Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle Education Centre Tanga ni mabingwa na kitovu cha kufaulisha wanafunzi na wenye kujiendeleza kielimu, Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MTANZANIA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani
ujumbe wenye maudhui ya ubaguzi ulioandikwa kwenye bango lililobebwa na
mmoja wa wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya sherehe za miaka
52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mawasiliano na Umma wa CCM, Daniel Chongolo, ilieleza kwamba chama hicho kimesikitishwa na ujumbe huo na kuwaomba radhi Watanzania.
“Tumesikitishwa sana na ujumbe
huo uliokuwa katika bango hilo, CCM kinaomba radhi kwa ujumbe huo,
kinapinga na kinakemea kabisa fikra, hisia na mitazamo yoyote yenye
maudhui ya kibaguzi.
“Ujumbe huo si tu kuwa una
maudhui ya kibaguzi, bali pia unaenda kinyume kabisa na falsafa na
shabaha ya waasisi wa Mapinduzi hayo matukufu ya mwaka 1964 na
unapingana na misingi na itikadi ya CCM inayohimiza umoja na mshikamano
wa kitaifa,” alisema Chongolo katika taarifa yake.
Hatua hiyo ya CCM imekuja baada ya
wananchi mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kulaani bango hilo
ambalo walionya kuwa halina nia njema na mshikamano wa Taifa.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo,
Zitto Kabwe, alisema siasa za namna hiyo hazifai na zinapaswa kulaaniwa
na kila mpinga ubaguzi nchini.
“Nitashangaa sana kama wakubwa CCM
hamtaomba radhi kwa siasa hizi mbaya kabisa ‘What will be the stop’,”
alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.
Kutokana na tafrani hiyo ya ubaguzi,
nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani kile
walichodai chembechembe za ubaguzi wa aina yoyote visiwani humo.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya
Mawasialino wa chama hicho, Tumaini Makene, ilieleza kwamba Chadema kwa
kusimamia misingi ya utaifa hasa haki, uadilifu, utu, umoja na uzalendo
haiko tayari kuona Taifa linafikishwa huko na hata kuhatarisha maisha ya
jamii nzima ya Watanzania.
“Chadema tunalaani na kupinga
kwa nguvu zote mipango, mikakati, tabia na chembechembe za ubaguzi wa
aina yoyote, ukiwemo huu wa kisiasa ambao sasa unaanza kusakafiwa kwa
ubaguzi wa rangi.
“Kwa sababu tunaamini wanaobeba
ajenda hii hawataishia hapo bali watazidi kutugawa Watanzania pia kwa
ukanda, ukabila, udini kama wamekuwa wakijaribu kuchochea,” alisema Makene.
Kutokana na kauli hiyo, alisema
wanamkumbusha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu,
kuhakikisha anawachukulia hatua wale wanaoeneza chuki na hatari ya
kuvurugika kwa amani kwa ujumbe wa kibaguzi.
MTANZANIA
Mwili wa marehemu Leticia Nyerere unatarajiwa
kusafirishwa kutoka Marekani kuja nchini kesho kwa ajili ya mazishi
yaliyopangwa kufanyika katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara.
John Shibuda ambaye ni msemaji wa
familia ya Musobi Mageni, alisema kuwa mwili wa marehemu Leticia
utasafirishwa kutoka Marekani alipofariki dunia na baadaye utaagwa
katika nyumba ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Msasani
jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa.
“Mwili wa marehemu unatarajiwa
kusafirishwa kuelekea Musoma siku ya Ijumaa kwa ajili ya mazishi na
suala lililokuwa limechelewesha ni pamoja na kupatikana haraka cheti cha
kifo nchini Marekani,” alisema Shibuda.
Naye Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa
aliyekwenda kutoa salamu za pole nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Msasani,
aliwaasa ndugu na jamaa wa marehemu kuendelea kumwombea marehemu huku
akisisitiza kuwa Leticia alikuwa ni mchapakazi wakati alipokuwa ni
mbunge.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Leticia
aliyewahi kuwa mbunge wake katika Bunge lililopita.
Taarifa ya Chadema iliyosainiwa na ofisa
habari wa chama hicho, Tumaini Makene ilisema: “Tunatoa pole kwa
familia, ndugu jamaa na marafiki katika wakati huu mgumu wa kuondokewa
na mpendwa wao.
“Mwenyezi Mungu awatie moyo wa ujasiri na subira katika wakati huu mgumu wa majonzi ya msiba huo.”
Taarifa hiyo ya Chadema ilisema kama
chama watamkumbuka Leticia kwa mchango na ushiriki wake wakati wote
alipokuwa mwanachama wao huku akiwa miongoni mwa watu waliopata fursa za
kuwa wabunge kupitia chama hicho.
Leticia ambaye alikuwa mbunge wa viti
maalumu katika Bunge la 10, alifariki dunia Januari 9 mwaka huu katika
Hospitali ya Doctors Community iliyopo MaryLand nchini Marekani ambako
alikuwa amelazwa tangu mwishoni mwa mwaka jana akitibiwa maradhi
yaliyokuwa yakimsumbua.
Aliolewa na mtoto wa Baba wa Taifa,
Madaraka Nyerere mwaka 1996 na kufanikiwa kupata watoto watatu ingawa
baadaye walitengana na kuhamia nchini Marekani ambako alichukua uraia na
kuishi kabla ya kurejea nchini ambapo mwaka 2010 aliteuliwa na Chadema
kuwa mbunge wa viti maalum kwa miaka mitano.
Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere,
Joseph Butiku alisema juzi kuwa mwili wa marehemu Leticia unatarajiwa
kusafirishwa kutoka nchini Marekani kwa ajili ya maziko.
MTANZANIA
Hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, jana
ameonekana hadharani katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya
Mapinduzi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Jecha ambaye inaaminika alikuwa
mafichoni tangu alipotangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar
Oktoba 28, mwaka jana, alionekana ameketi kwenye jukwaa kuu la
viongozi, jirani na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Kuonekana kwa Jecha hadharani kumezua
mijadala mitaani na hata katika mitandao ya kijamii, huku wengi wakihoji
alikuwa wapi mara baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi.
Watu mbalimbali wamekuwa wakihoji
kuonekana kwa Jecha hadharani jana, siku ambayo Dk. Shein alitumia
maadhimisho ya Mapinduzi kutangaza kwamba uchaguzi wa marudio Zanzibar
iwe isiwe utafanyika.
Oktoba 28, mwaka jana majira ya saa sita
mchana kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar zilizopo Kilimani
mjini Unguja, ilikuwa ndiyo siku ya mwisho kuonekana Jecha hadharani.
Siku hiyo huku akiwa chini ya ulinzi wa
vijana wawili wanaoaminika kuwa ni makomandoo wa Jeshi la Ulinzi wa
Tanzania (JWTZ) waliovaa kiraia, Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi wa
Zanzibar mbele ya vyombo vichache vya habari.
Alitumia dakika mbili tu kuvitangazia
vyombo hivyo vya habari juu ya adhima yake ya kuufuta uchaguzi na kutoa
sababu zilizomfanya kufanya hivyo ikiwamo kuharibiwa kwa uchaguzi
kisiwani Pemba.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa taarifa yake kwa vyombo hivyo, Jecha hakutaka kuulizwa maswali.
Oktoba 27, mwaka jana ikiwa ni siku moja
kabla ya kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi, Jecha pia hakuonekana
kwenye kituo cha kutangaza matokeo kilichokuwa katika Hoteli ya Bwawani
kwa kile kilichodaiwa alipata matatizo ya kiafya na hivyo kumwachia kazi
hiyo Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.
Siku hiyo majira ya saa kumi jioni,
askari wa JWTZ walizingira kituo cha Bwawani na kuwaamuru watu waliokuwa
ndani kutotoka nje na hata wale walioko nje ya kituo hicho kutosogea.
Watu waliokuwa ndani ya kituo hicho
wengi wao walikuwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya ndani na
nje ya nchi pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa
waliofika kusikiliza matokeo ya uchaguzi.
MTANZANIA
NI roho mkononi. Hivyo ndivyo unavyoweza
kusema kwa sasa juu ya hali ya usalama ilivyo katika Jiji la Dar es
Salaam na maeneo kadhaa nchini pindi mtu anapokuwa amebeba kiwango
kikubwa cha fedha.
Matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha
katika jiji hilo yamekuwa sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au
kutoa fedha benki kuvamiwa, kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na
majambazi wanaotumia pikipiki aina ya Boxer.
Hali hiyo inawafanya watumiaji wa huduma za benki zilizo ndani ya jengo la Mlimani City maisha yao kuwa hatarini, hasa wale wateja wanaotoa fedha nyingi kutokana na kukumbwa na matukio ya kuuawa na kuporwa fedha.
Hali hiyo inawafanya watumiaji wa huduma za benki zilizo ndani ya jengo la Mlimani City maisha yao kuwa hatarini, hasa wale wateja wanaotoa fedha nyingi kutokana na kukumbwa na matukio ya kuuawa na kuporwa fedha.
Jengo hilo lenye matawi ya benki sita, limekuwa likikumbwa na matukio ya mauaji kwa wateja wanaotoa fedha nyingi na majambazi.
Matukio mengi ambayo yamekuwa yakitokea
kwa wateja hao, majambazi wamekuwa wakitumia pikipiki aina ya Boxer
ambayo ina uwezo mkubwa wa kukimbia.
Miongoni mwa matukio ya kusikitisha
yakihusisha moja ya benki zilizopo Mlimani City ni lile lililotokea juzi
ambapo mtu mmoja aliuawa na taarifa zake kuzagaa kwenye mitandao ya
jamii.
Inaelezwa kuwa mtu huyo aliuawa na
majambazi wakati akitoka kwenye moja ya benki ndani ya jingo hilo
kuchukua kiasi cha Sh milioni 10 na kuanza safari ya kuelekea eneo la
Tegeta Salasala ambako alikuwa akifanya shughuli za ujenzi wa nyumba
yake.
Taarifa iliyosambaa mitandaoni inasema
kwamba tukio hilo lilitokea jirani na mtoa taarifa hiyo aliyeamua
kuwatahadharisha wananchi wengine kutochukua fedha nyingi katika benki
zilizo eneo hilo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema
kwamba mtu huyo alipotoa fedha hizo, majambazi walianza kumfuata kwa
nyuma, wakampita na kumzuia kwa mbele.
“Majambazi walipomzuia kwa mbele
walimtaka atoe milioni 10 aliyochukua benki, baada ya kutoa hiyo fedha
ndipo walimpiga risasi,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda
kutajwa jina lake gazetini.
Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya
kijamii zinaeleza kwamba katika matukio hayo yanayotokea mfululizo, hivi
karibuni maeneo ya Bamaga jirani na Hongera Bar, mtu mmoja na mkewe
walivamiwa na majambazi walipokuwa wanatoka kuchukua fedha kiasi cha Sh
milioni 13 katika benki mojawapo iliyopo Mlimani City.
Baada ya watu hao kuchukua fedha, majambazi yaliwafuata kuanzia hapo Mlimani City hadi Bamaga na kuwataka wawape fedha.
Inaelezwa kwamba jambo lililosaidia, mtu
huyo alikuwa amezitenganisha fedha hizo na kuwapa laki 5, lakini
walipatwa na hasira na kumhoji kuhusu fedha nyingine alikokuwa
amezipeleka hali iliyofanya wampige risasi begani.
Hali hiyo ilimfanya mke wake awaongeze
laki moja, na wakafanikiwa kubaki na kiasi kingine cha fedha walizokuwa
wamezificha kwenye mlango wa nyuma.
Taarifa nyingine inaelezea kwamba mama
mmoja aliyejulikana kwa jina la Mama Joshua alivamiwa na majambazi baada
ya kuchukua fedha kiasi cha milioni 4 kwenye benki mojawapo ya Mlimani
City.
Inaelezwa kwamba baada ya mama huyo
kufika eneo la Kwa Kakobe, majambazi walimpita na kumsimamisha baada ya
kujifanya kuwa wanamjua na aliposimama walimlazimisha kutoa kiasi hicho
cha fedha alichokitoa benki na akawapa kunusuru maisha yake.
Kwa sasa benki zilizopo Mlimani City
zinaonekana kuwa eneo hatari la kutolea fedha nyingi kutokana na taarifa
kwamba upo uwezekano wa kuwapo kwa wafanyakazi wa baadhi ya benki hizo
kushirikiana na majambazi.
Tukio jingine lilitokea mwaka jana na
kushuhudiwa na gazeti hili, ambapo mtu mmoja alipigwa risasi mbili
majira ya saa 6 mchana na kuporwa fedha akiwa katika gari maeneo ya
Sinza Kijiweni karibu na Baa ya Deluxe.
Dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo
lililoshambuliwa namba T 236 DDT aliyefahamika kwa jina moja la Abasi,
alisema fedha ambazo majambazi hao walichukua zilitolewa benki moja ya
eneo la Mlimani City.
“Baada ya kuingia na kuegesha gari hapa
jirani na hopitali hii ya watoto, alikuja mtu mmoja aliyekuwa amevaa
koti jeusi akiwa ameshuka kwenye pikipiki aina ya Boxer na alipofika
alisogelea gari letu na kufunua koti lake alilokuwa amebeba bunduki ya
SMG,” alisema.
Alisema mtu huyo alimwelekezea silaha
mtu aliyekuwa nyuma ya gari na kumwamuru kutoa fedha, lakini akaambiwa
hakukuwa na fedha ndani ya gari.
“Baada ya kuona anabisha alimpiga risasi
ya kwanza, akageuza SMG kwangu nikakimbia, akafyatua lakini hakunipata
ndipo nikasikia risasi nyingine ikipigwa.
“Baada ya muda kulikuwa kimya na
niliporudi tena nikakuta majambazi wakiwa wameshaondoka na mkoba wa
fedha ‘briefcase’ na kutokomea nao hali iliyofanya wananchi kusogea na
kumsaaidia mzee ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya kwa risasi,” alisema
Abasi.
MTANZANIA ilipomuuliza dereva huyo kiasi
cha fedha kilichoibiwa alisema majambazi hao waliondoka na kiasi kidogo
cha fedha na si zote Sh milioni 10.
Tukio jingine lililotokea mwaka jana
lilihusisha majambazi kumpora mama mmoja kiasi cha shilingi milioni 10
na kutokomea kusikojulikana.
“Alipotoka benki, majambazi hayo
yalimfuata na kuligonga gari lake na ndipo dada huyo aliposimama ili
aangalie nani kagonga gari yake ambapo jambazi mmoja alishuka na kumpiga
risasi ya kifuani na kutokomea na kiasi hicho cha pesa,” alisema
shuhuda wa tukio hilo.
Tukio jingine lilitokea eneo hilo Agosti
22, mwaka juzi likimuhusu Edson Cheyo mmiliki wa Kampuni ya Sowers
African iliyopo jirani na Mlimani City aliyeporwa Sh milioni 18.
Cheyo alipigwa risasi ya kifuani na
begani na majambazi waliomvamia wakiwa wamepanda pikipiki na walichukua
fedha zote na mwenyewe kufariki dunia akiwa anapelekwa hospitali ya
Mwananyamala.
Tukio jingine la mauaji ni lile la Sista
Brigita Mbanga, mkazi wa Makoka pamoja na dereva Mack Patrick ambao
waliuawa eneo la Ubungo Kibangu wakati wakitoka kuchukua fedha Mlimani
City.
Wananchi wamekuwa wakihoji ni kwa jinsi gani majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyekwenda benki ama kuweka au kuchukua fedha.
Hata hivyo, imekuwa ikidaiwa kuwa baadhi
ya benki nchini zimekuwa zikidaiwa kuajiri baadhi ya wafanyakazi walio
kwenye mtandao wa majambazi kutokana na wateja wengi kupigwa risasi na
kufa wakitoka kuchukua pesa.
“Haiwezekani hata mtu anapovamiwa na
majambazi kabla ya kuuawa au kujeruhiwa huambiwa tupe miliooni 10 ambazo
ndiyo zilizochukuliwa benki. Je, jambazi amejuaje kama wewe una kiasi
hicho cha fedha?” alisema mmoja wananchi anayefanya shughuli zake
Mlimani City.
Mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam,
Salum Mashati, alisema: “Haiingii akilini, utasikia mtu kaporwa fedha
akitoka benki. Eti majambazi wanasema kabisa toa hizo milioni 20,
wanajuaje kuwa una kiwango hicho? Huenda watu wa benki wanashiriki
uhalifu huu.”
Hata hivyo, meneja wa tawi moja la benki
lililopo Mlimani City, ambaye hakupenda jina lake litajwe, alikanusha
madai hayo na kusema hawana ushirikiano na majambazi hao wanaofanya
uhalifu katika maeneo hayo.
“Si kweli kwamba benki zinashirikiana na
majambazi kufanya uhalifu huu. Kwanza wahudumu (bank tellers)
hawaruhusiwi kuingia na simu wanapohudumia wateja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camillus Wambura, alipotakiwa kuelezea namna polisi ilivyojizatiti
kudhibiti matukio hayo yanayotokea katika benki hizo, alisema hakuna
tukio hata moja ambalo limewahi kutolewa taarifa polisi.
“Hivi kweli inawezekanaje tangu kumeanza
kutolewa taarifa hizo hakuna taarifa iliyowahi kutolewa polisi na mengi
ya matukio ambayo yemekuwa yakiripotiwa yakifanyiwa ufuatiliaji
yanakutwa ni uzushi, kwani hakuna tukio linalotokea hapa Dar es Salaam
na wahusika walimalize kwa kukaa kimya,” alisema Kamanda Wambura.
Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa endapo
hali hiyo haitadhibitiwa haraka, huenda wananchi wakapatwa na hofu ya
kuweka fedha zao benki kwa kuogopa kuporwa na kupigwa risasi wakienda
kuzichukua.
Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro, alikiri kuwapo kwa baadhi ya
wafanyakazi wa benki wenye mtandao na majambazi, huku akisema jeshi lake
limeweka mikakati kuhakikisha mtandao huo unasambaratishwa mara moja.
“Ni kweli kwamba baadhi ya mabenki, si
yote, yameajiri baadhi ya wafanyakazi, si wote wenye mtandao na
majambazi. Kwahiyo hata wao ni majambazi tu.
“Sasa tumejipanga vizuri ikiwa ni pamoja
na kukamata pikipiki zinazohusika katika uhalifu. Pia tumeamua kuweka
makachero nje na ndani ya mabenki, wapo polisi wa miguu, pikipiki na
magari. Nina uhakika tutawadhibiti,” alisema Kamanda Sirro.
MTANZANIA
Wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba mkoani Dodoma wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuwafuta kazi watendaji wa Serikali ambao wameuza nyumba za Serikali kinyume cha sheria.
Wafanyabiashara hao walisema wamekuwa
wakifanya biashara katika soko hilo kwa muda mrefu, lakini hivi sasa
wanashangaa kuelezwa kuwa wanatakiwa kuhama kwani jengo hilo limeuzwa
kwa mtu binafsi.
Walidai jengo hilo lilikuwa likimilikiwa
na Wizara ya Afya kwa muda mrefu, lakini wanashangazwa na hatua ya
Serikali kuliuza kwa mtu binafsi badala ya kutoa nafasi kwa wananchi
kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara zao.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Huseni Michuzi, alisema kwa muda mrefu wapo katika eneo hilo, lakini wanashangaa Serikali kuwataka kuhama wakidai eneo hilo si halali kwao.
“Hili ni soko, hapa tunafukuzwa
tupo zaidi ya watu 15, tunaambiwa hili eneo kauziwa mtu binafsi, sasa
tunajiuliza mtu binafsi anaweza kuuziwa mali ya Serikali? Tunamwomba
Waziri Lukuvi awafute kazi wote waliohusika na dili hili kwani wametumia
madaraka yao vibaya,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo,
Athumani Makole, alisema alipokea malalamiko ya wafanyabiashara 15
wakitakiwa kuhama katika eneo hilo ambalo linadaiwa ni mali halali ya
Solomoni Munuo.
“Lile eneo lilikuwa likimilikiwa na
Wizara ya Afya kwa ajili ya maonyesho ya Nanenane, baadae ofisi ya Mkuu
wa Mkoa ilitupa maelekezo kuwa ni eneo la walemavu sasa tunashangaa
Munuo kudai ni eneo lake,’’ alisema.
Kwa upande wa aliyeuziwa jengo hilo,
Munuo, alisema eneo hilo ni mali yake aliyokabidhiwa kihalali na Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kushirikiana na manispaa
baada ya kuona jengo hilo halitumiki.
Akifafanuzi kuhusu suala hilo, Ofisa
Masoko wa Manispaa ya Dodoma, Steven Maufi, alisema kutokana na
vielelezo vilivyo eneo hilo ni mali ya Munuo hivyo ana haki ya
kuwaondoa watu waliokuwa mbele ya nyumba yake.
“Hilo ni eneo halali la Munuo
ndiyo maana tukaamua kuwaondoa wafanyabiashara walio mbele yake, lakini
pia wamekuwa wakisababisha uchafu kutokana na kumwaga chini takataka,’’ alisema.
NIPASHE
Wakati, Rais John Magufuli,
akifikisha siku ya 70 ofisini leo tangu kuapishwa kwake Novemba tano
mwaka jana, gazeti hili limebaini kuwa mpaka sasa amepanda ndege mara
moja tu na kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam mara mbili tu.
Taarifa hizo ambazo zilithibitishwa na
mmoja wa wasaidizi wa Rais Magufuli, zinaeleza kwamba, jana ndiyo
ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda ndege tangu aingie madarakani.
Katika safari yake ya jana, Rais
Magufuli alitumia ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kuhudhuria
sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandaoni (Distance calculator), umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Zanzibar ni kilomita 73.43.
Muda wa kutoka Dar es Salaam kwa ndege
kwenda Zanzibar, kikokotozi hicho kinaonyesha ni dakika 14 mpaka dakika
20 kutegemea na ukubwa wa ndege na mwende kasi inayotumia.
Jana Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa
viongozi wa kitaifa waliokuwapo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar
kuuungana na Rais Ali Mohamed Shein katika kusherehekea kilele cha
maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi.
Wengine waliokuwapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa,
safari iliyomtoa Rais Magufuli kutoka Magogoni, Ikulu jijini Dar es
Salaam hadi Zanzibar ni ya pili tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 baada
ya kushinda kwa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa katika
uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Mbali na safari hiyo, safari nyingine ni
ile aliyotumia usafiri wa barabara kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma
kufungua Bunge la 11 na kupendekeza jina la Waziri Mkuu.
Katika safari hiyo ya Dodoma ambako
ndipo makao makuu ya nchi na kuliko na Ikulu ya pili kwa ukubwa ya
Chamwino ukitoa ile ya Magogoni, Rais Magufuli baada ya kuzindua Bunge
Novemba 20, 2015 alikaa kwa siku kadhaa kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha umbali,
kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma ni kilomita 583.64 ambazo kwa gari
linalotembea wastani wa mwendo kasi wa kilomita 112 kwa saa, litatumia
saa tano na dakika 12 kumaliza safari hiyo.
Wakati leo akifikisha siku ya 70
ofisini, Rais Magufuli hajawahi kusafiri nje ya nchi na mara kadhaa
amekuwa akitimiza ahadi yake ya kuhakikisha kuwa mabalozi wa Tanzania
katika nje ya nchi wanaliwakilisha taifa kwenye baadhi ya mikutano ili
kuondokana na gharama zinazoepukika.
“Lazima tukubaliane kuwa katika kubana
matumizi kuna faida na hasara zake, ndiyo maana hata kutosafiri kwake
kutakuwa na faida nyingi lakini kunaweza kuwa na hasara kidogo. Ila
lazima tu tukubaliane ukitaka kwenda mbiguni lazima kwanza ufe, vivyo
hivyo ukitaka kubana matumizi kutakuwa na hasara zake,” alisema mmoja wa
wasaidizi wa kiongozi huyo.
Wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli
alisema safari za nje zimeligharimu taifa Sh. bilioni 356.3, ambazo kati
yake Sh. bilioni 183.1 zilikuwa kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh.
bilioni 68.6 ziligharamikia mafunzo na Sh. bilioni 104.5 zilikuwa za
posho.
Rais Magufuli ambaye amebana safari za
nje za watumishi wa umma, aliliambia Bunge kwamba, fedha hizo zingeweza
kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.
Licha ya safari hizo za kikazi, Rais
Magufuli pia alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Msoga, mkoani Pwani
kwenye msiba wa dada wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Mpaka sasa, licha ya watumishi wengi wa
serikali kuomba kusafiri nje ya nchi na kunyimwa kibali, serikali
imewasimamisha kazi watumishi wanne wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa (Takukuru), kwa kwenda nje ya nchi bila kibali maalumu cha Ikulu.
Itakumbukwa pia kuwa, mpango wa Rais
Magufuli wa kubana matumizi, ulifanya utaratibu wa kusherehe siku ya
Uhuru ibadilishwe na watu kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi badala
ya kwenda uwanja wa taifa kuangalia gwaride na halaiki ambayo huwa
inagharimu mabilioni.
Kutokana na kuahirishwa kwa shamrashamra
hizo, Sh. bilioni nne zilizookolewa na kuelekezwa kwenye utanuzi wa
barabara ya Bagamoyo eneo la Mwenge mpaka Morocco ambako kazi hiyo
inaendelea kwa sasa.
Mpango huo wa kubana matumizi ya
serikali, pia ulifanya sherehe ya kufungua Bunge ifutwe na fedha zake
kuelekezwa kununua vitanda vya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Hatua ya Rais Magufuli kutosafiri mara
kwa mara huku pia serikali yake ikidhibiti safari za nje kwa viongozi na
watumishi wote wa serikali imekuwa ikiwavutia watu wengi nchini na
kwingineko nje ya Tanzania, akiwamo mgombea urais wa upinzani nchini
Uganda, Dk. Kizza Besigye.
Katika moja ya mikutano yake ya kampeni
akiwa kwenye wilaya ya Agago, nchini humo, Besigye alisema akiingia
Ikulu atafuata nyayo za Rais Magufuli kwa kupiga marufuku safari holela
za nje ya nchi na kuongeza kuwa ataiuza ndege anayoitumia mpinzani wake,
Rais Yoweri Museveni, aina ya Gulfstream V Jet.
Licha ya rekodi ya Rais Magufuli ya
kutosafiri kwenda Ulaya na nchi nyingine za nje ya Tanzania hata mara
moja tangu aingie madarakani kuwavutia wengi, baadhi ya watu
waliozungumza na Nipashe wamedai kuwa hali hiyo ni balaa kubwa la
kiuchumi kwa wasaidizi wa Rais ambao wengi wangetamani asafiri zaidi
kama ilivyo kwa wakuu wengine wengi wa nchi za Kiafrika waingiapo
madarakani.
Kutokana na rekodi ya safari za
Magufuli, ni wazi kuwa hadi sasa, wasaidizi wa Rais huyo wa awamu ya
tano watakuwa wamehusika katika safari za kutoka jijini Dar es Salaam
kuelekea kwenye Ikulu ndogo ya Chamwino, Dodoma na Unguja visiwani
Zanzibar alikokuwa jana.
“Rais yeyote anaposafiri ni lazima
aambatane na timu ya watu kadhaa wa karibu yake. Kama Rais anasafiri
mara kwa mara, ni wazi kwamba hawa pia hunufaika kwa safari hizi ambazo
huambatana na posho nzuri za safari. Hata hivyo, kwa hawa (wasaidizi) wa
Rais Magufuli hali iko tofauti… Rais amesafiri mara chache na hivyo wao
pia watakuwa wameguswa na ratiba hiyo kwa kusafiri mara chache,” chanzo
kimoja kiliiambia Nipashe jana kuhusiana na safari za Rais.
NIPASHE
Baadhi ya vyuo vikuu nchini viko hatarini kufutwa baada ya serikali kuamua kuvipitia ili kujiridhisha kama vina sifa stahiki.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, aliliambia gazeti hili kwamba uamuzi huo
unakuja baada ya kubaini kwamba licha ya vyuo vingi kuwa na ithibati,
bado baadhi havina sifa ya kuwa vyuo vikuu.
Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), takriban vyuo vikuu 60 ithibati na vinahesabika kuwa ni vyuo vikuu kamili.
“Hatutaki vyuo ambavyo vipo vipo tu.
Tutavikagua upya kuangalia kama vinakidhi vigezo na hata uhalali wa
ithibati vilivyopewa,” alisema Prof. Ndalichako.
Aliongeza kuwa vyuo vitakavyothibitika
kuwa havifai vitafungwa bila kusita kwa kuwa serikali haitaki Watanzania
wafanyiwe majaribio katika elimu. Alisema ni bora ijulikane wazi kuwa
hakuna chuo kikuu kuliko kumpeleka mwanafunzi mahali halafu akatoka
mtupu.
“Kuwa na vyuo vingi ambavyo havina sifa,
kunachangia kuwa na vijana wengi mtaani ambao hawana ajira, jambo
ambalo linawaongezea hasira,” alisema Ndalichako.
Prof. Ndalichako alisema serikali
itaangalia pia taratibu zinazotumiwa kutoa ithibati kwa sababu kumekuwa
na kilio kikubwa kwa umma, wengi wakilalamika kuwa wanafunzi wanamaliza
vyuo vikuu wakiwa hawana na uwezo hafifu.
“Kila mtu analalamika, lakini tumechukua
hatua gani? Je, tumekaa chini na kuangalia vigezo na kuona ili mtu awe
na chuo anatakiwa kuwa na sifa gani? Anatakiwa awe na watu wa aina
gani?.
“haiwezekani mtu mwenye shahada moja
amfundishe mwanafunzi wa shahada ya kwanza. Wa kumfundisha huyu
anatakiwa angalau awe na shahada ya uzamili, ingawa nayo haitoshi…
inatakiwa angalau asilimia 50 ya walimu wa kila chuo kikuu wawe na Ph.D
(shahada ya uzamivu),” alisema.
Profesa Ndalichako pia alisema kuna vyuo
ambavyo mtu akienda kufundisha hata kwa saa moja tu, anaingizwa kwenye
orodha ya walimu waajiriwa.
“Tunaposema walimu, tunamaanisha wale
ambao wameajiriwa na chuo. Tunaposema tunaangalia ubora wa elimu,
itabidi tuangalie utoaji wa ithibati na kujiridhisha kwamba mambo ambayo
tunasema yanatakiwa yawepo ili chuo kiitwe chuo kweli yawepo.
‘Kuna wengine wanafanya chuo kama sehemu
ya maonyesho. Siku ile unaenda kukagua unakuta maabara na vitu vingine,
kumbe vyote vimeazimwa,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema taasisi zilizopewa dhamana ya
kusimamia ubora wa elimu ya juu lazima ziwe na mfumo wa kukagua na
kufuatilia mara kwa mara na si kuangalia tu wanafunzi wakiwa vyuoni,
bali hata baada ya kumaliza na kwenda kwenye soko la ajira ili kusikia
waajiri wanawazungumziaje.
Alisema ili kufikia lengo la Tanzania
yenye viwanda na uchumi wa kati, kama ambavyo serikali ya awamu ya tano
inatamani, lazima viwango vya elimu viangaliwe upya.
Nipashe ilipotaka kujua sababu za
Profesa Ndalichako kutorudi Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania
(Necta) baada ya kumaliza likizo ya mwaka mmoja bila malipo, alisema ni
kwa sababu aliamua kujiendeleza kielimu.
“Necta nilikaa miaka tisa, niliona mambo
mengi niliyotamani kufanya nimefanya, hivyo nikaona pia kitaaluma watu
niliowaacha chuo kikuu (Dar es Salaam) wakiwa walimu wenzangu ni
maprofesa. Nikaoana na mimi nijiendeleze kitaaluma,” alisema.
Ili kupata daraja la uprofesa,
wanataaluma ambaye amefikia hatua ya mhadhiri mwandamizi, anapaswa
kufanya utafiti wa kitaaluma na ushauri elekezi. Utafiti wake huo
unatakiwa kuchapishwa kwenye majarida ya kitaaluma kitaifa na kimataifa.
Kutokana na kiu yake hiyo serikali ilimkubalia na baada ya likizo, alirudi chuo kikuu baada ya kuomba na wakamkubalia.
“Nisingerudi hata huu uprofesa
nisingeupata. Kwa hiyo kila jambo lina sababu yake na hata
nisingeteuliwa (kuwa Waziri) ningejiendeleza kwa sababu sasa hivi mimi
ni Associate Profesa (Profesa Mshiriki), lakini nisingeteuliwa kulikuwa
na miradi mingine ya utafiti ambayo nimeanza kuitafuta.
“Nilishapata ruzuku kutoka taasisi moja
ya Canada na kupata ruzuku ya dola za Marekani 248, 000 (Sh. milioni
530) kwa ajili ya utafiti niliokuwa nifanye Tanzania na Uganda kuangalia
walimu wanavyofanya upimaji wwa wanafunzi na humo ndani ningepata
machapisho pia,” alisema.
Aliongeza kuwa mwezi wa 12 kuna ruzuku
nyingine ambayo ni ya Uingereza, kwenye taasisi iitwayo ESRC aliomba
ili afanye utafiti kwenye eneo hilo hilo la upimaji ambalo ndilo eneo
lake la kitaaluma.
“Utafiti huu nilikuwa nifanye kwenye
shule zilizo kwenye watu wengi ambazo kwa kawaida mahitaji ni meingi
kuliko uhalisia. Kwa mfano, uwiano wa mwalimu na wanafunzi haulingani na
vitu vingine na nilishapata pauni 697,000 (Sh. bilioni 2.17), kati yake
pauni 193,000 (Sh. milioni 599.85) ingekuja kwangu na nyingine kwenye
vyuo vya nje ambavyo tungeshirikiana,” alisema.
Alisema licha ya kuwa eneo hilo halipo
kwenye wizara yake moja kwa moja, ameanza mazungumzo na mwenzake wa
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambapo
pamoja na mambo mengine, wataangalia madeni ya walimu na namna ya
kuyalipa.
MWANANCHI
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete
akiambatana na mkewe Salma, jana walimtembelea Waziri Mkuu mstaafu,
Frederick Sumaye aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
(JKCI) Muhimbili.
Kikwete ambaye alifika hospitalini hapo
saa 11 jioni, alianza kuwasalimia baadhi ya wagonjwa waliolazwa na
baadaye kuingia wodi aliyolazwa Sumaye.
Baada ya kuingia katika chumba hicho,
Kikwete alikaa kwenye kochi pamoja na Sumaye kisha kumpa pole na
kumtania Sumaye aliyekuwa na mkewe Esther kuwa amenenepa japokuwa
anaumwa.
Sumaye alisema ana siku ya tano
hospitalini hapo na kuelezea furaha yake kwa ujio huo wa Kikwete.
“Japokuwa nilikuwa katika hali mbaya ila sasa hivi naendelea vizuri.
Pia, nakupongeza mheshimiwa (Kikwete) kwa kuadhimisha miaka 52 ya
Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Sumaye.
Mbali na Kikwete, Waziri Mkuu, Kassim
majaliwa na mkewe nao walimtembelea kiongozi huyo jana. Kaimu Mkurugenzi
wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema kila siku hali ya Sumaye
inaimarika. Juzi, Rais Magufuli alimtembelea Sumaye na kumpa pole huku
akimuombea apone haraka
MWANANCHI
Wakati Serikali na wadau mbalimbali wa
watetezi wa haki za wanawake na watoto wakihimiza elimu kwa mtoto wa
kike, mama mmoja mkoani hapa anatuhumiwa kutaka kumuozesha mtoto wake
mwenye miaka 13 (jina linahifadhiwa) baada ya kupokea mahari ya
Sh600,000 na ng’ombe wanne.
Tukio hilo lilitokea leo katika Mtaa wa
Chikole, Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma. Mama huyo anadaiwa kutaka
kumfungisha ndoa binti huyo kwa kijana mmoja anayeishi mtaani hapo.
Hata hivyo, mpango huo wa ndoa
ulitibuliwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Nashoni Chinywa ambaye baada ya
kupata taarifa aliamua kuwaita polisi wauzuie.
Akizungumzia tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Mdala Mazengo
alisema aliamua kumuozesha binti yake baada ya kumtaarifu kuwa amepata
mchumba. Naye mtoto huyo alidai kukutana na kijana huyo mwenye umri wa
miaka 20 mtaani hapo na kumuahidi kufunga naye ndoa.
Hata hivyo, baadhi ya majirani walidai
kuwa mama huyo ambaye ni mjane, ana tabia ya kuwaozesha watoto wake wa
kike wakiwa na umri mdogo.
Chinywa alisema baada ya mahojiano, mama
huyo alikiri kufanya kosa hilo baada ya kuchoshwa na tabia za watoto
hao kwani hata dada yake alibebeshwa mimba akiwa nyumbani.
Hata hivyo, alisema kuwa hatua zaidi za
kisheria zitachukuliwa baada ya Kamati ya Serikali ya Mtaa kukutana na
Kamati ya Maendeleo ya Jamii kujua ni hatua gani zichukuliwe dhidi ya
mama huyo.
“Alikataa shule, sasa yeye mwenyewe aliniambia amepata mchumba na mimi niliamua kumuozesha kwa kuwa wao wenyewe wamependana,” alisema Mdala Mazengo na kuongeza:
“Walishatoa barua ya posa na kesho ndiyo tulikuwa tunapanga mahari ya
kulipa, wao walikuwa wanataka kunipa mahari kidogo, sasa wakati
tunabishana ndipo mwenyekiti na maaskari wakafika hapa nyumbani na
kutukamata.” Walidai kuna mtoto mwingine alimuozesha akiwa na miaka 14.
HABARILEO
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bilele ya Mjini Bukoba, mkoani Kagera, Siasa Phocus
amevuliwa madaraka kwa madai ya kuendelea na msimamo wa kutaka wazazi
wenye watoto shuleni hapo, waendelee kutoa michango kinyume na agizo la
serikali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro
Mnambila aliliambia gazeti hili jana mjini hapa kwamba mwalimu huyo
alishapewa utaratibu wa kuzingatia sera ya utoaji elimu msingi bure,
lakini alikaidi.
“Kwa mamlaka niliyonayo, nachukua hatua
hii kwa kumvua mamlaka mkuu wa shule Bilele kutokana na kushindwa
kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali…,” alisema Mnambila.
Alisema mwalimu huyo aliendelea na
msimamo wa kuwaambia baadhi ya wazazi waliofika kuuliza utaratibu wa
michango, kwamba hana taarifa na miongozo ya serikali, akiwasisitiza
kila mzazi kutimiza mahitaji yaliyopo kwenye fomu ya mwanafunzi.
“Mwalimu huyo aliendelea kutoa fomu kwa
kila mwanafunzi iliyoainisha kila mahitaji kama ilivyokuwa hapo awali
(miaka ya nyuma) huku akitaka michango ya madawati, karatasi za kuchapia
mitihani na mlolongo wa gharama nyingine nyingi,”alisema Katibu Tawala.
Michango mingine ambayo wanafunzi wa
sekondari wamekuwa wakitozwa kila mwaka ni ya fyekeo, ndoo, jembe, uji,
chakula cha mchana na uzio.
Katibu tawala alionya walimu wakuu na
wakuu wa shule, kuzingatia na kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi
bure, kama ilivyo kwenye taratibu za miongozo iliyotolewa kwao katika
idara ya elimu.
Fedha zafika mikoani
Wakati huo huo, mikoa mbalimbali
imethibitisha kupokea fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya
utekelezaji wa mpango wa elimu bure. Jumla ya Sh bilioni 18.77
zimetolewa na serikali kwa ajili ya shule zote za umma nchini.
Miongoni mwa mikoa iliyothibitisha kwa
waandishi wa habari kupokea fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya
kutekeleza elimu msingi bila malipo ni pamoja na Kagera, Morogo, Rukwa
na Mwanza.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Aloyce
Kamamba alisema wamepatiwa jumla ya Sh 810,157,000 ambazo
zimeshaelekezwa kwenye akaunti za shule zilizoko mkoani humo, ambapo za
msingi ni 888 na sekondari 190. Kati ya hizo, 17 ni sekondari za bweni.
Kiasi hicho kimetolewa na serikali kwa ajili ya kugharimia huduma
mbalimbali ikiwemo chakula.
Mkoani Rukwa, Mkuu wa Mkoa, Magalula
Said Magalula alisema wamepokea Sh milioni 336 ambapo Sh 143,859,000
zimepelekwa kwenye shule za msingi 360 na kiasi kilichobaki, kimepelekwa
shule 105 za sekondari. Kwa mujibu wa Magalula, fedha hizo ni kwa ajili
ya mwezi huu kwani kila mwezi serikali itakuwa ikitoa fedha kwa ajili
ya mpango huo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa
Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel Hokororo, alikiri shule yake kupokea Sh
milioni 1.4 kwa ajili ya Januari mwaka huu. Katika Mkoa wa Morogoro,
Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa huo anayeshughulikia elimu, Wariambora
Nkya, alithibitisha kupokea Sh milioni 724.7 kwa ajili ya shule 846 za
msingi na 179 za sekondari za bweni na kutwa.
Mkoa mwingine uliothibitisha kupokea
fedha hizo ni Mwanza wenye shule za sekondari 197, ambazo zimepewa Sh
642,648,000 kwa ajili ya fidia ya ada za kutwa na bweni na chakula kwa
shule za bweni. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema upande wa
Shule za Msingi, zipo 850 ambazo zimepokea Sh milioni 356,728,000.
Alisema hadi Desemba 30 mwaka jana, shule zote zilishawekewa fedha kwenye akaunti zake.
Walimu wakuu, wakuu wa shule, bodi
wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo na wakati huo huo
kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuhakikisha elimu msingi inatolewa
bure.
Licha ya wakuu wa mikoa na idara ya
elimu kuhadharisha juu ya hilo, pia Wizara ya Fedha na Mipango hivi
karibuni, ilionya wakuu wa shule za msingi na Sekondari watakaotumia
ovyo fedha hizo zilizotolewa na serikali kutoa elimu bure, ikisema
atakayebainika kuzitumia isivyo, atashughulikiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango iliwataka walimu katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika
ipasavyo, waweke wazi fedha walizopokea kutoka serikalini wananchi
wafahamu alichopewa na matumizi yake.
Bodi za shule zimepewa kazi ya
kuhakikisha zinasimamia matumizi na kutoa taarifa. Pia wakuu wa wilaya,
mikoa na wakurugenzi wamepewa wajibu wa kusimamia fedha hizo Sh bilioni
14.7, ambazo kati yake, Sh bilioni tatu zimepelekwa katika vyombo vya
usimamizi wa mitihani.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment