SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 51
ILIPOISHIA
Tukatoka tena. Tulijipakia
kwenye gari tukaondoka.
Breki ya kwanza ilikuwa mbele
ya hoteli moja iliyokuwa katika mtaa mwingine. Ilikuwa hoteli ndogo ya ghorofa
moja, Ilikuwa imeandikwa kwa herufi kubwa. AL ASAD.
“Hii ndio hoteli ambayo
nitakuachia wewe, itakuwa kama mali
yako kwani tutakuwa tunagawana faida kila mwezi na kila mwaka kama utapenda
kuendelea kubaki Somalia”
Abdi aliniambia tukiwa bado tupo kwenye gari.
Alipoona nilikuwa
nikiiangalia angalia ile hoteli, aliniambia.
“Tushuke uione vizuri”
Tukashuka.
Tuliingia ndani ya ile
hoteli. Kwa kweli ilikuwa imechangamka.
“Sasa nani anaiendesha kwa
hivi sasa?” nikamuuliza.
“Yuko mtu lakini nitamuondoa”
“Sasa ni kwanini umuondoe?”
“Lengo langu ni kukunufaisha
wewe rafiki yangu au nimefanya kosa?’
“Hapana. Ni vizuri”
Abdi alinitembeza hoteli
nzima kisha tukaingia katika ofisi ya meneja.
Meneja mwenyewe alikuwa mtu
mzima. Kichwa chake kilishaanza kutoka mvi.
SASA ENDELEA
Walizungumza kwa kisomali
huku meneja huyo akinikodolea macho.
Walizungumza kwa karibu robo
saa kisha tukatoka.
“Yule ndiye meneja aliyeko
sasa” Abdi aliniambia wakati tunatoka nje ya hoteli hiyo.
“Utamuhamishia mahali pengine
au unammuondoa kabisa?’ nikamuuliza.
“Nitamfikiria”
“Umeshamwambia?”
“Nilitaka kwanza nikubaliane
na wewe”
“Mimi nimeshakubali”
“Una uzoevu wa kuendesha
hoteli?”
“Kwa kweli sina uzoefu huo”
“Utajifundisha hapa hapa. Ninaamini
hutaweza kushindwa”
“Nitajaribu”
“Kazi yako itakuwa kuongoza
na kukagua. Kuna kijana ambaye amesomea uendeshaji wa hoteli yuko pale
atakusaidia”
“Nafikiri nitaweza. Usiwe na
wasiwasi”
Baada ya hapo hatukuzungumza
tena. Mwenzngu alikuwa amenyamaza, sikujua alikuwa akiwaza nini. Mimi nilikuwa
na mawazo ya kubaki Somalia
kuendesha shughuli ya hoteli.
Kikubwa kilichonipa tamaa ni
kuwa kazi ya umeneja wa hoteli ni ya heshima na aliniambia kuwa angenipa ile
nyumba pamoja na gari. Isitoshe tungegawana mapato ya hoteli..
Nilijiambia kama ningeweza
kuchuma pesa pale Somalia na
kurudi kwetu nikiwa na utajiri kama alivyoniahidi Abdi, sikuona haja ya
kung’ang’ania kurudi Tanga ambako sikuwa na hakika kama
nisingefukuzwa kazi kutokana na kutoonekana kazini kwa kipindi kirefu bila
taarifa yoyote.
Abdi akanipeleka nyumbani
kwake. Ilikuwa nyumba nzuri ya ghorofa moja iliyokuwa ndani ya geti. Mlinzi
wake alitufungulia geti. Gari la abdi likaingia.
Kulikuwa na banda la magari
lakini Abdi alilisimamisha gari hilo
mbele ya mlango wa nyumba yake ya kifahari.
Tukashuka. Abdi alikwenda
kufungua mlango akaniambia.
“Karibu kaka”
Tukaingia ndani. Alikuwa na
sebule ya kupendeza iliyokuwa imepambwa vizuri kwa fanicha za thamani. Wakati
tunaingia kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa akifanya usafi kwa kutumia kufaa
maalum cha kuondoa vumbi.
“Karibu ukae” Abdi aliniambia
huku naye akikaa. Akaongeza.
“Jisikie uko nyumbani. Hapa
ndio kwetu bwana”
Nikawa natupa macho huku na
huko kuiangalia sebule.
“Asante. Nimefurahi kupafahamu
nyumbani kwako”
“Utakunywa kahawa?” Abdi
akaniuliza.
“Hapana”
“Tangu uje Somalia
sijakuonesha nyumbani kwangu. Hii nyumba ni yangu na mimi ninaishi hapa” Abdi
aliendelea kuniambia kisha akaongeza.
“Unaweza kuona nyumba iko
kimya kwa sababu watoto hawapo”
“Wako wapi?”
“Shemmeji yako amekwenda kwao
Kismayuu. Mama yake ni mgonjwa. Atarudi pindi mama yake akipata nafuu”
Yule msichana aliyekuwa
akifanya usafi alikuwa ameshaondoka.
“Nilipomuona huyu msichana
nilidhani ndiye shemeji?”
“Hapana. Yule ni mfanyakazi
wangu. Kwa sasa ninaishi na wafanyakazi wangu tu”
Hatukukaa sana hapo. Abdi akainuka na kuniambia.
“Sasa acha nikurudishe kule
hoteli. Nataka niende shambani kwangu. Niliambiwa baadhi ya ng’ombe wangu ni
wagonjwa”
Tukatoka na kujipakia tena
kwenye gari, tukaondoka.
Abdi alinirudisha hotelini
akaniacha na kuondoka. Niliingia chumbani nikaketi. Mawazo ya Zena yakaanza
kunijia. Sikutaka kuendelea kumuwaza mwanamke huyo wa kijini lakini mawazo yake
yalinijia kwa nguvu na sikuweza kuyazuia.
Kikubwa kilichosababisha
nimuwaze ni kule kujitokeza nyumbani kwa yule mzee wa kisomali na kumpiga kibao
yule mzee. Mpaka muda ule tukio lile lilikuwa kama
kitendawili nilichoshindwa kukitegua.
Lakini jambo moja ambalo
halikuwa na shaka akilini mwangu ni kwamba Abdi na yule mzee wa kisomali
walikuwa wanajua ni kwanini Zena alitokea pale.
Kama walikuwa hawajui ni lazima Abdi angeonesha mshangao
wake na angenieleza kitu. Lakini hakutaka kunieleza chochote kama
vile ilikuwa ni siri.
Kadhalika sikuweza kujua yule
mzee alikuwa ni nani, ana uhusiano gani na Abdi na kwanini nilimuota usiku
akiniingiza ndani ya kaburi?
Pia nilijiuliza kile
walichokuwa wanasoma pale ni kitu gani na kwanini kuliwekwa vitu
mbalimbali kama vya uganga? Kwa kweli licha ya kujiuliza mara kadhaa
sikupata jibu la kuridhisha.
Kwa vile sikuweza kuelewa
kitu niliona nisiumize kichwa kwa kujiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu.
Nikayaacha mawazo yale.
Siku ile sikumuona tena Abdi
hadi siku ya pili yake ambapo alikuja hoteli asubuhi kunijulia hali.
“Nyumba yako itawekewa
fanicha mpya leo. Kesho utaanza kuishi kule na kesho kutwa utakwenda kuanza
kazi kule hotelini. Yule meneja ataondoka leo” Abdi akaniambia.
“Sawa”
“Amour unajua kuendesha?”
“Kuendesha nini?”
“Nina maana kuendesha gari”
“Ninajua lakini sikuja na
leseni yangu”
“Si tatizo. Tutakwenda studio
utapiga picha kadhaa za paspoti, baadhi
yake tutazitumia kukutengezea leseni ya hapa Somalia”
“Nitaipata lini hiyo leseni?’
“Kesho tu utaweza kuipata”
“Bila mimi mwenyewe kwenda
kujaribiwa?”
“Hiyo kazi niachie mimi. Hata
paspoti utapata bila kwenda wewe mwenyewe”
“Lakini hiyo paspoti itakuwa
ya nchi gani?”
“Wewe ulitaka ya nchi gani?”
“Ya Tanzania”
“Utaipata bila shaka yoyote.
Hapa kuna mabingwa wa kugushi. Nipe wiki moja tu. Utawekewa na mihuri ya tarehe
uliyoingilia hapa Somalia”
Aliponiambia hivyo
nilitabasamu.
“Inaonekana wewe hushindwi na
kitu hapa Somalia”
nikamwambia.
“Serikali yenyewe nimeiweka
mikononi mwangu. Kuna maafisa wa polisi ambao wanakuja kuchukua mishahara
kwangu kila mwezi kwa ajili ya kulinda miradi yangu. Wewe umeona mwenyewe juzi
meno ya tembo tulivyoyaingiza na kuyapakia kwenye meli. Usifikiri kuwa polisi
hawajui, wanajua. Baadhi ya mawaziri pia ni marafiki zangu. Likitokea tatizo
niwapigia simu”
“Ninakuamini. Mambo yako ni
makubwa!”
Nilipomsifu Abdi alicheka
akanipa mkono. Alionekana kuwa ni mpenda sifa.
Tuliondoka hapo Hoteli
tukaenda studio kupiga picha za papo kwa papo. Alichukua picha zangu kadhaa za
usawa wa paspoti.
Wakati ananirudisha hotelini,
nilimwambia kuwa nilikuwa ninahitaji saa.
“Saa tu, twende dukani
tukanunue” akaniambia.
NAAM. MAMBO YANAZIDI
KUPAMBA MOTO!
TUKUTANE TENA KESHO
No comments:
Post a Comment