Sunday, September 4, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 60

SIMULIZI A FAKI A FAKI
 
MWANAMKE 60
 
Baada ya kama nusu saa hivi yule jini aliyekuja kwanza akarudi peke yake akiwa ameshika bahasha.
 
“Begi lako ni lipi na lipi?” akaniuliza.
 
Nikamuonesha yale mabegi mawili niliyokwenda nayo. Yule jini akayabeba yote mawili kisha akaniambia.
 
“Twende”
 
Nikatoka naye katika lile jabali tukashika njia mbayo mimi na Zena tulikwenda nayo. Tukashuka chini baharini. Ikumbukwe kwamba muda ule ulikuwa ni usiku lakini ulikuwa usiku wa mbalamwezi.
 
Tulipofika pwani yule jini alinitafutia mahali chini ya mti akaniambia.
 
“Kaa hapa hadi saa tisa usiku. Utaona msafara mrefu wa majini unapita kutoka upande wa kusini kwenda kaskazini. Subiri mpaka utakapowaona mjini waliobeba kichanja (aina ya jukwaa). Ukiwaona majini hao wafuate uwasimamishe.
 
“Pale juu ya kichanja utamuona Sultani wa majini amebebwa, utamgundua kutokana na kilemba chake kikubwa cha rangi nyeupe, utampa hii barua iliyoandikwa na mzee Jabalkeysi” Jini huyo akaniambia nna kunipa ile bahasha aliyokuwa ameishika.
 
“Nikishampa itakuwaje?” nikamuuliza.
 
“Ataisoma halafu kuna kitu atakwambia. Hivyo ndivyo nilivyoagizwa na mzee Jabalkeysi”
 
Yule jini aliponiambia  hivyo akaondoka na kuniacha pale pale. Hapo mahalli palikuwa na mazingira ya kutisha sana, halafu niliambiwa nikae peke yangu hadi saa tisa uiku nisubiri msafara wa majini. Hao majini hawatanidhuru? Nikajiuliza.
 
Pamoja na hofu niliyokuwa nayo ilibidi nikae hapo kwani sikuwa na la kufanya. Hata kama ningetaka nikimbie nirudi kwetu ningerudi kwa njia gain?.
 
Nikakaa hapo huku nikitetemeka kwa baridi. Mawazo na hofu vilikuwa vimesonga kwenye moyo wangu. Nilikuwa nikijiuliza maswali chungu nzima yasiyokuwa na majibu. Nikatamani Zena atokee pale anirudishe kwetu lakini hakukutokea Zena wala yeyote.
 
Kila wakati nilikuwa nikitazama saa yangu kujua majira yalivyokuwa yanakwenda. Kwa mtu mwenye wasiwasi na hofu kama nilivyokuwa mimi, nilihisi muda ulikuwa hauendi kabisa na baridi ilikuwa ikizidi kuniingia kwenye mifupa.
 
Baada ya masaa machache lakini niliyoyaona marefu ikafika saa tisa usiku. Jinsi nilivyokuwa nimejificha pale chini ya mti haikuwa rahisi kuonekana labda kwa jini aliyekuwa karibu.
 
Ghafla nikauona ule msafara nilioambiwa. Walikuwa majini waliovaa nguo nyeupe tupu wameandamana wakitokea upande wa kusini kuelekea upande wa kaskazini. Niliouna msafara huo tangu ulipoanza kutokea.
 
Nilipotupa macho nikakiona kichanja kilichokuwa kimebebwa katikati ya msafara huo. Kilikuwa kimepembwa kwa vitambaa vyeupe na kilikuwa na vidirisha.
 
Nikajiuliza kama ningekuwa na moyo na ujasiri wa kujitokea na kusimamisha msafara huo wa majini? Lakini nikajiambia hilo ndilo nililokuwa nikilisubiri pale, kwa hiyo ilikuwa lazima nilitekeleze.
 
Ule msafara ulifika karibu, nikainuka ghafla na kuukimbilia huku nikipiga kelele.
 
“Jamani subirini, nina ujumbe wa Sultani!”
 
Mara moja nikaouna msafara huo umesimama. Majini hao wakawa wananitazama mimi.
 
Yalikuwa ni maingira ya kutisha sana lakini yale matatizo niliyokuwa nayo yalinipa ujasiri. Nikaufikia ule msafara.
 
“Jamani nina ujumbe wa Sultani” nikawambia huku nikimtazama Yule jinni aliyekuwa kwenye kile kichanja kilichotengezwa kama gari lililobebwa likiwa na madirisha yenye mapazia.
 
Jini aliyekuwemo kwenye kichanja hicho alikuwa mfupi na mnene mwenye ndevu na sharubu nyeupe. Alikuwa amevaa kilemba cheupe na joho la rangi nyeupe. Alionekana kama sultani hasa.
 
Kulikuwa na jinni mmoja allinipa ishara nisogee pale kwenye kichanja. Nikasogea na kumuona vizuri yule sultani.
 
“Assa;aam alaykum” akaniambia kwa sauti tulivu iliyonipa matumaini.
 
“Wa alayka salaam” nikamjibu na kunyoosha mkono wangu kumpa ile barua.
 
Aliipokea akaikunjua na kuisoma.
 
Alipomaliza kuisoma aliniuliza.
 
“Wewe ndiye Amour?”
 
“Ndiye mimi”
 
Nilipomjibu hivyo aliwambia walae majini.
 
“Subirini kidogo hapa kuna mashitaka”
 
Majini wote wakanyamaa kimya kusikiliza.
 
“Ni nani ambaye anamfahamu Zainush binti Jabalkeyss?”
 
Majini kadhaa wakajitokeza wakidai kuwa wanamfahamu.
 
“Ni nani ambaye anaweza kumleta hapa kwa haraka sana”
 
Wale majini wote wakanyoosha vidole juu, kila mmoja akionesha kuwa angeweza kumleta Zainush kwa haraka.
 
“Wewe unaweza kutumia muda gani kumleta hapa?” Sultani wa majini akamuuliza mmoja wa wale majini.
 
“Mimi naweza kumleta chini ya dakika moja tu”
 
“Utatuchelewesha” Sultani huyo wa majini alimwammbia akamtazama jinni mwingine.
 
“Je wewe unawea kumleta kwa muda gani?”
 
“Mimi naweza kumleta chini ya nusu dakika”
 
“Wewe pia utatuchelewesha. Hakuna anayeweza kumleta chini ya robo dakika?”
 
Akatokea jinni mmoja mzee lakini aliyeonekana kuwa na nguvu.
 
“Mimi nawea kumleta” akasema.
 
“Kwa muda gani?”
 
“Kwa kiasi cha kufumba na kufumbua tu, nitakuwa nimeshakuja naye”
 
“Wewe nenda kamlete. Tunakusubiri”
 
Hapo hapo Yule jinni alipotea mbele ya macho yangu. Hata kabla sijafumba macho yangu na kuyafumbua nikamuona Yule jinni akitua tena akiwa peke yake tena jicho lake la mkono wa kushoto likiwa linavuja damu.
 
“Yuko wapi Zainush?” Sulatani wa majini akamuuliza akiwa amekunja uso.
 
“Nimeshindwa kumkamata. Kwana nilihangaika sana kumtafuta. Nilimkuta katika visiwa vya Comoro akinywa mvinyo na wasichana wenzake wa kijini. Nilipotaka kumkamata wakatokea walinzi wao wakanishambulia na kunipasua jicho langu”
 
“Zainusha ndiye aliyekufanyia hivyo? Basi ataniona” Yule Sultani alliyeonesha kukasirika alisema kasha akawaita majini wawili kwa majina.
 
“Harishi na Kaikushi!”
 
Majini hao wakafika mbele yake. Walikuwa vibonge vya majini. Kila mmoja alikuwa ameshika jambia lililokuwa linameremeta.
 
“Mwende na huyu nyumbani kwake. Mtakapomuona Zainusha anamfuata mkateni kichwa chake mniletee au mkiweza mleteni kwangu akiwa mzima, nije nimfunze adabu. MMenisikia?”
 
“Tumekusikia bwana mkubwa” majini hao wakamjibu.
 
“Haya nendeni naye”
 
Msafara huo ukaendelea na safari. Mimi na wale majini tulifuatana hadi kwenye ule mti nilipokuwa nimeketi nikachukua mabegi yangu. Jini mmoja akanishika mkono na kuniambia nifumbe macho. Nikayafumba.
 
Baadaye nilisikia sauti yake ikiniambia.
 
“Sasa fumbua macho yako”
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment