SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713340572
MWANAMKE 55
ILIPOISHIA
“Nakushukuru sana mke wangu kwa kunizindua. Umejibu maswali yangu mengi
niliyokuwa nikijiuliza bila kupata majibu. Ninaamini kuwa wewe ni mke wangu wa
kweli”
“Na mimi nakushukuru sana mume wangu kwa
kunisikiza na kuniamini. Wewe utakuwa mume wangu wa kudumu”
“Asante
sana”
Shamsa alitabasamu kisha
akanipiga busu kwenye shavu langu.
“Hebu niambie ilikuwaje siku
ile kwenye ile boti wakati wale jamaa walipotaka kukutosa?” akaniuliza.
Nikamueleza Shamsa
ilivyokuwa.
“Lilipotokea hilo joka na kuwazamisha
hao waliotaka kukutosa, wewe ulifikiri nini?” akaniuliza.
“Leo ndio nimepata jibu
kutoka kwako. Hilo swali nilikuwa nikijiuliza sana. Nilikuwa sijui ni
kwanini lile joka limetokea na lilitoka wapi. Kumbe ni jini linalonifuata mimi”
“Kumbe wewe siku zote
tunaishi lakini kulikuwa na kitu unanificha!”
“Kitu gani?”
“Kwamba una jini wa kike
mwenye utajiri”
“Kwa kweli niliogopa kukutia
hofu. Huyu jini mimi simtaki na amekuwa akinifanyia vituko vingi sana mpaka nimekimbia huko
kwetu…”
SASA ENDELEA
Sikutaka kumueleza mengi
kwamba jini huyo hataki nioe mke wa binaadamu, anataka nimuoe yeye.
Nilidhani Shamsa angeniuliza
ni vituko gani alivyokuwa akinifanyia huyo jini lakini hakuniuliza.
“Sasa mwenzako anamtaka huyo
jini kwa udi na uvumba” akaniambia.
“Kwa kweli kama alifikia
kumuua mke wake kwa sababu ya jini ambaye hamjui, ni mtu hatari na mshirikina
sana”
“Ile mirungi anayokula
inaharibu akili yake lakini mwenyewe hajui. Inamfanya awaze utajiri wakati
wote. Na kila apatavyo hatosheki”
“Mtu namna ile mwisho wake ni
kufa tu. Wahenga wanasema tamaa mbele mauti nyuma binaadamu katikati”
Shamsa akacheka.
“Amour umenichekesha!”
akaniambia huku akiendelea kucheka.
“Kweli kabisa. Mtu namna ile
mwisho wake ni kufa tu”
“Akifa wewe na Yusufu
mtarithi mali
zake”
“Ni mpaka aandike hivyo”
“Hata asipoandika ni lazima
mtamrithi”
“Yusufu hatakubali”
“Labda kwa hapo. Lakini kama
atamwambia kuwa wewe ni ndugu yao, unaweza
kupata sehemu ya mali
yake”
“Siwazii sana huko, mimi nawazia maisha yangu
yatakavyokwenda. Naona sitakaa sana hapa Somalia”
“Hutakaa sana utakwenda wapi?”
“Nitarudi kwetu”
“Na mimi utaniacha na nani
wakati nimeshakuwa mke wako?”
“Nitakuomba twende tukaishi Tanzania,
si utakubali?”
Shamsa akabetua mabega yake.
“Nitakubali, nitafanyaje sasa
wakati umeshanioa!”
Jibu lake lilinifurahisha
nikamvuta kwangu na kumkumbatia. Shamsa alijilegeza nikamtuliza kifuani kwangu.
Nilikuwa nikiusikia moyo wake ulivyokuwa ukipiga taratibu, pu! pu! pu!
Kwa vile aliendelea kutulia
kifuani kwangu na mimi niliendelea kumkumbatia.
Asubuhi ya siku iliyofuata
nilikwenda kazini kwangu huku nikijua kuhusu mambo kadhaa ambayo nilikuwa
siyajui.
Moja ya mambo hayo ni kuhusu
Abdi kunileta pale Somalia
kinguvu na kunipa shughuli ya kufanya.
Sasa nilijua lengo la Abdi
lilikuwa ni kumtaka jini aliyekuwa akinisumbua ili apate utajiri.
Kama ni hilo tu nisingeshituka wala nisingejali. Abdi
amekwenda mbali zaidi kutaka kuniua. Jambo hilo halikuwa la kupuuza. lakini nilimtegemea sana Shamsa aliyenidokolea
siri hiyo.
Kutokana na mpango wake huo niliamini kwamba Abdi
alikuwa mpumbavu sana.
Ushirikina wake ulikuwa ni wa hatari na si wa kupuuzwa na mtu yeyote mwenye
akili timamu.
Nilipofika kazini kwangu
niliendelea kufanya kazi huku nikiwa nimetingwa na mawazo ya mchanganyiko. Mara
kwa mara Shamsa alikuwa akinipigia simu kuniuliza jinsi nilivyokuwa ninaendelea
na kazi.
“Naendelea vizuri” nilimjibu.
“Abdi hajafika hapo?”
“Hajafika bado”
“Tafadhali usimuulize
chochote”
“Sitamuuliza kitu”
“Na wewe pia kuwa na amani.
Usiwaze sana”
“Nisiwaze nini?”
“Yale niliyokueleza jana
usiku”
“Yale hayapo tena kichwani mwangu, naendelea na kazi yangu”
“Sawa”
Nilipomaliza tu kuzungumza na
Shamsa nilimuona Abdi akiingia ofisini kwangu. Uso wake ulikuwa umetaharuki.
Kabla hata ya kunipa salamu
aliniambia.
“Watu wengine sijui wana
tabia gani?”
Jinsi nilivyouona uso wake
umetaharuki na yale maneno aliyosema, vilinishitua nikamuuliza.
“Kuna nani?”
“Si huyu mpuuzi!”
“Nani?”
“Yusufu ameondoka nyumbani
kwake tangu jana. Hajamuaga mke wake anakwenda wapi. Mke wake sasa ananisumbua
mimi!”
“Una maana kwamba tangu jana
hajafika nyumbani kwake?”
“Hajafika na hajulikani yuko
wapi”“Kwani walikuwa na ugomvi?”
“Hawakuwa na ugomvi wowote.
Yule mdogo wangu tu hana akili. Ndio maana sielewani naye”
“Sasa atakuwa amekwenda
wapi?”
“Nitajuaje?”
“Mh…!”
Pakapita kimya kifupi Abdi
akionesha kuchukizwa akaniambia.
“Nimekufuata twende kituo cha
polisi kumuulizia”
“Unadhani atakuwa
amekamatwa?” nikamuuliza.
“Si lazima awe amekamatwa,
anaweza kuwa amepata ajali na ripoti yake kufikishwa polisi”
“Haya twende”
Tukatoka mimi na Abdi.
Tulijipakia katika gari lake
na kuelekea kituo cha
polisi.
Vile tulivyokuwa
tumekaa
pamoja ndani ya gari niliyakumbuka maneno ya Shamsa kuhusiana na Abdi,
nikaona kama niliyekuwa nimekaa na nyoka mwenye sumu kali.
Tukaendelea na safari.
Nilikuwa nikimfahamu vizuri
Yusufu mdogo wake Abdi ingawa hakuwa karibu sana na mimi. Muda mwingi alikuwa
akishughulika na mambo yake mwenyewe.
Niligundua pia kuwa Abdi
hakuwa akisikizana sana
na mdogo wake jambo ambalo lilifanya mara kwa mara wakwaruzane.
Lakini ndugu ni ndugu. Licha
ya kuwepo kwa hali hiyo, Abdi alipopata habari kuwa mdogo wake alikuwa
hafahamiki alipo ameanza kupata wasiwasi na kumuhangaikia.
Tulifika kituo cha polisi
ambapo Abdi alikuwa akifahamika vizuri. Aliwaeleza polisi tatizo lake.
Polisi hao wakamfahamisha
kuwa hawakuwa na taarifa yoyote ya mdogo wake.
“Amepotea tangu lini?” Polisi
mmoja akamuuliza.
“Si kwamba amepotea bali
hajulikani yuko wapi”
“Tangu lini?”
“Tangu jana alipoondoka
nyumbani kwake hajarudi hadi sasa na hajulikani yuko wapi”
“Ana mke na watoto”
“Ndio ana mke na watoto”
“Hakuwahi kumwambia mke wake
anakwenda wapi?”
“Huyo mke wake ndiye
aliyenifahamisha mimi kuwa Yufusu hajarudi nyumbani tangu jana”
ITAENDELEA KESHO
No comments:
Post a Comment