Wednesday, September 7, 2016

KUHARISHA NA KUTAPIKA KWA MTOTO ALIEKULA CHAKULA CHENYE SUMU

Kuharisha na kutapika kwa kula chakula cha sumu

Tatizo la kuharisha na kutapika linalosababishwa na usumu katika vyakula na maji. Linawapata zaidi watoto wanapokuwa safarini au katika matembezi ya burudani.

Watoto ndiyo wanakuwa rahisi kupata tatizo hili kwa kuwa mfumo wao wa kinga bado haujawa imara kupambana na maradhi. Ingawa ni mara chache tatizo hili la usumu kwenye vyakula husababisha mtoto kupoteza maisha.

Tatizo hili hujitokeza pale vyakula au maji ambayo hutumika kama mlo vinapochafuliwa kwa kugusana na kushikamana na vimelea wa maradhi, sumu na kemikali.

Vitu hivi vinapoliwa au kunywewa huweza kufika katika mfumo wa chakula na kuuathiri.
Chanzo cha tatizo hili, mara kwa mara ni bakteria na pia mara nyingine virusi, fangasi, sumu na kemikali huweza kuwa chanzo.

Vyakula na vinywaji vinaweza kushikamana na usumu wakati kutengenezwa kuhifadhiwa au kupikwa.

Nyama na maziwa ni moja ya vyakula ambavyo vikihifadhiwa katika joto lisilo sahihi ni rahisi kuharibika na kukaribisha vimelea kuzaliana.

Ndiyo maana inashauriwa kutumia zaidi kikombe kumnywesha mtoto maziwa badala ya chuchu za kunyonya ambazo zina ugumu katika kuzisafisha.

Sababu nyingine ni wakati wa kuandaa vyakula atakavyokula mtoto. Muandaaji hushika chakula hicho bila kunawa mikono yake na bila kuzingatia kanuni za afya.

Jambo jingine ni maji anayotumia mtoto yanaweza kutoka katika chanzo kilichochafuliwa kama vile chembe za kinyesi cha binadamu ambavyo ndiyo huwa na bakteria wanaoleta tatizo hili.
Kwa kawaida dalili zinaweza kujitokeza siku ya tatu baada ya kunywa au kula mlo uliochafuliwa.

Dalili ya awali na zinazojitokeza zaidi ni tumbo kuuma na kuharisha. Baadaye huweza kuambatana na kutapika.

Kuharisha ni hali ya haja kubwa laini au kama majimaji kwa zaidi ya mara tatu kwa saa 24. Choo kikubwa kinaweza kuwa kama cha malendalenda na damu kiasi.


Watoto hupata maumivu makali ya tumbo na wakati mwingine hushindwa kuvumilia na hujitupatupa au kujinyonganyonga tumbo kutokana na maumivu. Kwa mtoto anayejua kuongea atasema anaumwa na hupata ahueni baada ya kuharisha kwa kipindi fulani.

Joto la mwili kuwa juu au kupata homa kali, kuumwa kichwa na mara nyingine atahisi maumivu ya mwili.

Kutapika kunatokea lakini kunaweza kukoma kwa muda usiozidi siku nne na huku kuharisha kunaweza kupungua na akapata choo laini tu.

Madhara huweza kuwa makubwa endapo tu upungufu wa maji mwilini utajitokeza.

Tatizo hili linaweza kupoteza maisha ya mtoto kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
MGblog

No comments:

Post a Comment