Saturday, August 6, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 53

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 53

ILIPOISHIA

Abdi akacheka kisha hakunijibu chochote, akagonga mkono wangu na kuelekea kwenye mlango. Alikuwa kama aliyetaka  kutoka kisha akageuka na kunitazama.

“Suala lako ninalishughulikia, usijali. Nilikuahidi kukupatia gari, ungependa gari hii ninayotumia au nikupatie gari jingine”

“Wewe ndio utajua”

“Basi ngoja nikupatie leseni hapo kesho, nitakupa gari zuri”

“Sawa”

Nilipomjibu hivyo Abdi aligeka akafungua mlango na kutoka bila kuniambia chochote. Nilimchungulia kwenye dirisha nikaona akipanda gari lake na kuondoka.

Alikuwa kama aliyekwishamaliza kazi.

Niliingia katika chumba changu nikafungua kabati na kulikagua ndani. Lilikuwa tupu na safi. Nikaanza kupanga nguo zangu chache..

Nilipomaliza nilitoka nikaenda kukaa sebuleni kujipumzisha Siku ile nilishinda pale nyumbani. Saa saba mchana Abdi alikuja akanipa shilingi laki moja za kisomali kwa ajili ya matumizi yangu.

Akaniambia kwamba leseni yangu inashugulikiwa. Alinichukua kule hotelini kwake tukala chakula pamoja kisha akanirudisha nyumbani.

Saa mbili usiku alikuja tena tukaenda kula.

Siku ile nililala peke yangu katika ile nyumba. Asubuhi kulipokucha Abdi alinifuata kwa ajili ya kunipeleka kule hoteli kuanza kazi.

Tulipofika alinitambulisha kwa wafanyakazi kama meneja mpya. kuanzia siku ile. Abdi pamoja na mtu ambaye aliwekwa awe  msaidizi wangu walinitembeza katika hoteli nzima kabla ya kunikabdidhi ofisi pamoja na nyaraka zote zinanazihusu shughuli za hoteli.

Kutoka siku ile nikaanza kazi ya umeneja katika hoteli ya AL ASAD. Siku iliyofuata Abdi alinipatia leseni ya kuendesha na akanikabidhi moja ya magari yake.

SASA ENDELEA

Baada ya kuendesha kazi kwa mwezi mmoja Abdi akaniambia kuwa alikuwa ameshanitafutia mchumba.

“Ni nani?” nikamuuliza.

“Shamsa. Naona Shamsa anakufaa, au unasemaje?”

Shamsa alikuwa ni yule msichana wa kisomali aliyekuwa akifanya kazi katika ile hoteli ya Abdi niliyofikizia.

“Shamsa anafaa sana” nikamwambia.

“Yule baba yake ni msomali lakini mama yake ni mbarawa”

“Umeshazungumza naye?”

“Nimeshazungumza naye”

“Amekubali?”

“Kwanini akatae amri ya bosi wake. Kiufupi ni kuwa amekubali. Hivi leo ndio nataka kuwakutanisha mzungumze wenyewe”

“Utatukutanisha wapi?”

“Popote utakapotaka wewe”

“Anaweza kuja nyumbani ninakoishi?”

“Kwa mila za wasomali hawezi kuja nyumbani kwako ila wewe mfuate kazini kwake, gari si unayo?”

“Ndiyo gari ninato”

“Sasa wewe mfuate kazini, utakaa naye mtazungumza”

“Sasa nimwambieje?”

Nilipouliza swali hilo Abdi akacheka.

“Usicheke Abdi. Mimi sijui mila zenu huku!”

“Muulize umepata ujumbe wangu kutoka kwa Bwana Abdi. Sasa akikupa jibu ndio, mtaendeleza mazungumzo yenu”

“Sawa. Nitakwenda baadaye kidogo”

“Na mimi nitamjulisha kuwa utakwenda kuongea naye”

“Sawa”

Nilisubiri hadi nilipopunguza kazi zangu nikatoka kwa gari niliyokuwa nimepewa na abdi. Muda huo ilikuwa ikaribia kuwa saa tano.

Nilipofika nilitafuta meza nikakaa. Shamsa alishaniona akanifuata na kuketi na mimi.

“Asalaam alaykum” akanisalimia huku akinitolea tabasamu la aibu..

“Wa alayka salaam. Hujambo Shamsa?”

“Sijambo, sijui wewe”

“Mimi nashukuru sana”

Nikayakumbuka maneno ya Abdi.

“Je umepata ujumbe wangu?” nikamuuliza.

“Nimeupata”

Alponiambia hivyo nilitabasamu.

“Ndiyo nimefuata jibu”

Shamsa akanitazama kwa makini mpaka nikaona aibu. Labda alikuwa akinihakiki kama ni mume ninayeweza kumfaa.

“Mbona tulishakubaliana” akaniambia baada ya kimya cha sekunde chache..

“Mimi sielewi. Mlikubaliana nini?”

“Kwani wewe si ulikuwa unataka mchumba?”

“Ndiyo”

“Nimekubali kuwa mchumba wako”

Aliponiambia hivyo niliushika mkono wake aliokuwa ameuweka juu ya meza. Niliushika kirafiki tu kisha nikamtazama. Nilimuona alikuwa amevutiwa na kitendo changu.

“Shamsa una umri gani?” nikamuuliza.

“Miaka ishirini na mitano. Na wewe una umri gani?”

“Miaka ishirini na tisa. Ikifika mwakani mwezi wa nne nitatimiza miaka thelathini”

“Ni mwenyeji wa wapi?”

“Abdi amekwambia mimi ni mwenyeji wa wapi?”

“Sikumuuliza hivyo”

“Unaonaje kama utamuuliza yeye?”

“Kwanini nimuulize yeye wakati mwenyewe upo?”

Nikanyamaza kidogo kabla ya kumwammbia.

“Mimi natokea Tanzania”

“Wewe ni mzigua”

“Ndiyo mimi ni mzigua”

“Hata babu yangu mzaa mama alitokea huko huko zigua”

“Kwa hiyo wewe ni mzigua?”

Shamsa akacheka kidogo.

“Hapana. Babu yangu mzaa mama ndiyo alikuwa mzigua lakini mimi mwenyewe ni msomali, upande mwingine ni mbarawa”

“Mmezaliwa wangapi katika familia yenu?”

“Tulizaliwa wawili tu, mimi na dada yangu ambaye alishafariki zamani. Kwa hiyo nimebaki mimi peke yangu”

“Wazazi wako wapo?”

“Pia walishafariki. Kwa sasa hivi mtu pekee ambaye niko karibu naye ni Abdi”

“Oh Pole sana”

“Asante. Abdi ameniambia kama nitafunga ndoa na wewe, yeye ndiye atakayenisimamia kwa sababu sina ndugu”

“Nimekuelewa. Pole sana”

“Asante. Abdi ameniambia wewe ni ndugu yake, ni kweli?”

“Ni kweli”

Hapo nilisema uongo kumuunga mkono mwenyeji wangu. Abdi hakuwa ndugu yangu. Kwa vile alishamwambia  msichana huyo kuwa mimi ni ndugu yake, nikaona nikubali. Pengine Abdi alimwambia hivyo ili msichana huyo aweze kunikubali kirahisi.

“Kwa hiyo umeamua kuja kuishi hapa Somalia?” Shamsa akaniuliza.

“Ni ushauri wa Abdi, amenitaka nibaki huku”

“Ameniambia amekupa ile hoteli yake ya Al Asad?”

“Amenipa kwa maana ya kuiongoza”

“Lakini wewe si ndiye meneja wake?”

“Ndiyo”

“Sasa turudi katika mazungumzo yetu, unatarajia utanioa lini?”

“Hilo ni suala ambalo nitalipanga na Abdi. Kwa upande wangu ningependa tuoane haraka iwezekanavyo”

“Sawa”

KIJANA SASA YUKO TAYRA KWA NDOA NA MSOMALI. JE NINI KITATOKEA? JIBU NI KESHO

No comments:

Post a Comment