NIPASHE
Wafungwa wanaotumikia vifungo mbalimbali
katika gereza kuu la Lilungu, mkoani Mtwara, wanakabiliwa na hali ngumu
kimaisha kutokana na kupewa chakula kibaya na huduma mbovu za vyoo
hivyo kutishia kuanzisha mgomo.
Taarifa zilizoelezwa na wafungwa hao,
zilisema tatizo la kupewa chakula kibovu limekuwa la muda mrefu na
uongozi wa gereza umekuwa hauchukui hatua kila ukielezwa.
Wafungwa hao (majina tunayo)
walibainisha mambo sita wanayolalamikia kuwa ni kupewa chakula kibovu na
huduma mbaya za ndani na kwamba hadi sasa bado wanatumia mtondoo na
hakuna huduma ya matunda hadi wakati wa msimu wa maembe tu.
Malalamiko mengine ni kukosekana kwa
mboga za majani kutokana na bustani ya gereza kubinafsishwa kwa mkuu wa
gereza hilo ambaye hulazimika kuuza mboga kwa gereza na kutokuwapo
huduma ya nyama ambayo wanapewa mare nne tu kwa mwezi.
Kutokana na hali hiyo, Januari 14, mwaka
huu, wafungwa katika gereza hilo walianza mgomo baridi baada ya
kupikiwa mchele uliodaiwa kuwa na wadudu (funza).
Walisema malalamiko hayo kila
wanapowaeleza viongozi wao wamekuwa wakijibu kuwa ni kwa sababu serikali
haijawalipa wazabuni wanaotoa huduma ya chakula.
Ofisa Habari Jeshi la Magereza, Deogratius Kazinja,
alipoulizwa alisema ofisi yake bado haijapokea malalamiko ya wafungwa
hao na kwamba taarifa rasmi za masuala hayo zinaweza kutolewa na
viongozi wa juu wa jeshi.
Kazinja alisema migomo ya wafungwa
imekuwa ikijitokeza mara kadhaa katika magereza lakini haisababishwi na
uongozi wa magereza kushindwa kutatua malalamiko yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara, Mussa Kaswaka,
alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia malalamiko hayo kwa sababu kwa
utaratibu wa jeshi hilo ni hadi apewe ruhsa ya kuzungumza na Kamishna
Jenerali wa Magereza.
“Mimi si msemaji wa Jeshi la
Magereza. Nenda makao makuu kaonane na Kamisha Jenerali wa Magereza
halafu yeye ndiye atatoa maelekezo kama niyatolee ufafanuzi,” alisema.
NIPASHE
Serikali imekanusha uzushi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii ya ndani ya nchi na nje ya nchi kuwa Rais Dk. John Magufuli,
amewafukuza wageni kutoka nje waliokuwa wanafanyabiashara zao nchini
kwa kuwa serikali yake haitaki wageni kufanya biashara nchini.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar
es Salaam kwa vyombo vya habari jana ilisema serikali haijafukuza wageni
kutoka nje ya nchi kufanya biashara nchini na haina mpango wa
kuwafukuza wageni wanaoishi nchini kwa vibali vilivyotolewa kisheria na
Idara ya Uhamiaji.
“Uzushi huo usiokuwa na ukweli
umeenezwa kufuatia Idara ya Uhamiaji kutekeleza jukumu lake la
kufuatilia wageni wote wanaoishi nchini bila vibali halali vya ukaazi
ambapo kwa mwezi Novemba na Desemba, mwaka 2015 wageni 372 walioondoshwa
nchini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ilifafanua kuwa kazi ya kufuatilia
wageni wanaoishi nchini bila vibali halali vya kisheria, haijaanza
katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Ilieleza kuwa Idara ya Uhamiaji nchini
tangu Januari hadi Desemba, mwaka jana, iliondosha nchini jumla ya
wageni 1,642 waliokuwa wanaishi na kufanya shughuli zao nchini kinyume
na sheria.
“Uzushi unaoenezwa hauna ukweli
wowote na hauna nia njema na nchi yetu kwani kati ya mwaka 2014 na 2016,
Idara ya Uhamiaji imetoa vibali vya ukaazi (Residence Permits) 40,765
kwa wageni wawekezaji na wafanyabiashara, wageni wanaofanya kazi za
kuajiriwa, wageni wanaokuja kwa ajili ya masomo, matibabu, dini, utafiti
na wastaafu kuishi na kufanya shughuli zao nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Ilisema serikali inawakaribisha wageni
kuja nchini kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria, kanuni
na taratibu za nchi.
Ilisema aidha, kuna uzushi unaenezwa
kuwa Rais Dk. Magufuli, amepiga marufuku wanawake kuvaa nguo fupi kama
njia ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
“Rais tangu aingie madarakani, hajawahi
kuagiza wala kutoa tamko kuhusiana na uzushi wa kukataza uvaaji wa nguo
fupi ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi kama inavyoenezwa katika
mitandao ya ndani na nje ya nchi ambayo inanukuu habari hiyo kuwa
imeandikwa na Gazeti la Kenya la `The Standard,’ ilisema.
Ilisema serikali inautangazia umma kuwa
uzushi huo unaomhusu Rais Magufuli umetungwa na watu wasioitakia mema
Tanzania kwa lengo la kumdhalilisha Rais na hauna ukweli hivyo watu
wasishiriki kuueneza kwa njia yeyote ile.
MTANZANIA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako,
amefuta mfumo wa uwekaji matokeo wa ‘Grade Point Average (GPA)
ulioanza kutumiwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) mwaka 2014.
Mfumo huo uliofuta mfumo uliokuwapo wa Divisheni, ulianza kutumika kwa kidato cha nne na sita na vyuo vya ualimu.
Inaelezwa kuwa mfumo huo ulianzishwa
kujaribu kupandisha ufaulu baada ya kuonekana wanafunzi wengi
walishindwa mitihani ya kidato cha nne, hasa mwaka 2013.
Mfumo huo ulilalamikiwa na wadau wa elimu waliodai kuwa ulikuwa unashusha kiwango cha elimu na kuwachanganya wanafunzi.
Profesa Ndalichako, ambaye aliwahi kuwa
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), alisema baraza
hilo limeshindwa kueleza sababu za kutumia mfumo huo badala yake
limeishia kutoa utaratibu uliotumika tu.
“Kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu
cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania, sura ya 107,
naliagiza Baraza kufanya mapitio ya mfumo unaotumika sasa wa wastani wa
alama (GPA) kwa lengo la kurudi kwenye mfumo wa awali wa Divisheni.
“Viwango vya ufaulu vizingatie azma ya nchi kuelekea kwenye uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu mtihani wa pili (Paper two), aliitaka NECTA kuufuta kwa watahiniwa wa kujitegemea.
Mtihani huo ulianzishwa kama alama ya maendeleo wakati ni mtihani wa mwisho.
“Wizara haiwezi kufikia azma ya
kusimamia ubora wa elimu katika ngazi zote bila kuhakikisha viwango
vya ufaulu vinawezesha kutoa wataalamu wenye stadi na maarifa badala ya
kuwa na wahitimu wengi wenye vyeti lakini hawakidhi mahitaji ya soko la
ajira,” alisema Profesa Ndalichako.
Januari 7 mwaka huu, Waziri Ndalichako
alitembelea Necta na kuitaka itoe ufafanuzi wa kuacha kutumia mfumo wa
divisheni na kutumia GPA.
Pia aliitaka itoe maelezo ya kuanzishwa kwa mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea.
Hata hivyo alisema jana kuwa maelezo
yaliyotolewa yalikuwa yamejikita katika kueleza utaratibu badala ya
sababu za kuutumia mfumo huo.
“Taarifa imebainisha kuwa uanzishwaji wa
mfumo wa GPA ulitokana na maoni ya wadau bila kuwataja wadau husika na
kueleza sababu walizotoa.
“Taarifa ya utafiti uliofanywea na
Wizara ya Elimu haijataja idadi ya wadau waliojaza madodoso na wala
haionyeshi mikutano ya kupata maoni ya wadau ilihusisha watu gani,
ilifanyika wapi na lini,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu sababu kuwa NECTA ilipata
maelekezo kutoka wa Wizara ya Elimu mwaka 2014, Profesa Ndalichako,
alisema uchambuzi unaonyesha kuwa wizara ilikuwa imeelekeza baraza la
mitihani liandae mfumo huo na kuuwasilisha kwa Kamishna wa Elimu upate
kibali cha Serikali kabla ya kuanza kutumika.
“Hata hivyo, jambo hilo halikufanyika na
badala yake Baraza hilo likaanza kutumia mfumo huo mwaka 2014. Nyaraka
zilizowasilishwa hazionyeshi kama mapendekezo ya mfumo huo
yaliwasilishwa kwa Kamishna wa Elimu,” alisema.
Alisema Baraza lilieleza faida ya
kutumia GPA kuwa ni kueleweka kwake kwa urahisi na wadau jambo ambalo
linapingana na maoni ya wadau yanayojitokeza kwenye vyombo vya habari,
huku likishindwa kueleza udhaifu wa mfumo wa Divisheni.
“NECTA wameeleza kuwa mfumo wa GPA
umerahisisha udahili wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu (Collective
Admission System- CAS) jambo ambalo si sahihi.
“Mfumo wa CAS ulianza kutumika Aprili
2010 wakati mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka 2014. Isitoshe
huzingatia masomo mawili ya fani anayotarajia kusoma mwanafunzi siyo
ufaulu wa jumla,” alisema.
Waziri alisema mfumo wa GPA ulikuwa bado kwenye majaribio hivyo haukupaswa kutumika kufanyia majaribio kwenye maisha ya watu.
Kuhusu sababu ya kuongeza mtihani wa
pili kwa watahiniwa wa kujitegemea kama mbadala wa upimaji endelevu,
alisema maelezo ya NECTA kuwa mtihani huo ni mbadala wa upimaji endelevu
hayatekelezeki.
“Kitaalamu ‘paper two’ haiwezi kuwa
alama ya maendeleo ya kila siku kwa kuwa inafanyika sambamba na mitihani
mingine ya mwisho,” alisema Profesa Ndalichako.
Kwa sababu hiyo, Profesa Ndalichako,
alisema kitendo cha baraza hilo kuingiza mfumo huo wa GPA katika
marekebisho ya kanuni zake yaliyosainiwa na Waziri Oktoba 28 mwaka jana
na kuchapishwa Novemba 6 mwaka jana kwenye gazeti la Serikali, ni
kuonyesha kuwa mfumo huo ulianza kutumika bila kukamilika matakwa ya
sheria.
“Mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka mmoja kabla haujaingizwa kwenye kanuni za mitihani,” alisema.
Akizungumzia hasara ya mfumo huo, Waziri
Ndalichako alisema baadhi ya watahiniwa waliofaulu mitihani wanaonyesha
kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango cha ufaulu.
Alisema kuwapo daraja E kwenye alama za
ufaulu wakati haihesabiki katika upangaji wa GPA kunawafanya watahiniwa
waliopata E zote kwenye mitihani kujiona wako bora kuliko wenye D mbili
na F zote, ambaye anahesabika kuwa amefaulu mtihani.
“Uwepo wa pointi za mfiko kwenye
madaraja ya ufaulu kwa ngazi mbalimbali za elimu kunaleta mkanganyiko
kwani inakuwa vigumu kueleza tafsiri ya madaraja hayo. Kwa mfano
‘Distinction’ ya kidato cha nne inaanza pointi 3.6 wakati ya ualimu
inaanzia pointi 4.4,” alisema Waziri Ndalichako.
Pamoja na hatua hiyo aliyochukua, Profesa Ndalichako alisema bado Serikali haijaamua kuwachukualia hatua viongozi wa NECTA.
MTANZANIA
Mvua kubwa iliyonyesha Dar es Salaam
usiku wa kuamkia jana imesababisha maji kuingia na kujaa ndani ya
jengo maarufu la maduka ya biashara la Mlimani City lililopo pembezoni
mwa barabara ya Sam Nujoma.
MTANZANIA ilifika eneo hilo na
kushuhudia maji yakiwa yametuama na kujaa katika maduka mbalimbali
likiwamo duka kubwa la Nakumat, Duka la Sumsung na benki ya KCB Tawi la
Mlimani City huku wafanyakazi wa jengo hilo wakihangaika kuyatoa nje kwa
kuyachota.
Mmoja wa wafanyakazi wa Benki ya KCB,
alisema mvua hiyo ilisabababisha maji kujaa katika eneo ambalo ujenzi
unaendelea, lililopo pembezoni mwa jengo hilo na baadaye maji hayo
yaliingilia mlango wa nyuma uliopo karibu na benki hiyo.
Alisema maji hayo yamesababisha athari
kubwa kwa benki hiyo ikiwamo kuungua baadhi ya vifaa vya umeme na
kuchelewesha muda wa kufungua benki.
MTANZANIA
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
limepinga uamuzi wa serikali wa kulifuta kwenye daftari la msajili
gazeti la Mawio kwa madai ya kuandika habari za uchochezi.
Pia limeitaka Serikali kutafakari upya
na kwa kina uamuzi wake huo ambao TEF inautafsiri kama mwendelezo wa
ukandamizaji wa tasnia ya habari.
Tamko la TEF lilitolewa Dar es Saalam jana na Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda na Katibu wake, Neville Meena.
Walieleza kutoridhishwa na nia ya
serikali ya kupatikana kwa sheria bora ambazo imeahidi kuzifanyia kazi
kuhusu tasnia ya habari.
“Hii ni aina mpya ya
ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini kwani serikali
zilizopita zilikuwa zikipambana na vitendo vya kufungiwa kwa magazeti
kwa muda maalum lakini si kuyafuta”.
Meena alisema katika serikali zilizopita
adhabu kubwa iliyowahi kutolewa ilikuwa ni kulifungia kwa muda
usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kabla gazeti hilo kurejeshwa kwa umma
na mahakama, kufungiwa siku 90 gazeti la Mtanzania na siku 14 gazeti la
Mwananchi.
“Kwa kuwa hii inaonekana ni dhamira
rasmi ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli
kutumia sheria kandamizi kudhibiti demokrasia na uhuru wa habari,
tunatoa wito kwa watawala wetu kutafakari upya suala hili na kuachana
kabisa na dhamira hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu.
“Uamuzi wa kufuta Mawio (hata kama
lilifanya makosa) umetufikirisha sana, tumetafakari kwa kina na
kujiuliza kwamba habari ambazo ziliandikwa na gazeti hili zilikuwa
hatari kwa kiasi gani kwa nchi kiasi cha kufikiwa uamuzi huo? Ni
magazeti mangapi yatafuata baada ya Mawio ikiwa serikali itaendelea na
ubabe wa aina hii?” alihoji Meena.
Katika hoja zake TEF imesema mfumo wa
sasa wa kushughulikia matatizo au kasoro za taaluma katika vyombo vya
habari ni kandamizi kwa vile unamfanya Waziri kuwa ‘Mhariri Mkuu’ na
ana mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata kama
utakuwa unakinzana na misingi ya taaluma.
“Tunajiuliza ikiwa kwa miezi takriban
mitatu tu tangu kuanza kazi serikali mpya (Novemba 5 mwaka jana
alipoapishwa kuwa rais), serikali ya Dk Magufuli tayari imefuta gazeti
moja itakuwaje katika safari ya miaka mitano ambayo atakuwa madarakani?”
alihoji Meena.
Katibu huyo alisema kwa taaluma ya
habari, Serikali bado imeendelea kujipa mamlaka ya “kukamata, kushtaki,
kusikiliza kesi, kuhukumu na kufunga” kwa sababu kama ilikuwa ni kesi
iliyozaa hukumu ya kufutwa, basi uendeshaji wake ulifanyika katika
“mahakama ya siri”.
Alisema usiri huo matokeo yake ni
hukumu ya siri ambayo haikuwapa wahusika kutoa utetezi wa kile
kilichokuwa kikilalamikiwa dhidi yao.
MTANZANIA
Rais John Magufuli jana
aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Leticia Nyerere nyumbani
kwa familia ya hayati Mwalimu Nyerere, Msasani Dar es Salaam.
Rais aliwasili nyumbani hapo akiongozana na mkewe Janeth na moja kwa moja alikwenda kusaini kitabu cha maombolezo.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja
na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni
Sifue, marais na mawaziri wakuu wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya
Kikwete, Mizengo Pinda na Spika mstaafu, Anna Makinda.
Mwili wa Leticia aliyefariki dunia
Marekani alikokuwa amelazwa uliwasili juzi saa 9 alasiri na kupokewa
na ndugu, jamaa na marafiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Baadaye ulipelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Peter kwa ajili ya Ibada na neno la faraja kwa familia.
Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa waliongoza waombolezaji katika ibada hiyo.
Wengine waliohudhuria ibada hiyo maalum ni Spika mstaafu, Anna Makinda
na Jaji Joseph Warioba.
Jana mwili wa marehemu Leticia ulisafirishwa kupelekwa kijijini Butiama kwa mazishi.
Leticia ambaye ni mtoto wa mwanasiasa
mkongwe, Musobi Mageni alizaliwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza 1954 na
kupata elimu yake ndani na nje ya Tanzania kwa vipindi tofauti.
Marehemu Leticia ambaye ni mtalaka wa mtoto wa baba wa taifa, Madaraka Nyerere ameacha watoto watatu.
HABARILEO
Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda
amewataka wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kujenga hoja vizuri
katika Bunge linalotarajia kuanza vikao vyake wiki ijayo mjini Dodoma,
kwa kuwa wabunge wa vyama vya upinzani wameongezeka bungeni.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Pinda, baada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere, aliyefariki akiwa Maryland nchini Marekani akipatiwa matibabu.
Akizungumzia Bunge la sasa, Pinda
aliwashauri wabunge wanaounda Bunge hilo ambao wengi wao ni vijana,
kuzingatia maslahi ya taifa na sio itikadi za vyama vyao na kuwasisitiza
wabunge wa CCM, kujipanga na kwenda na hoja.
“Kila upande ujiandae kwenye
kuwasilisha hoja, kuna ongezeko la wabunge wa upinzani, sasa wabunge wa
CCM ni lazima nao wajipange na kujenga hoja vizuri,” alisema Pinda.
Alisema kwa mtazamo wake, Bunge ni zuri
na sio la mivutano kwa kuwa kila mmoja amejipanga kuwasilisha hoja
zitakazomgusa mwananchi kwa lengo la kumsaidia.
Akizungumzia utawala wa Awamu ya Tano wa
Rais John Magufuli, Pinda alisema kila zama zina kitabu chake; na kwa
utawala wa Rais Magufuli ameanza vizuri na kuomba Watanzania kumuunga
mkono ili kufanikisha azma ya maendeleo ya taifa.
Alisema katika uongozi wake, ndio muda
wa kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoisha baada ya miaka 10
ijayo, inapaswa kuwa imetekelezwa, hivyo hatua mbalimbali anazozifanya
rais, ikiwa ni pamoja na kubana matumizi, ni mambo muhimu.
“Hatua zinazofanywa na Rais Magufuli ni
za msingi katika kuhakikisha dira ya Taifa ya Maendeleo inatekelezwa, ni
vyema Watanzania wote tumuunge mkono juhudi zake”, alisema Waziri Mkuu
mstaafu Pinda. Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM wamepewa semina
elekezi za namna ya kutekeleza ilani ya chama hicho.
Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape
Nnauye alisema hayo jana wakati akizungumzia kikao cha wabunge wa CCM,
kilichofanyika kwa muda wa siku mbili. Alisema kikao hicho kilikuwa cha
mashauriano juu ya wajibu wa mbunge wa CCM kwa jimbo na chama chake,
kwani asilimia 68 ya wabunge ni wapya na wamefunzwa namna wabunge
watakavyotekeleza Ilani ya CCM.
Pamoja na hayo, aliwataka waandishi wa
habari wasiwe na mijadala yao kwani taarifa nyingi za magazeti wakati wa
kikao hicho, zilikuwa za mitaani kwani mengi yaliyoripotiwa
hayakujadiliwa kwenye semina elekezi. “Bora mngeniuliza kuliko kutafuta
habari za mtaani, mengi ya yaliyoandikwa ni ya kutunga,” alisema Nape.
Wakati huo huo, vikao vya Kamati za
Bunge vinaanza leo mjini Dodoma kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa
majina ya uteuzi wa wajumbe wa kamati. Atafanya hivyo kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha
Bunge, Owen Mwandumbya alisema kwa mujibu wa ratiba, leo kutakuwa na
uteuzi wa Kamati za Kudumu za Bunge na kufuatiwa na uchaguzi wa
Wenyeviti na Makamu wao na wajumbe wa kamati kuelezwa wajibu, kazi na
mipaka ya kazi za kamati, kupokea na kujadili mpango kazi wa kamati
unaoisha Juni 2016.
Mwandumbya alisema Januari 22 kutakuwa
ni mkutano wa wabunge wote na mada zitakuwa ni kanuni za kudumu za Bunge
na uendeshaji wa Bunge, nadharia ya mgawanyo wa madaraka katika mhimili
wa dola, haki na kinga na madaraka ya bunge, mamlaka ya spika na bunge,
kazi, wajibu na masharti ya mbunge.
Pia Januari 23 mkutano wa wabunge wote,
utaendelea na mada zitakuwa pamoja na maadili na miiko ya wbaunge,
nafasi ya mbunge katika usalama wa taifa na itifaki ya mbunge.
Jumapili kutakuwa na kikao cha Kamati ya
Uongozi na Jumatatu Januari 25 ni maelezo ya wabunge wote kuhusu Mpango
wa Taifa wa Miaka Mitano, unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya
Muungano.
HABARILEO
Chama cha Waongoza Watalii nchini(TTGA) kimetoa msaada wa dawa za kupambana na kipindupindu mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa TTGA, Zadocvk Mgeta
alimkabidhi Mkuu wa Mkoa Arusha, Felix Ntibenda dawa hizo huku akisema
dawa na vifaa walivyotoa vinaweza kusaidia kaya 840 kudhibiti
kipindupindu.
Alitaja dawa hizo kuwa ni sabuni, dawa za kuweka kwenye maji na dawa za kuzuia kuharisha.
Alisema wao kama mabalozi wa utalii,
wanajua athari za Arusha kuwa na kipindupindu kwani tayari watalii
wameanza kuogopa vyakula.
“Tumetoa msaada huu kama mchango wetu waongoza watalii lakini tuna imani wadau wengine watajitokeza kutoa misaada,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Ntibenda
alisema amewapa siku saba watendaji wa serikali katika ngazi mbali mbali
mkoani hapa kuhakikisha kipindupindu kinamalizika.
Alisema hadi sasa Arusha ina wagonjwa wanne wa kipindupindu waliolazwa.
Alisema ametoa maagizo kwa wakuu wa
wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wengine, kuhakikisha
wanafika katika maeneo ambayo yamekuwa yakitoa wagonjwa na kudhibiti
maambuikizi mapya.
“Leo nilikuwa na kamati ya ulinzi na usalama mkoa, nimetoa siku saba kipindupindu kiwe kimekwisha Arusha,”alisema.
Ntibenda alishukuru msaada wa TTGA wa dawa na vifaa mbalimbali vya kupambana na kipindupindu walivyokabidhi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Frida
Mokiti alisema msaada huo utapelekwa kwenye maeneo ambayo yamekuwa na
wagonjwa wa kipindupindu.
“Msaada huu utawafikia walengwa na tuna hakika utasaidia sana kupambana na ugonjwa huu,” alisema.
Chama cha waongoza watalii, kina jumla
ya wanachama 6,512 ambao wanafanya kazi ya kuwaongoza watalii katika
hifadhi za taifa na mbuga za wanyama na maeneo ya vivutio vya utalii.
MWANANCHIWakati Serikali ikihaha kuandaa mwongozo kwa vyuo na shule binafsi za msingi na sekondari ili kudhibiti viwango vya ada, hali ni tofauti kwenye shule za kimataifa ambazo zinaonekana kama zinachuana kwa kuwa na ada kubwa.
Wakati ada ya juu kwa shule zinazotumia Kiingereza kuanzia elimu ya msingi ni kati ya Sh2 milioni na Sh3 milioni, ada ya shule za kimataifa zilizopo nchini inafikia hadi Sh60 milioni mwa mwaka, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa mwanafunzi wa chekechea hutakiwa kulipa hadi Sh35 milioni kwa mwaka na fedha hizo hulipwa kwa kutumia dola ya Marekani.
Baadhi ya shule zinapokea wanafunzi wenye asili ya Asia, nyingine hupokea wanafunzi kutoka nchi tofauti bila ya kubagua na ni dhahiri kuwa hata wazazi wa watoto ni wale wa kipato kikubwa.
Shule nyingi zinatumia Kiingereza katika kufundisha masomo yote darasani kwa mitalaa ya kimataifa na walimu wa kigeni ambao wanalipwa mishahara kwa viwango vya kimataifa.
Wanafunzi wanaosoma katika shule hizo wanaishi mazingira tofauti na wanaosoma katika shule za kawaida. Mwananchi lilishuhudia baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwa wamevaa kaptura, bukta na sketi zinazoacha wazi mapaja, kufuga rasta huku wavulana wakiwa huru kufuga nywele, na kuvaa hereni bila kubanwa na sheria.
Shule na ada ni balaa Kwa kuzingatia nyaraka za kujiunga na shule ya International School of Tanganyika (IST) iliyoko Masaki, ada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea ni Sh35.9 milioni; darasa la tatu hadi la tano ada ni Sh 39.8 milioni na kwa wale wanaoingia darasa la sita, la saba na la nane ni Sh46. 3 milioni huku darasa la tisa na la kumi ada ni Sh49.2 milioni.
Mchanganuo wa ada kwa mwanafunzi anayeingia darasa la 11 na 12 ni Sh 59.4 milioni. Mbali ya ada hiyo, mwanafunzi hutakiwa pia kulipiwa gharama za ujenzi, ada ya dharura, fomu ya kujiunga shuleni pamoja na michango mingine ambavyo jumla ni Sh 19.8 milioni.
Shule nyingine ambayo tozo zake ada na michango mingine – imefuata mkondo huo Braeburn iliyoko barabara ya Bagamoyo, Africana.
Ada ya mwanafunzi wa chekechea ni Sh 12.7 milioni kwa mwaka. Mwaka wa kwanza na wa pili ambao ni sawa na darasa la kwanza na la pili hulipa Sh19.3 milioni.
Darasa la tatu hadi la sita Sh21.1 milioni na darasa la saba hadi la tisa (sekondari) ni Sh25.4 milioni. Mwanafunzi anayejiunga na shule ya msingi ya Readers Rabbit iliyoko Masaki hutakiwa kulipa kiasi cha Sh24.1 milioni kwa mwaka.
MWANANCHI
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Zanzibar, Asha Bakari Makame amefariki dunia leo huko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Taarifa zilizothibitishwa na wanafamilia pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo visiwani Zanzibar, Salama Aboud Talib zinasema kiongozi huyo alikuwa ametoka nchini India kwa matibabu.
Naibu Katibu huyo amesema kuwa baada ya Makame kutoka India kwa matibabu, alipitia Dubai kwa mwanae, mahali ambapo mauti ilimkuta mapema leo.
Mbali na wadhifa huo ndani ya UWT, Asha Bakari Makame ameshawahi kuwa Waziri wa Wanawake na Watoto katika serikali ya awamu ya tano visiwani Zanzibar iliyokuwa chini ya Rais Salmin Amour.
Mbali na wadhifa huo, mwanasiasa huyo ameshawahi kuwa mwakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na aliwahi kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
MWANANCHI
Polisi wilayani Mwanga Mkoa wa
Kilimanjaro, wanadaiwa kumlinda raia wa China, anayetuhumiwa kufyatua
risasi kiholela na kuwatisha wananchi.
Hata hivyo, Kamanda Polisi Mkoa
Kilimanjaro, Ramadhan Mungi alisema jana kuwa, hana taarifa ya tukio
hilo lililotokea Julai mwaka jana lakini atalifuatilia.
“Kila mtu anatakiwa kuheshimu sheria za
nchi awe ni mgeni au Mtanzania, matumizi ya silaha yana masharti yake
ambayo ni lazima yaheshimiwe. Nitafuatilia jambo hili,” alisema.
Mlalamikaji katika tukio hilo, Ally
Ng’anzo ambaye ni mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Mega Copper alisema
alishatoa maelezo yao polisi. “Siku hiyo nilipigiwa simu na wafanyakazi
na wananchi wanaoishi jirani na Mchina aliyefyetua risasi kwenye mgodi
wangu.
Nilikwenda lakini namshukuru nilikuta hakuna aliyejeruhiwa,” alisema Ng’anzo.
Alifafanua kuwa wafanyakazi walimweleza
kuwa raia huyo alifyatua risasi tatu, mbili alizielekeza kwenye njia ya
mgodi na nyingine alifyatua hewani na hawakujua sababu.
Hata hivyo, alisema baada ya kufungua
jalada hilo, yeye na mashahidi waliandikisha maelezo yao lakini hadi
sasa wanasubiri kuitwa mahakamani kutoa ushahidi.
Diwani wa Kata ya Shighatini, Enea Mrutu
alisema raia huyo hana uhusiano mzuri na majirani zake lakini
wanashangaa polisi kutochukua hatua dhidi yake.
“Hivi tujiulize kuna Mtanzania anaweza
kwenda China akapewa kibali cha kumiliki silaha. Tuseme amepewa, anaweza
kutisha watu kiasi hiki?” alihoji Mrutu.
Diwani huyo aliwataka polisi kukamilisha
haraka uchunguzi wake akisema ushahidi dhidi ya Mchina huyo ulikuwa
dhahiri lakini hajashtakiwa.
Kwa habari matukio na michezo ni hapa hapa Tangakumechablog
No comments:
Post a Comment