MTANZANIA
Kamati ya Migogoro na Usuluhishi ya
Bunge la Afrika Mashariki (EALA), imepanga kuanza kusikiliza maelezo ya
Serikali ya Burundi na chama tawala dhidi ya hoja za wanaharakati wa
haki za binadamu na vyama vya kiraia kutaka ifutiwe uanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC).
Vikao hivyo vinatarajiwa kuanza Januari
25 hadi Februari 4, mwaka huu kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu
baada ya wanaharakati hao kuwasilisha maombi mbele ya kamati hiyo ya
Bunge.
Katika hoja yao, wanaharakati hao
wanaliomba Bunge hilo likutane, kujadili na kutoa azimio la mgogoro wa
kisiasa unaoendelea nchini humo, baada ya Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunziza kutangaza kujiongezea muhula wa utawala.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Migogoro na Usuluhishi, Dk. Abdullah Mwinyi, alisema tayari wameshafanya mawasiliano na Serikali ya Burundi kwa ajili ya kikao hicho.
Alisema siku ya kwanza walalamikaji ambao ni vyama vya kiraia walipata fursa ya kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalisikilizwa.
Mwenyekiti huyo alisema siku ya pili
ilifuatia zamu ya wadau ambao ni watu kutoka taasisi na asasi zisizo za
kiserikali, walisikilizwa na kuhojiwa.
“Tulipokea barua yao na
tukawashukuru kwa kukubali kufika. Lakini tumewaomba wafike Januari 25,
mwaka huu kwa ajili ya kuwasikiliza, watasema watakayoyasema na
tutawauliza maswali baada ya hapo tutakaa kamati yetu kupitia yote
yaliyozungumzwa,” alisema Mwinyi na kuongeza:
“Baada ya hapo tutatayarisha
ripoti tutakayoiwasilisha ndani ya Bunge ambako nako itajadiliwa na
wabunge kisha kupitisha maazimio yatakayowasilishwa kwenye Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao nao watawasilisha mbele ya
wakuu wa nchi wanachama,” alisema.
Alisema dhamira ya kamati yake ni
kuhakikisha wanamaliza kusikiliza pande zote wakati wa vikao vya Bunge
vinavyotarajiwa kuanza Januari 25, mwaka huu mjini Arusha.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewatia
mbaroni wahamiaji haramu 83, raia wa Ethiopia, waliokuwa wakisafirishwa
na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T478 DFE mali ya Frola Mwambenja, ambao walikuwa wakitokea Kongowe jijini Dar es Salaam kuelekea Kyela mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema jeshi hilo linamshikilia pia dereva wa gari hilo, Hans Mwakyoma (28) mkazi wa Tukuyu Mbeya na msaidizi wake Alex Adam (32) mkazi wa Mbeya mjini, kwa tuhuma za usafirishaji wa watu hao.
Kamanda Kakamba alisema gari hilo
lilikamatwa na askari wa doria wa jeshi hilo saa 3.30 usiku katika
Kijiji cha Mahenge, barabara kuu ya Iringa Mbeya likiwasafirisha watu
hao kuelekea Kyela ambako ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.
“Lilipokamatwa
roli hilo, dereva alisema halina mzigo, lakini askari wetu
walipolifungua walikuta watu hao wakiwa wamelaliana, baadhi yao wakiwa
na hali mbaya na wengine wakiwa wagonjwa,” alisema.
Alisema baada ya kuwakamata, wahamiaji
hao walipewa chakula na wale walioonekana wagonjwa wamepatiwa matibabu
wakati taratibu zingine za kuwafikisha katika vyombo vya sheria
zikiendelea.
“Jambo la kushangaza ni kwamba
watu hao walipakiwa katika gari hilo Kongowe jijini Dar es Salaam. Kila
mtu anajua Kongowe si Ethiopia kwa hiyo kuna swali la kujiuliza ni namna
walivyofika Kongowe hadi wakapata huduma ya kusafirishwa kuelekea
wanakoelekea,” alisema.
Alisema biashara haramu ya usafirishaji
watu ni jipu kubwa linalohitaji nguvu ya pamoja katika kulitumbua kwani
inahusisha mtandao wa watu wengi ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kupambana na biashara
hiyo, taarifa za kiintelejensia za jeshi hilo zinaelekea kuunasa mtandao
wa biashara hiyo na mkakati huo utakapofanikiwa wahusika wake
watatumbuliwa majipu hadharani.
Alisema watu hao wamekuwa wakiitia
gharama kubwa serikali, kwani baada ya kuwakamata imekuwa ikilazimika
kuwahudumia na kuwasafirisha hadi walipotoka.
MTANZANIA
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea
(CHADEMA) amesema anatarajia kufufua hoja ya kujadiliwa upya kwa ripoti
ya fedha zilizokwapuliwa za Tegeta Escrow zaidi ya Sh bilioni 200.
Akizungumza jana alisema sababu za
kutaka mjadala huo kurejeshwa ni kutaka kujua iwapo fedha hizo ni za
umma au ni mali ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Sababu nyingine aliyoitaja Kubenea ni kutaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa sakata hilo, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) katika Bunge la 10, iliwasilisha bungeni mapendezo zaidi
ya 10 likiwemo azimio namba moja la kuitaka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
kumkamata Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP)
Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya
utakatishaji wa fedha na ukwepaji kodi.
Kamati inaelekeza Serikali kutumia
sheria za nchi, ikiwamo sheria ya Proceeds of Crime Act, kuhakikisha
kuwa Singh Sethi anarejesha fedha zote alizochota kutoka Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG iliyothibitishwa na TAKUKURU, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu binafsi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC,
Zitto Kabwe, alisema kamati yake ilijiridhisha kuwa fedha iliyotumika
kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa
bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya IPTL.
Fedha hizo zilizua mjadala mkubwa
bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka msimamo wa Serikali
kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, akisema kuwa fedha
hizo hazikuwa za umma na hivyo kuzidisha mjadala.
MTANZANIA
Utafiti mpya wa ugonjwa wa Virusi vya
Ukimwi (VVU), unatarajiwa kuleta faraja kwa wenzi, ambapo mmoja anaishi
na virusi hivyo na mwingine akiwa hana.
Faraja hiyo inahusisha kufanya tendo la
ndoa bila kutumia kinga na hivyo kupata watoto bila kusababisha
maambukizo yoyote mapya baada ya unywaji wa dawa.
Ugunduzi wa dawa hiyo mseto ya
kimiminika ijulikanayo kama PrEP, tayari imetumiwa na wanaume mashoga
nchini Uingereza na Marekani.
Dawa hiyo huweza kuondoa hatari ya
kuambukizwa hadi asilimia sifuri, itaondoa changamoto iliyokuwapo katika
njia namba moja ya kujikinga na virusi, yaani kutumia kondom wakati wa
kufanya tendo la ndoa.
Matumizi ya kondom yalimaanisha kuwa
wenzi wa aina hiyo hawawezi kupata watoto bila uwezekano wa kuhatarisha
mwenzi ambaye hana VVU.
Kwa sababu hiyo, mamlaka nchini Kenya zimeanzisha mradi wa kuwasaidia wenzi kuwa na familia bila kuhatarisha afya zao.
John na mkewe Josephine, wanaoishi
kaskazini mwa Nairobi ni mfano wa wenzi wa aina hiyo, ambapo Josephine
anaishi na VVU wakati John hana maambukizo hayo.
Mume huyu anasema kuwa hali kama hiyo inaweza kuwa ngumu na anawajua wenzi ambao wameshatengana kwa sababu hiyo.
Kuna wenzi 260,000 nchini Kenya, ambako mmoja anaishi kwa VVU huku mwenzake akiwa hana.
Wenzi wa aina hiyo wanaojulikana
kitaalamu kama serodiscordant, wanachukua asilimia 44 ya mambukizo mapya
ya VVU katika taifa hilo. Pamoja na asilimia hiyo wamezaa watoto.
“Lakini nia ya kupata watoto kwa wenzi
wa aina hii bado huwa na nguvu mno –utafiti mmoja wa hivi karibuni kwa
wenzi wa serodiscordant umeonesha asilimia 17 ya wanawake walipata
mimba.
“Kwa sasa majaribio mapya ya dawa yametoa mwanga wa matumaini na faraja kwa wenzi wa aina hii,” anasema John.
Imebainika kwamba njia mpya ya kutumia
dawa za kukabiliana na VVU, ambazo kwa kawaida hupewa watu wanaoishi na
virusi hivyo, inaweza kutumika kwa wenzi wa aina hiyo kujaribu kuzaa
watoto wasio na VVU bila pia kumwambukiza mwezi asiye na virusi hivyo.
Dk. Nelly Mugo kutoka Taasisi ya Utafiti
wa Tiba ya Kenya na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Washington
cha nchini Marekani kwa pamoja wanaendesha majaribio hayo.
Majaribio hayo yalihusisha wenzi 4,700, ambao mmoja ana VVU na mwingine hana maambukizo.
Katika majaribio hayo, mtu ambaye hakuambukizwa VVU alikunywa PrEP katika kipindi cha miezi 36.
“Tulibaini kwamba kuwa na dawa katika mfumo wako mwilini kulipunguza kiwango cha maambukizo kwa zaidi ya asilimia 90.
“Lakini pia iwapo mwenzi mwenye
VVU pia alichukua dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs), uambukizo wa
VVU ulipunguzwa hadi asilimia sifuri au karibu na sifuri,” alisema.
Katika baadhi ya jamii shinikizo la
kijamii la kutaka kuwa na watoto linaweza kuwa kubwa huku familia zisizo
na watoto mara nyingi zikipata shida kueleza kwanini hazijazaa.
Katika utafiti wa karibuni, wenzi
walieleza kwamba walijisikia kutokuwa na la kufanya na wako katika
hatari ya kupata VVU iwapo watajaribu kupata mimba.
Lakini katika mradi wa sasa, wenzi
wasioambukizwa walipata faraja baada ya kubakia salama bila kuambukizwa
walipofanya tendo la ndoa bila kinga, hali iliyosababisha imani kwa dawa
hiyo kuwa na uwezo wa kuwalinda.
Dk. Mugo anasema: “Hisia za kawaida
zilizozoeleka kwa kuzaa watoto ni pamoja na kutimiza matarajio ya wenzi
husika ya ukubwa wa familia waitakayo, kupata watoto wao wenyewe wa
kuwazaa na kuendeleza uhusiano imara na mara nyingi muhimu zaidi ikiwa
ni kukabiliana na shinikizo la nje kutoka kwa jamii” alisema.
VVU haitibiki, kwa sababu mara
inapoingia katika mwili, hujificha katika mahali ambapo ni vigumu
kupafikia, na kusababisha hodhi, hali inayomanisha kwamba kamwe haiwezi
kuondolewa kutoka humo hodhini.
Nadharia iliyo nyuma ya PrEP ni kwamba kuchukua dawa za ARVs kabla ya kuambukizwa kunamaanisha tayari zipo ndani ya mwili.
Lakini watafiti wameonesha kuwa iwapo
mtu asiyeambukizwa tayari atakuwa na dawa za PrEP katika mifumo yao ya
mwili wakati virusi vinapoingia katika miili yao hiyo huuawa.
Hili linamaanisha kuwa virusi huwa havina nafasi ya kujificha katika hodhi, na hivyo ni vigumu kwa mtu kuambukizwa.
“PrEP ni kitu kizuri kinachoweza kuwafaa
wenzi hawa,” anasema Dk. Mugo, kwa sababu inaweza kutatua kile
alichokiita ‘hali tete ya ufarakano.
“Wakati unapobaini mwenzi wako ana VVU
husababisha maumivu makubwa ya kihisia,” aliongeza. “Lakini uhusiano na
hisia na mapenzi vina nguvu kuliko virusi.
“Wengi wa wenzi hutaka kubakia
pamoja, lakini wanashindwa kurejea katika hali ya kawaida ya uhusiano wa
tendo la ndoa. PrEP ina uwezo mkubwa wa kutatua tatizo hilo,” anasema.
Jaribio hilo lilikuwa na mafanikio kwani
kufikia Septemba 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza kuwa
watu walio katika hatari ya kupata VVU wapatiwe PrEP kama chaguo la
pili la kujikinga, kama sehemu ya uzuiaji wa maambukizo.
NIPASHE
Rungu la faini kutokana na ukiukwaji wa sheria za mazingira limeendelea kuviandama viwanda mbalimbali vya mkoa wa Morogoro.
Hivi sasa viwanda vya sukari vya Mtibwa
na Ilovo kilichoko Kilombero pamoja na kile cha kutengeneza ngozi cha
ACE, vimetozwa jumla ya sh. milioni 40 kwa makosa ya aina hiyo katika
maeneo yao.
Uamuzi huo ulitolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina,
akiwa katika mwendelezo wa ziara yake mkoani hapa akiambatana na
maofisa wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Kiwanda cha Ilovo kimetozwa faini ya sh.
m,ilioni 25 baada ya kubainika kuwa na mfumo mbovu wa utunzaji taka
ngumu na kushindwa kuhifadhi vyema mabaki ya mabati yanayotolewa
kiwandani hapo. Mbali na faini ambayo inatakiwa kulipwa ndani ya siku
saba, walitakiwa kurekebisha upungufu huo ndani ya siku 30.
Naibu waziri huyo aliutaka uongozi huo
kuhakikisha upungufu 40 uliotajwa kwenye ripoti ya ukaguzi, iliyofanywa
na Nemc zaidi ya miezi mitatu iliyopita, unafanyiwa marekebisho sambamba
na kuutolea taarifa uwanja wa ndege ulioko ndani ya kiwanda hicho ambao
hauna cheti chochote cha ukaguzi.
Kwa upande wa kiwanda cha ngozi cha ACE
cha mjini Morogoro, serikali imekitoza faini ya Sh. milioni 15 kutokana
na kubainika kuwa na mfumo mbovu wa utiririshaji na uhifadhi wa maji
taka.
Mpina pia aliiagiza menejimenti ya
kiwanda kudhibiti harufu mbaya inayolalamikiwa na wananchi, hususan
walio jirani na kiwanda hicho.
Naibu Waziri Mpina alifanya ziara pia
katika soko kuu la mjini Morogoro na kuagiza ujenzi mpya wa soko
kuzingatia vizimba vya uhifadhi wa taka ili zisitawanyike na kuutaka
uongozi wa manispaa kutofanya mlundikano wa taka katika eneo hilo kama
ilivyoonekana.
Ziara hiyo ya Mpina iliyafikia pia
maeneo ya kituo kikuu cha mabasi cha Msamvu, kiwanda cha kutengeneza
mafuta ya kula cha Abood (Moproco), Kiwanda cha maturubai, Kiwanda cha
nguo cha 21st Century, Kiwanda cha Magunia na mabwawa yanayopokea
majitaka yatokayo viwandani.
Kutokana na maagizo ya Naibu Waziri,
mtaalamu wa mazingira kutoka Ilovo, Mary Kigula, alisema watahakikisha
wanatekeleza ikiwa pamoja na kupanda miti na kutoa huduma za kijamii
katika maeneo yanayowazunguka.
Naye Mkuu wa Idara ya Uzingatiaji wa
Sheria ya mazingira kutoka Nemc, Alfred Msokwa, alisema baraza limekuwa
likitoa ushauri na maelekezo kwa uongozi wa viwanda lakini wengi
wamekuwa wakipuuza.
Msokwa alisema tangu mwaka 2013 NEMC
imefanya ukaguzi katika viwanda takribani vyote mkoani Morogoro na
kutoa ushauri ambapo baadhi ya viwanda bado vipo katika utekelezaji wa
marekebisho yake huku vingine vikipuuzia maelekezo hayo na kujikuta
vikitakiwa kulipa faini kwa mujibu wa sheria.
NIPASHE
Kashfa ya benki ya Stanbic Tanzania
iliyotokana na mkopo wa Sh. trilioni 1.3 ambao Serikali ya Tanzania
ilikopa benki ya Standard ya Uingereza, imeingia kwenye sura mpya baada
ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuitoza benki hiyo faini ya Sh. bilioni
tatu kutokana na kuvunja taratibu za kibenki.
Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwaka
jana, Mahakama ya London, Uingereza ilibaini ufisadi kwenye mchakato wa
mkopo huo ambao serikali ya Tanzania ilikopa benki ya Standard ya
Uingereza kupitia mshirika wake Stanbic Tanzania.
Katika hukumu yake, mahakama hiyo
iliamuru Serikali ya Tanzania ilipwe dola za Marekani milioni saba (Sh.
bilioni 15), ikiwani ni asilimia moja ya riba iliyoongezwa na tozo ya
Sh. bilioni moja.
Katika mkopo huo, serikali ilitakiwa
kulipa asilimia 1.4, lakini benki ya Stanbic Tanzania, ikaingiza
kinyamela kampuni ya Kitanzania ya EGMA kama mtu wa kati pamoja na
kuongeza asilimia moja ya mkopo huo kisi cha dola za Marekani milioni
sita.
Fedha hizo zinadaiwa kuingizwa kwenye akanti ya EGMA na baada ya siku chache kutolewa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango,
alisema kwa kuzingatia upungufu wa miamala iliyohusisha kampuni ya
EGMA na Stanbic Tanzania, BoT imeiandikia barua benki ya Stanbic ya
kusudio la kuitoza faini ya Sh. bilioni 3.
Alisema faini hiyo imetozwa kutokana na kifungu namba 67 cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Alisema sheria hiyo inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kitaisha Januari 30, mwaka huu.
Alisema endapo BoT haitaridhika na utetezi huo, Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
Kuhusu kampuni ya EGMA, Dk. Mpango
alisema uchunguzi bado unaendelea kufanywa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na utakapokamilika taarifa itawekwa wazi.
“Benki Kuu imechukua hatua hizo
kama onyo kwa benki ya Stanbic ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha
shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na
kuzingatia sheria,” alisema.
Dk. Mpango alisema Julai, 2013 BoT
iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo, huku
baadhi ya wafanyakazi wake kuacha kazi na wengine kuondolewa kazini
wakiwamo viongozi waandamizi wa benki hivyo, hivyo kuagiza kufanyika
kwa ukaguzi maalum.
Alisema ukaguzi huo ulibaini kuwapo kwa
miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya EGMA iliyohusika
katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo huo.
Alisema malipo hayo kwa kampuni ya EGMA
yalikuwa yamefanyika kinyume cha taratibu za kibenki na yalihusisha
uongozi wa benki ya Stanbic.
Dk. Mpango alisema taarifa ya ukaguzi
huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic na BoT iliagiza Bodi ya
Wakurugenzi wa benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro
zilizoonekana.
Alisema pia Stanbic iliagizwa kutoa
taarifa kwa Kitengo cha Kupambana na Utakatishaji Fedha ( FIU) kilichopo
Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka na
Stanbic walitekeleza na kutoa taarifa FIU.
Alisema Septemba 29, mwaka jana, BoT
ilipokea barua kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Kughushi na Rushwa
ya nchini Uingereza (SFO), ikiiomba BoT ruhusa ya kutumia ripoti yake
ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya benki ya Standard ambayo
ni mshirika wa Stanbic Tanzania.
Dk. Mpango alisema katika kesi hiyo
benki ya Standard ilikubali makosa na ilitozwa faini ya dola za Marekani
milioni 32.20, ambazo kiasi cha dola milioni 7 zinalipwa kwa serikali
ya Tanzania, dola milioni 6 zikiwa ni fidia na dola milioni moja zikiwa
kama ni riba.
“Faini waliyopewa Stanbic kwa benki na
taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume
cha taratibu za kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema.
Dk. Mpango alionya kuwa, hatua kali
zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote
itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na sheria ya benki
na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Nipashe lilimtafuta msemaji wa benki ya
Stanbic, Annette Nkini, kuelezea hatua ya BoT kuindikia barua ya
kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha, alisema hawezi kulizungumzia
suala hilo kwa kuwa kuna wakubwa wake ambao wanapaswa kulizungumzia.
NIPASHE
Wakati mazungumzo ya kutafuta muafaka wa
uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana yakiendelea
kufanyika , Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya
mwenyekiti wake, Abdallah Bulembo, imejipanga kupiga kambi visiwani
Zanzibar kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.
Chama hicho kimeridhia kurudiwa kwa
uchaguzi huo, huku chama kikuu cha upinzani visiwani humo CUF ambacho
mgombea wake ni Seif Shariff Hamad kikikataa kurudiwa kwa uchaguzi huo
na kutaka atangazwe mshindi kwa kuzingatia uchaguzi mkuu uliopita ambao
matokeo yake yalifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa madai ya
kufanyika udanganyifu.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa, Abdallah Bulembo, alisema baraza hilo limeridhia jumuiya hiyo kuhamia Zanzibar kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa marudio.
“Tutahamia Zanzibar tutakapotangaziwa ni tarehe ngapi imepangwa uchaguzi huo kufanyika,” alisema Bulembo.
Aidha, alisema kikao hicho cha baraza kuu pia kilimpongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.
Kuhusu kujaza nafasi za watu waliohamia
vyama vya upinzani, Bulembo alisema baraza limeteua watu kujaza nafasi
za walioondoka CCM kwenda vyama vya hivyo wakati wa uchaguzi mkuu wa
mwaka jana wakiwa wajumbe wa baraza hilo.
“Mkoa wa Kagera mjumbe wa baraza kuu
alihamia Chadema, mkoa wa Pwani alihamia CUF, mkoa wa Njombe alihamia
ACT-Wazalendo, kwahiyo nafasi zile tumepitisha majina matatu matatu ili
yarudi kwenye mikoa kujaza hizo nafasi,” alisema.
Bulembo pia alisema amemteua, Shehe
Hamis Hamdani, kuwa mjumbe wa baraza hilo kutoka Pemba na katika nafasi
ya mjumbe wa kamati ya utekelezaji taifa baraza limemchagua Jaffari
Mwenyemba ambaye ni Meya wa Manispaa ya Dodoma na Godfrey Mheluka kuwa
Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Bara.
Bulembo alisema mwaka huu wiki ya wazazi
itafanyika mkoani Morogoro na kwamba sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa
kwa CCM zitakazofanyika mkoani Singida, jumuiya hiyo itapiga kambi huko
kufanya kazi za chama.
Kuhusu elimu, Bulembo alisema Baraza
limeagiza watu wote wanaohusika na ubadhirifu katika shule
zinazomilikiwa na jumuiya hiyo wapelekwe mahakamani.
Alisema kuna shule zimefanyiwa ukaguzi na kubainika kuwapo na ubadhirifu wa fedha nyingi na watumishi wote waliohusika watapelekwa mahakamani.
NIPASHE
Chama cha Alliance for Democratic Change
(ADC) kimesema kimejiandaa kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio
unaotarajiwa kufanyika Machi, mwaka huu visiwani Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Ayubu Kimangale, wakati akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wao kama chama cha siasa lengo
lao ni kukuza chama kupitia chaguzi kama hizo, hivyo ni lazima washiriki
kwa hali na mali.
Kimangale alisema wamejiandaa kusimamisha wagombea katika ngazi za urais, uwakilishi katika kila nafasi.
Aidha, baraza hilo la wadhamini limeteua
viongozi wa muda baada ya wale waliokuwapo kusimamishwa kwa ajili ya
kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za kushindwa kuwajibika
zinazowakabili.
Kimangale alisema uongozi huo wa muda
utafanya kazi kwa kipindi cha miezi sita na baada ya hapo chama
kitafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wapya.
Alisema viongozi waliosimamishwa ambao hawatakutwa na hatia wataruhusiwa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa walioteuliwa kushika nafasi
hizo kwa muda ni Jumapili Kaliki, nafasi ya Mwenyekiti, Khamisi Kombo,
Makamu Mwenyekiti, Zamila Mrisho, Katibu Mkuu na Mvita Mangupili, Naibu
Katibu Mkuu.
NIPASHE
Viongozi wa kampuni ya Victoria Media
inayomiliki gazeti la Mawio wameelezea kusikitishwa kwao na uamuzi wa
serikali wa kulifuta gazeti hilo huku wakidai kushangazwa na uamuzi huo
mzito uliotangazwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na
Sanaa, Nape Nnauye.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo ambaye pia ndiye aliyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Mawio lililokuwa likitoka kila wiki, Simon Mkina,
alisema wameshItushwa na uamuzi wa kufutwa kwa gazeti hilo na kwamba,
pamoja na hatua hiyo kali dhidi yao, kinachowashangaza ni ukweli kuwa
hadi sasa hawajapata taarifa yoyote rasmi ya serikali kuwaarifu jambo
hilo ili wajue ni hatua gani wachukue.
“Sisi (Mawio) ndiyo waathirika wakubwa
wa taarifa hii. Kinachotushangaza ni kuwa hadi sasa hatujapata barua
yoyote ya serikali kuhusiana na jambo hili. Nasi tumemsikia tu Waziri
(Nape) akitangaza kutufuta na kwakweli tumeshtushwa sana. Tutakaa na
kuamua ni hatua gani tuchukue kutokana na uamuzi huu,” alisema Mkina
wakati akizungumza na Nipashe jana.
Kadhalika, Mkurugenzi wa Fedha na
Utawala wa kampuni hiyo, Yusuf Abood, alisema hadi jana uongozi wa
kampuni ya yao (Victoria Media) ulikuwa haujapata barua yoyote ya
kufutwa kwa gazeti hilo bali wanasikia kupitia katika mitandao ya
kijamii na vyombo vingine vya habari.
Alisema serikali inapaswa kutoa sababu
zilizosababisha kufutwa kwa gazeti hilo kwa maandishi kwani kuna adhabu
za kulifuta gazeti na adhabu za kulifungia gazeti.
Alisema kulifuta gazeti la Mawio
kutakuwa kumeminya haki ya wananchi ya kupata habari na pia kuwanyima
wananchi haki ya kupata taarifa.
Akieleza zaidi, alisema uongozi wa
kampuni ya Victoria Media ulikuwa ukipokea barua kila baada ya wiki
mbili kutoka serikalini iliyokuwa inawataka kujieleza au kutoa maelezo
kuhusu habari fulani na hivyo, hadi kufutwa kwa gazeti hilo, uongozi
wao bado haujafahamu ni habari gani iliyosababisha gazeti lao kufutwa.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema Serikali imelazimika kulifuta
gazeti la Mawio kutoka katika orodha ya magazeti yaliyopo nchini
kutokana na kukithiri kwake katika kutoa habari zisizozingatia miiko ya
uandishi wa habari licha ya kuwahi kuonywa mara kadhaa katika kipindi
cha takribani miaka nane.
Alisema amri ya kulifuta gazeti hilo
imetolewa katika tangazo la Serikali namba 55 la Januari, mwaka huu, kwa
mujibu wa Sheria ya Magazeti Sura ya 229, kifungu cha 25(1).
Nape alisema mojawapo ya habari
zilizosababisha gazeti hilo kufungiwa ni pamoja na ile iliyokuwa na
kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar” pamoja na ile ya “Seif Rais
Zanzibar, maandalizi ya kumtangaza yaiva.”
Alisema hatu hiyo inalizuia gazeti hilo
kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao kwa
mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306.
“Serikali kwa masikitiko makubwa
imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo
usioridhisha na kuandika na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa
uchochezi na pia kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi,” alisema
Nape.
Alieleza kuwa serikali haikukurupuka
kulifuta gazeti hilo, kwani Msajili wa Magazeti amekuwa akifanya juhudi
kubwa na za muda mrefu kuanzia Juni, 2013 hadi Januari 2016, kwa kumtaka
Mhariri wa gazeti hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala
bila ya mafanikio.
Alisema Msajili wa Magazeti aliwahi
kufanya mawasiliano na Mhariri wa gazeti hilo mara nane lakini mhariri
wa gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri aliopewa.
HABARILEO
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA) kwa kushirikiana na Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na
Usalama wa Taifa wamekamata madini yenye thamani ya jumla ya Sh milioni
11.2 ambayo yalikuwa yakitoroshwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA).
Aidha serikali kupitia Wizara ya Nishati
na Madini, imesema inatoa motisha kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa kwa
Kamishna wa Madini ama Wakala za utoroshaji/magendo na biashara haramu
ya madini zitakazowezesha ukamataji wa madini.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na
Mawasiliano wa TMAA, Yisambi Shiwa alisema raia mmoja wa kigeni na
Mtanzania, walikamatwa wakiwa na madini hayo bila kuwa na kibali
chochote cha usafirishaji kama ambavyo Sheria ya Madini ya mwaka 2010
inavyoelekeza.
“Raia huyu wa kigeni ambaye jina lake
linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi kwani tayari ameshafunguliwa
kesi mahakamani, alikuwa anasafiri kwenda mji wa Bangkok Thailand na
alikamatwa akiwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo almasi,
aquamarine, sapphire, green tourmaline, quartz na rhodolite,” alisema
Shiwa.
Shiwa alisema tukio lingine, Mtanzania
ambaye alikuwa anasafiri kwenda Ujerumani alikamatwa akiwa na madini na
kufikishwa katika vyombo vya dola. Alisema katika kipindi cha kuanzia
Julai mwaka jana hadi Januari 13 mwaka huu, kumekuwepo na matukio 14 ya
utoroshaji madini.
Alisema madini yenye thamani ya Sh
bilioni 3.2 yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya
Ukaguzi yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA),
Kilimanjaro (KIA) na Mwanza ambapo yote yalitaifishwa na Serikali.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
amesema operesheni inayoendelea ya kukamata wageni wanaoishi na kufanya
kazi nchini kinyume na sheria, haiwalengi raia wa Kenya kama
inavyodhaniwa.
Agizo la kuwaondoa raia wa kigeni
wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria lilitolewa na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipotembelea makao makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Waziri Masauni alisema kumekuwapo na
ongezeko la wageni nchini wanaoishi kwa vibali vya kufanya kazi za
kitaalamu au wawekezaji, lakini wanafanya biashara zisizo na tija na
wengine kufanya kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya na hivyo
kuagiza waanze kusakwa na kurejeshwa kwao.
Utekelezaji wa agizo hilo ulichukuliwa
kuwa unawalenga raia wa Kenya, ambayo ina vitega uchumi vingi na ambayo
raia wake wana muingiliano mkubwa na Watanzania.
Lakini Waziri Kitwanga alisema fikra
hizo ni tofauti na nia ya Serikali na kwamba operesheni hiyo itakuwa
endelevu. Alisema mpaka kufikia Ijumaa ya wiki iliyopita, raia 409 wa
kigeni walikuwa wamekamatwa, na wengi ni kutoka nchi za India na China.
“Tunataka raia wa kigeni anayeingia nchini afuate utaratibu,” alisema
Waziri huyo.
“Wapo wanaosema kuwa tunawalenga zaidi Wakenya, lakini kati ya raia hao 409 waliokamatwa, Wakenya ni wanane tu.”
Alisema raia kutoka Kenya wanaoishi nchini ni zaidi ya 6,000 na wote
wana vibali, isipokuwa hao wanane ambao pia walibainika kujihusisha na
uhalifu.
“Nchi za Afrika Mashariki zina
makubaliano maalum ndiyo maana hakuna usumbufu kwa raia wa nchi za
ukanda huo zaidi ya hao Wakenya tu,” alisema.
Mwaka jana kulikuwa na matukio kadhaa
yaliyohusishwa na harakati za kigaidi. Vituo viwili vya polisi vya
Mkuranga na Sitakishari vilivamiwa na watu waliopora silaha, wakati watu
takriban 10 walikamatwa mkoani Morogoro wakiwa na vifaa ambavyo polisi
walisema hutumiwa na watu hao.
Pia polisi walihitaji msaada wa askari
wa Jeshi la Wananchi kupambana na vijana waliokuwa kwenye mapango ya
Amboni Tanga, huku vituo watoto kadhaa wakibainika kufundishwa mafunzo
ya kigaidi kwenye nyumba za mkoani Kilimanjaro.
Waziri Kitwanga alisema katika
kuhakikisha mipaka na bandari inalindwa ipasavyo, wizara yake kwa
kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA), wapo katika majadiliano ya kuanza kuweka polisi
kulinda bandari, badala ya kampuni binafsi.
“Tunajadili idadi ya askari tutakaowatumia, tutawaweka sehemu gani, pia iwapo wavae sare au wawe kiraia,” alisema.
“Watanzania watambue kwamba kila
mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anaishi kwa usalama na utulivu.
Kila Mtanzania anaweza kutafuta haki yake lakini akumbuke kuwa upande
mwingine kuna wajibu anaotakiwa kuufanya. Haki na wajibu viende
sambamba.” Kuvamiwa vituo vya polisi Waziri Kitwanga pia
alizungumzia tishio la vitendo vya ugaidi kwenye ukanda wa Afrika
Mashariki, akisema matukio ya kuvamiwa kwa vituo vya polisi, yana harufu
ya ugaidi. “Ugaidi haujakomaa Tanzania, na magaidi hawajawa na nguvu.
Wanachofanya ni kuvamia kituo cha polisi, kuchukua silaha na kuzitumia
kufanya uhalifu kupata fedha ili kuendesha maisha yao. Kuna dalili kubwa
kwamba huu ni ugaidi,” alisema.
Alisema licha ya Serikali kuwakamata,
wapo wanaoendelea kuingia nchini na ili kumaliza suala hilo ni lazima
uwekwe mpango wa muda mrefu.
“Kwa sasa tunaendelea kujadiliana kuhusu
mpango wa kutambua raia wetu na wanafunzi katika shule mbalimbali.
Lazima tujue wangapi wameacha shule na wamekwenda wapi.
Ugaidi ukikomaa katika nchi unakuwa
tatizo kubwa,” alisema. “Magaidi hawatengenezwi nchini, wanatoka hapa
wanakwenda Somalia wanafundishwa na kisha wanarudi kufanya ugaidi.
Lazima tutambue raia waliotoka Tanzania
walikwenda nchi gani na kwa sababu gani. Bado tunajadiliana tuone
tutaliendesha vipi jambo hili.” Kitwanga alisema ili polisi iweze
kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima iwe na mfumo imara kuanzia makao
makuu hadi ngazi ya chini ya ulinzi shirikishi.
Alisema moja ya changamoto alizokumbana nazo baada ya kuteuliwa kuwa waziri ni dosari katika mfumo wa utendaji kazi.
Alisema nchi ina polisi 45,000 na kati
yao wanaoishi kambini ni 10,000 tu na kwamba kuishi uraiani kunashusha
nidhamu. “Hii ni changamoto kwa sababu ukitaka kuwakusanya wote hutaweza
maana wengi wanaishi uraiani.
Kwa viwango vya kimataifa, askari mmoja
anapaswa kulinda watu 350. Kwa Afrika askari mmoja analinda kati ya watu
500 hadi 700 lakini kwa Tanzania analinda watu 1,000 hadi 1,200,”
alisema
MWANANCHI
Wakati katibu mkuu wa zamani wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa akitangaza kujiondoa chama hicho, aliacha maswali ya
kutathmini ujio wa Edward Lowassa kama utakuwa mzigo au mali kwa vyama
vya upinzani, na sasa wilaya za Ilala na Kinondoni zimekamilisha majibu.
Ushindi wa kwanza wa vyama vya upinzani
katika nafasi ya umeya za manispaa hizo mbili umeonyesha nguvu ya waziri
huyo mkuu wa zamani aliyotoka nayo chama tawala.
Ushindi huo ambao unavifanya vyama vya
Chadema na CUF kuelekea kutwaa umeya wa Jiji la Dar es Salaam, pamoja na
mwingine kwenye majiji ya Mbeya na Arusha umedhihirisha nguvu ya
Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono
na vyama vingine vitatu, CUF, NLD na NCCR Mageuzi vilivyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa). “Lowassa ameiteka Dar,” alisema Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kwenye mahojiano na gazeti la Mwananchi
kabla ya madiwani wa CUF na Chadema kushinda viti vya umeya wa Ilala na
Kinondoni mwishoni mwa wiki.
“Tangu upinzani uingie nchini haujawahi
kuishika Dar.” Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema
Lowassa ameweza kuvipa vyama hivyo nafasi ya kuongoza halmashauri jambo
ambalo linathibitisha kuwa alikuwa ni mali na si mzigo kwao.
Katika uchaguzi wa meya wa Manispaa ya
Kinondoni, diwani wa Ubungo, Boniface Jackob alishinda kwa kupata kura
38, huku Jumanne Mbulu wa CUF akitwaa unaibu meya.
Kwenye Manispaa ya Ilala, Charles Kayeko
(Chadema) alishinda umeya na Omari Kumbilamoto wa CUF alitwaa unaibu.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa vyama vya upinzani jijini Dar es Salaam
tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Mbali na ushindi huo, Ukawa imefanikiwa
kutwaa viti kadhaa kwenye halmashauri ambazo zilikuwa mikononi mwa CCM
hivyo kuongeza wigo wao kwenye uongozi. Mkoani Kilimanjaro, Chadema
imeshika halmashauri sita kati ya saba ambazo ni Moshi Mjini, Hai,
Rombo, Moshi Vijijini na Siha wakati mkoani Mbeya, Chadema imechukua
halmashauri ya jiji hilo, pamoja na ile ya mji wa Tunduma.
Mkoani Arusha na Manyara, Chadema na
Ukawa zimechukua Halmashauri ya Jiji la Arusha, Monduli, Karatu, Arumeru
Mashariki, Arumeru Magharibi na Babati Mjini, wakati mkoani Kagera
Ukawa imechukua Manispaa ya Bukoba na mji mdogo wa Kayanga.
Mkoani Mtwara, CUF na Ukawa zimechukua
halmashauri ya Tandahimba, Mtwara Mjini na Newala Mjini huku mkoani
Lindi ikichukua Kilwa. Mkoani Mara, Chadema kupitia Ukawa inaongoza
halmashauri ya Serengeti, Tarime Vijijini na Tarime Mjini.
Mkoani Morogoro, Ukawa imechukua
halmashauri ya Kilombero na Ifakara huku mkoani Iringa ikichukua ile ya
Iringa Mjini. Kwa mujibu wa Lissu ongezeko la halmashauri kuwa chini ya
wapinzani limechangiwa na waziri huyo mkuu wa zamani aliyejiuzulu mwaka
2008.
Alipoulizwa kuhusu nguvu hiyo ya
Lowassa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema
mbunge huyo wa zamani wa Monduli ameleta chachu ya kupata madiwani na
wabunge wengi ingawa muungano wa Ukawa nao umesaidia. “Ukawa ndiyo kiini
cha mafanikio, lakini chachu kubwa ni Lowassa kujiunga na Chadema kwa
kuwa alikuwa na wafuasi wengi,” alisema Profesa Mpangala. Alisema hata
kusingekuwa na Ukawa wala Lowassa kujiunga na Chadema, Chadema imekuwa
ikikua mwaka hadi mwaka kwa kuongeza idadi ya wawakilishi katika
uchaguzi.
MWANANCHI
Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Jude
Ruwa’ichi amewataka wenye dhamana nchini, kufanya uamuzi mgumu kwa
ustawi wa Tanzania, akionya kuwa iwapo Zanzibar kutawaka, Bara haitakuwa
salama.
Askofu Ruwa’ichi ameyasema hayo wakati
hali ya kisiasa Zanzibar ikiwa kwenye mgogoro baada ya mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya
uchaguzi wa Rais wa visiwa hivyo, wawakilishi na madiwani, uamuzi ambao
unapingwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, huku mazungumzo ya amani
yakionekana kupoteza mwelekeo.
Akizungumaa wakati wa hafla ya kusimikwa
kwa Askofu Mkuu Kanisa Katoliki Mkoa wa Mtwara, Titus Mdoe mkoani hapa,
Askofu Ruwa’ichi aliwataka wananchi waendelee kuombea amani, lakini
wenye dhamana lazima wachukue uamuzi mgumu. “Tuzidi kuomba amani itawale
na hali inayoendelea Zanzibar tuangalie isitufikishe hatua ya
kutugawa,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
“Zanzibar pakiwaka na Bara hapatakuwa
shwari. Tumwombe Mungu atuepushe na mafarakano yote yanayoweza kuharibu
amani yetu. “Wenye dhamana wafanye maamuzi magumu kwa ustawi wa jamii.”
Kukwama kwa hali ya kisiasa Zanzibar kulifanya wagombea wa urais kutoka
vyama vyenye ushindani mkubwa, Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) na Dk Ali
Mohamed Shein (CCM) kuanza mazungumzo pamoja na marais wa zamani wa
visiwa hivyo na Jakaya Kikwete, lakini hadi sasa hakuna muafaka
uliopatikana na badala yake kila upande unatoa kauli inayopingwa na
mwingine.
Wakati Dk Shein anawataka Wazanzibari
kuanza kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi kama yalivyoahidiwa na ZEC,
Maalim Seif anataka mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 atangazwe
na vyama hivyo vikutane kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia, Maalim Seif, ambaye alikuwa Makamu
wa Kwanza wa Rais kwenye serikali ya SUK inayomaliza muda wake,
ameshamwandikia barua kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis kumuomba
atumie ushawishi wake kutatua mgogoro huo mapema. hafla hiyo
ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera,
Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama aliyekuwa mgeni rasmi.
Lakini Mhagama hakugusia suala hilo, badala yake alisema Taifa halina
maadili kuanzia ngazi ya viongozi hadi wananchi, kulitaka kanisa
kuwajenga wananchi kiimani na kimaadili na kuwa Serikali itasimamia
sheria na misingi ya maadili.
Alisema vitendo vya rushwa na mauaji ya albino yanapaswa kukemewa na kila mmoja. “Tumaini la Serikali liko kwako Mdoe.
Viongozi wa dini mtatusaidia kulea
Watanzania kwa kufuata misingi ya dini huku sisi viongozi wa Serikali
tukiwalea kwa kufuata sheria na taratibu za kisheria,” alisema. “Tabia
za kifisadi, ujambazi, kishirikina na rushwa zimeendelea kutawala
nchini. Niwahakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga
kupambana na hayo yote,” alisema Mhagama.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment