SIMULIZI ZA FAKI A FAKI0713 340572
MWANAMKE 56
ILIPOISHIA
Vile tulivyokuwa
tumekaa
pamoja ndani ya gari niliyakumbuka maneno ya Shamsa kuhusiana na Abdi,
nikaona kama niliyekuwa nimekaa na nyoka mwenye sumu kali.
Tukaendelea na safari.
Nilikuwa nikimfahamu vizuri
Yusufu mdogo wake Abdi ingawa hakuwa karibu sana na mimi. Muda mwingi alikuwa
akishughulika na mambo yake mwenyewe.
Niligundua pia kuwa Abdi
hakuwa akisikizana sana
na mdogo wake jambo ambalo lilifanya mara kwa mara wakwaruzane.
Lakini ndugu ni ndugu. Licha
ya kuwepo kwa hali hiyo, Abdi alipopata habari kuwa mdogo wake alikuwa
hafahamiki alipo ameanza kupata wasiwasi na kumuhangaikia.
Tulifika kituo cha polisi
ambapo Abdi alikuwa akifahamika vizuri. Aliwaeleza polisi tatizo lake.
Polisi hao wakamfahamisha
kuwa hawakuwa na taarifa yoyote ya mdogo wake.
“Amepotea tangu lini?” Polisi
mmoja akamuuliza.
“Si kwamba amepotea bali
hajulikani yuko wapi”
“Tangu lini?”
“Tangu jana alipoondoka
nyumbani kwake hajarudi hadi sasa na hajulikani yuko wapi”
“Ana mke na watoto”
“Ndio ana mke na watoto”
“Hakuwahi kumwambia mke wake
anakwenda wapi?”
“Huyo mke wake ndiye
aliyenifahamisha mimi kuwa Yufusu hajarudi nyumbani tangu jana”
SASA ENDELEA
“Mmemtafuta kwa ndugu na
jamaa?”
“Yusufu si mwendawazimu.
Hawezi kwenda kwa ndugu na jamaa na kubaki huko huko bila mke wake kuwa na
habari”
“Sasa nakushauri uende ukamtazame
mahospitalini huenda amepata ajali bila ya nyinyi kujua”
“Basi ngoja twende
tukamtazame huko” Abdi akawambia polisi.
Tukatoka tena na kujipakia
kwenye gari.
Tulizunguka katika
mahospitali mbalimbali kuanzia yale ya serikali na ya binafsi lakini Yusufu
hatukumkuta.
Wakati tunarudi, Abdi akiwa
amekasirika aliniambia.
“Huyu ni mtu mzima si mtoto.
Asisumbue akili zetu. Ngoja nikurudishe hotelini kwako na mimi niende zangu,
atajua mwenyewe na mke wake”
Abdi akanirudisha hotelini na
kuniacha, akaenda zake.
Ilipofika saa tisa mchana
Abdi akanipigia simu.
“Nisubiri ninakuja twende
polisi”
“Kuna nini tena?”
nikamuuliza.
“Polisi wameniita.
Wameniambia kuna mtu wanataka nikamtambue kama
ndiye huyo mdogo wangu ninayemtafuta”
“Yuko wapi?”
“Hawakuniambia. Wameniambia
niende nitajua huko huko”
“Sawa. Nakusubiri”
Baada ya muda mfupi Abdi
akafika, tukaondoka na gari.
Tulipofika kituo cha polisi
tukaambiwa kuwa kuna mtu ameonekana karibu na sehemu inayotupwa taka taka za
jiji.
Polisi hao hawakutufafanulia
vizuri isipokuwa walituambi tufuatane nao kuelekea sehemu hiyo ili tukamuone
huyo mtu.
Polisi waliondoka na gari lao
na sisi tukaondoka na gari letu na kuwafuata.
Tulipofika katika hilo eneo tuliloambiwa
tulikuta polisi wengine pamoja na watu kadhaa wamezunguka mahali palipokuwa na
shimo.
Na sisi tukaenda mahali hapo.
Tulijipenyeza katika kundi la watu tukasogea katika kingo za shimo hilo na kutazama ndani.
Kusema kweli mimi na Abdi
tulishituka tulipoona mtu tuliyeambiwa tukamtambue ni maiti ya Yusufu iliyokuwa
imelazwa ndani ya shimo hilo.
Abdi akanitazama kwa macho
yaliyokuwa yametaharuki.
“Yusufu ameuawa!” akaniambia.
“Sasa ameuawa na nani?”
nikamuuliza.
“Sisi sote ndio tumefika hapa
na kuikuta hii maiti. Polisi ndio watatueleza.
“Ndiye yeye mliyekuwa
mnamtafuta?” Polisi mmoja akatuuliza.
“Ndiye yeye. Ni kitu gani
kimemtokea?” Abdi akauliza.
Abdi akaelezwa kwamba polisi
waliarifiwa kwamba kulionekana mwili wa mtu aliyeuawa katika eneo hilo akiwa ndani ya shimo, ndipo polisi walipofika na kuukuta
mwili huo ambao ulionekana ulikuwa umelala ndani ya shimo hilo kutoka jana yake.
“Itakuwa ndugu yangu
ameuawa?” Abdi akawauliza polisi.
“Hatujafahamu lakini marehemu
amekutwa na alama ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani mwake”
“Hicho kitu alichopigwa nacho
ndicho kilichomuua”
“Tunafikiri ndio hivyo lakini
polisi tutakuwa na uchunguzi wetu”
“Uchunguzi huo ni lazima
ubainishe nani amemuua mdogo wangu na kwa sababu gani?”
“Hiyo ndiyo kazi yetu, tunao
wataalamu wetu wa uchunguzi”
Abdi akaitazama tena maiti ya
mdogo wake kisha akatikisa kichwa kusikitika.
“Sijui amewakosea nini hao
watu”
Sikumjibu kitu kwa vile na
mimi nilikuwa nimefadhaika. Yule mtu jana yake tu nilimuona akiwa mzima na
mwenye afya njema.
Mwili wa Yusufu ulitolewa
kwenye lile shimo baada ya polisi kumaliza kuupiga picha na kuchukua vipimo
vyao.
Mwili huo ulipakiwa katika
gari la polisi na kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
Mimi na Abdi tulitakiwa
kurudi tena kituo cha polisi ambapo Abdi alitakiwa kuandikisha maelezo yake.
Baada ya kuandikisha maelezo yake tulifuatana na polisi hadi nyumbani kwa
Yusufu.
Mke wa Yusufu alipoona polisi
alishituka na kuuliza.
“Kuna nini?”
Abdi akamueleza kwa utulivu
kilichokuwa kimetokea.
Mwanamke huyo hakuamini
alichoelezwa akataka kwenda kuiona maiti ya mume wake.
ITAENDELEA KESHO
No comments:
Post a Comment