ZIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 57
ILIPOISHIA
Abdi akaelezwa kwamba polisi
waliarifiwa kwamba kulionekana mwili wa mtu aliyeuawa katika eneo hilo akiwa ndani ya shimo, ndipo polisi walipofika na
kuukuta mwili huo ambao ulionekana ulikuwa umelala ndani ya shimo hilo kutoka jana yake.
“Itakuwa ndugu yangu
ameuawa?” Abdi akawauliza polisi.
“Hatujafahamu lakini marehemu
amekutwa na alama ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani mwake”
“Hicho kitu alichopigwa nacho
ndicho kilichomuua”
“Tunafikiri ndio hivyo lakini
polisi tutakuwa na uchunguzi wetu”
“Uchunguzi huo ni lazima
ubainishe nani amemuua mdogo wangu na kwa sababu gani?”
“Hiyo ndiyo kazi yetu, tunao
wataalamu wetu wa uchunguzi”
Abdi akaitazama tena maiti ya
mdogo wake kisha akatikisa kichwa kusikitika.
“Sijui amewakosea nini hao
watu”
Sikumjibu kitu kwa vile na
mimi nilikuwa nimefadhaika. Yule mtu jana yake tu nilimuona akiwa mzima na
mwenye afya njema.
Mwili wa Yusufu ulitolewa
kwenye lile shimo baada ya polisi kumaliza kuupiga picha na kuchukua vipimo
vyao.
Mwili huo ulipakiwa katika
gari la polisi na kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
Mimi na Abdi tulitakiwa
kurudi tena kituo cha polisi ambapo Abdi alitakiwa kuandikisha maelezo yake.
Baada ya kuandikisha maelezo yake tulifuatana na polisi hadi nyumbani kwa
Yusufu.
Mke wa Yusufu alipoona polisi
alishituka na kuuliza.
“Kuna nini?”
Abdi akamueleza kwa utulivu
kilichokuwa kimetokea.
Mwanamke huyo hakuamini
alichoelezwa akataka kwenda kuiona maiti ya mume wake.
SASA ENDELEA
“Utapelekwa ukaione maiti ya
mume wako lakini tulikuwa tunahitaji maelezo yako” Polisi mmoja akamwambia
mwanamke huyo.
“Maelezo gani?”
“Tuambie marehemu aliondoka
lini hapa nyumbani?”
“Aliondoka jana”
“Majira ya saa ngapi?”
“Aliondoka mchana baada ya
kula chakula, ndio hatukumuona tena”
“Kwa kawaida anapoondoka
nyumbani huwa anakwenda wapi”
“Huwa haniambii”
“Na jana alipoondoka
hakukwambia anakokwenda?”
“Hakuniambia”
“Sasa ngoja upelekwe
hospitali ukauone mwili wa marehemu halafu tutakuhitaji kituo cha polisi
uandikishe maelezo yako” Polisi aliyekuwa akizungumza na mke wa Yusufu
alimwambia.
Baada ya hapo sisi na polisi
hao tukaenda hospitalini ambako mke wa Yusufu aliuona mwili wa mume wake na
kuangua kilio. Alimpa Abdi kazi ya ziada ya kumnyamazisha.
Mwanamke huyo aliponyamaza
tulikwenda kituo cha polisi ambako mke wa Yusufu alitoa maelezo yake ambayo
yaliandikishwa. Kisha tukarudi nyumbani kwa Yusufu.
Abdi akaniambia
atashughulikia mpango wa mazishi ya ndugu yake ambayo alitaka yafanyike jioni
ya siku ile ile. Kwa hiyo alituma watu
kutoa taarifa ya kifo hicho kwa ndugu na jamaa mbali mbali.
Mpaka inafika saa nane mchana
mwili wa marehemu ulishachukuliwa na wanafamilia kutoka hospitali na kuletwa
nyumbani kwake ambako uliandaliwa haraka haraka kwa ajili ya mazishi.
Saa kumi na moja jioni Yusufu
akazikwa. Abdi akatangaza kuwa hakukuwa na matanga. Aliwambia watu kuwa matanga
ni mila za kizamani ambazo zimepitwa na wakati na hazimo katika dini.
Siku ile nilirudi hotelini
saa nne usiku kwani muda wote nilikuwa bega kwa bega na Abdi katika shughuli
zote za mazishi.
Baada ya kupita wiki moja mke
wangu akaniambia tena.
“Unajua kuwa Abdi anaweza kupata kichaa!”
“Kwanini” nikamuuliza.
“Tamaa yake ya kupata utajiri
imepita kiasi. Kila anapokaa anawaza utajiri tu, sasa mbaya zaidi anafanya
mambo mabaya yasiyostahili”
“Anafanya mambo gani?”
“Nataka nikupe siri nyingine,
unaju Abdi ndiye aliyemuua Yusufu!”
Nikashituka.
“Unasema kweli?”
“Abdi ndiye aliyemuua ndugu
yake, alikwenda naye kule akampiga chuma kisha akajifanya anamtafuta”
Nikatikisa kichwa changu
kusikitika.
“Sasa kwanini amuue ndugu
yake?”
“Si ile tamaa yake ya
utajiri! Aliambiwa na yule mganga wake kwamba kabla ya kukushika wewe na
kukutoboa utosi kwa msumari, kwanza amuue Yusufu”
“Amuue kwa kisa gani?”
“Kwa sababu yule mganga
alimwambia yule jini akitoka kwako anaweza kuingia kwa Yusufu kwa sababu wao ni
ndugu tumbo moja”
“Ndio akaamua amuue?”
“Ndio akamuua”
“Yule ni chizi kweli!”
“Sasa jihadhari, nadhani
wakati wowote anaweza kushughulika na wewe”
“Yaani aniue mimi”
“Sasa akishakutoboa utosi kwa
msumari unadhani utapona, si utakufa!”
“Haniwezi. Nitapambana naye.
Yule mtu dhaifu sana,
hana afya hata kidogo. Nikimpiga ngumi moja sidhani kama
ataamka”
Wakati ninazungumza na
Shamsa, ghafla Abdi akaingia.
Akatusalimia kisha
akaniambia.
“Nimekufuata twende shamba”
“Kuna nini?” nikamuuliza.
“Matembezi tu”
Nilitaka kumkatalia lakini
nilishindwa. Nikamwambia.
“Sawa”
Nikamuga Shamsa na kutoka na
Abdi.
Huko nje akaniambia tutatumia
gari lake. Tukajipakia kwenye gari lake
na kuondoka.
Shamba la Abdi lilikuwa
umbali wa kilometa kumi na mbili nje ya jiji la Mogadishu. Lilikuwa shamba kubwa la mitufaa
na mimea mingine mchanganyiko ikiwemo minazi na mikorosho.
Katikati ya shamba hilo alikuwa amejenga
nyumba yake kubwa ambayo alikuwa akiitumia akiwa shambani hapo.
Lakini baada ya muda kidogo
niligundua kuwa tulikuwa hatuelekei shambani kwa Abdi kwani nilikuwa nakufahamu.
Abdi alikuwa ameacha
njia ya kuelekea shambani kwake akakata
kushoto na kuingia katika njia
iliyoelekea katika msitu.
Kwa vile alikuwa
akinizungumzisha, nilighafilika kumuuliza alikuwa anaelekea wapi. Ghalfla
akakata tena kushoto. Tukawa tumeingia kwenye msitu.
Alilisimamisha gari chini ya
mti akafungua mlango na kushuka bila kuniambia tulifuata nini mahali pale.
Aliposhuka nilimuona
akielekea kwenye vichaka. Na mimi nikashuka na kumfuata. Alikuwa ameshatokomea
kwenye kichaka kimojawapo, nilipoona watu watatu wakitokea kwenye kichaka hicho
na kunifuata.
Walikuwa mapandikizi ya watu
wenye sura za kijahili. Nilipoona wamenizunguka nikasimama.
“Amekwenda wapi huyu jamaa?”
nikawauliza.
Hakukuwa na yeyote aliyenijibu zaidi ya kunitazama
kiubabe. Kitendo hicho kikanishitua sana.
Mmoja wa watu hao ambao
alikuwa amekata sharubu zake kama herufi ya M
alinisogelea akanishika ukosi.
Kabla sijajua nini
kingetokea, alinitandika ngumi moja ya shavu. Mwenzake mmoja aliishika mikono
yangu miwili kwa nyuma.
Wakawa wananikokota kuelekea
kule alikoelekea Abdi.
“Mbona mnanipiga?”
nikawauliza.
“Ulitaka tukubusu sio?”
Mwenye sharubu akaniuliza kwa dharau.
Waliniingiza kwenye kile
kichaka. Nilipoona siwaelewi nikapiga kelele kumuita Abdi.
Abdi sikumuona. Tukatokea
upande wa pili wa kile kichaka. Palikuwa na mti wa mwembe. Chini ya ule mti
palikuwa na shimo. Urefu wa shimo hilo ulikuwa
kama mita sita hivi na upana wake ulikuwa kama
wa kisima cha maji.
Kulikuwa na watu wawili
waliokuwa ndani ya shimo hilo
wakiwa wameshika kamba. Walikuwa wamesimama kama
waliokuwa wakisubiri kitu.
Juu ya lile shimo palipita
tawi la ule mwembe. Juu ya tawi hilo
palikuwa na mtu mwingine aliyekuwa amekaa.
Mimi nilikuwa nimekazana
kumuita Abdi ambaye nilikuwa simuoni. Wale jamaa walinikokota hadi karibu na
lile shimo kisha ghafla wakanisukuma nikaangukia ndani ya shimo hilo.
Wale jamaa wawili waliokuwa
ndani ya shimo hilo
walinidaka wakaniangusha chini. Mmoja alinishika mikono yangu ili nisiinuke,
mwingine aliishika miguu yangu na kunifunga ile kamba.
Baada ya kunifunga miguu
yangu, ncha moja ya ile kamba walimrushia yule mtu aliyekuwa juu ya tawi,
akaidaka. Aliivuta na kuikunja. Ilikuwa kamba ndefu.
Baada ya kuikunja kamba yote,
aliwarushia wale watu waliokuwa juu ya shimo. Watu hao waliidaka na kuanza
kuivuta.
Ile kamba ilipita juu ya lile
tawi la mti kisha ikaenda kwa wale watu, hivyo walipoivuta ilipitia juu ya lile
tawi. Waliivuta hadi mwisho. Sasa miguu yangu ambayo ilifungwa kwa kamba hiyo ikaanza kuinuliwa. Iliinuliwa hadi
ikawa juu.
Kamba iliendelea kuvutwa.
Mwisho nikawa nimenin’ginizwa kichwa chini kama
mkungu wa ndizi. Kamba iliendelea kuvutwa hadi mwili wangu wote ukawa
unanin’ginia kichwa chini miguu juu.
Ghafla nikamuona Abdi
akiingia kwenye lile shimo akiwa ameshika kikombe cheupe na nyundo.
“Abdi ndio nini hivi”
nikamuuliza.
Abdi hakunijibu chochote.
Aliimpa mtu mmoja ile nyundo akatoa msumari kutoka mfukoni mwake na kumpa.
“Sasa mtoboe utosi wake. Mimi
nitakinga damu yake kwenye kikombe” alimwambia yule mtu aliyempa ile nyundo na
msumari.
Jamaa akaupachika msumari
kwenye utosi wangu. Nikajua ni yale aliyoniambia Shamsa. Nikaanza kupiga
kelele.
“Abdi mbona unataka kuniua…nimekukosea nini…?”
Wakati napiga kelele Abdi alikuwa
akimuihimiza yule mtu aupige nyundo ule msumari ili atoboe utosi wangu.
“Mpige nyundo haraka
Garbela…toboa utosi huo…?”
LOH! MASIKINI JAMAA ANAUAWA!
HEBU ENDELEA KUFUATILIA HAPO KESHO UONE NINI KITATOKEA?
No comments:
Post a Comment