Monday, January 11, 2016

UCHAMBUZI HUU UNALETWA KWENU NA KITUO CHA ELIMU CHA CANDLE

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kiielimu, Kituo kinaendelea kusajili wanafunzi wapya, Wahi kuchukua fomu kwani nafasi ni chache, Candle wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB  Simu 0715 772746
NIPASHE
Wakati baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakihitimisha jana vikao maalum vya kila mwaka kujadili yale waliyofanya katika mwaka, imefahamika kuwa sifa walau tisa anazotakiwa kuwa nazo mrithi wa Dk. Willibrod Slaa, kwa nafasi ya ukatibu mkuu ni miongoni mwa mambo mazito yanayopasua vichwa vya baadhi ya wengi ndani ya chama hicho.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema jana, ilieleza kuwa viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, walikuwa wakiendelea na vikao vyao mjini Moshi, Kilimanjaro hadi jana jioni kwa ajili ya tathmini kuhusu mwaka uliopita na ushiriki wao katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kuangalia mambo gani ya kufanya katika kipindi cha kuanzia sasa hadi uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
Kadhalika, ajenda kuhusu jina la katibu mkuu ilipata nafasi huku jina la waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, liking’ara kwa kupendekezwa na wengi ili lipelekwe kwenye vikao vya juu vya uamuzi.
Sumaye alijiunga rasmi Chadema hivi karibuni akitokea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako jina lake liliondolewa wakati wa mchakato wa kuwania urais ndani ya chama hicho tawala.
Jitihada za mwandishi kumpata Mbowe jana kuelezea yanayojiri kwenye kikao chao, ikiwamo harakati za uteuzi wa jina la katibu mkuu, zilishindikana kwani hadi jioni, bado kikao chao kilikuwa kikiendelea huku ikielezwa kuwa simu za viongozi wote wa juu (akiwamo yeye) ziliwekwa mbali na wajumbe hao.
“Ni vigumu kumpata Mbowe wala viongozi wengine wa juu kwa sasa kwa sababu wamejifungia kwa ajili ya kikao na simu zao ziko mbali na wao… ila kwa ufupi, jina la Sumaye bado linatawala katika mjadala kuhusu katibu mkuu wa chama,” mmoja wa viongozi wa Chadema alimweleza mwandishi jana kwa sharti la kutoandikwa jina.
Kabla ya kikao cha jana kilichotarajiwa kuhitimisha mfululizo wa vikao vilivyoanza wiki iliyopita, ilielezwa kuwa ajenda kubwa ni tathmini ya mwaka uliopita na pia kujadili watakayofanya mwaka huu.
“Vikao hivyo vinaendelea kufanya tathmini na uchambuzi wa mpango kazi wa mwaka 2010-2015 na kupanga kwa ajili ya 2016-2020 kabla ya kuwasilisha kwenye vikao vya uamuzi kwa mwaka huu, ambavyo vitafanyika kwa mujibu wa utaratibu wa kikatiba,” ilisema sehemu ya taarifa ya Chadema kwa umma kuhusiana na vikao hivyo mjini Moshi.
Wakati mfululizo wa vikao hivyo ukifikia tamati jana, imefahamika kuwa harakati za kumpata mtu mwenye sifa za kuwa katibu mkuu wa chama hicho kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Slaa bado ni kitendawili.
Chanzo kutoka ndani ya Chadema kiliiambia Nipashe kuwa uteuzi wa jina la mtu atakayerithi mikoba ya ukatibu mkuu uliokuwa ukishikiliwa na Slaa, unavuta hisia za wengi kwa kuwa ni nafasi muhimu kwa mustakabali wa chama na kwamba jambo hilo limeongezeka umuhimu sasa kutokana na ukweli kuwa chama  kimekuwa kikubwa zaidi na kuungwa mkono na mamilioni ya Watanzania.
Katika uchaguzi mkuu uliopita, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, aliyekuwa akiungwa mkono pia na muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 39.97 ya kura zote halali zilizopigwa huku Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiibuka mshindi kwa kupata asilimia 58.46.
“Sumaye amekuwa akitajwa sana. Lakini kwa ufupi ni kwamba jina la mrithi wa Slaa (Katibu Mkuu) linasubiriwa kwa hamu kubwa. Hii ni nafasi nyeti kwa chama kikubwa kama Chadema, hivyo haishangazi kusikia wengi wakifuatilia ili kujua ni nani atakayekuwa na sifa za kukamata usukani huo,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki.
Dk. Slaa aliitumikia Chadema katika nafasi ya ukatibu mkuu kuanzia mwaka 2002 hadi Julai, mwaka jana, wakati uongozi wa juu wa chama hicho uliporidhia kuwa apumzishwe na kisha yeye mwenyewe kutangaza baadaye kuwa amejiuzulu na kustaafu siasa, akipinga uteuzi wa Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho.
Tangu Slaa alipokosekana katika nafasi hiyo, Chadema bado haijatangaza mrithi wake na nafasi yake imekuwa ikikaimiwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu.
“Hakuna sababu ya kujaza nafasi hiyo (katibu mkuu) haraka… ni lazima uongozi wa juu uwe makini zaidi kwa sababu chama ni kikubwa hivyo changamoto zake ni kubwa pia.  Mtu anayeteuliwa kushika nafasi hiyo ni lazima achunguzwe kwa undani ili kujiridhisha kuwa kweli ana sifa zinazostahili,” chanzo kingine kilisema.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema walitaja sifa takribani nane kuwa ni sehemu ya zile anazopaswa kuwa nazo mwanachama yeyote atakayekuwa katibu mkuu wa chama hicho na kukiwezesha kupiga hatua zaidi katika kipindi hiki chenye ushindani mkubwa wa kisiasa.
Baadhi ya wale walizoungumza na Nipashe na kutaja sifa hizo , kwa mtazamo wao, na ambazo jumla yake ni nane, ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Mwesige Baregu; Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Arumeru, Samweli Nnko na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Vincent Nyerere.
“Chama kina taratibu zake, miongozo yake, kanuni, katiba na sifa…mambo hayo ndiyo hufuatwa katika kumpata kiongozi wa nafasi hiyo (katibu mkuu), “ alisema Prof. Baregu kabla ya kutaja sifa anazoona kuwa zinafaa kuangaliwa kwa mtu anayeshika nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Baregu, sifa mojawapo ni kwa mtu huyo kuwa na uelewa mpana si tu wa mambo ya Chadema, bali na vyama vingine vya siasa nchini. Awe mzoefu wa kutosha kwenye uwanja wa siasa na pia awe mvumilivu kwa kuwa madongo ya kiasiasa yanayotupwa mengi huelekezwa kwa Katibu Mkuu.
Baregu alisema kuwa pili, awe mzuri katika kushirikiana na wengine kwa kuwa anaweza kuwa Katibu Mkuu anayejiamulia mambo peke yake bila kuwashirikisha wengine na hilo halipaswi kutokea kwa sababu mawazo ya wengine yanaweza kuwa mazuri katika kukisaidia chama.
Sifa ya tatu ina uhusiano na ya pili. Kwamba, katibu mkuu ajaye wa Chadema ni lazima awe msikivu na hapaswi kuwa mbishi au anayefikiria anayoamini yeye ndiyo sahihi na si ya wengine. Ni lazima awe na uwezo wa kusikiliza wengine kwani ni kawaida ndani ya vyama kuwa na malumbano na tofauti za hapa na pale, matukio ambayo baadhi ya watu huyatafsiri tofauti na yeye (katibu mkuu) awe wazi kupokea maoni ya watu tofauti na kuyapa nafasi.
NIPASHE
Chama cha Wafanyakazi Madereva wa Malori Tanzania (CHAWAMATA), kimetoa wito wa kukutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ili kumfikishia malalamiko ya posho ndogo wanazolipwa kwa safari za ndani na nje ya nchi.
Malipo yaliyopendekezwa katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Usafiri na Usafirishaji chini ya Mwenyekiti Hawa Wenga, ni Sh. 32,250 kwa siku kwa safari za ndani na dola 25 kwa safari za nje.
Katibu wa Chamawata, Greyson Wimile, katika kikao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha madereva hao, alisema Januari 7, mwaka huu, walimpelekea barua Waziri Mkuu malalamiko yao ili atatue.
Alisema barua hiyo iliambatana na orodha ya majina 763 ya madereva  ambao hawakubaliani na posho wanayolipwa kwa siku.
Wimile alisema mapendekezo yao ni kulipwa sh. 70,000 kwa safari za ndani na dola 75 kwa safari za nje ya nchi bila kujali aina mzigo alioubeba dereva.
“Dereva anayesafiri nje ya nchi kulipwa dola 15 kwa malori yanayibeba ‘ dry cargo’ na dola 25 wanaobeba mafuta kwa siku ni ndogo haikidhi mahitaji kukingana na kazi,” alisema Wimile.
Alisema malipo ya dereva kwa safari za ndani anayeendesha malori yanayobeba ‘dry cargo’ kulipwa sh. 32,250  na malori ya mafuta ni sh. 53, 750 kwa siku, hayakuzingatia kwa makusudi maazimio ya kikao cha Oktoba 13, mwaka jana.
Alisema dereva, kulingana na aina ya mzigo anaobeba, anastahili kulipwa sh. 70,000 kwa siku na dola 75 kwa siku safari za nje.
Mmoja wa madereva hao, Dominic Lyaro, alisema madereva huchangia uchumi wa nchi kwa asilimia kubwa, hivyo madai hayo yashughulikiwe mapema.
“Kasi ya serikali hii tunaitaka na kwetu. Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu (mstaafu) Mizengo Pinda, haikuwa na maana, hivyo tunamtaka Majaliwa atumbue majipu haya,” alisema Lyaro.
Madereva wa malori nchini wameilalamikia serikali kwa muda mrefu kwa kutosimamia kuwapo kwa malipo yanayokidhi mahitaji yao na kusababisha migomo ya mara kwa mara.
NIPASHE
Mkoa wa Dodoma, leo unatarajiwa kufanya kongamono la siku tano la kuombea taifa pamoja na viongozi, ambalo pia litawashirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini na wa serikali.
Katibu wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma, Askofu Dk. Eliya Mauza, alisema kongamano hilo limeandaliwa na Nyumba ya Maombi Taifa kwa kushirikiana na Umoja wa Madhehebu ya Kikristo mkoani Dodoma.
Dkt Mauza alisema lengo la kongamano ni kuiombea serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Dk. John Magufuli pamoja na Baraza la Mawaziri ili iweze kufanya kazi zake chini ya ulinzi wa Mungu.
“Lengo la kongamano hili ambalo viongozi wake wanatarajia kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, ni kuombea taifa na viongozi wetu wa kitaifa ikiwemo na Zanzibar ambayo mpaka sasa iko kwenye mvutano wa kumpata rais wake,” alisema.
Katibu huyo wa umoja alisema kuwa kongamano hilo pia litachukua kipindi hicho kuombea Umoja wa Makanisa ya Tanzania kutokana na kutokuwa na ushirikiano wa kiroho na kimwili.
MTANZANIA
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif  Hamad, leo anatarajia kufichua siri ya mazungumzo ya kusaka suluhu, baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufutwa mwaka jana.
Habari za uhakika zinasema kwamba, Maalim Seif atakutana na waandishi wa habari kueleza kwa kina mwenendo wa mazungumzo hayo baina ya CUF na  CCM yalipofikia.
Maalim Seif, anachukua uamuzi huo wakati hali ya kisiasa visiwani humo ikizidi kuwa ngumu kwa pande zote, licha ya Rais Dk. John Magufuli kuahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Maalim Seif anajitokeza leo, wakati wiki iliyopita Rais Magufuli  alikutana na  viongozi wastaafu, ambao kwa pamoja walizungumza mambo mazito ya kitaifa pamoja na kutakiana heri ya mwaka mpya.
Wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alimhakikishia kumpa ushirikiano atakapohitajika kufanya hivyo.
Katika kumhakikishia kuwa yuko tayari kufanyakazi atakayomtuma, taarifa za ndani zinaeleza kuwa moja ya jambo kubwa ambalo Mkapa anaweza kulisimamia ni suala la kusaka suluhu ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Mkapa alisema lengo la mkutano huo ni kumpongeza Rais Dk. Magufuli kwa dhamana aliyopewa na Watanzania na kumtakia heri ya mwaka mpya.
Mkapa alimhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote na kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Licha ya Mkapa, Rais Magufuli pia alikutana na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye alikabidhi baadhi ya nyaraka kwa Rais Magufuli.
Kikwete alikabidhiwa nyaraka hizo zinazohusiana na mgogoro huo na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 4, mwaka jana.
Inaelezwa kuwa Maalim Seif alikabidhi nyaraka mbalimbali, zikiwamo fomu za matokeo ya Uchaguzi  Mkuu kwa vituo vyote vya Zanzibar.
Mbali na kukutana na watangulizi wake hao pia alikutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba.
Katika mazungumzo hayo, licha ya Jaji Warioba, kumtakia heri ya mwaka mpya, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri, lakini pia wakazungumzia mchakato wa Katiba mpya na hali ya kisiasa Zanzibar.
Naye Maalim Seif,  leo natarajia kuzungumza na waandishi wa habari kueleza hatima ya mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta mwafaka Zanzibar
“Maalim Seif kesho (leo), atazungumza na wahariri na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.
Desemba 24, mwaka huu Rais Magufuli alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu, Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa mazungumzo hayo na hali ya kisiasa visiwani humo.
Mazungumzo hayo yalifanyika, ambapo taarifa ya kukutana kwa viongozi hao ilitolewa kwa vyombo vya habari jioni na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Taarifa hiyo ilieleza baada ya mazungumzo ya viongozi hao, Rais Shein alieleza kuwa lengo la mazungumzo yao ilikuwa ni kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu hali ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar.
Taarifa ilieleza kuwa Dk. Shein alisema mazungumzo hayo  yanaendelea vizuri chini ya Kamati Maalumu ya kutafuta suluhu iliyopo chini ya uenyekiti wake.
Mbali ya Dk. Shein, wajumbe wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Wengine ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Rais Mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Salmin Amour.
Dk. Shein alisema amemtaarifu Rais Magufuli kuwa kamati yake ilianza mazungumzo Novemba 9, mwaka huu  na hadi sasa bado inaendelea na kazi yake.
“Nimekuja kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni jukumu letu kumpa taarifa,” ilieleza taarifa hiyo.
Kabla ya kukutana na Rais Shein, tayari Desemba 21, mwaka jana Rais Magufuli alikutana na Maalim Seif, Ikulu Dar es Salaam na kuzungumzia mgogoro huo wa Zanzibar.
MTANZANIA
Spika wa Bunge, Job Ndugai, anatarajia kutangaza kamati za Bunge leo.
Ndugai alisema atatangaza kamati hizo chini ya utaratibu mpya na kwamba leo atatangaza Kamati ya Kanuni pekee.
Baada ya kuitangaza kamati hiyo, nyingine zilizobaki atazitangazia mjini Dodoma wakati vikao vya Bunge vitakapokuwa vikiendelea mwishoni mwa mwezi huu.
Utaratibu huo umebainishwa na Ndugai alipoulizwa na gazeti hili ambalo lilitaka kujua iwapo Kamati za Bunge zitatangazwa kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo Januari 26, Mwaka huu.
“Kesho (Leo) nitatangaza kamati moja tu ya kanuni na nyingine nitazitangazia mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo,” alijibu kwa ufupi.
Taarifa ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema kwamba Spika Ndugai amepanga kupunguza wingi wa Kamati za Bunge ili kuendana na uchache wa wizara zilizopo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kamati zinakuwa chache lakini zilizo na uwezo wa kufanyakazi kwa kasi ambayo itaisaidia serikali ya awamu ya tano.
Baada ya leo kutangaza Kamati ya Kanuni, Spika Ndugai atabaki na jukumu la kutangaza kamati nyingine 14 mjini Dodoma, iwapo hakutakuwa na ongezeko la kamati.
Kamati za Bunge huundwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 96, likiwa limepewa madaraka ya kuunda kamati za Bunge za aina mbalimbali na muundo wake umefafanuliwa na Kanuni za Kudumu za Bunge.
Katika muundo huo zipo kamati za kisekta na zile zisizokuwa za kisekta, ambazo kwa pamoja hufanyakazi na kutekeleza majukumu yao kwa niaba ya Bunge.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 89 Bunge limeunda Kamati 15, ambapo baadhi ya kamati hizo ni Kamati ya Haki, Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara.
MTANZANIA
Wananachi wa Kunduchi Mtongani,  jijini Dar es salaam wameokota mwili wa mtoto mchanga aliyenyofolewa kichwa kwa kuliwa na mbwa.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Thomas John aliliambia MTANZANIA kwamba wananchi walikibaini kichanga hicho baada ya kuburuzwa na mbwa kutoka kichakani kilikokuwa kimetupwa.
“Mtoto mchanga naona amezaliwa alfajiri ya leo (jana) na kutelekezwa na mama yake ambaye hadi muda huu wa saa 11 jioni bado hatujamtambua.
“Hili linaonekana sasa kuwa tatizo sugu kwa wanawake wenye roho za kinyama. Leo binadamu analiwa na mbwa kweli jamani Mungu wangu dunia yetu hii tunakwenda wapi,” alisema kwa masikitiko John
Alisema baada ya kubainika kwa mwili wa kichanga hicho walitoa taarifa kwa Mjumbe wa Nyumba Kumi ambaye aliwasiliana na polisi ili waje kwa ajili ya hatua za uchunguzi, lakini hadi kufikia saa 12 jioni hakuna askari aliyefika katika eneo hilo.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Juma alisema kwamba iwapo tukio hilo litaachwa bila kufanyika kwa uchunguzi wa kumpata muhusika upo uwezekano mkubwa kwa wanawake kuendelea kutupa watoto.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema hana taarifa hizo,  huku akiahidi kufutilia tukio hilo kwa ajili ya uchungu wa kina.
“Kwa kifupi sijapata taarifa hizo ndiyo kwanza unanipatia ila Jeshi la Polisi litafuatilia kwa karibu na likifanikiwa kumpata mtuhumiwa wa tukio hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na tutatoa taarifa kwa umma,” alisema Kamanda Wambura.
MTANZANIA
Viongozi wa Kitongoji cha Kasalazi, kilichoko katika Kijiji cha Kanyara, Kata ya Bulyaheke, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, wanadaiwa kuwachapa fimbo hadharani wanawake wanaovaa nguo fupi zinazoonyesha baadhi ya sehemu zao za siri.
Pia, viongozi hao wanadaiwa kuwatoza faini ya Sh 20, 000 wanawake wanaokutwa na nguo hizo kama njia ya kuwafanya wasiendelee kuvaa nguo hizo.
Mmoja wa wasichana waliowahi kuchapwa na viongozi hao aliyejitambulisha kwa jina la Juliana Mafuru, alichapwa fimbo baada ya kufika kijijini hapo kwa lengo la kununua dagaa.
“Cha kushangaza ni kwamba, baada ya kufika katika kitongoji hicho, mgambo walinikamata na kunichalaza bakora mbele za watu nje ya boti niliyokuwa nimepanda.
“Pia waliamuru nivue suruali niliyokuwa nimeivaa na kuanza kuichana chana nyembe.
“Wakati wananifanyia hivyo, walitokea wasamalia wema ambao walinipatia shuka la kimasai ili niweze kujisitili, yaani waliniabisha kweli.
“Baadaye, walinipeleka kwenye ofisi ya kitongiji hicho na walinitoza faini ya shilingi 20,000, kisha wakaniachia,” alisema Juliana.
Nao wakazi wa kijiji hicho, Lafael Bitulo na Mariamu Chacha, walisema mwenyekiti wa kitongiji hicho na katibu wake, ndiyo vinara wa tabia hiyo kwa kuwa wamekuwa wakinufaika nayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Andrea Mkama, alikiri kuwachapa fimbo wanawake wanaovaa nguo fupi na zinazobana kwa mavazi wanayovaa ni ya udharirishaji.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kanyara, Lazoro Mgonzo, alithibitisha wanawake kuchapwa fimbo ingawa alisema ni kitendo cha udharirishaji.
Mkuu wa Wilaya Sengerema, Zainabu Terack alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema hana taarifa ingawa aliahidi kulifuatilia
MTANZANIA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano, Mazingira), January Makamba, amefanya ziara na kujionea namna wananchi waliobomolewa nyumba zao wanavyoishi kwa kukosa makazi.
Kutokana na hali hiyo, amesema  hakuna mwananchi anayeonewa au anayeteseka na kunyanyasika katika kazi ya kuwaondoa wakazi wanaoishi katika Bonde la Msimbazi ila kazi hiyo inafanyika kwa mujibu wa sheria.
Hayo aliyasema  jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuwatembelea wananchi wa maeneo mbalimbali ambao nyumba zao zimebomolewa na nyingine kuwekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.
Katika ziara hiyo, Makamba alijionea hali mbali ya uchafuzi wa mazingira hasa katika maeneo ya Kigogo,Mburahati na na Kinondoni Mkwajuni.
Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, Makamba alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuendelea kuwaona wananchi wanakufa kila mwaka kutokana na mafuriko na wengine wanaishi katikati ya bonde na kwenye kingo za mito, huku wakielekeza majitaka yao kwenye mito na mifereji.
Alisema kazi ya kuondoa wakazi itazingatia misingi ya ubinadamu.
“Hakuna mtu atakayekurupushwa na kubomolewa nyumba anayoishi bila yeye na Serikali kuthibitisha kama hakumilikishwa kiwanja au nyumba, na kwamba anapoishi hapastahili kwa makazi na shughuli za binadamu.
“Mtu yeyote ambaye amemilikishwa eneo na Serikali na amepewa kibali cha ujenzi, hataondolewa hadi atakapopewa kiwanja mbadala, ila Serikali yetu inataka sheria zifuatwe lakini pia ina sura ya kibinadamu,” alisema January.
Akiwa katika eneo la Kinondoni Mkwajuni, Waziri Makamba alikagua uzoaji wa kifusi kilichotokana na ubomoaji wa nyumba zilizokuwa katika bonde hilo.
“Tunataka eneo hili liwe safi kabisa ili tuonyeshe mfano wa maendelezo bora na rafiki kwa mazingira ya maeneo ya mabondeni,” alisema .
Akiwa katika eneo hilo,alikutana na wananchi ambao waliomba ufafanuzi kuhusu kero mbalimbali wanazozipata.
Alisema Serikali imeomba taarifa kupitia mamlaka za Serikali za mitaa kuhusu watu wote wenye kuhitaji msaada maalumu wa kibinadamu na jitihada zitafanyika ili kuweza kuwasaidia watoto waliokuwa wanaishi mabondeni kuhamishiwa katika shule nyingine.
Kutokana na hali hiyo, January alitoa siku saba kwa viongozi hao kuhakikisha mito hiyo inakuwa safi kwa kuwashirikisha wananchi kufanya usafi na kuomba halmashauri husika zitoe magari.
Alisema iwapo viongozi hao watashindwa kutekeleza agizo hilo, basi kibarua chao kitakuwa shakani, ni pamoja na kuwawajibisha kwakuwa wamechangia uchafuzi wa mazingira.
Alisema Benki ya Dunia na serikali ya Marekani zimetoa Sh bilioni 100 kwa ajili ya kusafisha mito na kuijengea ili ipitishe maji kwa mtiririko ambao hautasababisha mafuriko.
“ Hali hii inatisha, haiwezekani kiongozi wa mtaa unaongoza wananchi katika eneo chafu hivi, ninaondoka leo (jana), Jumapili ijayo nakuja, kama nitakuta hivi, kazi utakuwa huna leo na kusamehe…itisha mkutano panga wananchi wako,mfanye usafi,” aliagiza Januari.
Bomoabomoa jijini Dar es Salaam ilianza Desemba 17, mwaka jana ambapo hadi sasa tayari nyumba kadhaa  zimebomolewa na nyingi zimewe kuwekewa alama ya X.
HABARILEO
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema operesheni kwa lengo la kuwachukulia hatua raia wa nje wanaofanya kazi nchini bila kufuata sheria za nchi, ni endelevu na itagusa maeneo yote ikiwemo wafanyakazi wa majumbani.
Msemaji wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alisema hawakukurupuka kuendesha operesheni hiyo, bali hakuna mgeni anayeruhusiwa kufanya kazi nchini bila vibali.
Tamko hilo la kusisitiza limekuja huku takwimu zikionesha kwamba, hadi mwishoni mwa wiki, watu 79 walishakamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma nazo.
“Lengo la Wizara ni kuhakikisha operesheni hii inaenda kwa kasi na kwa ufanisi, tutagusa maeneo yote, iwe viwandani, mashambani na hata majumbani lazima lengo letu litimie,” alisema Nantanga.
Alisisitiza, “Nawatahadharisha wale wote wanaodai kuwa tumekurupuka, watambue kuwa hakuna mgeni yeyote anayeruhusiwa kufanya kazi nchini kinyume cha Sheria, hivyo wale wote wanaoendelea kuwaajiri wageni wa aina hiyo wamevunja Sheria.”
Alisema Serikali inafanya kazi kuhakikisha nchi inakuwa salama na watu wote wanafuata Sheria. Alisema kuendelea kuwepo kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi bila vibali ni kuvunja Sheria.
Aliwataka raia wa kigeni wanaotambua kuwa wanafanyakazi kinyume cha sheria, ikiwemo kutokuwa na vibali, kujisalimisha wenyewe ofisi za Uhamiaji kabla ya kufikiwa na operesheni hiyo.
Aidha aliwataka waajiri wote kuhakikisha raia wote wa kigeni waliowaajiri wanafanya kazi kihalali. Alisisitiza, endapo kuna raia wa kigeni asiye na kibali au yuko kinyume cha Sheria, asalimishwe Uhamiaji mara moja kabla sheria haijachukua mkondo wake, au kuwasili sha taarifa zake.
Alitoa mwito kwa wananchi wenye taarifa za kuwepo kwa raia wa kigeni, wanaoishi au kufanyakazi kinyume cha sheria, kuziwasilisha wizarani ziweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
“Natoa onyo, watu wasije wakajificha na kudhani kuwa wako salama kwa sababu operesheni hii ni endelevu, popote walipo tutawafikia,” alisema. 79 wakamatwa Hadi mwishoni mwa wiki watu 79 walishakamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma nazo.
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule, watuhumiwa hao wanatoka katika nchi 15. Nchi hizo na idadi ya waliokamatwa kwenye mabano ni Nigeria (4), China (20), Ethiopia (23), Korea (9), Jamhuri ya Kidemokrasia ya CongoDRC (6), Somalia (3),Uganda (2), Madagascar (5), Burundi (2), Ivory Coast (1), Lebanon (1), India (1), Zimbabwe (1) na Ghana (1).
Naibu Waziri Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alipofanya ziara Makao Makuu Idara ya Uhamiaji, aliagiza ichunguze kampuni zote nchini zinazotoa ajira kwa wageni wakati ajira hizo wangeweza kupewa Watanzania wenye sifa.
Masauni aliwaambia watendaji wakuu wa idara hiyo kwamba lazima kuwe na mfumo thabiti wa kudhibiti tatizo hilo kwa ajili ya manufaa ya nchi nzima. Aliagiza idara hiyo kuimarisha ulinzi na ukaguzi wa mipaka nchini, kurahisisha mapambano dhidi ya wageni wanaoingia nchini kiholela.
Hata hivyo, alitaka idara hiyo kushughulikia haraka tatizo la vibali vya ukazi, kwa kile alichosema imebainika kuwepo wakazi wengi wa kigeni nchini waishio na kufanya kazi nchini kinyume na sheria za nchi
MWANANCHI
Wachungaji wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) wametangaza kumfukuza kazi Askofu wa Dayosisi hiyo, Boniface Kwangu kwa madai ya kuhusika na ubadhilifu wa Sh500 milioni.
Hii si mara ya kwanza kwa wachungaji wa kanisa hilo kumkataa Askofu Kwangu, baada ya mpango kama huo kushindikana Septemba 2012 walipomtaka ajiuzulu kwa sababu mbalimbali.
Akisoma tamko la kumfukuza kazi askofu huyo jana mbele ya waumini wa kanisa hilo, Mwenyekiti wa wahudumu wa kanisa, Mchungaji Andrew Kashilimu alidai askofu huyo amekikuka viapo vyake, Katiba ya Jimbo hilo, Katiba ya DVN, utumiaji mbaya wa madaraka, mali na fedha za kanisa, kanuni na maadili ya kanisa hilo.
Mchungaji Kashilimu alidai baada ya kikao cha wachungaji kilichofanyika Septemba mwaka jana kilithibitisha kwamba askofu huyo hafuati kanuni na taratibu za kanisa Anglikana Tanzania na amekuwa akiendeleza matabaka ndani ya wahudumu na waumini na utoaji ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.
“Baada ya kuchanganua mambo yote kwa ujumla, kikao kikaridhia Askofu Boniface Kwangu ajiuzulu kwa ajili ya afya ya Kanisa la Mungu.
Taarifa zilifika Jimbo Kuu Anglikana Tanzania na Jimbo kupendekeza iundwe Tume ya kushughulikia mgogoro wa DVN,” alisema Mchungaji Kashilimu na kuongeza: “Baada ya kuundwa kwa tume hiyo, taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya shule ya Isamilo ambayo inamilikiwa na kanisa ilibainisha kwamba kulikuwa na upotevu wa zaidi ya Sh500 milioni.
Katika hili Askofu Kwangu alihusika na ufisadi huo.” Kashilimu alidai askofu huyo aligundulika kufungua akaunti binafsi katika benki ya Mkombozi anayotumia kujipatia fedha kutoka kwa wahisani kwa kutumia jina la dayosisi hiyo. “Mbali na yote alichukua dola 3,000 ambazo ni sawa na Sh6,000,000 kutoka kwa mhasibu wa shule ya Isamilo kwa ahadi ya kuzirejesha, baada ya kudaiwa aliamua kumfukuza kazi na mpaka sasa hajazirejesha.
Kipindi cha mwaka 2008/2012 alichukua tena Sh15,364,560 kutoka kwa mhasibu huyo nazo hajazirejesha,” alidai.
Kashilimu alidai kutokana na tuhuma hizo Askofu huyo amesababishia dayosisi hiyo kudaiwa na waajiriwa waliofukuzwa na kusimamishwa kazi kinyume na utaratibu wa utumishi wa umma, hivyo kanisa hilo lina deni la zaidi ya Sh60 milioni na kwamba ameuza gari la dayosisi hiyo.
“Kutokana na mambo yote aliyoyafanya Askofu, kanisa limekosa imani naye na limeridhia kwa kauli moja afukuzwe kazi, kwani amefanya ubadhirifu mkubwa kwa kanisa na kwamba kwa kipindi cha miaka saba aliyokuwa askofu hakuna taarifa ya mapato na matumizi aliyoitoa.
Katika hatua nyingine Kashilimu alisema wametoa taarifa dhidi ya askofu huyo katika Kituo cha Polisi Mkoa wa Mwanza na kupewa RB namba MW/RB/265/2016. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mwanza, Justus Kamugisha alipoulizwa alisema hajapata taarifa hizo na kuahidi kufuatilia tuhuma hizo kwa kuwa zinahitaji uchunguzi ili kutolea ufafanuzi.
Juhudi za kumpata askofu aliyeelezwa kuwa yuko nchini Marekani kwa miezi mitano sasa ili azungumzie tuhuma hizo zilishindikana na hata alipoandikwa ujumbe kwa baruapepe gazeti halikupata majibu hadi linakwenda mitamboni.
Pia juhudi cha kuwapata Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jacob Chimeledya na Katibu mkuu wa kanisa hilo, Johnson Ching’ole hazikuzaa matunda baada ya simu zao za kiganjani kutopatikana.
MWANANCHI
Baadhi ya watu waliokuwa wakiishi katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) wamedai kuporwa mali zao na kudhalilishwa na mgambo wa jiji la Dar es Salaam, wakati wakiwatimua mwishoni mwa wiki. Madai hayo waliyatoa jana katika ofisi za gazeti hili zilizopo barabara ya Mandela Tabata jijini hapa.
Kuanzia Alhamisi iliyopita, gazeti hili limekuwa likiripoti habari za kuwapo kwa watu wanaoishi kituoni hapo kwa miaka kadhaa wakijifanya kuwa ni wasafiri bila ya uongozi kuchukua hatua.
Baada ya habari hizo, mgambo hao waliendesha operesheni kuwatimua watu hao kituoni hapo. Hata hivyo, Meneja wa UBT, Juma Iddy alisema hawezi kufahamu kama watu hao walikuwa wakiishi kituoni hapo kwa sababu wamekuwa wakifanya operesheni mara kwa mara ya kuwatimua.
“Operesheni hapa ni endelevu kwa sababu kila siku watu wanaingia na kutoka, miundombinu ya kituo chetu ni vigumu kuwadhibiti wasiingie, hivyo mara kwa mara tunawaondoa na wengine kuwafikisha polisi,” alisema.
Wakizungumza jana, watu hao walisema wanatoka mikoa mbalimbali nchini na kwamba walifika jijini Dar es Salaam kupatiwa matibabu, kufuatilia mirathi, mafao ya uzeeni huku mmoja akidai kutelekezwa na mume wake. Askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Hamisi Mohamed (101) mkazi wa Ngara, mkoani Kagera, alisema yupo Dar es Salaam kupatiwa matibabu ya mguu katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, lakini hana ndugu jijini hapa, hivyo amelazimika kuishi kituoni hapo.
“Nilikuwa mmoja wa wapiganaji wa vita ya Tanzania na Uganda, nikapigwa risasi ya mguu, nilifanyiwa upasuaji na kuondolewa risasi, lakini kikabaki kipande ndicho ambacho kinanisumbua hadi sasa,” alisema.
Alisema wakati anasubiri kufanyiwa upasuaji hawezi kulazwa kwenye wodi za hospitali hiyo, hivyo amelazimika mwezi mzima kulala katika kituo hicho. “Juzi usiku walikuja mgambo wamenipiga, wakanimwagia maji na kuchukua simu zangu mbili na kutufukuza na watu wengine,” alilalamika na kusisitiza kuwa yeye na wenzake leo watakwenda kutoa taarifa za upotevu wa mali zao Kituo cha Polisi cha Urafiki.
Kwa upande wake, mmoja wa wafanyakazi wastaafu wa Jiji la Dar es Salaam, mkazi wa Kihesa mkoani Iringa, ambaye aliomba asitajwe jina lake, alisema anafuatilia mafao yake, lakini kwa sababu hana ndugu, amekuwa akiishi katika kituo hicho.
Alisema katika oparesheni ya kuwafukuza, begi la nguo lilipotea katika mazingira ya kutatanisha na anahisi mgambo walilichukua.
Kwa upande wake, Catherine Raphael kutoka mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, alisema yuko Dar es Salaam kushughulikia mirathi ya marehemu mumewe Mahakama Kuu.
Agnes Daniel (20), mkazi wa Singida akiwa amembeba mwanae wa mwaka mmoja, alidai alitelekezwa na mumewe na kuamua kuishi kituoni hapo. Alisema alipoteza begi lenye nguo na Sh30,000 za nauli ya kurudi kwao Singida.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment