Thursday, September 1, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU SEHEMU 68

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
 
MWANAMKE
 
ILIPOISHIA
 
Yule jinni aliyeonekana kukasirika akatoka na kumuacha Zena akigomba peke yake.
 
“Najuta  kuja huku! Wazee gani hawa wasiolewa mambo. Wamekuwa washamba kiasi hiki!”
 
Ghafla nikamuona mzee mwingine aliyekuwa amefuatana na yule mzee aliyeondoka pamoja na mzee mwingine.
 
“Wewe mtoto mwenye laana ulimjibu nini huyu Subyani?” Yule mzee akamuuliza Zena kwa sauti ya ukali.
 
“Lakini baba ungenisikiliza mimi mwenyewe badala ya kusikiliza watumishi wako. Hao wanaongeza maneno”
 
“Mimi sihitaji kukusikiliza kwa sababu najua wewe umekuwa jeuri na asi. Ninachokwambia ni kwamba mrudishe huyu kijana ulikomtoa na kwamba sitaki kusikia tena kwamba unataka kuoana na binaadamu!”
 
Zena akafura kama chatu.
 
“Mimi lazima nitaoana naye, iwe itakavyokuwa. Kama hamtaki nitajiozesha mwenyewe!”
 
Zena akainuka pale alipokuwa ameketi akatoka kwa hasira huku yule mzee niliyemdhania kuwa ndiye Jabalkeys akimtazama.
 
“Huyu mtoto amekuwa shetani kabisa, si jini tena” akasema kisha akanisogelea mimi.
 
SASA ENDELEA
 
“Mwanangu amekutoa wapi yule shetani?” akaniuliza.
 
“Amenitoa kwetu”
 
“Wapi”
 
“Tanga”
 
“Mlikubaliana mje muoane huku?”
 
“Yeye ndiye aliyekuwa analazimisha. Amenitia kwenye matatizo mengi. Naomba msaada wako”
 
“Hata kama nitawambia hawa watumishi wangu wakurudishe, bado ataendelea kukufuata na atakusumbua lakini suala lake nitalipeleka kwa Sultani wetu. Wewe subiri hapa hapa”
 
Majini hao wakaondoka. Nikabaki peke yangu. Sikujua Zena alikuwa amekwenda wapi na angerudi saa ngapi. Na pia sikujua ningeendelea kukaa pale hadi muda gani. Kusema kweli ile hali ya Zena kuanza kutibuana na wazazi wake iliana kunitia hofu.
 
Baada ya kama nusu saa hivi yule jini aliyekuja kwanza akarudi peke yake akiwa ameshika bahasha.
 
“Begi lako ni lipi na lipi?” akaniuliza.
 
Nikamuonesha yale mabegi mawili niliyokwenda nayo. Yule jini akayabeba yote mawili kisha akaniambia.
 
“Twende”
 
Nikatoka naye katika lile jabali tukashika njia mbayo mimi na Zena tulikwenda nayo. Tukashuka chini baharini. Ikumbukwe kwamba muda ule ulikuwa ni usiku lakini ulikuwa usiku wa mbalamwezi.
 
Tulipofika pwani yule jini alinitafutia mahali chini ya mti akaniambia.
 
“Kaa hapa hadi saa tisa usiku. Utaona msafara mrefu wa majini unapita kutoka upande wa kusini kwenda kaskazini. Subiri mpaka utakapowaona majini waliobeba kichanja (aina ya jukwaa). Ukiwaona majini hao wafuate uwasimamishe.
 
“Pale juu ya kichanja utamuona Sultani wa majini amebebwa, utamgundua kutokana na kilemba chake kikubwa cha rangi nyeupe, utampa hii barua iliyoandikwa na mzee Jabalkeysi” Jini huyo akaniambia na kunipa ile bahasha aliyokuwa ameishika.
 
“Nikishampa itakuwaje?” nikamuuliza.
 
“Ataisoma halafu kuna kitu atakwambia. Hivyo ndivyo nilivyoagizwa na mzee Jabalkeysi”
 
Yule jini aliponiambia  hivyo akaondoka na kuniacha pale pale. Hapo mahalli palikuwa na mazingira ya kutisha sana, halafu niliambiwa nikae peke yangu hadi saa tisa uiku nisubiri msafara wa majini. Hao majini hawatanidhuru? Nikajiuliza.
 
Pamoja na hofu niliyokuwa nayo ilibidi nikae hapo kwani sikuwa na la kufanya. Hata kama ningetaka nikimbie nirudi kwetu ningerudi kwa njia gain?.
 
Nikakaa hapo huku nikitetemeka kwa baridi. Mawazo na hofu vilikuwa vimesonga kwenye moyo wangu. Nilikuwa nikijiuliza maswali chungu nzima yasiyokuwa na majibu. Nikatamani Zena atokee pale anirudishe kwetu lakini hakukutokea Zena wala yeyote.
 
Kila wakati nilikuwa nikitazama saa yangu kujua majira yalivyokuwa yanakwenda. Kwa mtu mwenye wasiwasi na hofu kama nilivyokuwa mimi, nilihisi muda ulikuwa hauendi kabisa na baridi ilikuwa ikizidi kuniingia kwenye mifupa.
 
Baada ya masaa machache lakini niliyoyaona marefu ikafika saa tisa usiku. Jinsi nilivyokuwa nimejificha pale chini ya mti haikuwa rahisi kuonekana labda kwa jini aliyekuwa karibu.
 
Ghafla nikauona ule msafara nilioambiwa. Walikuwa majini waliovaa nguo nyeupe tupu wameandamana wakitokea upande wa kusini kuelekea upande wa kaskazini. Niliouna msafara huo tangu ulipoanza kutokea.
 
Nilipotupa macho nikakiona kichanja kilichokuwa kimebebwa katikati ya msafara huo. Kilikuwa kimepembwa kwa vitambaa vyeupe na kilikuwa na vidirisha.
 
Nikajiuliza kama ningekuwa na moyo na ujasiri wa kujitokea na kusimamisha msafara huo wa majini? Lakini nikajiambia hilo ndilo nililokuwa nikilisubiri pale, kwa hiyo ilikuwa lazima nilitekeleze.
 
Ule msafara ulifika karibu, nikainuka ghafla na kuukimbilia huku nikipiga kelele.
 
“Jamani subirini, nina ujumbe wa Sultani!”
 
Mara moja nikaouna msafara huo umesimama. Majini hao wakawa wananitazama mimi.
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment