MWANANCHI
Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume amemshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein kuachia madaraka.
“Dk Shein lazima aondoke kwa sababu kuendelea kubaki madarakani ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi,” alisema Fatma ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Fatma alisema kuwa mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria kufanya hivyo.
Fatma alisema Jecha hana mamlaka
kikatiba na kisheria kufuta matokeo hayo kwa kuwa maamuzi kama hayo
yanatakiwa kufanywa na ZEC yenye mwenyekiti, makamu mwenyekiti na
wajumbe watano; watatu kutoka CCM na wengine wawili kutoka CUF. “Akidi
ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na wajumbe wanne.
Kama kikao kilifanyika, akidi ilitimia
na jambo hilo likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi
walipokubali wajumbe wengine.
Hata makamu mwenyekiti hajashiriki
kwenye maamuzi hayo kwa sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila
kupata akidi hiyo,” alifafanua Fatma.
Mwanasheria huyo alisema kuwa amekuwa
akiwasikia baadhi ya wana CCM Zanzibar wakisema kuwa Jecha ndiyo tume na
tume ndiyo Jecha, hivyo ana haki ya kufuta uchaguzi. Lakini Fatma
alisema Jecha hana mamlaka kusema jambo ambalo halijakubaliwa na tume.
Alipoulizwa ikiwa hatua ya aliyekuwa
mgombea urais kupitia CUF, Seif Sharrif Hamad ya kutangaza matokeo
aliyodai yalimpa ushindi si kosa, Fatma alisema, “Sikumuona Maalim Seif
alipokuwa anatangaza matokeo hayo hivyo sijui kama alijitangaza kuwa
mshindi au alitangaza matokeo kama yalivyobandikwa kwenye vituo.
“Katika nchi zilizokomaa
kidemokrasia mgombea anaweza kuona mwelekeo wa matokeo na akampigia
mwenzake kumpongeza. Nadhani Maalim Seif alisoma jumla ya matokeo ya
uchaguzi kama yalivyobandikwa kwenye vituo, hivyo hilo si kosa ati,” alisema na kuongeza: “Ninasikitishwa na tabia hii.
Sikutegemea kama CCM watatumia nguvu
kutaka kubaki madarakani kwa njia hii. Sikutegemea kama watavuruga
katiba…ndiyo maana nina huzuni.” Jambo jingine alilosema litazua mgogoro
Zanzibar ni mamlaka yenye haki ya kuidhinisha fedha za uchaguzi wa
marudio ikiwa watalazimisha ufanyike.
“Kisheria fedha hizo ni lazima
zikubaliwe na Baraza la Wawakilishi. Baraza lipo wapi? Ili mtu awe
waziri lazima awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Rais alivunja Baraza Agosti na kwa hiyo
hadi ilipofika siku ya kuapishwa rais mpya, Zanzibar hakuna Baraza wala
Waziri. Ina maana fedha za wananchi zinatumiwa bila idhini ya Baraza, ”
alisema.
Alisema kinachofanyika Zanzibar ni
‘ukoloni’ wa watu weusi dhidi ya watu weusi ambao unawakosesha
Wazanzibari haki yao msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
“Hali si shwari Zanzibar. Watu
wamekata tamaa kwa sababu unapokuwa na Serikali ambayo inanyang’anya
haki ya wananchi ya kupiga kura, kuandamana, watu wanakosa imani na
Serikali hiyo,” alisema.
Kurudia uchaguzi Kuhusu kurudiwa
uchaguzi nchi nzima, Fatma alisema ulipofanyika uchaguzi mwaka 2000
ambao Amani Karume aligombea kwa mara ya kwanza, zilitokea dosari katika
majimbo 10 ya Unguja.
CUF walipotaka uchaguzi urudiwe nchi
nzima, CCM chini ya Benjamin Mkapa waligoma wakasema ni katika majimbo
yenye dosari tu. “Nini kimetokea mwaka huu? Kama dosari zilijitokeza
Pemba kama wanavyodai kwa nini urudiwe Unguja? Kwa nini hawataki kutumia
uamuzi wa mwaka 2000 wa kurudia maeneo yenye dosari tu?” alihoji.
“Mkapa alisema wazi kwenye kipindi cha
Hard Talk cha BBC akihojiwa na mtangazaji Tim Sebastian uchaguzi hauwezi
kufutwa ila utarudiwa tu katika baadhi ya majimbo.
Kwa nini leo mambo yamebadilika na CCM
inataka uchaguzi mpya?” alihoji. Fatma ambaye alikataa kueleza msimamo
wake kisiasa, alisema iwapo uchaguzi huru na wa haki utafanyika leo
Zanzibar, CCM haiwezi kushinda kwa sababu Wazanzibari wanajionea yale
ambayo wanafanyiwa na chama hicho.
“CCM imeshindwa Zanzibar kwa sababu
ilishindwa kuwashawishi watu wake na badala inawakemea, ikawanyima haki
zao. Kisaikolojia wapiga kura wanataka haki zao na wasibaguliwe lakini
ukiwapelekea jeshi na vifaru, unazidi kuwapoteza,” alisema.
Sherehe za Mapinduzi Wakati zikiwa
zimesalia siku nne kufikia kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Sikukuu
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma alisema kwa hali ilivyo haina maana
kutokana na CCM kung’ang’ania kukaa madarakani kwa nguvu. “Ninajisikia
kusalitiwa.
Madhumuni ya Mapinduzi haikuwa kuiweka CCM madarakani milele bali kurejesha madaraka kwa wananchi,” alisema.
Alisema aliambiwa kuwa waliofanya
mapinduzi (wakiongozwa na Abeid Amani Karume) walitabiri kuwa ipo siku
Zanzibar itakuwa na uchaguzi au Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini CCM
hawataki. “Wakati hao waliofanya mapinduzi wakisema hivyo, CCM
haikuwepo, ilikuwepo ASP.
Hao ASP hawakuwa wakijiaminisha kuwa
watakaa madarakani milele,” alisema. “Wakati tunaadhimisha mapinduzi ya
Zanzibar, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa malengo ya mapinduzi hayo
yalikuwa ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote na kuweka misingi ya
kidemokrasia lakini CCM wamevuruga,” alisema Fatma.
MWANANCHI
Operesheni ya bomoabomoa inayoendelea
kwa waliojenga nyumba mabondeni jijini Dar es Salaam itawaacha zaidi ya
watu 200,000 wakiwa hawana makazi.
Ubomoaji huo ulioanza katikati ya
Desemba mwaka jana, umezikumba nyumba takriban 600 katika mitaa ya
Hananasif na Suna, Manispaa ya Kinondoni.
Wakazi hao ni wale ambao Baraza la Taifa
la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeziwekea alama ya X nyumba zao
ambazo ni zaidi ya 10,000 hadi kufikia juzi, kwa mujibu wa Ofisa
Mazingira Mwandamizi wake, Arnold Kisiraga.
Hadi jana mchana, Kisaraga alisema
walikuwa wakiweka alama ya X katika nyumba za mabondeni zilizopo eneo la
Stakishari, Segerea na kwamba wataendelea hadi Pugu, nje kidogo ya jiji
la Dar es Salaam.
Idadi hiyo imefikiwa kwa kuzingatia
takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ambayo inabainisha kuwa
kila kaya jijini hapa inakadiriwa kuwa na wastani wa watu wanne chini
kidogo ya wastani wa Tanzania Bara wa watu watano (4.7) kwa kaya.
Mkurugenzi wa Sensa za Watu na Takwimu
za Jamii, Ephraim Kwesigabo alisema kwa sasa wana takwimu za kaya pekee
ambazo sehemu kubwa ya watu wake wamepanga.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Suna, Salim Hamis
alisema katika mtaa wake kuna nyumba zaidi ya 900 ambazo kila moja
inaweza kuwa na kaya kati ya tano hadi saba. “Wapangaji ni wengi katika
nyumba hizi usione nyingi ni ndogo. Wengi wana hali ya chini ndiyo maana
tumebanana hapahapa kwa kuwa hakuna namna tena,” alisema Hamis.
Kisiraga alisema makadirio ya awali ya
nyumba 8,000 yalijikita kwa kuangalia zinazotambuliwa na Wizara ya Ardhi
na manispaa lakini wamebaini “vijumba vidogo” vinavyoonekana kama vimeungana na nyumba kubwa za jirani kumbe vinajitegemea. Sehemu kubwa ya nyumba hizo zipo Kinondoni.
Alisema kadri wanavyozidi kupita
mabondeni kuweka alama ya X ndivyo idadi ya nyumba zilizojengwa maeneo
hatarishi zinavyoongezeka.
“Hii inatokana na mito kuendelea
kupanuka kutokana kingo zake kuharibiwa na wachimba mchanga na kufanya
nyumba za jirani kuingia kwenye mita 60 zinazokatazwa kisheria.
Kuna baadhi ya nyumba zilikuwa maeneo
salama miaka 10 iliyopita lakini kwa sababu mto umesogea kwao basi
watabomolewa kwa kuwa wapo maeneo hatarishi,” alisema Kisiraga.
Kuhusu hatua hiyo, mmoja wa wakazi
walioathirika, George Mkondoa alisema: “Bado tupotupo tu hapa hatuna pa
kwenda. Baadhi ya vitu nimejaribu kuvipeleka nyumbani Bagamoyo lakini
vimebaki nusu.
Hivyo ilinibidi nijenge kibanda kidogo
kwa muda tuishi na familia yangu.” Chiku Salim aliyekuwa na nyumba ya
vyumba viwili aliyoibomoa mwenyewe, alisema hana pa kwenda kujenga licha
ya kuokoa mabati na vifaa vingine katika nyumba yake.
Mmoja wa wapangaji, Steven Herman alisema: “Ubomoaji
ulikuja ghafla na wengi unakuta walikuwa wamebakiza miezi mitatu au
minne kodi zao ziishe hivyo kuhamishwa ghafla kumeleta mtihani wa kupata
nyumba haraka ndiyo maana unakuta tunahaha hapa.” Alisema shida hizo zingeepukika iwapo wangekuwa na elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya ardhi na mipango miji.
Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya
ardhi na makazi ya Space & Development, Renny Chiwa alisema: “Ili
kuwaokoa wananchi hao, ni lazima kuweka mazingira rafiki ya ukuaji wa
sekta binafsi katika maendeleo na makazi. Kampuni zikipata mikopo ya
nyumba kwa riba na masharti nafuu ushindani utakua na zitajenga
maghorofa ambayo vyumba vyake vinaweza kupangishwa kati ya Sh30,000 hadi
100,000 kwa mwezi.
” Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu, Patience Mlowe alisema wananchi walifanya makosa kuvamia
maeneo hayo kinyume na sheria na Serikali ilikosea kwa kuwaacha
waendeleze makazi kwa kuwasogezea huduma za Serikali za Mitaa, maji na
umeme hivyo kuwapa uhakika wa maisha ya kudumu na kushauri utengenezwe
mpango maalumu wa kuwasaidia.
“Hakuna Mtanzania anayeunga mkono
wananchi hawa waendelee kukaa maeneo hatarishi ya mabondeni. Ila
kinachoendelea sasa kinawaathiri kisaikolojia, kinawaumiza.
Wale ni Watanzania, Serikali lazima
iwasaidie tu. Watafutiwe makazi mbadala kwa muda wanapojipanga kusimama
tena,” alisema Mlowe. Alisema ubomoaji huo, unaowaacha wananchi hao kama
wakimbizi katika nchi yao, unavunja haki za binadamu na unalitia doa
Taifa kimataifa. “Hatujui mpaka sasa mpango wa Serikali juu ya watoto
wadogo waliobaki bila makazi na ambao wanasubiri kwenda shule baada
kuanza kufunguliwa,” alisema.
MWANANCHI
Wizara ya Mambo ya Ndani imeanza
operesheni ya kuwasaka raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini
kinyume cha sheria ili warudishwe makwao.
Operesheni hiyo imeanza ikiwa zimepita
siku chache tangu Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Anthony Mavunde
kumuagiza kamishna wa kazi nchini kufuta vibali vya kazi vya muda kwa
wageni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema wameanza
operesheni hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa raia wengi wa kigeni
wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria. “Serikali haiwezi
kukaa kimya wakati vijana wanakosa ajira huku kazi zile walizotakiwa
kufanya zikifanywa na raia wa kigeni.
Kibaya zaidi kuna baadhi ya kampuni,
viwanda na taasisi zilizoajiri wageni zinawadhalilisha na kuwanyanyasa
wafanyakazi wa Kitanzania, tumeanza kuwabaini na wataondolewa,” alisema.
Masauni aliwataka maofisa Uhamiaji
kuwachukulia hatua za kinidhamu wote watakaobainika kuhusika kutoa
vibali kinyume cha sheria. Aliiagiza Uhamiaji kutoa ripoti ya kila
kinachoendelea kwenye operesheni hiyo.
Aidha, alitaka operesheni hiyo
isitafsiriwe kuwa Tanzania haitaki raia wa kigeni, isipokuwa lazima
sheria na kanuni zilizopo zifuatwe.
Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam,
John Msumile aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wa operesheni
hiyo na kwamba, wanatarajia kuwakamata wageni zaidi ya 350.
“Tumeanzia Kariakoo na tutasambaa kwenye
manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam, naomba kila mmoja ashiriki
kwenye operesheni hii ya kuwaondoa raia hawa wa kigeni wanaoingia nchini
kinyume cha sheria,” alisema.
Kuhusu vibali vya muda, Masauni alisema
Serikali inaandaa utaratibu mwingine wa kushughulikia wageni waliotakiwa
kupewa vibali vya muda baada ya kupata malalamiko juu ya suala hilo.
“Tumepata malalamiko kupitia balozi zetu
juu ya kufutwa vibali hivi kwa sababu vilianza kutolewa kwa kukiuka
sheria, kwa kuwa vina umuhimu wake, Serikali inaangalia namna ya
kushughulikia jambo hili,” alisema.
Alisema ushughulikiaji wa suala hilo
utakwenda sambamba na kuwabaini waliokuwa wakikiuka sheria kwa kutoa
vibali hivyo kiholela na kuisababishia Serikali hasara.
Pia, alisema Serikali ipo kwenye
mchakato wa kuanzisha mahakama ya kijeshi ya Uhamiaji ili kukomesha
vitendo vya rushwa na ukiukwaji mwingine wa sheria unaofanywa na baadhi
ya watumishi wa idara hiyo.
MWANANCHI
Serikali ya Awamu ya Tano imekusanya
ziada ya Sh900 bilioni kupitia kodi katika kipindi cha miezi miwili
tangu aingie madarakani.
Wakati Novemba makusanyo hayo yalikuwa
Sh1.3 trilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh400 bilioni, Desemba makusanyo
hayo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalifikia Sh1.4
trilioni sawa na ongezeko la Sh500 bilioni kutoka wastani wa makusanyo
ya Sh900 bilioni zilizokuwa zinakusanywa kila mwezi na Serikali ya Awamu
ya Nne.
Iwapo makusanyo hayo ya ziada ya Sh900
bilioni yangeelekezwa kwenye ununuzi wa magari ya wagonjwa,
yangenunuliwa magari 3,000 kwa gharama ya Sh300 milioni kila moja na
kuwezesha kila mkoa kupata magari 120.
Takwimu za ongezeko la Desemba
zilitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata
ambaye alisema kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, mamlaka yake
ilikuwa imekusanya wastani wa Sh6.4 trilioni ambayo ilikuwa ni sawa na
asilimia 95.5 ya lengo la kukusanya Sh6.5 trilioni.
Kidata alisema sababu za ongezeko la
makusanyo hayo ni kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuweka mifumo
mizuri ya ufuatiliaji.
Katika hatua nyingine, Kidata alisema
jumla ya Sh11.8 bilioni zimekusanywa kutoka kwa wafanyabiashara
walioondosha makontena katika Bandari Kavu kinyume na taratibu za
forodha. Alisema kuwa makusanyo hayo yanajumuisha Sh5.3 bilioni kutoka
kwa kampuni na wafanyabiashara 19 ambao wamemaliza kulipa kodi za
makonteza yao na wengine 19 ambao wamelipa sehemu ya kodi wanayodaiwa.
Yafafanua madai ya Bakwata Wakati
huohuo; TRA imefafanua madai ya kuwapo upendeleo katika kutoa masharti
ya ufuatiliaji wa misamaha ya kodi kwa taasisi zisizo za kiserikali na
mashirika ya dini, ikisema unafanywa kwa kufuata taratibu na sheria.
Tamko la Kidata kwa vyombo vya habari
limekuja kufuatia kauli iliyotolewa hivi karibuni na Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), kuwa kumekuwapo na sintofahamu katika agizo
la TRA lililowataka kupeleka taarifa kuhusu magari yaliyosamehewa kodi
na matumizi yake ndani ya siku saba, likihoji iwapo agizo hilo
lilitolewa pia kwa taasisi nyingine.
Kidata alisema Sheria ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania inaipa mamlaka hiyo kusimamia, kukagua na kuhakiki
mapato ya Serikali na kuzuia aina yoyote ya ukwepaji wa kodi kwa
maendeleo ya Taifa.
“Mamlaka inayo dhamana ya kusimamia
kusiwepo na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi ambayo hutolewa kwa
mujibu wa sheria kifungu cha 5 (3) cha TRA,” alisema Kidata.
Alisema TRA haina upendeleo na haibagui
wala kulenga taasisi moja ya kidini. Katika taarifa hiyo Kidata alisema
kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2015, TRA iliwaandikia barua
walipakodi 65 na katika wahusika hao kuna taasisi na mashirika ya dini
ni 39.
Kidata alisema ukaguzi huo husaidia TRA
kupata taarifa muhimu ili kuishauri Serikali namna bora ya kutoa
misamaha kwa manufaa ya Taifa
HABARILEO
Serikali imekataa viwango vya nauli mpya
vilivyopendekezwa na Kampuni ya Uda Rapid Transit (UDA-RT), itakayotoa
huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam. Pamoja na
kukataa imeweka bayana kuwa viwango hivyo viko juu ambavyo wananchi
wengi watashindwa kuvimudu.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ameagiza wizara zote
zinazohusika kukutana haraka iwezekanavyo na kujadili viwango vipya vya
nauli vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi. “… sasa nataka
mamlaka zote zilizohusika wakutane na kuja na viwango vipya vya nauli
kama huyu mwekezaji ameshindwa aseme, Serikali inaweza kuendesha mradi
yenyewe,” alisisitiza Majaliwa.
Wizara na taasisi zilizoagizwa kukutana
ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi); Wizara ya
Ujenzi na ya Uchukuzi; Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra) pamoja na kampuni ya UDA-RT.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam muda mfupi baada ya kurejea akitokea Ruvuma, alikokamilisha
ziara yake ya kikazi jana, alisema viwango hivyo vilivyopendekezwa na
vinavyotarajiwa kujadiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra) havifai na havikubaliki.
Alisema Novemba 25, mwaka jana
alitembelea mradi huo wa DART na kumuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi,
Mtendaji Mkuu wa DART pamoja na Wakala wa Barabara (Tanroads) kupitia
mfumo mzima wa uendeshaji wa mradi huo, lakini hadi leo hakuna mpango
wowote wa biashara uliowasilishwa serikalini na UDA-RT.
Alisema pamoja na hayo, pia kampuni hiyo
imeshindwa kuweka bayana gharama za uendeshaji wa mradi huo, uliotakiwa
kuanza rasmi Januari 10, mwaka huu. Majaliwa alisema wakati kampuni
hiyo ikishindwa kuweka wazi mpango wake wa kibiashara, alishangaa juzi
kusikia imewasilisha vi wango vya nauli vilivyopendekeza ambavyo
vilikuwa vya gharama ya juu.
“Kwa kukosekana tu gharama halisi za
uendeshaji mradi, ni dhahiri kuwa nauli zilizopendekezwa hazina
uhalisia,” alisema. Kampuni hiyo ilipendekeza safari kwenye njia kuu
kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1,400 na
wanafunzi nusu ya nauli hizo. “Gharama hizi ni kubwa mno.
Mradi huu unalenga kumlinda na kumsaidia
mwananchi wa kawaida, wakiwemo watumishi wa umma ambao wengi wao
wamejenga pembezoni mwa mji kuweza kusafiri kutoka maeneo ya pembeni
hadi katikati ya jiji kwa gharama nafuu na kwa urahisi na si
kumkandamiza,” alisema Majaliwa.
Alisema kipato cha wananchi kwa ujumla
wakiwemo watumishi wa umma, bado si kikubwa. Alitoa mfano kwamba,
mtumishi anayelipwa mshahara wa Sh 250,000 kwa mwezi, kwa nauli
iliyopendekezwa pamoja na watoto wake, fedha yote inaishia kwenye nauli.
Alisema kwa hali ilivyo, Serikali
haiwezi kuridhia viwango hivyo ambavyo ni wazi vitamkandamiza mwananchi
badala ya kumsaidia. “Bado tunayo nafasi ya kuendesha mradi huu, si
lazima tuanze Januari 10 kama ilivyopangwa, ni bora tuchelewe na kuanza
tukiwa na viwango vya nauli vinavyoridhisha badala ya kuanza na nauli
hizi ambazo ni gharama kubwa mno.”
Juzi Sumatra ilikutana na wadau kwa
ajili ya kujadili mapendekezo hayo ya nauli, ambayo hata hivyo
yalipingwa na wadau wengi wa sekta ya usafiri. Walishauri nauli iwe kati
ya Sh 400 na Sh 500 kutimiza malengo ya kusaidia wananchi wa kipato cha
kawaida.
Pamoja na hayo wadau hao wakiwemo
wananchi na Baraza la Walaji la Sumatra (Sumatra CCC), walihoji sababu
za mabasi hayo yanayobeba watu wengi kwa safari moja na yanayotumia
barabara zisizo na foleni, yatoze nauli kubwa wakati daladala
zinazochukua abiria wachache na kukabiliwa na msongamano mkubwa katika
barabara za kawaida, wanatoza nauli za chini.
HABARILEO
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
amesema yeye bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar huku akiwataka wasioamini
katiba hiyo, wapeleke shauri hilo Mahakama Kuu ya Zanzibar yenye uwezo
pekee wa kutafsiri katiba.
Amebainisha kuwa yeye anaongoza nchi kwa
mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba kama si uwezo huo aliopewa
kikatiba hana sababu ya kuendelea kukaa madarakani pamoja na serikali
anayoingoza.
“Tuko madarakani na uongozi wote wa
serikali… yupo Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na
mawaziri,” alisisitiza Dk Shein na kuongeza kuwa hao wanaodai kujiondoa
serikalini huo ni uamuzi wao wenyewe.
Alibainisha kuwa yeye na serikali
anayoiongoza kuendelea kuwepo madarakani si kwa uamuzi wake na wala hana
ubavu wa kujiweka madarakani bali ni Katiba ambayo inajieleza wazi.
Dk Shein alitoa kauli hiyo jana kwa
nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kusini
Pemba katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu kisiwani
humu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.
Aliwaambia wananchi kuwa yako mengi
yanayosemwa lakini hawapaswi kuyasikiliza kwa kuwa kama ni serikali yeye
ndiye Rais hivyo wanapaswa kumuamini anachowaeleza.
“Ya mjini yapo yasikilizeni lakini kwa
Serikali mimi ndiye Rais na nisiposema mimi nitawatuma wasaidizi wangu
kuwaeleza,” Dk Shein alisema na kuongeza kuwa ya vyama kila mtu ana
chama chake.
Alisema kama ni suala la Chama Cha
Mapinduzi (CCM) yeye ndiye Makamu Mwenyekiti Zanzibar na kama kuna la
kuwaeleza wana CCM na wananchi atawaeleza yeye na viongozi wenzake wa
chama hicho pamoja na taarifa za vikao vya chama vyake.
Dk Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ushindani wa kisiasa si ugomvi bali ni utaratibu wa kupeana changamoto katika uongozi
HABARILEO
Wazir Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza
kufukuzwa kazi kwa madaktari na wahudumu ya sekta ya afya katika
hospitali ya mkoa wa Ruvuma, wanaojihusisha na vitendo vya utoaji mimba
kwa wanafunzi na hata watu wazima.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo jana,
wakati akizungumza na madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa
hospitali ya mkoa wa Ruvuma, baada ya kumaliza kutembea idara na vitendo
mbalimbali vilivyopo chini ya hospitali hiyo.
Alisema amepata taarifa kuwa baadhi ya
madaktari na wauguzi katika hospitali hiyo, wamekuwa na tabia ya utoaji
mimba na kutumia vifaa vya serikali kutekeleza vitendo hivyo jambo
ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi.
Amemuagiza Mganga mkuu kufanya ukaguzi
wa kushtukiza katika hospitali hiyo ili kubaini watumishi wanaojihusisha
na tabia ya kutoa mimba wanafunzi na kuwachukulia hatua kali.
“Wodi ya wazazi namba tano kuna watu
wanaojihusisha na vitendo vya utoaji mimba wanawake, nina taarifa za
kutosha juu ya tabia hiyo, ni marufuku kwa daktari yeyote kutumia vifaa
vya hospitali kufanya vitendo vichafu vya kuwatoa mimba wasichana wadogo
hususan wanafunzi.
“Hatutakuwa na msamaha kwa daktari
yeyote anayeshiriki vitendo vya kutoa mimba, mganga mkuu na mganga
mfawidhi tafadhalini sana chukueni hatua kwa mtumishi mwenye tabia hii,
sitaki kusikia tena kwamba wodi ya wazazi inatumika kwa ajili ya utoaji
mimba,” alionya.
Mbali na hilo, amewataka watumishi hao
kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili na miiko ya utumishi wao
kwa sababu kazi yao ni muhimu kwa kuwa inashilikia maisha ya watu.
Pia ameupongeza uongozi wa hospitali
hiyo kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) katika kukusanya mapato
ya hospitali, hatua iliyosaidia kuongeza mapato yake kutoka Sh 600,000
kwa mwezi hadi kufikia Sh milioni 2.4.
MTANZANIA
JENGO la Polisi Makao Makuu, jijini Dar
es Salaam limenusurika kuteketea kwa moto baada ya kutokea hitilafu ya
umeme katika jengo hilo.
Moto huo uliwashtua wafanyakazi wa polisi makao makuu ambao walikuwa wakikimbizana kutoka nje ili kunusuru maisha yao.
Akizungumzia tukio hilo, Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, alisema moto huo ulianzia katika dari
kwenye jengo la ghorofa ya nne ambao baada ya kuanza kuungua moto na
moshi kuenea katika baadhi ya maeneo ya jengo hilo.
Alisema wafanyakazi walipoona cheche
katika ghorofa hiyo ndipo walipoanza kutoa taarifa kwa wafanyakazi
wenzao na kutoka nje ili kujiokoa.
“Moto ulianzia katika dari ambapo
kulikua kunatoa cheche nyingi na baadae tumetoa taarifa katika kikosi
cha ulinzi na uokoaji zimamoto wamekuja kuuzima,” alisema.
Alisema moto huo haujaleta madhara yoyote kwa wafanyakazi wala katika vitu vyovyote vya ofisi.
“ Tunashukuru kikosi cha zimamoto kufika
mapema na kwa wakati hata hivyo watu walikuwa wakisema tulikuwa katika
mazoezi lakini si hivyo bali ni moto tu na tayari umedhibitiwa,”
alisema.
MTANZANIA
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imejitwisha mzigo wa deni la Sh bilioni 4 ambalo Bodi ya Utalii inadaiwa.
Deni hilo ni ambalo linahusu matangazo
yanayoanzia mwaka 2013/ 2014 ambalo lilikuwa likihusu matangazo yote ya
utalii yaliyokuwa yakifanyika ndani na nje ya nchi katika viwanja
mbalimbali vya soka vya Ulaya.
Akizungumza na viongozi wa bodi hiyo,
jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghebe alisema wizara inachukua jukumu la kulipa deni hilo ili
bodi hiyo iweze kufanya kazi kwa amani.
“Deni hilo lisukumiwe wizara ili
tulifanyie kazi, kwa kuwa kama mkiendelea kubaki nalo nyinyi mtashindwa
kufanya kazi kwa amani,”alisema Maghembe.
Alisema kutangaza utalii ni zoezi
endelevu kwa kuwa ndio chanzo cha mapato kikubwa kuliko sekta yeyote
nchini, hivyo aliwataka viongozi wa bodi hiyo kubadili namna ya kufikiri
na kutumia rasilimali ilizonazo katika kuwashawishi wawekezeji.
“Lazima tubadili namna ya kufikiri kwa
kutenga maeneo mazuri ya uwekezaji na kujitangaza kwa wadau wanaohusika
juu ya kujenga hotel kwa vile viwanja tunavyo vya kutosha,”alisema
Maghembe.
Pia Maghembe alisema kwamba ni wakati
sahihi wa kuwa na mfuko wa kuwawezesha wawekezaji wadogo wa ndani ili
kufika viwango vya kimataifa.
Waziri huyo alisisitiza kwamba mbali na
kutoa elimu juu ya wawekezaji hao, bodi hiyo inatakiwa kujitahidi katika
miaka miwili ijayo kufikisha watalii milioni 2 badala ya milioni 1
iliyopo sasa.
Aidha Maghembe aliitaka bodi hiyo kuacha
kulalamika juu udogo wa bajeti na kuwataka kupanga mipango yao kuendana
na kiwango cha fedha walizonazo.
“Serikali ya awamu yatano imedhamiria
kupambana na changamoto zinazotokana na watu binafsi, hivyo hakuna haja
ya kulalamika juu ya suala la bajeti badala yake ni muhimu kuangalia
vipaumbe muhimu ili kuendana na fedha mlizonazo,”alisema Maghembe.
Profesa Maghembe aliitaka bodi hiyo
kuruhusu matangazo yote ya utalii yaliyokuwa tayari kuendelea kuoneshwa
katika maeneo mbalimbali ndani na nje, huku akiahidi kuzifanyia kazi
changamoto zilizojitokeza katika bodi hiyo
MTANZANIA
Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi imezuia
nyumba anayoishi Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God Mikocheni,
Dk. Getrude Lwakatare kubomolewa.
Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa juzi na
Jaji John Mgeta, baada ya Wakili wa Lwakatare, Emmanuel Muga
kuwasilisha maombi ya kupinga ubomoaji huo chini ya hati ya dharura.
Jaji Mgeta alizuia ubomoaji wa jengo hilo ama kuchukua hatua yoyote kuhusu jengo hilo lililopo Kawe Beach.
Muga aliwasilisha maombi akimwakilisha
mdai ambaye ni mtoto wa Mchungaji Lwakatare, Robert Brighton dhidi ya
wadaiwa NEMC, Manispaa ya Kinondoni na wadau wengine wote.
“Mheshimiwa jaji, nawasilisha maombi ya
zuio la kubomoa nyumba ya mteja wangu chini ya kifungu namba 95 cha
Sheria ya Mwenendo wa Madai na kifungu namba 2(3) cha JALA vinavyotoa
mamlaka kwa mahakama kutoa nafuu stahili pale kunapokuwa na ukiukwaji wa
kuvunja haki ya wazi,” alidai.
Akitoa uamuzi huo alisema tayari pande
husika zilikuwa na kesi namba 70 ya mwaka 2012 na ikamalizika kwa kutoa
hukumu na kukazia hukumu iliyompa haki ya ushindi mdai.
“Mahakama ilimpa haki mdai, lakini
chakushangaza mdaiwa anakiuka matakwa ya hukumu na kutaka kubomoa
nyumba, kwa hali isiyokuwa ya kawaida mdai anahitaji ulinzi wa mahakama
hii ya haki,”alisema Jaji Mgeta.
Alisema nyumba hiyo ipo katika kiwanja namba 2019 na 2020 ambapo hati yake ilitolewa mwaka 1979.
Inadaiwa mwaka 2011 NEMC ilitoa notisi
ya kuvunja nyumba hiyo baada ya kushinikizwa na wakazi wa eneo hilo
wakidai ujenzi wake unaziba Mto Ndumbwi na uko jirani na mikoko.
Wakili Muga aliwasilisha maombi ya
kuzuia nyumba ya mteja wake kubomolewa baada ya Wizara ya Maliasili
na Utalii kupitia wakala wa misitu Tanzania (TFS ), kuweka alama
ya X wakidai imo katika hifadhi ya bahari.
MTANZANIA
Kamati za Bunge zinatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, kabla ya mkutano wa pili wa Bunge la 11 kuanza Januari 26.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Ofisi
za Bunge zimelieleza gazeti hili kwamba, suala hilo lipo jikoni na wiki
hii Spika anatarajiwa kutangaza kamati za Bunge.
Akizungumzia hilo jana jijini Dar es
Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Owen Mwandumbya alikiri suala la
kamati za Bunge kushughulikiwa na Spika, Job Ndugai, huku akisisitiza
kuwa suala hilo lipo katika hatua nzuri.
“Spika anashughulikia suala la
kamati naamini hivi karibuni zitakuwa zimekamilika na kutangazwa
hadharani hata kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo,” alisema Owen.
Kamati hizo zinatarajiwa kutangazwa
mapema kwa sababu kabla ya kuanza kwa Bunge Januari 26 taratibu zinataka
kamati za Bunge zianze kwanza mikutano yake.
Kamati za Bunge huundwa kwa mujibu wa
Katiba Ibara ya 96, likiwa limepewa madaraka ya kuunda kamati za Bunge
za aina mbalimbali na muundo wake umefafanuliwa na Kanuni za Kudumu za
Bunge.
Katika muundo huo zipo kamati za kisekta
na zile zisizokuwa za kisekta, ambazo kwa pamoja hufanyakazi na
kutekeleza majukumu yao kwa niaba ya Bunge.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 89 Bunge
limeunda Kamati 15 ambazo ni Kamati ya Uongozi, Kamati ya Fedha na
Uchumi, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Kamati ya Uwekezaji na
Biashara na Kamati ya Mambo ya Nchi za Nje.
Nyingine ni Kamati ya Kanuni za Bunge,
Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge, Kamati ya Huduma za Jamii na Kamati ya Maliasili na Mazingira.
Nyingine ni Kamati ya Maendeleo ya
Jamii, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), Kamati ya Kilimo na Ardhi pamoja, Kamati ya Miundombinu
na Kamati ya Huduma za Jamii.
Hata hivyo kanuni ya 88 (12) imetoa
fursa kwa kila kamati kuunda kamati nyingine ndogo kwa ajili ya
uendeshaji bora wa shughuli zake.
NIPASHE
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
Mwigulu Nchemba, ameivunja Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika vya
Wakulima wa Tumbaku mkoani Iringa (ITICOJE).
Sambamba na hatua hiyo, amewafukuza kazi
viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika vya wakulima wa tumbaku,
waliojaribu kujimilikisha matrekta yaliyokopwa na vyama vyao.
Nchemba alitoa kauli hiyo jana
alipozungumza kwenye kikao alichokiitisha kwa kushirikiana na viongozi
wa mkoa wa Iringa kwa lengo la kusikiliza malalamiko ya wakulima wa
tumbaku waliokuwa wakiwalalamikia viongozi wao.
Malalamiko hayo ya wakulima nusura
yamponze Mkurugenzi wa Benki ya CRDB tawi la Iringa, Kisa Samuel, ambao
waliotoa mkopo huo wenye kila dalili ya ufisadi. Mkurugenzi huyo
alitakiwa kujibu kwa nini benki imetoa mikopo hiyo yenye harufu ya
ufisadi.
Nchemba alisema CRDB mbali na kutaka
fedha za watu ambao ni wanachama, imewaacha wanaohodhi matrekta wakati
tangu mwanzo walijua wanatumia mwavuli wa vyama kuwatapeli wakulima.
Hata hivyo, Kisa alisema wameingia
mkataba na vyama vya msingi na si mtu mmoja mmoja, ndiyo maana hata kadi
zina majina ya vyama.
Katika mkutano huo ulidumu takriban saa
nne, Nchemba alihitimisha kwa kusema: “Kuanzia leo nitamke kwamba yale
matrekta kuanzia kadi zile, umiliki wa kadi, ratiba na mwonekano wake
yaende kwenye vyama vya msingi ambavyo ndivyo vimelipia matrekta.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment