Tangakumekuchablog
Tanga, WAZAZI
na Walezi wa watoto wenye ulemavu Tanga, wametakiwa kuacha kuwafungia ndani na
badala yake kuwapeleka shule na kuweza kupata elimu ambayo itaweza kuwasaidia
katika maisha yao mbeleni.
Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano ya kuibua vipaji vya
kuchora na kutunga mashairi jana, Afisa Utamaduni jiji la Tanga, Rose Sempoli,
alisema kuna baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwafungia ndani.
Alisema kitendo hicho kinawanyima
haki ya kupata elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao mbeleni hivyo
kutakiwa kuacha tabia hiyo na kuwataka kuwapeleka katika vituo vya walemavu na
kuwapeleka shule.
“Kuwa na ulemavu sio dhambi wala
vibaya kwani ni maumbile ya kibinadamu ambapo mtu yoyote anaweza kuupata katika
maisha yake, kwa pamoja tukomeshe vitendo vya ufungiaji wa watoto ndani”
alisema Sempoli na kuongeza
“Jamii hii wako na vipaji wakati
mwengine zaidi ya wengine hivyo kuwafungia ndani kwa ulemavu wao ni kuwakatili
na kuwaharibia maisha yao ya mbeleni” alisema
Aliitaka jamii kwa pamoja kushirikiana na kuwaibua
watu wanaowafungia ndani watoto wenye ulemavu na kusema kuwa anaamini ziko
familia ambazo zimewafungiia ndani watoto hao hivyo kutakiwa kuwaibua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Baraza la Watoto wenye Ulemavu kituo cha Watoto (YDPC) Mtindi Jonathan, alisema
kituo hicho kiko na watoto wenye ulemavu vipaji lakini hawana watu ambao
wanaweza kuwaendeleza.
Alisema kuna wachoraji wa michoro na
watunga mashairi na insha lakini vipaji vyao vinaishia kituoni hivyo kuwataka
watu wenye mapenzi mema na jamii hiyo kuwasaidia.
“Hapa kituoni tuko na watoto wenye
vipaji tena nazweza kusema zaidi ya jamii nyengine, tumeona hapa wakichora
michoro utadhani imechorwa na mashine, hii ni kuonyesha kuwa walemavu nao wako
na mchango katika Taifa” alisema Jonathan
Alisema kama watoto hao watapatiwa
misaada ya hali na mali wanaweza kuwa msaada kwa Serikali kwa kutoa watu wenye
vipaji mbalimbali na kuweza kupunguza uhaba wa wataalamu wa fani mbalimbali.
Mwisho
Watoto wenye ulemavu wa viungo, viziwi, ngozi na akili wakiwa katika foleni ya chai kabla ya kuingia ukumbini kuingia katika mashindano ya kutafuta vipaji fani mbalimbali ikiwemo ya kuchora michoro na Insha yaliyoandaliwa na kituo cha watoto wenye ulemavu wa viungo (YDPC) cha Tanga
Mwenyekiti wa baraza la watoto wenye ulemavu kituo cha watoto wenye ulamavu cha Tanga (YDPC), Mtindi Jonathan, (kushoto) akimpa zawadi ya begi mshindi wa kwanza wa kutunga Insha, Enjo Kimaro (kulia) wakati wa mashindano ya kuibua watoto wenye ulamavu
No comments:
Post a Comment