MTANZANIA
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye aliungwa mkono na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, amesema anajipanga upya kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Lowassa aliweka wazi dhamira yake hiyo,
jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara
wanaomwunga mkono wanaojulikana kama Timu Mabadiliko wa Soko la Kariakoo
ambao walitaka kusikia kauli na hatima yake kisiasa baada ya kumalizika
kwa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Lowassa ambaye alipata kuwa waziri mkuu,
alisema bado hajakata tamaa ya kuwaongoza Watanzania, licha ya
vizingiti kadhaa alivyowekewa vikiwamo vya kumzuia kufanya ziara za
kuwashukuru wananchi waliompigia kura nchi nzima.
“Wale walio na nia ya kutaka kujua
mustakabali wangu kisiasa nawaambia kwamba pamoja na kuwepo kwa mambo ya
kutaka kunikatisha tamaa, lakini sitakata tamaa na nipo tayari kuwania
urais na kushinda kwa kipindi kijacho cha mwaka 2020.
“Niko fiti na morali yangu iko
juu naiona kazi hiyo ndiyo kwanza imeanza najua kama Mungu amepanga
nitakuwa rais wa Tanzania niko tayari kuanzia sasa na ninaamini
tutashinda kama tulivyoshinda katika uchaguzi uliopita Oktoba 25, “alisema Lowassa.
Kiongozi huyo aliwataka wananchi nao pia
kutokata tamaa ya kupata mabadiliko ya kweli kwa sababu yuko tayari
kugombea hata mara tano ili apate haki yake kwa sababu anaamini kwa
nguvu za Mwenyezi Mungu atakuja kuwa rais wa Tanzania.
“Sitakuwa kiongozi wa kwanza
kuwania mara tano kwani yupo rais mmoja wa Marekani aliyewahi kuwania
zaidi ya mara nne na alipogombea mara ya tano alifanikiwa kupata urais,
mwingine ni rais wa Senegal Abdoulaye Wade,” alisema Lowassa.
Katika mkutano huo, Lowassa pia
alizungumzia sababu za kutochukua hatua za kuwaruhusu wanachama na
wafuasi wake kuingia barabarani kwa maandamano kudai ushindi.
Kwa mujibu wa Lowassa, hatua hiyo ilichangiwa na dhamira yake ya kutaka kulinda amani ya nchi.
“Matokeo yaliwashangaza wengi nikiwamo
mimi mwenyewe, hali iliyosababisha wengi kuniomba nitoe kauli ya kuingia
mitaani, lakini nikatumia busara kuwatuliza kwani ningewaruhusu
wangechinjana lakini sikutaka kuingia Ikulu kwa kumwaga damu.
“Nawashukuru Watanzania kwa kuwa
watulivu na kunisikiliza ombi langu lililowezesha Tanzania kuendelea
kuwa na amani kwani sikuwa tayari kuona inavurugika kwa muda mfupi
wakati imedumu tangu tulipopata uhuru kwa sababu ya kwenda Ikulu,’
alisema.
Lowassa alisema pamoja na kupokonywa
ushindi wake, lakini anaamini vyama vya upinzani vimetoa changamoto
kubwa kwa CCM na serikali ya awamu ya tano ambao wameamua kutumia baadhi
ya sera zilizokuwa kwenye ilani yao ya uchaguzi.
“CCM wanatakiwa kuwa waungwana pindi
wanapo nakili Ilani za Chadema, wanatakiwa kusema ukweli pindi
wanapoichukua sera ya chama kama ile ya elimu bure kwa kuwa si jambo
baya kwa sababu wanatimiza yale tuliyokuwa tukitaka kuwafanyia
Watanzania,” alisema Lowassa.
MTANZANIA
Askari wa Jeshi la Polisi na raia
wengine watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya
Kinondoni, Dar es Salaam wakikabiliwa na tuhuma za unyang’anyi kwa
kutumia bastola.
Mbele ya Hakimu Amalia Mushi, Wakili wa Serikali Masini Musa,
aliwataja watuhumiwa hao ni askari E.7879 Koplo (CPL) Uswege (44) wa
Kituo cha Polisi Mbezi – Kimara, David Kabadi (23), Kasu Gulam (60) na
Hilal Ibrahim (70).
Wakili Musa alidai mahakamani hapo kuwa tukio hilo lilitokea Juni 10 mwaka jana maeneo ya Mbezi Afrikana.
Katika shtaka la kwanza, Musa alidai
kuwa watuhumiwa waliiba magari mawili aina ya Toyota Prado na Mitsubishi
Canter yote yana thamani ya Sh milioni 95 mali ya Abdul Said.
Musa aliongeza kuwa watuhumiwa kabla ya
kufanya tukio hilo walimtishia kwa bastola Shaban Kasim ambaye alikuwa
mlinzi katika karakana ya magari hayo.
Katika shtaka la pili, watuhumiwa hao
wanadaiwa kufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha ambapo katika maelezo
yaliyosomwa na wakili Musa waliiba gari aina ya BMW yenye thamani ya Sh
milioni 30 mali ya Jay Madeleka.
Baada ya kusomewa maelezo hayo watuhumiwa walikana mashtaka hayo na upelelezi bado unaendelea.
Mahakama ilisema kuwa shtaka hilo halina
dhamana kisheria hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 28 mwaka huu
ambapo itatajwa tena kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali na
watuhumiwa walirudishwa mahabusu.
MTANZANIA
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EALA), limeombwa kuiondoa nchi ya Burundi katika uanachama wa jumuiya
hiyo na ile ya Umoja wa Afrika (AU) hadi hapo mgogoro wa kisiasa na
kijamii utakapomalizika nchini humo.
Ombi hilo limewasilishwa mjini hapa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika, Donald Deya,
alipowasilisha maombi ya mashirika sita yasiyo ya kiserikali kutoka EAC
yaliyoomba kuzungumza na Bunge juu ya mgogoro wa Burundi.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Mambo ya Ndani ya Bunge na Usuluhishi wa migogoro ya EALA inayoongozwa na Mwenyekiti Abdullah Mwinyi, Deya alisema nchini Burundi bado kuna shida ya kisiasa na kuna Serikali iliyochaguliwa, lakini si halali kisheria.
Alisema pamoja na maombi ya kuondolewa
kwa nchi hiyo, bado itaendelea kushiriki kwa karibu katika meza ya
mazungumzo kwa ajili ya kutafuta mwafaka utakaowezesha kupatikana kwa
amani na kuondoa shida zinazowakabili kwa sasa.
“Kitu cha msingi ambacho
tunaliomba Bunge hili, litumie mbinu zote kuhakikisha Warundi wote
wamefika mezani kwenye mazungumzo ya kutoa mwafaka wa shida yao. Na
mbinu wanazoweza kutumia zipo nyingi,” alisema Deya na kuongeza:
“Sisi tunasema kwa sasa Serikali
ya Burundi iwekwe ‘suspended’ (pembeni) kabisa kwenye uanachama wa
Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ule wa Umoja wa Ulaya (AU),” alisema Deya.
Akiwasilisha maombi hayo ndani ya ukumbi
wa Bunge uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini hapa,
Deya alisema kumekuwapo na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na
kijamii huku baadhi wakiogopa na kuiona nchi hiyo inaweza kuteketea na
kuingia kwenye mauaji ya kimbari.
“Kwa maoni yetu ukilinganisha
mazungumzo ya utatuzi wa mgogoro wa Burundi na mazungumzo yaliyosaidia
kuiondoa Kenya kwenye machafuko mabaya ya kisiasa mwaka 2008, utaona
tofauti kubwa kabisa,” alisema Deya.
Akifafanua kuhusu mazungumzo
yaliyoinusuru Kenya kutumbikia kwenye wimbi la mauaji zaidi, alisema
aliyekuwa Mwenyekiti wa AU na Rais wa Ghana, John Kufor, aliiwezesha
nchi hiyo kurejea kwenye amani tofauti na ilivyo kwa Burundi leo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge EALA, Mwinyi alisema kwamba maombi yaliyowasilishwa na mashirika
hayo sita kupitia jopo la wanasheria wa Afrika yamesikilizwa na wajumbe
wa kamati hiyo.
“Kuna mambo mengi wamependekeza,
leo wajibu wetu Kamati ya Bunge ni kuyasikiliza na kutafuta ufafanuzi
wa kina, ushahidi na baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyajadili
na baadaye tutaandika ripoti na kuipeleka Bunge ili nalo lijadili na
kutoa maazimio ya mapandekezo,” alisema Mwinyi na kuongeza:
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ichunguze iwapo kuna wizi unaofanywa na kampuni za simu kwa wateja wake.
Ngonyani alitoa maagizo hayo jana katika
hafla ya uzinduzi wa duka la ‘Airtel EXPO’ linalotoa huduma mbalimbali
za simu na elimu ya matumizi ya vifaa vya mawasiliano akisema amepokea
malalamiko ya aina mbili kutoka kwa Watanzania wanaotumia huduma za
kampuni za simu nchini.
Ngonyani alisema kutokana na mazingira
hayo, imekuwa ikijengeka taswira kwamba, watumishi wa kampuni za simu
wanahusika katika wizi huo.
Aliiagiza TCRA kuchunguza tuhuma hizo
huku akiwataka wananchi kuwasilisha malalamiko yao katika mamlaka hayo
ili kutafuta ufumbuzi.
Kwa mujibu TCRA, Watanzania milioni 32
wanatumia huduma simu za mkononi, sawa na asilimia 67 huku takriban
wateja milioni nane wakitumia za intaneti.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisema malalamiko yote
ya wateja wao yamekuwa yakitafutiwa ufumbuzi kwa njia mbalimbali.
“Wateja wote tunawasaidia kupitia kituo cha huduma kwa mteja ambacho
kinafanya kazi wakati wote.
Kwa upande wetu, wateja wanasikilizwa,”
alisema. Msemaji wa TCRA, Innocent Mungy alisema wamepokea maagizo ya
naibu waziri na wataanza kuyatekeleza kwa mujibu wa Sheria ya TCRA ya
2003 na ile ya Mawasiliano na Posta ya 2010. “Lakini pia tuna kanuni
zinazotusaidia katika utekelezaji wa sheria hizo, kwa hiyo agizo hilo
litashughulikiwa, lakini siwezi kusema lini,” alisema.
Mungy alisema malalamiko ya wateja
kuhusu hisia za kuibiwa yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi kila siku na
kupokewa sehemu husika ili kutafutiwa ufumbuzi. “Kwanza malalamiko
yanayohusu kampuni fulani yanapokewa na kampuni husika ili kujibiwa,
kabla ya TCRA hatujahusika kumaliza malalamiko ya mteja huyo,” alisema.
Hata hivyo, alisema bado elimu
inahitajika zaidi katika matumizi ya ofa za vifurushi vya intaneti na
muda wa maongezi. “Kuna mambo mengine yanachangiwa na simu zetu za
kisasa, kwani unaweza kuliwa fedha zako kwa kosa la kujiunganisha au
kutokujua jinsi ya ulaji wa vifurushi kwenye simu,” alisema.
Desemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa
TCRA, Dk Ally Simba alitoa adhabu ya faini ya Sh125 milioni kwa kampuni
tano za simu za mkononi kwa kushindwa kuweka mazingira salama kwa
wateja.
Kampuni hizo ni Airtel, Tigo, Smart,
Halotel na Zantel ambazo zilitakiwa kulipa faini kwa sababu zilishindwa
kutii agizo la mamlaka hiyo ya kulinda wateja wake huku vitendo vya
utapeli wa kutuma ujumbe wa udanganyifu na ulaghai kwenye mitandao
vikiendelea.
MWANANCHI
Mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa
nne jijini hapa jana, imesababisha kifo cha mwanafunzi na uharibifu wa
mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Wananchi wamedai kuwa mvua hiyo,
iliyonyesha kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri, haijawahi
kushuhudiwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne iliyopita.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabatini, Ntobi
Ntobi pamoja na kaimu kamanda wa kikosi cha Zimamoto jijini Mwanza,
Hamidu Nguya walithibitisha kutokea kwa kifo cha mtoto huyo, Jenipher
Joseph (6), aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mabatini.
Kamanda Nguya alisema mtoto huyo
alisombwa na maji na baba yake, James Joseph walipoteleza na kuangukia
mtoni wakati wakivuka daraja la Mto Mirongo uliokuwa umefurika.
“Baada ya kuanguka mtoni, baba alijikuta
akimwachia mikono mtoto wake katika harakati za kujiokoa na aliposhtuka
tayari mtoto yule alikuwa amesombwa na maji na juhudi za kumwokoa
zilishindikana,” alisema Kamanda Nguya.
Miongoni mwa waliopoteza mali ni pamoja
na Juma Said, mmiliki wa duka la vifaa vya shule na ofisi zenye thamani
ya zaidi ya Sh7.5 milioni.
Licha ya ubovu wa miundombinu, eneo la
Mabatini hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na ujenzi holela
uliobana kingo za Mto Mirongo. Hadi saa 12:00 jioni jana, Kikosi cha
Zimamoto na Uokoaji kilikuwa kikiendelea na juhudi za uokoaji na
kutafuta miili ya watu wanaodhaniwa kuwa wamesombwa na mafuriko hayo.
MWANANCHI
Wakati Serikali ya Awamu ya Tano
ikisisitiza kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, mpango
huo umesababisha adha kwa baadhi ya shule ikiwamo kukosekana walimu wa
ziada, kuibwa vifaa vya kufundishia na ongezeko la wanafunzi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
katika shule za msingi na sekondari katika wilaya za Ilala, Kinondoni na
Temeke, umebaini kuwa mpango huo badala ya kuwa msaada kwa walimu
umekuwa mzigo unaowapasua kichwa.
Fedha za ruzuku zinazopelekwa katika
shule kwa mchanganuo maalumu kulingana na idadi ya wanafunzi, hazikidhi
matumizi ya shule hizo hata kwa wiki mbili.
Mchanganuo wa fedha za ruzuku Wilaya ya
Kinondoni, unaonyesha kuwa ni shule tano pekee ambazo zimepewa fedha ya
chakula ni Kawe A, Mbuyuni, Msasani A, Msewe na Sinza Maalumu, huku
nyingine zote zikiwa hazina fedha za kulipa walinzi, bili ya maji,
umeme, ukarabati wa madawati, madarasa na vyoo.
Katika Wilaya ya Temeke, shule kadhaa
zimevunjiwa madarasa, ofisi za walimu na kuibwa vifaa vya kufundishia,
meza, viti kutokana na kukosekana walinzi ambao walikuwa wakilipwa kwa
ushirikiano wa shule na wazazi.
Mlinzi mmoja hulipwa kati ya Sh150,000
hadi 200,000. Mpango huo umekuwa mwiba mchungu kwa walimu wa shule hasa
za sekondari ambao walitakiwa kuwa wabunifu kwa kutafuta jinsi ya
kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kushirikiana na wazazi kulipa walimu wa
ziada hasa wa masomo ya sayansi.
“Nimeajiri walimu sita wa masomo ya
sayansi kwa kushirikiana na wazazi, ambao hapa kwangu nina mahitaji
makubwa huku akiwapo mmoja aliyeajiriwa na Serikali.
Kwa mwezi nawalipa Sh300,000 hadi
350,000, najiuliza nitawalipa nini na fedha ya ruzuku haina fungu hilo?
Bado mlinzi, bado maji, bado umeme, nimechanganyikiwa natamani kurudi
kijijini nikalime kuliko fedheha hii, ”alisema mmoja wakuu wa shule ya
sekondari wilayani Temeke ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe
gazetini.
Alisema mwaka huwa ana mitihani minne wa
Machi, Juni, Septemba na Desemba, ambayo kila mmoja hadi unamalizika
humgharimu Sh1.5 milioni, kwa bahati mbaya fedha ya ruzuku aliyopata kwa
mchanganuo wote ni Sh4.8 milioni hivyo kwa mitihani pekee anatumia Sh6
milioni ambazo hafahamu atazitoa wapi huku fedha za ruzuku zikiacha hayo
yote bila majibu wala ufafanuzi. “…Wazazi wametangaziwa elimu bure kwa
kishindo, sielewi itakuwaje na waliendelea kufundisha mwezi uliopita
wananidai na sifahamu mwezi huu nitawapa nini,” alisema mwalimu
mwingine.
Katika shule za msingi, tatizo kuu
lililojitokeza ni wanafunzi kuwa wengi kuliko uwezo wa shule. “Mwaka
jana na mwaka juzi, wiki ya kwanza shuleni nilikuwa nimekadiria
kuandikisha wanafunzi 250, wakaongezeka hadi 300, lakini hadi asubuhi ya
leo (jana) nimeandikisha wanafunzi 600, ” alisema mwalimu mkuu wa shule
moja wilayani Temeke ambaye pia aliomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Alisema kwa ongezeko hilo kila darasa
watakaa wanafunzi 150 badala ya 50 waliokuwa wanakaa awali. “Hatuwezi
kuwakataa tutaambiwa tunakataa wanafunzi, bado wanakuja hadi Machi,
sijui itakuwaje,” alisema mwalimu mwingine wa shule ya msingi wilayani
humo.
Alisema mbali ya hilo wamelazimika kutoa
elimu ya ziada kwa wazazi, kutokana na wengi wao kuwaleta wanafunzi
wakiwa hawana kitu chochote hadi begi la kubebea madaftari.
“Ukiwauliza wazazi mbona mtoto hana kitu
zaidi ya sare alizovaa anakuambia wametangaziwa elimu bure, kibaya
zaidi hata nembo hawana, tunashindwa kuwaambia walipe Sh500 au 1,000 ya
nembo watasema tunawalipisha,” alisema. Alifafanua ikitokea wanafunzi
wamepata matatizo itakuwa ngumu kuwatambua, kutokana na kutokuwa na
nembo,” alisema.
Akizungumzia changamoto ya ruzuku, Ofisa
Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda alisema shule zinazopata
tabu ya ruzuku ni zenye wanafunzi wachache kwani zilizo na wengi
hazipati adha hiyo kwa kuwa zinapata fedha nyingi.
Alisema Serikali imepanga kila
mwanafunzi kwa mwaka atumie Sh10,000 hivyo zitatolewa kidogokidogo hadi
zitimie: “Hizo changamoto zilizopo zitafanyiwa.
NIPASHE
Mwalimu wa Shule ya Msingi Peramiho,
Songea mkoani Ruvuma, Baraka Mwakajila (29), amekutwa amefariki dunia
baada ya kujinyonga kwa kutumia shati ndani ya nyumba alimokuwa akiishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma,
Revocatus Malimi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea juzi saa sita
mchana katika mji mdogo wa Peramiho, nje kidogo ya Manispaa ya Songea.
Malimi alisema inadaiwa kuwa siku hiyo
ya tukio, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Rashid Pilly, aligundua kujinyonga kwa
mwalimu huyo, baada ya kupita eneo la nyumba aliyokuwa anaishi na kuona
nzi wengi wametapakaa kwenye eneo la dirisha la chumba alichokuwa
analala.
Alifafanua zaidi kuwa Mwalimu Pilly
baada ya kuona hali hiyo, alisogea hadi mlangoni na kukutwa mlango ukiwa
umefungwa huku eneo hilo likiwa na harufu kali iliyoashiria kuna kitu
ambacho kimeoza.
Alisema baadaye Mwalimu Pilly
alilazimika kwenda kutoa taarifa kwenye kituo kidogo cha Polisi cha
Peramiho na baadaye askari polisi wakiwa wameongozana na mganga,
walifika eneo la tukio.
Baada ya kufika, alisema walivunja
mlango na kuingia ndani ya nyumba hiyo ambako walimkuta Mwalimu
Mwakajila akiwa tayari ameshakufa muda mrefu baada ya kujinyonga.
Alisema Mwakajila alijinyonga ndani ya
nyumba ambayo ni mali ya shule na askari walikuta barua chini ya sehemu
aliyojinyongea iliyokuwa imeandikwa Januari 4 mwaka huu na mwanamke
(jina linahifadhiwa), anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake, ambaye alimtaka
aachane naye na aendelee na maisha yake.
Malimi alisema polisi baada ya kuiona na
kuisoma, waliendelea kuufanyia upekuzi mwili wa marehemu na kukuta pia
karatasi kwenye mfuko wa suruali yake, ambayo Mwakajila aliandika
Januari 2, mwaka huu, akimtuhumu mpenzi wake huyo kuwa amekuwa malaya na
mlevi
Kamanda Malimi alisema polisi
wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo na mwili wa
marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajiki ya taratibu za mazishi.
NIPASHE
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, amesema ni umuhimu taasisi zote za
serikali kuwa na mfumo wa kielekroniki (EAR) wa mahudhurio kazini ya
watumishi wake.
Akizungumza mara baada ya kujisajili
katika nfumo huo katika wizara yake jijini Dar es Salaam jana, Prof.
Mbarawa alisema kwa kuanzia utaratibu huo utatumika katika sekta
uchukuzi na ujenzi na kisha utafungwa katika taasisi zote za serikali
ili kuhakikisha watumishi wa umma wanafika ofisini kwa wakati na
kupunguza utoro.
“Hakikisheni watumishi wote wanatumia
mfumo huu wa kielektroniki ili kudhibiti utoro na watu kufanyakazi kwa
muda unaokubalika kiserikali”, amesema.
Aidha, waziri huyo aliwataka wafanyakazi
wa mapokezi wa wizara hiyo kuacha kuwafungulia wafanyakazi watoro na
wanaochelewa kuingia ofisini bila ya kupitia mfumo huo ili kuwatambua
watumishi watoro waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Amesisitiza mfumo huo utakapofungwa
katika taasisi zote za umma utadhibiti watoro kwa kuwa unaweka
kumbukumbu ya muda mtu anaokuwa kazini na hivyo kuwawezesha viongozi
kupata taarifa sahihi za mahudhurio.
NIPASHE
Jeshi la Polisi Mkoani Katavi
linamshikilia mkazi wa mji wa Mpanda, kwa tuhuma za kumnyanyasa kwa
kumnyima mahitaji muhimu mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha
pili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini
hapa juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari,
alisema polisi walipata taarifa hiyo kupitia kituo kimoja cha radio
kilichopo mkoani humo wakati mtoto huyo akihojiwa.
Alisema baada ya polisi kusikia kipindi
hicho, walifuatilia na kumpata mtoto huyo na kumhoji na kubaini kuwa
mzazi wake amekuwa akimnyima mahitaji muhimu ya kimaisha kama mavazi,
chakula, matibabu na mahitaji ya shule.
Kamanda Kadavashari alisema mtoto huyo
tangu mama yake mzazi afariki dunia mwaka jana na baba yake kuoa mke
mwingine, maisha yake yalibadilika na kuanza kuishi maisha ya
manyanyaso na mateso, hali iliyomsababisha hata kushindwa kuendelea
vizuri na masomo.
Alisema katika kanisa ambalo mzazi huyo
anasali pamoja na mtoto huyo, imekuwa ikitolewa michango kwa lengo la
kumsaidia lakini mtoto huyo hamfikii na kwamba hivi karibuni baba yake
alimfukuza nyumbani na kuanza kuishi kwa kutangatanga mitaani.
Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Katavi,
alisema baada ya baba wa mtoto huyo kusikia kipindi hicho cha radio,
alikwenda polisi kutoa taarifa za kupotelewa na mtoto wake huyo na
polisi kumshikilia na walipomuhoji walibaini amekuwa akimnyanyasa mtoto
wake na tayari amefunguliwa mashtaka na atafikishwa mahakamani kujibu
tuhuma zinazomkabili.
NIPASHE
Zikiwa zimepita siku tano tangu Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, aagize mabasi ya mwedo kasi yaanze kutoa huduma
jijini Dar es Salaam, Nipashe limebaini kwamba mbali ya kasoro lukuki
zinazotajwa, mabasi yaliyoingizwa nchini kwa kazi huduma hiyo,
hayajalipiwa kodi.
Itakumbukwa kwamba mradi huo ulitarajiwa kuanza kutoa huduma jijini Dar es Salaam Oktoba, mwaka jana, lakini haikuwa hivyo.
Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea mradi
huo Desemba, mwaka jana na kuagiza kuwa mabasi hayo ya mwendo kasi
yaanze kutoa huduma jijini Dar es Salaam Januri 10, mwaka huu, agizo
ambalo halijatekelezwa.
Agosti 16, mwaka jana, serikali ilizindua mafunzo kwa madereva 330 wa kuendesha mabasi hayo.
Aidha, Septemba 20, mwaka jana, mabasi
138 yaliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam na kuelezwa kwamba
yataanza kutoa huduma Oktoba, mwaka jana.
Akiwa bandarini hapo kushuhudia mabasi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alisema:
“Tumefikia hatua nzuri na naipongeza
Kampuni ya Uda Rapid Transit (Uda-RT) kwa kuleta mabasi haya kwa ajili
ya kuanza kutoa huduma ya usafiri katika kipindi cha mpito. Hii
itasaidia kuondoa adha ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.”
Alisema kampuni hiyo imepewa jukumu la
kuendesha kipindi cha mpito ili wapate uzoefu na zabuni ya mwendesha
mradi kipindi cha kudumu itakapotangazwa itasaidia wao kushindana.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili
umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya mabasi hayo bado yapo chini ya
Kamishna wa Forodha kutokana na kutolipiwa kodi.
Jana, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na
Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alithibitisha kuwa
magari hayo yapo chini ya Kamishna wa Foforodha ikiwa ni taratibu za
kawaida kwa magari ama vitu vingine ambavyo havijalipiwa kodi.
“Sisi kwa kawaida mzigo mpaka ulipiwe
kodi ndipo unapotolewa. Kama haujalipiwa kodi unakuwa chini ya Msimamizi
wa Forodha. Huu ni utaratibu wa kawaida sana.
Kwa hiyo haya mabasi yapo chini ya
Msimamizi wa Forodha, ni kama magari mengine yaliyo huko `show room’
(maeneo ya kuuza magari), hayajalipiwa kodi, lakini yakiuzwa, wahusika
huja kulipia kodi na hivyo kuanza kufanya kazi,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, Kayombo hakuwa tayari kusema
ni kiasi gani kinachodaiwa kwa magari hayo kwa maelezo kwamba hilo ni
suala la kujadili na mlipa kodi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Uda, Simon
Kisehna, alisema tayari ofisi yake iko katika mchakato wa kukamilisha
masuala ya kodi TRA na kwamba mradi utaanza kama ilivyoagizwa na Waziri
Mkuu ili kutoa huduma kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Kisehna alisema miundombinu ya mradi huo kwa sehemu kubwa iko sawa na huduma zitaanza kutolewa hivi karibuni.
NIPASHE
Wakati utekelezaji wa kuanza darasa la
kwanza mpaka kidato cha nne ukiendelea kuleta mkanganyiko kwa wazazi
kutojua wanachopaswa kuchangia ama kutochangia, imebainika kwamba
mwongozo uliotolewa na serikali unaelekeza wazazi kuendelea kujitolea
nguvu na mali kwa shule zilizo maeneo hayo.
Katika mwongozo huo, eneo linalozungumzia majukumu ya wazazi na walezi, linasema: “Wazazi
na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na
mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.”
Kutokana na kipengele hicho, ni wazi
kwamba baadhi ya shule bado zitaendelea kuwatoza wazai michango ama
kuchangia vitu vingine tofauti na ambavyo wazazi wengi waliamini kwamba
kwa sasa hawatachangia chochote kwa elimu ya watoto wao.
Tayari kumekuwa na malalamiko kutoka kwa
baadhi ya wazazi wakisema watoto wao wamerudishwa nyumbani wakitakiwa
kuchangia vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula na fedha tasilim.
Kwa mujibu wa mwongozo huo wa Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, wazazi wanatakiwa pia kununua sare
za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia yakiwamo madaftari na kalamu
na chakula kwa wanafunzi wa kutwa pamoja na matibabu kwa watoto wao.
“Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda
shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa
likizo, kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi
wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli,” unasema mwongozo
huo.
Alipopigiwa simu kutoa ufafanuzi,
Kamishna wa Elimu, Prof. Eustella Bhalalusesa, baada ya kuulizwa swali
na mwandishi alikata simu na kusema yupo kwenye kikao.
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha
Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema mishahara midogo kwa
walimu, mazingira mabovu ya kazi na ongezeko la wanafunzi lisiloendana
na miundombinu, ni changamoto nyingine kwenye kutimiza lengo hilo la
elimu bure.
“Serikali haijaangalia matatizo ya
walimu kama mishahara midogo. Siku zote walimu wamekuwa wakilipwa
mishahara midogo na ujue hata watoto ambao hawakutaka kuja shule
watakuja,” alisema.
Alisema mishahara midogo ni kikwazo kwa kuwa walimu wanakata tamaa.
Taarifa zinaonyesha kuwa mwalimu mpya wa
Daraja 3A wa shule ya msingi aliyeajiriwa Julai, mwaka jana, anaanza na
mshahara wa Sh. 477,000 kwa mwezi ambao baada ya makato hupokea Sh.
360,000.
HABARILEO
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza kukamatwa kwa watu waliohusika
kuwaozesha watoto wao wa umri wa miaka 13 na kuwakatisha masomo katika
mkoa wa Shinyanga na Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa
Wizara hiyo, Erasto Ching’oro alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa
kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Ching’oro alisema wakati mtoto ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa
Shinyanga ameozeshwa kwa nguvu kwa mahari ya ng’ombe 13 na kukatishwa
masomo akiwa darasa la sita, mtoto mwingine wa mtaa wa Chikole kata ya
Msalato, Dodoma inasemekana ameozeshwa kwa mahari ya Sh 600,000.
Alisema kutokana na kuwepo kwa matukio
hayo, Wizara ilivitaka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Kamati za
Ulinzi wa Mtoto katika mikoa yote, kuhakikisha kuwa watuhumiwa
wanachukuliwa hatua kali.
“Tukio
la kuwaoza watoto wadogo katika umri mdogo siyo tu linakinzana na haki
za msingi za mtoto bali pia linamkosesha mtoto haki ya kuendelezwa akiwa
ni pamoja na kuhatarisha uhai wake kwa kupatiwa majukumu ya mtu mzima
katika umri mdogo,” alisema Ching’oro.
Alisema wizara inawataka wazazi na
walezi kubadilika na kuachana na tabia ya kuwaoza watoto wao katika umri
mdogo, maana vitendo hivyo ni vya kikatili.
Aliongeza kuwa jamii inatakiwa kutambua
kuwa vitendo vya kikatili kama hivyo, vinapofanywa katika familia
vinarudisha nyuma juhudi za serikali za kupambana na ukatili, maana kwa
kiasi kikubwa familia inatakiwa kuwa mahala salama panapofaa watoto
kuishi na kulindwa.
Pia alisema wizara inakumbusha wazazi,
walezi na wadau wengine kuwa ndoa za utotoni ni kinyume cha Sheria ya
Mtoto ya Mwaka 2009 na mikataba ya kimataifa kuhusu haki na ustawi wa
mtoto.
Alisema ni wajibu wa kila mtu,
kuhakikisha kuwa watoto wanaishi katika usalama na kuhakikishiwa haki
zao zote za msingi, ikiwemo kulindwa, kuendelezwa, kuishi na
kushirikishwa katika maisha ya kila siku ili kujenga taifa linaloheshimu
maslahi ya watoto.
Juzi gazeti hili liliripoti kuwa mtoto
mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la sita katika shule ya msingi
Wishiteleja wilayani Kishapu, ameozeshwa kwa nguvu na wazazi wake baada
ya kupokea mahari ya ng’ombe 13.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la
AGAPE, John Myola, mwanafunzi huyo alifungishwa ndoa ya kimila Septemba
25, mwaka jana katika kitongoji cha Nyamikoma kijiji cha Buchambi
wilayani Kishapu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ngh’umbi
aliyekiri kupokea nakala ya barua kutoka Agape iliyozungumzia juu ya
kufungishwa ndoa kwa mtoto huyo, alikemea kitendo hicho na kuahidi
kumsaka mtuhumiwa akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Mkoani Dodoma, mama mmoja anatuhumiwa
kutaka kumuozesha mtoto wake mwenye miaka 13 (jina linahifadhiwa) baada
ya kupokea mahari ya Sh 600,000 na ng’ombe wanne.
HABARILEO
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro
imewatia mbaroni wahamiaji haramu 48 na kuwafukuza nchini na baadhi yao
kufikishwa mahakamani kwa kuingia nchini na kufanya kazi kinyume cha
sheria.
Wahamiaji haramu hao walikamatwa kwa
nyakati tofauti kuanzia Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu
kutokana na msako mkali uliofanywa na maofisa wa idara hiyo katika
maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji wa Mkoa wa Morogoro, Agustino Haule,
alisema hayo jana ofisini kwake mjini hapa alipokuwa akielezea hatua
mbalimbali zinazochukuliwa na idara hiyo katika hatua ya kukabiliana na
wimbi la wahamiaji haramu na walioingia nchini na kufanya kazi kinyume
cha sheria.
Alisema wahamiaji haramu kutoka mataifa
mbalimbali walipatikana katika msako uliofanyika maeneo mbalimbali
ikiwemo viwandani, shuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali
zilizopo mkoani Morogoro. Hivyo aliwataja wahamiaji haramu hao ni kutoka
katika nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC).
“Msako huu wa kuwakamata
wahamiaji haramu unaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali mkoani
Morogoro na hadi sasa wahamiaji haramu 48 wamekamatwa katika maeneo
mbalimbali kwa kipindi cha Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu,” alisema Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Morogoro.
Hivyo alisema baadhi ya wahamiaji hao
tayari wameshafikishwa mahakamani na kutozwa adhabu na pia kurejeshwa
nchini kwao na wengine kesi zao zikiendelea kusikilizwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mkoa.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment