusifungue hii chupa tuone nini kitatokea”
“Wewe achana naye, kama akitoka mwenyewe na atoke, potelea mbali!”
Nilikuwa nimesimama kando ya
lile kabati. Yasmin alisimama karibu na kitanda. Macho yetu sote yalikuwa
kwenye ile chupa.
Ingawa nilikuwa nimejikaza
kiume, hofu ilikuwa ikitambaa kwenye mishipa yangu. Yasmin hakuonesha kuwa na
hofu hata chembe. Nilishangaa kuona msichana ambaye siku zote nilimuona dhaifu,
siku ile alikuwa amejaa ujasiri usio kifani. Hapo niliamini kweli kuwa Yasmin
alikuwa amejitolea kufa kupona.
Ile sauti ya Harishi
iliyokuwa ikitoka kwenye chupa ilipotea lakini ule moshi uliendelea
kuonekana. Kwanza ulionekana moshi wa rangi nyeusi kisha ukabadilika
na kuwa wa rangi nyeupe. Baada ya muda kidogo ulibadilika tena na kuwa
wa rangi
nyeusi.
Mawazo yangu yote yalikuwa
kwenye kifo kibaya kilichokuwa kinatungoja.
. Nilijua kuwa Harishi
angekizibua mwenyewe kile kizibo na kutoka. Hapo hasira zake zisingekuwa na
kifani. Nilipata wazo la kumwambia Yasmin tukimbie lakini nikajiuliza
tutakimbilia wapi usiku ule? Na ni wapi ambapo Harishi hataweza kufika?
Muda uliendelea kupita.
Tuliona Harishi hatoki kwenye ile chupa kama
ilivyo kawaida yake. Aliendelea kututaka tukifungue kizibo kwa sauti ya upole
akiahidi kwamba hatamuua yeyote.
Nikahisi inawezekana kwamba
kitendo kile cha kuwahi kukifunga kile kizibo cha cha chupa wakati Harishi yumo
ndani ya chupa ile akiwa katika umbile la moshi, kilikuwa kimemzuia kutoka na
hakuwa na uwezo tena wa kutoka mwenyewe.
Hapo hapo nikazikumbuka
simulizi za wazee wa zamani ziizosema kwamba majini walikuwa wakifungiwa ndani
ya chupa na kutoswa baharini pindi wanapofanya makosa.
Kumbe ni kitu kinachowezekana
kweli, nikajiambia.
“Sisi tunaiondoa hii chupa!”
nikasema kwa sauti ili kusikia Harishi atajibu nini.
“Usiiondoe. Nataka
mnifungulie niende zangu” Sauti ya Harishi ikasikika kutoka kwenye ile chupa.
“Hakuna atakayekufungulia
muuaji wewe”Yasmin akamwambia.
“Nifungulie nitakurudisha
kwenu”
“Mbona siku zote
hukunirudisha?”
“Nakwambia kweli kabisa.
Ukinifungulia nitakurudisha kwenu Comoro”
“Kwenda zako, mimi si mjinga
wa kukufungulia wewe.. Bora ubaki humo humo. Siku zako zimeshafika”
Yasmin akanigeukia mimi na
kuniambia.
“Twende tukaizike hii chupa”
“Hapana.. hapana. Msiizike!”
Sauti ya Harishi ikalalamika.
“Mimi naona tukaizike
baharini” nikamwambia Yasmin.
“Hapana…hapana. Msiitose
baharini!” Ilikuwa sauti ya Harishi lakini hatukuipatiliza.
“Niliwahi kusikiakule kwetu
kwamba majini wanafungiwa kwenye chupa na kutoswa baharini” nikamwambia Yasmin.
“Tukiitosa baharini itaelea
na kisha itarudishwa ufukweni na mawimbi”
“Labda tuifunge kamba na jiwe
ili izame chini”
“Nyinyi msifanye hivyo. Mimi
nimeshwambia sitawaua. Nifungulieni niende zangu” Harishi akatuambia.
“Basi tutaifunga na jiwe
tizamishe” Yasmin akasema.
“Hamsikii hivi ninavyowambia.
Nyinyi mnataka mfe?” Sauti ya Harishi ikasikika kutoka kwenye chupa.
“Utakufa wewe, mbona huwezi
kutoka !” Yasmin akamwambia.
“Tusubiri kuche” nilimwambia
Yasmin.
“Linaweza likatoka!”
“Usiku huu hatutaweza kwenda
baharini”
“Basi tusubiri”
Tukasubiri. Harishi sasa
alikuwa amenyamaza. Sauti yake haikusikika tena. Lakini ule moshi uliendelea
kuonekana ndani ya ile chupa. Ulikuwa unabadilika rangi kila mara.
Nipoona kunaanza kupambazuka
nilijaribu kuishika ile chupa. Ilikuwa nyepesi kama
chupa tupu.
Yasmin alileta kapu.
Akaniambia tuitie kwenye kapu.
“Tutapata wapi kamba?”
nikamuuliza.
“Twende nayo, tutapata kamba
huko huko”
Tukatoka nje ya lile jumba.
Mimi ndiye niliyeshika lile kapu. Kulikuwa na baridi kali lakini tulijikaza
hivyo hivyo. Wakati tunaelekea baharini tuliokota kipande cha kamba na jiwe
tukavitia kwenye kapu.
Tulipofika ufukweni mwa bahari
tuliitoa ile kamba tukaifunga kamba kisha ile kamba tukaifunga na jiwe.
Tulimsikia Harishi akisema
maneno ndani ya ile chupa lakini sauti yake ilikuwa ya chini kiasi kwamba
hatukuelewa anasema nini.
Mimi na Yasmin tulijitosa kwenye
maji. Tukatembea kwa miguu hadi tulipofika kwenye maji mengi tukaanza kuogelea
kwenda mbali zaidi tukiwa na ile chupa tuliyoifunga jiwe.
“Tuizamishe hapa hapa” Yasmin
akaniambia.
Nikaiachia ile chupa, ikazama
ndani ya maji taratibu. Hatukuiona tena.
“Sasa turudi. Zama za Harishi zimekwisha” Yasmin akaniambia.
Tukaogelea kurudi ufukweni.
Tulipofika ufukweni nilimwambia Yasmin.
“Sidhani kama atatoka tena”
“Hawezi kutoka. Labda atokee
mtu aifungue ile chupa”
“Na huyo mtu atatokea wapi?”
“Labda wavuvi”
“Wavuvi ni watu wanaojua.
Wakiona chupa chini ya bahari hawaifungui. Na pia hakuna wavuvi wanaofika huku”
“Lakini ni kitu cha ajabu.
Ujanja wote ule alionao ameshindwa kujitoa kwenye chupa!”
“Ndio maana tunaambiwa kiumbe
hakukamilika kwa maumbile wala kwa ujuzi. Mkamilifu ni Mungu peke yake”
“Tungejua mapema tungemfungia
tangu tulipofika, tungesalimika sote”
“Hatukujua. Hata mimi
ningeweza kumfungia. Sasa nimeshajua sababu ya kunisisitiza kila siku kuwa
niweke mbali kile kizibo na nisiifunge hata siku moja”
ITAENDELEA KESHO,USIKOSE MTU WANGU NIKO TAYARI KUPOTEZA MUDA WANGU UPATE KILE UNACHOPENDA
No comments:
Post a Comment