Tuesday, January 26, 2016

UCHAMBUZI NA CANDLE EDUCATION CENTRE TANGA

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni kituo kilichojizolea umaarufu mkubwa kwa kuibua vipaji na kufaulisha wanafunzi na wanaojiendeleza kielimu, Candle wapo Tanga mkabala na bank ya CRDB simu 0715 772746
MTANZANIA
Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Mussa Msafiri (23), alipandishwa kizimbani  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jana akituhumiwa kumwingizia vidole sehemu za siri mtoto (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka minne.
Mbele ya Hakimu Issa Kasailo, Wakili wa Serikali, Matarasa Maharagande, alidai  mtuhumiwa alitenda kosa hilo   Januari 7 mwaka huu maeneo ya Sinza alikokuwa anaishi mwanafunzi huyo.
“Mtuhumiwa ulitenda kosa hilo wakati ukitambua kwamba ni kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alidai wakili.
Baada ya maelezo hayo mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na upelelezi  unaendelea.
Hakimu Kasailo alisema   shtaka hilo linadhaminika hivyo alimtaka mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili waaminifu watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Febuari 27 mwaka huu na mtuhumiwa aliachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Wakati huohuo, Mwalimu wa kujitegemea wa Shule ya Tumaini Nursary School iliyopo Kibamba Hospitali, Rose John (46), amefikishwa  katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na tuhuma za kumjeruhi kichwani mwanafunzi Samwel Isaya kwa kipande cha tofali.
Mbele ya Hakimu Obadia Bwegoge, wakili wa Serikali, Nancy Mushumbusi, alidai   mtuhumiwa alitenda kosa hilo Agosti 27, mwaka jana eneo la Kibamba Hospitali.
MTANZANIA
Sintofahamu kubwa imeghubika  uchaguzi wa  kumpata  mwenyekiti  na makamu  wa Halmashauri ya Wilaya  ya Kilombero baada ya kuzuka vurugu kubwa na kusababisha uchaguzi huo kutofanyika.
Katika vurugu hizo, Mbunge wa Kilombero, Ambrose Elijualikali aliambiwa si mjumbe halali wa mkutano huo jambo ambalo lilipingwa na kuzua vurugu na kuwalazimu  polisi kuingilia kati kumtoa kwa nguvu ukumbini.
Hali hiyo ilitokana na kile kilichodaiwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitaka kuingiza wajumbe ‘mamluki’ ambao ni wabunge wa viti maalum kutoka Singida na Tabora.
Hatua hiyo ilionekana kama  kuongeza idadi na kuwazidi madiwani wanaotokna na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).  Idadi ya wajumbe halali wa Ukawa ni 19 na CCM 18.
Habari kutoka Kilombero zilidai kuwa, awali wajumbe halali wa CCM walisusa kwa muda kuingia katika kikao na baadaye waliingia wakiwa pamoja na nyongeza ya wajumbe wawili ambao ni Asha Matembe (Viti maalum Tabora)    na Fatuma Patrick (Singida).
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Suzan Kiwanga alisema baada ya kuona wenzao CCM wameingiza mamluki walimshauri mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutumia kanuni iliyotumika katika halmashauri za Kinondoni na Ilala, Dar es Salaam lakini aligoma na kutaka kulazimisha wabunge hao kushiriki katika uchaguzi huo.
“Mbunge halali wa Kilombero amedhalilishwa akiambiwa hapaswi kupiga kura si diwani… ni aibu mkurugenzi kushindwa kuongozwa na sheria ili kuwabeba CCM.
MTANZANIA
Kasi ya Rais John Magufuli imeendelea  baada ya kuhamia katika Mamlaka  ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Hivi sasa alichokifanya ni kutengua uteuzi na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo,  Dickson  Maimu na wenzake wanne.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli imetekelezwa  siku chache baada ya kufuta uteuzi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk. Feisail Issa, ambaye ilidaiwa alitaka kupigana na Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo.
Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais   amechukua hatua hiyo baada ya kupata taarifa ya matumizi ya Sh bilioni 179.6 kiasi ambacho alisema ni kikubwa ikilinganishwa na kazi iliyofanywa na NIDA.
Mbali na Maimu,   waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande,  Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
“Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo (jana), baada ya utenguzi huo, Maimu na wenzake wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi,” alisema Balozi Balozi Sefue.
Alisema Rais Magufuli amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya Taifa licha ya kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika.
Kutokana na  hatua hiyo mkuu huyo wa nchi amezielekeza mamlaka mbalimbali za uchunguzi na ukaguzi zifanye uchunguzi na ukaguzi wa namna fedha hizo zilivyotumika.
“Rais amezielekeza Mamlaka ya Udhiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa ununuzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwamo ukaguzi wa ‘value for money’ (thamani ya fedha zilizotumika na vitambulisho vilivyotolewa) baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
“Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la,” alisema.
Mchakato wa mradi wa vitambulisho vya Taifa  ulianza   mwaka 1972 ambako sheria ya vitambulisho hivyo ilitungwa mwaka 1986 na mwaka 1995 tenda ya kwanza ikatangazwa ambayo hata hivyo haikufanikiwa.
Mwaka 2004 upembuzi yakinifu ulifanyika na Febuari mwaka 2007 ushauri ukakubaliwa na kuiteua kampuni ya Gotham kuwa mshauri mwelekezi wa mradi huo.
Wakati wa kutangaza  tenda ya utengezaji wa vitambulisho vya Taifa, zaidi ya kampuni 140 ziliomba tenda hiyo na  Kampuni ya Iris Corporation Bhd ya Malaysia ilishinda tenda   kwa kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya Sh bilioni 200.
HABARILEO
Mtoto wa miaka 11, Nchambi Tungu, ameuawa kikatili na mama yake mzazi kwa kuchapwa fimbo kisha kumfunga kamba shingoni na kumning’iniza kwenye tawi la mwembe ili ionekane kuwa amejinyonga mwenyewe.
Inaelezwa kuwa mama wa mtoto huyo, Sado Roketi (26) mkazi wa kitongoji cha Mnyakasi, kijijini Ikuba, wilayani Mlele, mkoa wa Katavi alimuua mwanawe huyo baada ya kukataa kumfulia nguo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho alipozungumza na gazeti hili kwa simu jana kutokea wilayani Mpanda.
Alisema tukio hilo ni la Januari 23, mwaka huu saa moja jioni katika Kitongoji cha Mnyakasi. Alisema siku ya tukio mtuhumiwa alimpatia mwanawe huyo nguo amfulie lakini mtoto huyo alikataa kuzifua akaendelea kucheza na wenzake.
“Ndipo mama huyo kwa hasira alipoamua kuchukua fimbo na kuanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia kifo, aliubeba mwili na kuutundika kwenye matawi ya mti wa mwembe baada ya kumfunga kamba shingoni na kumwacha akining`inia ili ionekane alijinyonga mwenyewe,” alieleza Kidavashari .
Alisema mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
MWANANCHI
Wataalamu wasema kuna hatari ya kuwindwa na majangilihivyo wanatakiwa kupewa ulinzi wa kutosha Mwanasayansi Dk Derek Lee amegundua twiga albino kwenye hifadhi ya mbuga ya Tarangire iliyopo katika Mkoa wa Arusha nchini Tanzania.
Mtafiti huyo Dk Derek Lee, alipiga picha mbalimbali zikiwa zinamwonyesha mnyama huyo akiwa katika kundi kubwa la twiga, huku akiwa na rangi ya kipekee ikilinganishwa na twiga wengine duniani.
Dk Lee, alimgundua twiga huyo wakati akifanya utafiti kwenye mbuga hiyo na nyingine za wanyama za barani Afrika, Taarifa iliyoripotiwa na shirika la habari nchini Uingereza kupitia gazeti la Dailymail zimeeleza kuwa, twiga huyo adimu kupatikana duniani iwapo atahifadhiwa atakuwa kivutio cha pekee katika mbuga hiyo.
Twiga huyo anayejulikana kitaalamu kwa jina la ‘Omo’ likimaanishwa twiga mweupe/mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino’, alionekana akizunguka katika mbuga hiyo katikati ya twiga wengine.
Dk Lee ambaye pia ni mtaalamu wa viumbe na mwanzilishi na mwanasayansi kutoka Wild Nature Instute, alimnasa twiga huyo katika kamera yake wakati akifanya uchunguzi huo kuhusu wanyama. Lee (45) alisema: “Omo ni ‘leucistic’ hii inamaanisha seli zake nyingi katika ngozi hazina uwezo wa kutengeneza rangi, hivyo anakuwa ni albino, lakini hawi mweupe katika ngozi yake yote na wakati mwingine anakuwa na macho mekundu au ya bluu kama ilivyo kwa albino.
“Ni hali ya kimaumbile ‘Omo’ni aina pekee ya twiga ambaye anajulikana duniani na ndiye pekee aliyeonekana Afrika kwa takribani miaka mitatu sasa, pia tuligundua uwapo wa wanyama kadhaa wakiwamo nyati na mbuni albino katika mbuga ya Tarangire,” alisema “Omo anaonekana kwa nadra sana na mara nyingi anapoonekana huwa pamoja katika kundi kubwa la twiga wengine ambao huwa hawaonyeshi kushangazwa na rangi aliyonayo.” “Kwa utafiti uliofanyika twiga huyo kwa sasa ana umri wa miezi 15, aliishi mwaka wake wa kwanza kwa kunusurika kuuawa na wanyama wakali kulingana na utofauti wake, kipindi ambacho ni cha hatari kwa twiga wadogo hasa kutokana na kushambuliwa zaidi na simba, chui na fisi ambao huwatafuna,” alisema.
Alisema uwezekano wa twiga huyo kukua kwa sasa ni mkubwa, lakini bado wanyama wakubwa wamekuwa wakimwinda na binadamu kwa ajili ya nyama za porini, na huenda rangi aliyonayo inaweza kumfanya yeye kuwindwa zaidi.
“Sisi na washirika wetu ambao wanafanya kazi katika mbuga mbalimbali na wanaopambana na ujangili tupo kwenye mazungumzo ili kumsaidia Omo huyu na wengine watakaopatikana kuhifadhiwa vizuri ili waishi kwa muda mrefu.
Tunaimani kwamba wataishi miaka mingi na baadaye atazaa na kupata watoto watakaofanana na yeye na hivyo kuongeza vivutio vya twiga weupe duniani,” alisema Dk Derek.
MWANANCHI
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, amemvua madaraka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Augustino Kapinga kwa kushindwa kusimamia watumishi wa chini yake.
Waziri Simbachawene alifikia uamuzi huo, baada ya usimamizi duni wa Kapinga kusababisha wafanyakazi hao kutoa maagizo ya kuchangisha michango ambayo Rais aliizuia.
Mbali na Kapinga, Waziri Simbachawene jana alimsimamisha Ofisa elimu vifaa na takwimu­wa msingi katika Manispaa hiyo, Josephine Akimu kwa kudharau maelekezo ya kiongozi wake na kusaini barua kwa niaba ya mkurugenzi huku akitumia jina la Ofisa Elimu, Scola Kapinga ambaye pia amepewa onyo kali.
Sababu za kuwavua madaraka watumishi hao ni kutokana na kuandika barua yenye kumbukumbu HMD/ED/50/2/VOL 11/61 ya Januari 17, mwaka huu iliyosambazwa kwa walimu wakuu wote wakitakiwa kuchangisha michango katika shule za msingi wakati Serikali ilishazuia.
Barua hiyo ilikuwa na maelekezo ya kuwataka walimu wakuu kuchangisha michango ya maji, mlinzi na umeme, jambo ambalo lilimfanya waziri kufanya safari ya kushtukiza Shule ya Msingi Dodoma Makulu, na kujionea michango hiyo lakini akabaini kulikuwa na barua za maelekezo kutoka ofisi ya mkurugenzi.
“Ieleweke kuwa uchangiaji ulioelekezwa katika barua ya mkurugenzi ni kinyume na maelekezo ya Rais John Magufuli, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ibara ya 3.1.5 na ilani ya Uchaguzi ya CCM ibara ya 52 (a) ya mwaka 2015 ya kutoa elimu bure bila ya malipo,” alisema Simbachawene.
Alisema maelekezo ya maofisa hao ni kinyume na mwongozo namba DB.297/507/01/39 wa Desemba 28, 2015 uliotolewa na ofisi ya Tamisemi kwa makatibu Tawala wa mikoa, wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri zote kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi za Serikali katika kutekeleza kaulimbiu ya elimu bure.
Kuhusu mkurugenzi, waziri alisema mtumishi huyo amekuwa na shida kwani hivi karibuni watumishi walio chini yake katika kitengo cha biashara walisimamishwa baada ya kukiuka sheria na taratibu, jambo linaloonyesha kuwa amekuwa akichangia kwa kutoa maelekezo au ufuatiliaji duni.
Hata hivyo, Waziri alisema michango inaweza kuchangishwa kwa w
NIPASHE
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kwa madai ya kumtukana Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Katika hati ya madai, inadaiwa kuwa Kafulila alitoa ligha ya matusi kuwa “mtu kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa Wilaya. Unamchukua shangingi la mjini huko unasema aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya akija hapa mana yake polisi wampigie saluti, kuna polisi wenye akili hapa kuliko huyu Mkuu wa Wilaya, wanampigia saluti kwa basi tu mana yake hana akili.”
Kutokana na maneno hayo inaonyesha kuwa Hadija si mtu wa maadili, kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Kafulila alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, George Buyamba, na kusomewa mashitaka hayo.
Hata hivyo, Kafulila alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana ya mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. 500,000.
Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Raymond Kimbe alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo  umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali.
Hakimu Buyamba alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Febuari 18, mwaka huu.
Kafulila anadaiwa kutoa lugha ya matusi Agosti Mosi, 2013 katika Kata ya Nguruka eneo la Nyumba ya Wageni ya Wilaya ya Uvinza, dhidi ya Hadija.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo jana ya saa tatu  asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na umati mkubwa wa watu pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, wapambe wake na madiwani wa vyama mbalimbali vya siasa.
Awali, kesi hiyo yenye namba 6/2015 ilifutwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma, Slivester Kainda, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani zaidi ya siku 60.
Baada ya Hakimu Kainda kufuta kesi hiyo, DPP ameirudisha tena mahakamani hapo na kusomwa tena kwa mara ya pili.
NIPASHE
Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya, amewashinda wakazi wanne wa jimbo hilo waliofungua kesi ya kupinga ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na  kumshinda mpinzani wake, Stephen Wasira, kutoka CCM.
Katika kesi hiyo, Bulaya alikuwa akitetewa na mwanasheria maarufu nchini, Tundu Lissu, huku watuma maombi wakitetewa na Constantine Mutalemwa.
Akitoa uamuzi ya ‘kuipiga’ chini kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Gwae, alidai walalamikaji katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo wala hakuna sehemu waliyoonyesha kuathirika na uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 2015, mjibu maombi wa kwanza (Bulaya), alikuwa akishitakiwa na Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira, ambao walikuwa na mawakili wawili, ni Mutalemwa na Denis Kahangwa.
Aidha, watuma maombi hao walikuwa wakimlalamikia msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambaye ni mjibu maombi wa pili na mwanasheria mkuu wa serikali, ambao wote walikuwa wakitetewa na wakili Paschal Malongo.
Jaji Gwae alisema malalamiko ya waombaji hao hayakuonyesha  walivyoathirika baada ya Bulaya kushinda uchaguzi na ‘kumgaragaza’ Wasira.
Awali ilidaiwa na walalamikaji hao kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, haukuzingatia sheria na taratibu kwa mgombea wa CCM (Wasira), baada ya kuomba kura zihesabiwe upya lakini alikataliwa na wala hakupewa nakala ya matokeo.
Pia walidai idadi ya kura zilizotolewa katika fomu namba 24B, zinatofautiana na idadi ambayo ilitolewa na Tume ya Uchaguzi (Nec) iliyoonyesha idadi ya wapiga kura ni 69,369 wakati idadi ya vituo vya kupigia kura vikitofautiana na ile iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi ya vituo 199 huku vya Nec vikiwa 190.
Wakati uamuzi huo ukitolewa, Bulaya na wakili wake, Lissu hawakuwapo mahakamani hapo.
NIPASHE
Mkutano wa Pili wa Bunge la 11 unatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma huku pamoja na shughuli nyingine zilizopangwa kufanyika, wabunge watajadili mpango wa maendeleo awamu ya pili na hotuba aliyoitoa Rais Dk. John Magufuli bungeni, lakini shughuli pevu ikionekana kuwa upande wa upinzani ambao umejipanga kuibana serikali juu ya hali ya kisiasa ya Zanzibar, Escrow pamoja kero ya maji inayowakabili wananchi.
Kwa mujibu wa wabunge wa upinzani, watalazimika kutumia mwanya wa kuomba mwongozo wa kiti cha spika na maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu kuwasilisha hoja zao.
Hata kwa wale ambao watachangia hotuba ya Rais Magufuli, wengi watajikita kujadili kasoro za serikali zilizoonyeshwa na yale ambayo yanaonekana ni magumu kutekelezeka.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, kuhusu ratiba ya mkutano huo wa bunge, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Bungeni, Owen Mwandumbya, alisema mkutano utaanza leo na kumalizika Februari 5, mwaka huu ukiwa na shughuli za kujadili hotuba ya rais, kujadili na kuridhia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango.
Mbali na shughuli hizo, alisema kutakuwa na kiapo cha uaminifu kwa wabunge 11, ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na rais mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kwanza wa bunge.
Mwandumbya alisema katika mkutano huo, jumla ya maswali ya msingi ya kawaida 125, yanategemewa kuulizwa na kujibiwa.
“Chini ya Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari 2016, utaratibu wa kumuuliza waziri mkuu maswali ya papo kwa papo kila Alhamisi utaendelea. Hivyo kwa kufuata uzoefu, inakadiriwa kuwa maswali ya msingi 16 yataulizwa na kujibiwa na waziri mkuu,” alisema Mwandumbya.
Aidha, alisema kutakuwa na shughuli za chaguzi mbalimbali za kuwapata viongozi wa bunge na wawakilishi wa bunge katika vyombo na taasisi mbalimbali.
Alifafanua kuwa, leo utafanyika uchaguzi wa wenyeviti watatu wa bunge na kwamba juzi Kamati ya Uongozi ilipendekeza majina ya wabunge watatu ambao ni Najma Giga, Andrew Chenge na Mary Mwanjelwa kuwania uenyekiti huo.
Mbali na uchaguzi huo pia kutakuwa na uchaguzi  wa wajumbe saba wa Tume ya Utumishi wa Bunge, wajumbe watano wa Bunge la Afrika (PAP), wajumbe watano wa Jukwaa la Wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF), Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe 12 wa Kamati ya Utendaji wa Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA) pamoja na  wajumbe watano wa Umoja wa Mabunge duniani (IPU).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Viti Maalum, Rose Kamili (Chadema), alisema kwa sasa wanaangalia suala la Zanzibar na hatma yake.
Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche(Chadema), alisema kabla ya kuanza kujadili mpango wa maendeleo ya taifa, watahakikisha bunge linajadili hali ya kisiasa Zanzibar kwa sababu mpango unajumuisha na Zanzibar na ni kwa Watanzania.
Alisema katika kujadili hotuba ya rais na mpango huo, lazima serikali iseme wamefikia wapi kuhusu suala la Escrow kwa watu waliochukua fedha kwa magunia katika benki ya Stanbic ili wajulikane ni akina nani.
“Katika mpango wa miaka mitano ambao tumeuona, Janeth Mbene ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, amekiri serikali ilifanya makosa kubinafsisha viwanda, hivyo serikali inatakiwa ikiri kuwa ilifanya makosa kuuza nyumba hizo.
“Kwenye mpango huu, wamezungumza kupunguza matumizi ya serikali wakati majaji, makatibu wakuu na wakuu wa idara mbalimbali wanakaa kwenye mahoteli Dar es salaam,”alisema Heche.
Alisema lazima serikali ikiri pia katika hilo, na kwamba mpango huo umejaa takwimu za uongo, huku akitolea mfano upatikanaji wa maji ambao alisema mpango uliweka wazi kuwa unasema maji yamepatikana kwa asilimia 68 wakati hata katika jimbo lake hakuna huduma hiyo.
“Maji hayapo kule, hizi ni takwimu za uongo za kupika, hakuna kitu kilichofanyika, hizo asilimia 68 wamezitoa wapi? Haya kwenye afya juu ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto, sera ya afya inasema kila kata kutakuwa na zahanati na kituo cha afya lakini kwenye jimbo langu lenye kata 26, tatu tu ndio zina vituo vya afya, vijiji vingi havina zahanati, nadhani ni mambo ambayo yataibuka katika kujadili huu mpango,”alisema Heche.
Alisema ukizungumzia kipindupindu, ni dalili kuwa bado hakuna maji safi na salama, hivyo mpango kama unasema uongo haiwezekani kujadili kwenda mbele, lazima useme ukweli kwa takwimu halisi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Pendeza, alisema kwanza watataka serikali iseme ni kwa vipi itashirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha uwekezaji wa viwanda unakuwa na tija.
“Kwenye hotuba yake rais, alisema mambo ya viwanda, lakini ukiangalia kwenye maeneo mengi wanazungumzia kuacha suala  hilo kwa sekta binafsi, kwa hiyo sisi tunataka aeleze vizuri kwa namna watakavyoshiriki kwenye suala la viwanda na ajira ziongezeke kwa vijana,” alisema Pendeza.
Mbunge wa Mtera Livingston Lusinde (CCM),  alisema ataibua suala la Bandari Kavu Dodoma.
Pia, alisema takwimu ambazo serikali imewasilisha bungeni juu ya maji vijijini kupitia mpango wa maendeleo ya awamu ya pili hazipo sahihi kwa hiyo ataitaka serikali iwasilishe majina ya vijiji vilivyopata maji.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment